BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tec) limeilaumu Serikali kuwa, inawakingia kifua watu wanaoendesha mihadhara ya kidini inayokashifu dini nyingine.
Rais wa Tec anayemaliza muda wake, Askofu Mkuu, Yuda Thadeus Ruwaichi alisema jana kuwa, licha ya kwamba jambo hilo linaweza* kuleta chuki na vurugu nchini, Serikali haichukui hatua zozote dhidi yake.
Serikali na mamlaka za dola zinawakingia kifua wadau wa harakati wanaoendesha mihadhara yenye kukashfu dini nyingine, pamoja na kufahamika lakini hawachuliwi hatua zozote, alisema.
Rais huyo ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa ibada maalumu ya kutangaza uongozi mpya wa baraza hilo.
Katika uchaguzi huo Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo la Iringa, alichaguliwa kuwa rais mpya kwa kipindi cha miaka mitatu.
Askofu Ruwaichi aliitaka Serikali kupiga marufuku mihadhara na makongamano ya kidini, kwani ikiendelea baada ya miaka michache nchi itaingia katika machafuko makubwa yatakayoleta maafa.
Ruwaichi* ambaye alikuwa akitoa tamko hilo kwa niaba ya maaskofu wote, alisema wameshangazwa na ukimya wa Serikali katika kushughulikia vurugu za kidini zinazoendelea kutokea hapa nchini na kuwataka wasiogope kuchukua hatua, kwani hiyo ndiyo dhamana waliyopewa na wananchi.
Tunalaani vikali vurugu na vitendo vya uchomaji moto makanisa vilivyotokea huko Zanzibar na kuwafanya wananchi waishi kwa wasiwasi kwa sababu ya kushindwa kupewa ulinzi na vyombo vya dola, alisema Askofu Ruwaichi.
Alisema maaskofu wanatoa pole kwa waathirika wa vurugu hizo huko Zanzibar ambao wanaendelea kuishi kwa wasiwasi kutokana na vitisho vinavyoendelea kutolewa dhidi yao.
Alisema Serikali kama inataka kujenga imani mbele ya wananchi wake, inatakiwa kuchukua hatua ili kuhakikisha vurugu za kidini hazipati nafasi.
Watanzania na mamlaka husika za Serikali zinatakiwa kutafakari kwani mwanzo wa makubwa ni madogo, na mdharau mwiba mguu huota tende, alisema na kuongeza kuwa vurugu hizo zikiachwa ziendelee zitasababisha matatizo makubwa.
Askofu Ruwaichi alisema kati ya mwaka 2001 na sasa jumla ya makanisa 25 yalichomwa moto Zanzibari, lakini hakuna aliyekamatwa wala kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kama hakuna mtu yeyote aliyechukuliwa hatua kwa uchomaji moto makanisa hayo, unadhani tatizo hili litamalizika, alihoji.
Aidha, Askofu Ruwaichi* alitaka vyombo vya habari vinavyoeneza uzushi na chuki za kidini vifungiwe vinginevyo ndiyo kitakuwa chanzo cha vurugu.
Baadhi ya vyombo vya habari vinaeneza uzushi na chuki za kidini kama vile hakuna Serikali. Serikali isikae kimya kama vile hakuna linalojiri, ichukue hatua na kutoa ufafanuzi kwa wananchi, alisema.
Akizungumzia ukosefu wa ajira, Askofu Ruwaichi* alisema Serikali inatakiwa kuangalia suala hili kwa umakini, kwani vijana ni rahisi kujiunga na makundi hayo yenye vurugu kwa sababu za kutokuwa na kazi za kufanya.
Alisema katika mkutano huo wameamua kutenga siku moja kwa ajili sala ya kuliombea taifa na kwamba wataendelea kutumia idara za kanisa hilo kujenga masikilizano* na dini mbalimbali, ili kujenga umoja licha ya tofauti zao za kiimani.
Madaktari na Serikali
Askofu Ruwaichi* alisema, Watanzania wanaangamia nchini mwao kwa kukosa tiba na ulinzi, jambo ambalo ni hatari na kuiomba Serikali kukaa meza moja na madaktari ili kumaliza mgomo huo.
Hata hivyo, aliwaonya madaktari kuangalia njia nyingine za kutumia katika kudai haki zao badala ya mgomo ambao unapoteza maisha ya wananchi wasiokuwa na hatia.
Tungependa matatizo haya ya Serikali na madaktari yafikie mwisho kwa kufanya mazungumzo kwani wanaoumia ni wananchi, alisema.
mwisho
Askofu Malasusa
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa amewataka wananchi kuacha tabia ya kujilimbikizia mali,* huku wakishuhudia jamii ikiangamia* kwa kukosa mahitaji muhimu kama elimu na afya.
Kuna watu wamejaliwa kuwa na kila kitu hata baadhi ya mali zao hawazifahamu pale zinapopotea, lakini kuna kundi la jamii nyingine kati yao ambalo linaishi maisha magumu ambayo linahitaji msaada wa kutosha, alisema.
Askofu Malasusa aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam *wakati wa harambee ya kuchangia mfuko wa kusomesha wanafunzi wasio na uwezo wa Educate The Children wa Shule ya Mtakatifu Josephs Mbezi Beach kuwa hivi sasa watu wamekuwa na tabia ya kujilimbikizia fedha nyingi.
Hivi sasa watu wanajilimbikizia mabilioni ya fedha, huku wakijua kuna kundi la watu ambao linahitaji msaada wao, lakini wamekuwa hawatambui hilo, alisema Askofu Malasusa.
Mwenyezi Mungu ametufundisha kugawana kile unachokipata kwa manufaa ya wengine hususan wasio na uwezo, lakini hivi sasa imekuwa tofauti kwa baadhi ya watu kupenda kumiliki mabilioni ya fedha.
Kauli hiyo ya Askofu Malasusa *inakuja siku chache ambapo Kitengo cha Polisi wa Kimataifa (Interpol) nchini kinachunguza Sh303.7 bilioni ambazo zinadaiwa kukutwa kwenye akaunti sita za Watanzania, wakiwamo Wanasiasa,katika benki mbalimbali nchini Uswisi.