Wakati tume ya mabadiliko ya katiba ikiwa imewasilisha rasimu ya pili ya katiba, na kupendekeza muundo wa serikali tatu (Serikali ya jamhuri wa muungano wa Tanzania, Serikali ya jamhuri ya watu wa Zanzibar na ile ya jamhuri ya Tanganyika), jicho la tatu linahitajika kuona ni kwa jinsi gani serikali hizi zinaweza kufanya kazi pasipo migongano.
Kwa muundo uliopo sasa wa serikali mbili, Rais wa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar anaruhusiwa kuunda wizara azitakazo (maji, nishati, miundombinu n.k) na kuteua mawaziri na manaibu waziri. Na ukiangalia kazi zinazofanywa na mawaziri wa serikali kuu (ukiacha waziri mkuu) zimejikita zaidi bara. Hoja ni kwamba kukiwa na serikali ya Tanganyika yenye rais wake na mawaziri wake, kazi za mawaziri wa serikali kuu (ya jamhuri ya muungano) zitakuwa ni nini.
Kuhusu swala la uwakilishi wa wananchi, sasa kuna bunge kwa serikali kuu na baraza la wawakilishi kwa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar. Gharama za uendeshaji wake hazionekani kama ni mzigo sana kwani baraza la wawakilishi lina wajumbe wachache. Sasa kukiwa na lile la Tanganyika lenye wajumbe zaidi ya 200 (majimbo ya bara), gharama za uendeshaji zitakuwaje.
Rais wa nchi husika (mfano sasa yule wa serikali ya Zanzibar) ndiye mwenye watu (watu wanamuona kama ndiye aliye karibu nao zaidi). Sasa tukiwa na yule wa Tanganyika ataekuwa na ushawishi kwa watu wa bara, rais wa serikali kuu anakuwa na watu gani.
Tukija kwenye swala la uwakilishi kwa uwiano wa ki-nchi washiriki (yani Tanganyika na Zanzibar), kuwa mwenye dhamana akitoka bara basi naibu/makamu atoke zanzibar na kinyume chake, je inaleta mantiki ukichukulia tofauti kubwa ya idadi ya idadi ya watu kati ya nchi hizi mbili (zaidi ya milioni 35 kwa bara na pungufu ya milioni 5 kwa Zanzibar) na ukubwa wa maeneo ya nchi hizi mbili.
Nadhani hili swala linahitaji kuangaliwa kwa jicho la tatu zaidi ya kuliorodhesha kwenye katiba mpya