Serikali kupitia TIC yaingia mikataba ya Tsh Trilioni 4.2 na kampuni binafsi za wazawa kuzalisha bidhaa ndani

ChoiceVariable

JF-Expert Member
May 23, 2017
43,076
49,774
My Take: Hongera Serikali,hii ni hatua nzuri Ili kuacha kuagiza bidhaa ambazo tunaweza uzalishaji ndani ya Nchi.

=========

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimesaini mikataba 10 yenye thamani ya zaidi ya Sh4 trilioni ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa uwekezaji kwa kuwezesha viwanda katika sekta za kilimo, ujenzi na nishati.

Mikataba hiyo itakapotekelezwa inatarajiwa kutoa ahueni katika upatikanaji wa sukari, saruji, mafuta ya kupikia na vifaa vya ujenzi.

Minane kati ya miradi hiyo ni mipya na miwili ni makubaliano ya nyongeza ambayo kwa pamoja itatengeneza ajira za moja kwa moja 16,355, huku zile zisizo za moja kwa moja zikiwa 229,250.

Mradi

Miongoni mwa mikataba iliyosainiwa ni upanuzi wa kilimo cha miwa kwa ajili ya uzalishaji wa sukari katika kiwanda cha Kilombero ambao ukikamilika utazalisha tani 271,000 za sukari.

Mwingine ni wa kilimo cha miwa katika kiwanda cha Mufindi Paper Mills unaotekelezwa mkoani Kigoma ambao ukikamilika utazalisha sukari tani 340,000.

Takwimu kwa mujibu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka ni tani 482,000. Kwa mwaka 2021/2022 uzalisahji wa ndani ulikuwa tani 379,280.83.

Mwaka 2022/2023 uzalishaji ulifikia tani 456,019.73.

Kwa mujibu wa wizara, kiwanda cha sukari cha Bagamoyo kitakapokamilika kitapunguza pengo la uzalishaji na uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.

Kiwanda hicho kinatarajiwa kukamilika 2024/2025 na kitazalisha sukari tani 70,000 na kutoa ajira takriban 1,000.

Usindikaji mafuta

Nafuu inatarajiwa kwenye mafuta ya kupikia kupitia mradi wa usindikaji katika kiwanda cha Wild Flower and Oil Mills mkoani Singida utakaozalisha mafuta tani 75 kwa siku.

Mahitaji nchini ni takriban tani 570,000, huku viwanda vya ndani 771 vikizalisha tani 205,000 na zilizosalia tani 365,000 huagizwa kutoka nje kutosheleza mahitaji nchini.

Serikali inapendekeza kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 25 kwa kila tani moja ya ujazo badala ya asilimia 35 kwa kipindi cha mwaka mmoja kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha mwisho (refined).

Vifaa vya ujenzi

Mradi wa upanuzi wa kiwanda cha uzalishaji saruji cha Lake Cement utaongeza uzalishaji hadi kufikia tani milioni moja kwa mwaka. Mradi mwingine utakaotekelezwa ni wa kiwanda cha saruji cha Dangote mkoani Mtwara ambap ulishapewa hadhi ya uwekezaji mahiri.

Uzalishaji saruji unaofanyika kwenye viwanda 14 vilivyopo nchini, takwimu za uzalishaji kwa mwaka 2022 zinaonyesha vinazalisha tani 10,850,000 kwa mwaka ambapo mahitaji ya ndani ya nchi ni tani 7,100,000 kwa mwaka.

Ziada ya tani 3,750,000 huuzwa katika soko la nje hususan katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC), Rwanda, Uganda, Malawi, Zambia na Msumbiji.

Katika bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/24 inapendekeza kutoza ushuru wa Sh20 kwa kila kilo moja ya saruji ambayo ni sawa na Sh1,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 50.

Kauli ya Waziri

Akizungumza baada ya kusaini mikataba hiyo, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji alisema miradi hiyo imepewa msukumo mkubwa kwa kuwa inalenga kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.

“Tumeipa miradi hii hadhi ya kimkakati kwa sababu itasaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje kama vile sukari na mafuta ya kupikia, hii ina maanisha kwamba wakulima watakuwa na fursa kuuza mazao yao lakini uchumi wa nchi utakua,” alisema.

Aliwataka wawekezaji kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo unakwenda sambamba na makubaliano katika mikataba na endapo kutatokea vikwazo ni muhimu watoe taarifa mapema.

“Uwekezaji huu ni matokeo ya mageuzi tuliyoyafanya katika sheria ya uwekezaji inayotoa mazingira wezeshi ya uwekezaji, hivyo ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha pande zote zinanufaika,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuugenzi Mtendaji wa kiwanda cha sukari Kilombero, Guy Williams alisema, “Uwekezaji wetu ni wa muda mrefu na lengo letu ni kupanua wigo wa uzalishaji wa sukari nchini. Idadi ya watu inaongezeka hivyo ni muhimu pia kwa uzalishaji kuongezeka. Tutahakikisha mradi unatekelezwa kwa muda uliopangwa.”

Mwenyekiti wa kongani ya viwanda ya Sinotan Kibaha, Janson Huang alisema, “Tunashukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji. Tulianza kazi mwaka uliopita, tumepata ushirikiano wa kutosha kutoka, TIC tupo katika hatua za utekelezaji.”

Maoni ya wadau

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Lawi Yohana alisema uwekezaji huo utakuwa na tija kwa kuwa bidhaa zitakazozalishwa ni zile ambazo viwanda vya ndani havizalishi kwa kiwango kikubwa.

“Uzalishaji ukiwa chini maana yake tunahitaji ziada kutoka nje ya nchi, tukiaagiza bidhaa nje mojawapo ya madhara ni kutengeneza ajira kwa nchi nyingine na kutumia fedha za kigeni kwenye uagizaji,” alisema.

Dk Timoth Lyanga, mtaalamu wa uchumi alisema mikataba hiyo itakwenda kuchochea uzalishaji wa ndani.

“Mikataba hii itakwenda kuongeza uzalishaji sukari ambayo itatosheleza wananchi na kutengeneza unafuu kwa walaji kwa sababu bidhaa ikiwa nyingi sokoni bei inashuka,” alisema.

Kuhusu saruji alisema uzalishaji utaongezeka hivyo kutakuwa na unafuu wa wananchi kujenga nyumba na kuboresha makazi.

Naye Greyson Mgonja, mchambuzi wa siasa na uchumi alisema kupitia uwekezaji unaofanyika Serikali itapata fedha nyingi ambazo zitaelekezwa katika kuboresha huduma muhimu za afya, elimu na miundombinu.

Ajira zitakazopatikana

Mradi wa kongani ya viwanda wa Sinotan unatarajiwa kuwa na viwanda zaidi ya 200. Utakapokamilika utagharimu Dola za Marekani 327 milioni na utaleta ajira 2,000 za moja kwa moja na 50,000 zisizo za moja kwa moja.

Kilombero Sugar unaohusisha upanuzi wa kilimo cha miwa na kiwanda cha uzalishaji wa sukari unagharimu Dola 238.5 milioni, utazalisha ajira 1,404 za moja kwa moja na 15,000 zisizo za moja kwa moja.

Mradi wa Wilmar unahusisha uchakataji wa nafaka. Utagharimu Dola 51.5 milioni, utakapokamilika utaleta ajira mpya za moja kwa moja 360 na 1,000 zisizo za moja kwa moja.

Mradi wa upanuzi wa kiwanda cha uzalishaji saruji cha Lake Cement ambao awali uwekezaji wake ulikuwa Dola 101 milioni umeongezewa Dola 26 milioni na kufikia uwekezaji wa Dola 127 milioni. Ukikamilika utazalisha tani milioni moja kwa mwaka na kutoa ajira 401 za moja kwa moja na 450 zisizo za moja kwa moja.

Mradi wa kusindika na kuhifadhi gesi ya LPG na miundombinu ya gesi ya Oilcom utakaogharimu Dola 111.87 milioni, utatoa ajira 1,600 za moja kwa moja na 160,000 zinazotokana na mnyororo wa thamani wa mradi huo.

Mradi wa Wild Flower and Oil Mills utagharimu Dola 24 milioni. Mradi huu utatengeneza ajira 190 za moja kwa moja na 400 zisizo za moja kwa moja.

Mradi wa kilimo cha miwa na kiwanda cha uzalishaji sukari cha Mufindi Paper Mills utagharimu Dola 320 milioni. Utaleta ajira mpya 3,000 za moja kwa moja na 2,000 zisizo za moja kwa moja.

Mradi wa kiwanda cha uzalishaji mabati cha Lodhia Steel utakaogharimu Dola 45 milioni utaleta ajira 400 za moja kwa moja na 150 zisizo za moja kwa moja.


Chanzo: Mwananchi
 
Ungejua hata ulichoandika hakisomeki, ungeenda msaidia Dada yako kufua nguo za shemeji kuliko kukaa hapo na kulishwa na hufanyi chochote zaidi ya kuja mitandaoni.
Wivu tuu huna lolote ,kama ni maandishi walaumu mods wa jf ya machadomo ndio wametumia fonts mbaya Kwa sababu ya wivu Ili ujumbe usifike 😆😆
 
Back
Top Bottom