Sekondari ya Wembere yageuka pango la popo na mijusi

jamadari

JF-Expert Member
Feb 13, 2010
295
92
MKOA wa Singida umepata mafanikio makubwa mno kwa upande wa ujenzi wa shule za sekondari za kata. Shule hizi ambazo wakati mwingine zinajulikana kwa jina la shule za wananchi, zimejengwa kwa kasi ya kutisha. Mwaka 2005 idadi ya shule za sekondari hizo zilikuwa 31 na sasa zimeongezeka na kufikia 135 mwishoni mwa mwaka jana. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 335.5. Maendeleo haya sio madogo, ni makubwa sana katika sekta hii muhimu ya elimu ambayo yamepatikana kwa kipindi kifupi, cha miaka minne na miezi saba tu. Sina uhakika, lakini kwa kasi hiyo kubwa ya ujenzi wa shule za sekondari za kata, mkoa wa Singida utakuwa ni miongoni mwa mikoa michache hapa nchini, iliyopata mafanikio hayo ya kihistoria na ya kujivunia. Huwezi kuzungumzia mafanikio hayo makubwa ya kujivunia, bila kutaja jina la mkuu wa mkoa huu wa Singida, Dk Parseko Kone. Mkuu wa mkoa huyu, kwa kushirikiana na wasaidizi wake wamelisimamia kwa ukaribu mno zoezi zima la ujenzi wa sekondari hizo. Lengo la serikali mkoa na wananchi wake kwa ujumla, ni kupambana na maadui ujinga, umasikini na maradhi ili kupata maendeleo ya kweli. Inaaminika kuwa mtu akielimika, ni rahisi kwake kupambana na maadui wawili waliobaki ambao ni umaskini na maradhi. Lakini juhudi hizo kubwa, zinaelekea kupata pigo kubwa baada ya shule ya kutwa ya sekondari Wembere iliyoko kata ya Mugungira tarafa ya Sepuka Wilayani Singida, kuhamwa na wanafunzi wote na kubaki kuwa pango la popo na mijusi ya kila aina. Shule hiyo yenye vyumba vya madarasa 11, mabweni mawili na nyumba za kuishi walimu tatu, ipo umbali wa kilomita 120 kutoka makao makuu ya wilaya ya Singida. Shule hiyo ambayo ni ya kidato cha kwanza hadi cha nne, ilikuwa na walimu watatu tu. Kwa hali hiyo, shule hiyo ya sekondari Wembere itaendelea kufungwa tena mwaka huu, baada ya wanafunzi saba waliopangiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu, kuhamishiwa katika shule zingine wilayani Singida. Uamuzi wa kuwabadilishia shule wanafunzi hao, ulifikiwa na mkutano maalumu kwa ajili ya kutangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba kitaifa mkoani Singida. Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Singida, Illuminata Mwenda, aliuambia mkutano huo kuwa wanafunzi hao saba waliopangiwa shule hiyo hawatadumu kuendelea shuleni hapo kutokana na mazingira yake kuwa magumu. Ametaja baadhi ya matatizo yanayochangia shule hiyo kukimbiwa na wanafunzi kuwa ni pamoja na usafiri kuwa mgumu, shule kutokuwa na walimu wa kutosha na hakuna kabisa mawasiliano ya simu. "Wakati kama huu wa masika, hakuna usafiri wa uhakika wa kuingia na kutoka kata ya Mgungira. Upo mto wa Msosa ambao ukijaa maji, hakuna mtu wa kukatisha na wakati mwingine maji hupungua baada ya siku tatu au zaidi," anasema na kuongeza kuwa; "kuna pori nene kati ya kijiji cha Igombwe na Mgungira lenye wanyamapori wakali." Mkurugenzi huyo, anasema kutokana na hali ilivyo Mgungira, hakuna mzazi/mlezi atakayethubutu kumpeleka mtoto wake kwenye shule hiyo iliyopo kilomita 120 kutoka makao makuu ya wilaya. Kwa upande wake, makamu mkuu wa shule hiyo, Hassan Rashidi, ametaja changamoto zingine zilizochangia shule hiyo kuhamwa na wanafunzi, kuwa ni pamoja na walimu wapya wanaopangiwa kufundisha kwenye shule hiyo, kugoma kufanya kazi hapo. Anasema ameshuhudia walimu wengi wapya wakifikishwa shuleni hapo, wamekuwa wakigoma kushuka kwenye gari na badala yake huomba warudishwe Singida mjini. Wakisharudishwa Singida mjini, basi hawarudi tena Mgungira. Anasema mbaya zaidi ni kuwa mkuu wa shule ya Wembere, hafanyi jitihada zozote za kuiweka shule hiyo katika mazingira ya kuvutia walimu na wnafunzi. "Inashangaza kuona kuwa ni mkuu huyo huyo wa shule ndiye aliyesimamia zoezi la kuwapatia uhamisho na kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa kwa kuwasiliana na wakuu wa shule zingine wilayani humo," anafafanua mwalimu Hassan. Aidha, mwalimu Hassan ameendelea kudai mwalimu mkuu amekuwa akitumia muda mwingi kuwa nje ya kituo chake cha kazi kitendo kilchochangia vikao vya bodi ya shule visifanyike kwa mujibu wa sheria. Hassan anasema mwalimu mkuu wa shule hiyo iliyohamwa amekuwa akidai kuwa mwanafunzi kuhama shule ni haki yake wala kwa kitendo hicho, hatendi kosa lolote la jinai. Hoja hiyo inaungwa mkono na afisa elimu mkoa, Yusufu Kipengere ambaye amewahi kusema kuwa mwanafunzi kuomba kuhama shule asiyoipenda, ni haki yake ya msingi. Kama shule hii iliyogharimu mamilioni ya fedha na nguvu nyingi za wananchi, itaachwa bila kuwa na wanafunzi, maana yake ni kwamba wananchi wa kata ya Mgungira, watavunjika moyo na kukosa ari, nguvu na mwamko wa kuchangia miradi mbalimbali ikiwemo ya sekta muhimu kama hii ya elimu. Wako watu wengi tu ambao wanahoji busara iliyowaongoza viongozi wa ngazi mbali mbali, kuamua kutumia fedha nyingi za umma kujenga shule mahali penye mazingira magumu kupindukia. Wakazi wengi wa kata ya Mgungira, ni wahamiaji kutoka mikoa ya Shinyanga, Tabora na Mwanza ambao ni wafugaji. Hawa maisha yao yanaendeshwa na mifugo. Majani/malisho ya mifugo yanapoonyesha dalili ya kukosekana, wafugaji hao haraka sana huhama na kuhamia sehemu yenye malisho ya kutosha. Kutokana na tabia yao hiyo ya kuhamahama, imechangia wafugaji hao wasiwe na mwamko kabisa wa kuhakikisha watoto wao wanapata elimu au kunakuwa na mazingira mazuri ya kusomea. Shule chache za msingi katika kata hiyo, zina vyumba vichache vya madarasa, utakuta vina wanafunzi wasiozidi watano. Pamoja na uchache huo wa wanafunzi, watoto hao wa wafugaji, huambiwa na wazazi/walezi wao kuwa wahakikishe hawafaulu kabisa mtihani husika. Huagizwa kwamba endapo atafaulu kuendelea na masomo, basi ajiandae kujigharamia masomo. Mfano hai ni huu wa mwaka huu ambapo ni wanafunzi saba tu kata nzima ndio walichaguliwa kuanza kidato cha kwanza. Hicho nacho ni kikwazo ambacho viongozi walitakiwa kukigundua mapema kabala ya kujenga shule hiyo. Wananchi hao ambao wamedai kuwa wao ni wakereketwa wakubwa wa sekta ya elimu, wanasema kuwa endapo viongozi wangetafakari mapema juu ya mazingira ya Mgungira na staili ya maisha ya wakazi wake, hawangefikia uamuzi wa kujenga shule ya sekondari ya Wembere. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mwenda, ofisi yake iliomba wizara ya mafunzo na elimu kuichukua shule hiyo na kuifanya iwe ya bweni, lakini imekataa. Wizara hiyo imeishauri Halmashauri yenyewe ifanye juhudi za makusudi ili iweze kuiendesha shule hiyo. Kutokana na hali hiyo, ni dhahiri kwamba majengo hayo mazuri ya shule hiyo, sasa yatabaki kuwa makazi rasmi ya popo, mijusi, nyoka, buibui na kila aina ya wadudu watambaao na warukao. Hilo halina ubishi kwa sababu majengo hayo sio rahisi yakatumika kuwa kituo cha afya (tayari kuna zahanati) mahakama ya mwanzo, kanisa au msitiki wa wilaya. Sababu kuu ikiwa ni ugumu wa kufika huko Mgungira kutokana na barabara kuwa si nzuri na hakuna mawasiliano ya simu ya aina yo yote. Wakati wa masika ndio ngumu mno kuingia na kutoka kata ya Mgungira. Labda majengo hayo mazuri, sana sana yanaweza kufaa zaidi kama yatatumiwa kuwa gereza la kuhifadhi wahalifu sugu. http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=17979
 
Back
Top Bottom