Serikali kupokonya wasioendeleza mashamba ya mkonge

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa tahadhari kwa walioomba mashamba kwa ajili ya kilimocha mkonge na kusema serikali haitasita kuwapokonya ardhi iwapo watabainika kulima mazao tofauti na zao hilo.

Alitoa kauli hiyo jana alipomtembelea mkulima mdogo wa mkonge katika shamba la Magoma lililopo wilayani Korogwe.

Alisema nia ya serikali ya kugawa mashamba hayo ni kwamba yaendelezwe, wananchi walime mkonge na siyo kuyachukua na kulima mazao mbadala kama vile mahindi .

"Tumedhamiria kuleta mapinduzi kwenye mkonge tayari tumeshaielekeza bodi na Benki ya Kilimo kuwapatia mikopo yenye riba nafuu wakulima wadogo wa zao hilo ili waweze kulima sasa nitashangaa kwa jitihada zote hizo atokee mkulima kaomba ardhi kapewa halafu anakuja kulima zao jingine," alisema Waziri Mkuu.

Aliwataka wananchi ambao wamepeleka maombi ya kuomba maeneo ya ardhi kwenye mashamba ya bodi kujiandaa katika kushiriki kwenye kilimo hicho kwani ndio lengo la serikali yetu.

Waziri Mkuu alisema kuwa utaratibu huo wa kuwapokonya maeneo utakwenda mpaka kwa wawekezaji wakubwa ambapo wanamaeneo lakini wameshindwa kuyaendeleza.

"Wapo wakulima wakubwa humu nchini wameomba maeneo makubwa lakini wameshindwa kuyaendeleza na wengine wanalima mazao mengine niwaambie tu tutawapokonya na kuyagawa kwa wananchi walime mkonge," alisema.

Alisema kuwa serikali haitavumilia kuona watu wachache wanarudisha nyuma dhamira yetu ya kutimiza malengo ya kulima kilimo cha mkonge wanalima mazao mengine.

Aliitaka bodi ya mkonge kuwapatia ushauri na namna bora ya kilimo bota kwa zao hilo ili kuhakikisha wakulima hao wanafanikiwa lakini na lengo la serikali la kuongeza uzalishaji linaweza kufikiwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliitaka benki ya kilimo kuweka utaratibu wa mikopo kwa wakulima hao kwa riba isiyo zaidi asilimia kumi.

"Nimeshatoa maelekezo kwa bodi na benki wakapange utaratibu mzuri wa kuwawezesha wakulima na kwa kuanzia waanze na hawa wa mashamba ya bodi kuwakopesha ili wapate mikopo ambayo itawawezesha kulima kwa ufanisi, " alisema Naibu Waziri.

Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigela alisema kuwa changamoto kubwa ni ubovu wa miundombinu ya barabara kufikisha mazao yao kiwandani na wakati mwingine hulazimika kufanya ukarabati wenyewe.

"Niiombe Wakala wa Huduma za Barabara vijijini (Tarura) kujipanga kuzifanyia marekebisho hizi barabara zilizoko kwenye mashamba ili iwe rahisi mkonge uliovunwa kufikishwa kiwanda kwa urahisi bila ya hofu ya ubovu wa barabara," alisema Shigela.

Alisema kuwa kwa mikakati iliyopo sasa mkoa wa Tanga unarudi kuwa katika enzi yake ya kilimo cha mkonge kwani unakwenda kuinuka kiuchumi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Mwenyekiti wa wakulima wadogo, Shamba la Magoma, Shedrak Lugendo alisema kuwa kwa mwaka jana waliweza kuzalisha tani 721.4 na baaada ya kuuza walipata Sh bilioni 2.3.

"Baada ya makato yote wakulima waliweza kupata fedha taslim sh bilioni 1.1, kodi ya serikali ilikuwa Sh milioni 63.2, " alisema Lugendo.

Mkulima mdogo, Erasto Urio alisema kuwa anamiliki eneo lenye ekari 200 katika shamba la Magunga lakini eneo aliloliendekeza ni ekari 182.

Shamba la mkonge la Magunga linaukubwa wa ekari 35, 000 lakini zilizoendelezwa mpaka sasa ni ekari 28000 pekee ambapo ni miongonj mwa mashamba ambayo yapo kwenye utaratibu wa kugaiwa kwa wananchi ili kulima zao hilo.
 
Kulima tulime sisi, kuuza tunapangiwa,
Tukikataa uasi, tena tunaadhibiwa,
I wapi yetu nafasi, ile tuloahidiwa?
Huo uhuru wakweli, mwenzenu sijauona.
 
Back
Top Bottom