Seif, Karume waitibua CCM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Seif, Karume waitibua CCM

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Ujengelele, Dec 30, 2009.

 1. U

  Ujengelele JF-Expert Member

  #1
  Dec 30, 2009
  Joined: Jan 14, 2008
  Messages: 1,256
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Seif, Karume waitibua CCM

  Mwandishi Wetu​
  Disemba 30, 2009
  [​IMG]Yadaiwa wamekwenda kinyume cha maagizo ya NEC Butiama

  [​IMG]CUF: Ni uoga wa vigogo CCM

  MARIDHIANO ya Rais Amani Karume na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad yamewachanganya wana Chama Cha Mapinduzi (CCM), na hasa wa Zanzibar, wanaoona kuwa ni mbinu ama ya kuendeleza utawala wa Karume au kumlinda kama ikilazimu Seif ndiye akawa mkuu wa nchi, Raia Mwema imeambiwa.
  Tayari vigogo kadhaa wa CCM Zanzibar wameanza kuamini kuwa maridhiano hayo yanaweza kuhitimishwa kwa Rais Karume, kuwania tena urais wa Zanzibar, baada ya Katiba ya Visiwa hivyo kufanyiwa mabadiliko mahsusi.
  Aidha, vigogo hao ambao wengine wangetamani kumrithi Karume, wanayatazama maridhiano hayo kwa hadhari kubwa, wakiamini kuwa yanakwenda kinyume cha maelekezo ya mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) iliyokutana kijijini Butiama, mwishoni mwa mwaka jana.
  Katika kikao hicho cha NEC iliazimiwa kuwa Serikali ya mseto iundwe baada ya kufanyika kwa kura ya maoni Zanzibar (referendum), ambayo yatakuwa chanzo cha mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar.
  Hata hivyo, baada ya kikao hicho CUF walipinga wakisema hapakuwa na haja ya kura za maoni na kwamba mabadiliko ya Katiba yamekuwa yakifanyika kila inapobidi kwa kuzingatia hali halisi na mahitaji ya nchi kwa wakati husika.
  Kutokana na msuguano huo, CUF walikataa kuendelea na mazungumzo ya muafaka wakitaka utekelezaji lakini CCM, akiwamo Rais Jakaya Kikwete walitoa wito wakitaka warejee kwenye meza ya mazungumzo.
  Lakini upepo umegeuka wiki kadhaa zilizopita, baada ya Rais Karume na Seif kukutana katika kikao kisicho rasmi lakini kilichoonekana kuwa na nguvu kuliko hata vikao vilivyokuwa na nguvu za kisheria.
  Katika kikao hicho kulifikiwa maridhiano ambayo matokeo yake ni pamoja na CUF kutambua urais wa Karume, na yeye kuwateua baadhi ya viongozi wa CUF kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, akiwamo Juma Duni Haji.
  Wakati hayo yote yakitokea mtafaruku umeibuka CCM Zanzibar, Karume na Seif wakitajwa kuwa na ajenda zenye malengo ya kuwanufaisha kama timu mpya ya watu wawili, iliyolenga kubeba siasa za Visiwa hivyo.
  Wao wenyewe wamekuwa wakinukuliwa kusema kwamba kwa hali ya siasa zilivyo tete Zanzibar wanaona kwamba bila hatua kama hii uchaguzi wa mwakani unaweza kuzua machafuko makubwa ambayo yataweza kusababisha hata damu kumwagika.
  Kwa hali hiyo wamedai kwamba wao kama viongozi hawawezi kuruhusu hayo yatokee na hivyo wameingia katika maridhiano kuepuka wao kama watu binafsi kushitakiwa baadaye katika Mahakama ya Kimataifa ya The Hague, Uholanzi kwa kusababisha maafa.
  Kwa nyakati tofauti, vigogo ndani ya CCM wameieleza Raia Mwema kuwa kuna uwezekano wa kutaka kuunda serikali ya mseto Zanzibar, ndoto ambayo haiwezi kutimia hadi Katiba ibadilishwe na mabadiliko hayo yatahitaji muda jambo ambalo litalazimu Rais Karume kubaki madarakani mwakani, hadi uchaguzi ufanyike, hoja ambayo inaelezwa pia kubeba ajenda ya viongozi hao wa vyama pinzani.
  Hoja nyingine inayochomoza ni kwamba mkewe Rais Karume, Shadya ana Upemba kiasi kwa kuwa mama yake ana asili ya Pemba, ikibidi Seif kuibuka kuwa kiongozi mkuu wa Zanzibar, familia ya Karume, ambaye inadaiwa sasa ana mali nyingi zinazomfanya abandikwe jina la Hapa Pangu itazidi kuwa katika neema endapo itafanikisha ushindi wa Maalimu Seif Shariff Hamad, kuwa Rais ajaye wa Zanzibar, ikidaiwa na vigogo hao kuwa hayo ni sehemu ya makubaliano yao ya siri.
  Kama si Maalim Seif, vigogo hao wameieleza Raia Mwema kuwa mabadiliko ya Katiba mahsusi kuruhusu serikali ya mseto, yanaweza kumbakisha kwa muda Karume na baada ya baadhi ya vipengele kumruhusu agombee kwa mujibu wa Katiba hiyo mpya au yenye mabadiliko, na ikiwa hivyo naye pia atalinda maslahi ya Maalim Seif, kwa hoja ya mwingiliano wa asili ya familia (kutoka Pemba).
  Lakini duru huru za habari zimedokeza kuwa msingi wa Rais Karume na Seif kuridhiana katika wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu, ni kuhofia machafuko na vifo na hivyo kuepusha mashitaka ya mauaji, kama ilivyo kwa Omar Bashiri wa Sudan, anayewindwa kufikishwa mahakamani The Hague kwa makosa anayodaiwa kuruhusu ukiukwaji wa haki za binadamu Darfur.
  Kutokana na hofu hiyo ya baadhi ya vigogo wa CCM Zanzibar, Raia Mwema iliwasiliana na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, kujua maazimio ya NEC iliyokutana Butiama kuhusu kura ya maoni yamefutika vipi na jambo gani hasa linaloendelea kwa kuzingatia mwongozo wa CCM kama chama kwenda kwa Rais Karume.
  Lakini Makamba alisema yupo likizo na akapendekeza Raia Mwema imtafute Naibu Katibu Mkuu George Mkuchika ambaye hata hivyo alikataa kuweka bayana hali halisi ya mambo.
  Mazungumzo kati ya Raia Mwema na Naibu Katibu Mkuu, George Mkuchika, yalijenga mazingira kuwa yapo masuala mazito zaidi yanayoweza kutokea baada ya makubaliano ya Rais Karume na Seif.
  “NEC Butiama lengo la msingi tulitaka mazungumzo ya muafaka yaendelee, yamefanyika na wahusika walikuwa wakitoa ripoti kwenye vyama vyao. CCM tumepongeza maridhiano ya Rais Karume na Seif Shariff Hamad,” alisema Mkuchika, lakini alipoulizwa kwa nini CCM imetoa tamko wakati baadhi ya viongozi wake Zanzibar wakitoa kauli za kutoridhishwa tena wakiwa na wasiwasi kuhusu hatima ya chama chao katika uchaguzi ujao, alijibu;
  “Hayo ni maoni yao. Hatukatazi watu kuwa na maoni binafsi. Lakini katika masuala rasmi ya chama yanafanyika kupitia vikao rasmi. Kwa hiyo, kama hayo yapo kuna vikao vya chama kama NEC na vingine. Mimi sikuwapo wakati wanatoa maoni kwa hiyo siwezi kuyajadili hapa, isipokuwa najua kuna uhuru wa maoni.”
  Alipoulizwa kama Rais Karume atalazimika kutoa muhtasari wa makubaliano yake na Seif kwenye kikao kijacho cha NEC, Mkuchika alijibu; “Siwezi kuzungumzia hayo, wala usinifikishe huko. Taratibu zetu zinajulikana huwa tunajibizana kwenye vikao ni utamaduni aliotuachia Mwalimu (Julius) Nyerere si kwenye magazeti.”
  Maalim Seif Shariff Hamad hakupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini Salum Bimani ambaye ni Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma, aliliambia Raia Mwema kwamba, kilichopo CCM Zanzibar sasa ni homa ya wanaotarajiwa kuwania urais kutouzika na kwamba kauli za Rais Karume ya kuwa atahakikisha anasimamia uchaguzi huru na wa haki na kukabidhi madaraka kwa mshindi halali zimewatikisa.
  “Kuhusu suala la maridhiano ya Seif na Rais Karume siwezi kujibu. Lakini hayo maoni ya hao wana-CCM ni homa yao tu. Kuna mambo mawili, kwanza ni kauli ya Rais Karume kusema atasimamia uchaguzi huru na wa haki, pili kusema Rais wa Zanzibar anaweza hata kutoka Pemba kwani ni sehemu ya nchi.
  “Wao wanatarajia kugombea urais na kushinda kwa hila kama ilivyozoeleka. Sasa kuna mambo ya msingi ya wazi kati ya Seif na Rais Karume ambalo ni kuleta mshikamano Zanzibar.
  “Hawa wapambe wanaotaka urais wametishika pia na kauli ya Rais Karume kwamba hakutakuwa na uchaguzi kama kila anayestahili kuandikishwa kupiga kura hayajaandikishwa. CCM wamezoa vya kunyonga, vya kuchinja hawawezi.
  “Wagombea wote wanaotarajiwa hawauziki,” alisema Bimani na alipoulizwa majina ya wagombea hao watarajiwa aliwataja kuwa ni Dk. Gharib Bilali, Shamsi Vuai Nahodha na Ally Juma Shamhuna na akasisitiza: “soko lao dogo Zanzibar kwa kuwa wako mbali na CCM, achilia mbali kuwa mbali na wananchi”.
  Kuhusu Rais Karume na Seif kuwa na malengo ya siri yenye kutanguliza maslahi ya usalama wa familia zao katika siasa za Zanzibar kwa kuwa Seif anatoka Pemba na Mkewe Karume anatoka huko huko, Bimani alisema huo ni uzushi.
  “Ngoja nikwambie ukweli. Mama yake Rais Karume ni Muunguja, baba na mama yake mke wa Rais Karume wote ni wa-Unguja, sio wapemba, kwa hiyo hilo suala halipo. Nasisitiza kilichotangulizwa hapo ni Zanzibar. Hizi kauli zote chanzo chake ni misimamo aliyotoa Rais Karume kuhusu Uchaguzi Mkuu,” alisema Bimani.
  Hata hivyo, Raia Mwema imethibitishiwa kwamba mkewe Karume ana nasaba Pemba na hata Unguja nasaba yake inahusishwa na chama maarufu cha Hizbu kinachotajwa kuwa ndio mzizi mkuu wa chama cha CUF.
  Raia Mwema iliwasiliana na Mwanasheria na Wakili maarufu, Tundu Lissu, ili kutaka maoni yake kuhusu uwezekano wa Rais Karume kubaki madarakani kwa kuongezewa muda wakati mchakato wa mabadiliko ya Katiba ukifanyika na baadaye hata kuweza kugombea tena.
  “Kugombea anaweza kutegemea na aina ya mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar. Katika Katiba ya Zanzibar ya sasa hakuna ruksa ya kikatiba kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Sasa wanaweza kubadilisha vifungu tu vya Katiba kuruhusu hilo.
  “Vifungu hivyo vitakavyobadilishwa vinaweza kuruhusu tu serikali ya mseto, lakini masharti mengine ya Rais aliyepo kuondoka baada ya mihula miwili yakabaki pale pale, au mnaweza kubadili na kuruhusu hata Rais aliyepo madarakani kugombea kwa masharti ya katiba mpya, ambayo kimsingi haitazingatia vipindi vilivyopita,” alifananua Tundu Lissu akitoa mfano wa Namibia.
  Nchini Namibia, aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Sam Nujoma aligombea tena urais baada ya mabadiliko ya Katiba, ingawa pia kabla ya mabadiliko hayo alikuwa amekwishahitimisha ukomo wa mihula ya urais Kikatiba.
  Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, hali ya kisiasa ya Zanzibar imekuwa ikizorota hasa kila baada ya kufanyika uchaguzi kutokana na chama cha CUF kupinga matokeo ya uchaguzi kwa madai ya kutokuwa huru na wa haki.
  Makubaliano ya Seif na Karume yameendelea kuchukuliwa kwa hadhari kubwa hata na wananchi wa kawaida ambao Raia Mwema limeelezwa kwamba wamekuwa wakiyaona kama makubaliano ya “wakubwa” ambayo wao kama wanachama wa kawaida wa CCM na CUF hayatawafaidisha.
  Mwananchi wa Nungwi aliyejitambulisha kwa jina la Salum aliliambia Raia Mwema kwamba anashangaa hata baada ya mazungumzo hayo bado hali ya ubaguzi imekuwa ikiendelea na matatizo yaliyojitokeza katika uandikishaji katika daftari la wapiga kura hayajarekebishwa hadi sasa.
  “Sina hakika kama kuna jipya, hawa wanasiasa wanaendelea kutudanganya kila ukikaribia uchaguzi na baadaye wanaanza kutuvuruga. Wajue kutatokea maafa zaidi baada ya uchaguzi hasa wananchi wakiona hakuna mabadiliko na hapo hakutakuwa na kiongozi atakayesikilizwa awe wa CUF ama wa CCM, na hapo ndipo itakuwa hatari zaidi ya mwaka 2001,” alisema Salum.
   
 2. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #2
  Dec 30, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Mimi sina cha kusema nitaweza kusema kuwa wote wana agenda zao ngoja ufike wakati wa uchaguzi mwakani ndio mkweli anaweza kupatikana au vipi na tena CuF wanapaswa kujua wao ni chama cha upinzani hivyo kuna umuhimu wa kwenda kwenye uchaguzi, na baada ndio wanaweza kuunda mseto lakini demokrasia funganishi kama hii haifai katika bara la Africa
   
 3. MrFroasty

  MrFroasty JF-Expert Member

  #3
  Dec 30, 2009
  Joined: Jun 23, 2009
  Messages: 701
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 35
  Kama kawaida Tanganyika na CCM yake wameingia kitumbo joto baada ya kuona Karume na Seif wanahubiri umoja.

  Hapo Tanganyika hamuoni ndani, hiyo ni chenga ya kisigino!
   
 4. N

  Ngekewa JF-Expert Member

  #4
  Dec 30, 2009
  Joined: Jul 8, 2008
  Messages: 7,730
  Likes Received: 23
  Trophy Points: 135
  Hii habari naiona kama ni mtazamo wa mwandishi zaidi kuliko ukweli wa hali ilivyo. Chakshangaza ni kuwa habari hiyo yote umemnukuu mtu mmoja tu kwa jina na waliobaki imetumika vigogo tu.
  Mwandishi apende asipende Wazanzibari wameshapitia mambo mengi na wanaweza kuyakabili. Wazanzibari hawaoni tabu kusubiri na kuona iwapo maafikiano hayo yatawasaidia au ni mkenge kama anavyodai mwandishi. Wazanzibari wanafanya maamuzi kwa wakati muafaka siku zote. Ieleweke kuwa wazanzibari wanafuatilia kila kitu na wala si mbumbumbu kama wengi wanavyoamini.
   
 5. Jayfour_King

  Jayfour_King JF-Expert Member

  #5
  Dec 30, 2009
  Joined: Nov 15, 2009
  Messages: 1,142
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  Binafsi napongeza sana mapatano yao kwani kutoelewana kwao wanao athirika muda wote huwa ni wananchi wa kawaida, kwangu mimi hakuna mapatano mabaya wapewe nafasi mambo yaende salama.
   
Loading...