Serikali sasa yalea mafisadi wa BoT

Kimbembe

Senior Member
May 14, 2006
122
15
Serikali sasa yalea mafisadi wa BoT

Waandishi Wetu Machi 5, 2008



Ukusanyaji wa fedha za EPA BoT

UAMUZI wa kupokea fedha zilizoibwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) bila kuwachukulia hatua wahusika, unaashiria uchafu na Serikali kukumbatia ufisadi waziwazi, imeelezwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wiki hii katika mahojiano ya simu na Raia Mwema, baadhi ya watu mashuhuri, wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa, wamesema fedha zinazorejeshwa hazikuwa madeni wala mikopo, bali ziliibwa, wahusika wajitambue kuwa walifanya uhalifu, na hivyo wanapaswa kukamatwa, kutangazwa hadharani na kufikishwa mahakamani.

Waliozungumzia ufisadi wa fedha za BoT na hatua ya sasa ya kurejesha fedha hizo kinyemela, ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Dk. Wilbroad Slaa, Kiongozi wa Upinzani bungeni na Mbunge wa Wawi (Chama cha Wananchi - CUF), Hamad Rashid Mohamed na Mwenyekiti wa United Democratic Party (UDP), na Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo.

Dk. Slaa ameiambia Raia Mwema kwamba anazo taarifa kwamba wahusika wanakwenda kurejesha fedha hizo wakiwa na mawakili wao, ambao wanawasaidia kuingia mikataba na Serikali, ya kutoa pesa kidogo na baadaye kuendelea kulipa pole pole na kwa muda mrefu.

Dk. Slaa ndiye anatajwa kuwa mwanasiasa mwenye ushahidi mkubwa kuhusiana na sakata zima la BoT na amepania kuendelea kulivalia njuga kwa nguvu zake zote.

Wiki iliyopita Serikali kupitia Waziri wake wa Fedha, Mustafa Mkulo, ilitangaza ya kuwa zaidi ya sh. bilioni 50 zilizochukuliwa kwa njia ya ufisadi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika BoT zimerudishwa.

Kiasi hicho cha fedha zilizorejeshwa ni sehemu ya sh. bilioni 133 ambazo ziligundulika kuchukuliwa na mafisadi kwa nyakati tofauti.

Serikali pia imedai kwamba inakadiria kukusanya kiasi cha Sh. bilioni 106 kati ya hizo na hivyo kuzua maswali zaidi ya uhakika huo unatoka wapi na kiasi kinachosalia kilikwenda wapi huku baadhi ya watu wakielekeza moja kwa moja matumizi ya fedha hizo katika Uchaguzi Mkuu wa 2005.

Dk. Slaa yeye anasema: “Wahusika wanapokwenda na mawakili wao kurejesha fedha hizo, halafu kuingia mikataba na Serikali, ni sura nyingine ya ufisadi unaosimamiwa na Serikali yenyewe.

“Suala la kurejesha fedha za BoT lina sura nyingi. Serikali inachokifanya hivi sasa ni kuwapotosha wananchi ili wafurahi kuwa fedha zinarejeshwa wakati wahusika wanafichwa na wanaingia mikataba na Serikali.

“Ni kweli tunataka fedha zirejeshwe. Lakini kwa kuwa fedha hizi si madeni wala mikopo bali ziliibwa BoT, wahusika wanapaswa kukamatwa,” anasema Dk. Slaa.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, kitendo cha Serikali kuwafuta kazi wafanyakazi waliohusika kuidhinisha fedha hizo za EPA halafu kuwakumbatia mafisadi kwa kutowakamata, kuwatangaza na kuwachukulia hatua za kisheria, ni kujenga matabaka katika nchi, ni kinyume cha utawala bora na ni uvunjaji wa sheria.

“Serikali haisemi watachukuliwa hatua gani, badala yake inapokea pesa tu. Ifahamike tu kwamba sisi hatutaacha kupiga kelele,” anasema Dk. Slaa.

Kwa upande wake, Cheyo aliliambia Raia Mwema kwamba hatua ya kurejesha fedha hizo za EPA katika BoT bila wahusika kutangazwa na hatua kuchukuliwa dhidi yao, imemshangaza mno na anashindwa hata kusema.

“Hivi sasa nipo Denmark. Nilipopata taarifa hizo nilishangazwa sana. Si vizuri mtu kuzungumza mambo ya nyumbani ukiwa nje ya nchi, lakini inatosha kusema tu kwamba nimeshangaa sana,” alisema Cheyo kwa simu akieleza kuwa yuko Denmark.

Hamad Rashid alisema kwamba mtindo unaotumiwa na Kamati ya Rais kuhusu fedha hizo za EPA si mbaya kwa kuwa ni njia ya kukusanya ushahidi pole pole, na baadaye wahusika watachukuliwa hatua za kisheria.

“Mimi nadhani Kamati ya Rais imetumia busara kunyamaza kwanza, ili kupata fursa ya kutosha kukusanya ushahidi na vielelezo vingine. Hii itasaidia kuwabana wahusika, kwamba kama hawakuhusika na ufisadi ni kwanini walirejesha fedha hizo.

“Kwa hiyo, hatua ya sasa inayochukuliwa na kamati inayochungumza suala hilo inaisaidia Serikali katika sura mbili: Ya kwanza ni kupata ushahidi wa kutosha na ya pili ni kurejesha mapato hayo ya Serikali.

“Ndiyo maana sisi wapinzani pia tumechukua hatua ya kunyamaza kwamba, tukiamini kuwa hatimaye Serikali itawatangaza wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria kwa uhakika zaidi,” anasema Hamad Rashid kuondoa hisia kwamba Upinzani unashirikiana na Serikali katika kubariki ufisadi katika suala hilo la BoT.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, alisema haijawahi kutokea mwizi akaambiwa kurudisha alichoiba bila kukamatwa na kushitakiwa, kinachoonekana sasa ni Serikali kujenga tabaka la wanaolindwa na wale wanaoshitakiwa na kufungwa.

“Inawezekana kwamba Serikali inalenga kupata fedha na wanaogopa kuzikosa lakini inasahau kwamba inaweka mfano mbaya sana kwa wananchi wanaofungwa kwa wizi mdogo mdogo huku wezi wakubwa wanaachwa,” alisema.

Zitto aliongeza kwa kusema, “hatari kubwa zaidi ni kutotendewa haki kwa watendaji wa Serikali na BoT ambao wamechukuliwa hatua akiwamo aliyekua Gavana, Daudi Ballali, aliyetimuliwa kazi kwa aibu kwa fedha ambazo sasa waliochukua wanabembelezwa.”




MWANASHERIA Mkuu, Johnson Mwanyika

Mbunge huyo alisema hata watendaji wa BoT ambao wamechukuliwa hatua na wanasheria walioshiriki kusimamia kisheria hawatetendewa haki ikiwa wahusika hawatachukuliwa hatua.

Ofisa mmoja wa ngazi ya juu serikalini, aliyezungumza na Raia Mwema kwa masharti ya kutotajwa, anasema hatua hiyo ya Serikali inaweza kuitia aibu zaidi Serikali yenyewe kwa kuwa wahusika wa sakata hiyo hawakupaswa kubembelezwa na badala yake wangebanwa na kuchukuliwa hatua madhubuti ili kuwa fundisho kwa wengine.

“Hii ni aibu kubwa kwa Serikali na tukiendelea na mtindo huu, tutakuwa tumerudi nyuma zaidi katika kupiga vita ufisadi, kwani sasa tunauhalalisha wenyewe. Lazima wahusika wakamatwe hasa wale walioghushi nyaraka waziwazi,” anasema ofisa huyo ambaye ofisi yake inahusika na masuala ya fedha.



MKURUGENZI wa TAKUKURU, Edward Hosea

Ofisa mwandamizi wa BoT ambaye naye alizungumza na Raia Mwema kwa masharti ya kutokutajwa, alisema kwamba maamuzi yote juu ya hatua gani zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao wa EPA yako mikononi mwa timu aliyounda Rais Jakaya Kikwete inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu Johnson Mwanyika na wajumbe Inspekta Jenerali wa Polisi Said Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Edward Hosea.

“Shughuli ya kurejesha fedha hizo na hatua zote za kisheria na nyinginezo zitakazochukuliwa ni ya kamati ya Mwanyika,” alisema ofisa huyo wa BoT.

Aliongeza: “Kama ni kurejesha fedha, kuzuia akaunti au mali za watuhumiwa, ni juu ya watu hao watatu.

“BoT haiwezi kuhusika kwa sababu ya mgongano wa kimaslahi na pia kwa sababu ya uhusiano wake na baadhi ya benki nyingine.”

Habari zaidi zinaeleza kwamba hata wahusika wa ile kampuni hewa ya Kagoda, wamegawana dhima ya kuilipa sehemu ya Shilingi Bilioni 40 (Dola za Marekani Milioni 30.8) na tayari imethibitika kwamba tayari mfanyabiashara mmoja maarufu amekwisha kulipa zaidi Shilingi Bilioni 12 na kuahidi kulipa zaidi ya Sh bilioni 20 ifikapo Juni mwaka huu.

Hata hivyo, kuingizwa kwa mfanyabiashara huyo kunaelezwa kuzua utata mkubwa hasa ikizingatiwa kwamba uhusika wake unaweza kuwa katika hatua za mwisho kabisa za kuhamisha fedha na kwamba wahusika wakubwa wa mchakato mzima wamekua wakilindwa kwa nguvu zote na maofisa wa Serikali.

Imeelezwa kwamba sakata hilo kwa sasa linaweza kuwaingiza hata baadhi ya viongozi wa upinzani ambao wanatakiwa sasa kutolizungumzia kabisa suala hilo kwa kile kinachojaribu kuaminishwa kwamba ni kwa “Maslahi ya Taifa”.

“Tayari wanataka sasa kuwarubuni wapinzani ili waingie katika mkakati wa kutetea wanaorudisha fedha kwa maelezo kwamba wanalinda na kutetea Maslahi ya Taifa, lakini lengo kuu ni kulinda wahalifu kwani Watanzania wengi wanafuatilia kwa makini na hivyo ukiwachezea hakutakua na amani ya kweli,” anasema Mbunge mmoja wa CCM.
 
Back
Top Bottom