mangaukawa
Senior Member
- Dec 5, 2014
- 153
- 63
Nimependa uchambuzi huu wa sakata la Escrow. Soma hapa.
Hapana shaka Sakata la Fedha za Akaunti ya Escrow limekwisha baada ya hotuba ya Rais katika mkutano wake na Wazee wa Dar es Salaam. Kilichobaki sasa ni kupata burudani ya hoja na mantiki kwa mnasaba wa sakata hilo.
Makala hii sio tu inatoa burudani hiyo bali pia inamjengea msomaji maarifa ya kujenga hoja sanjari na uwezo wa kuhoji mambo kwa mfumo wa hoja na mantiki.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, PAC, ilijaribu kujenga hoja kwa kutumia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG, kuwa Fedha nyingi za Nchi zimechotwa au zimeibwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Msingi wa kadhia nzima au Sakata kama lilivyoitwa ulikuwa ni "Wizi" wa fedha. Mtu mwingine akisema lolote lile atakuwa muongo. PAC ilipania kuitikisa nchi kwa madai hayo kuwa fedha zimeibwa.
Na hivi sasa jambo lolote ukitaka linoge au lisikilizwe kwa makini basi lizungumzie pesa. Pesa ndiyo inayotawala akili za watu kwani bila pesa, maisha aghalabu yanakuwa magumu kama si mabovu. Kwa kutumia Fedha za Escrow, PAC walikuwa na uhakika wa asilimia nyingi wa kulishitua Taifa na kulijaza hasira!
Lakini hoja gani walitumia Wanakamati wa PAC kulitikisa Taifa? Hili ni swali linalohitaji sayansi ya hoja na mantiki ili liweze kujibiwa kwa ufasaha. Izingatiwe kuwa Ripoti ya Kamati hiyo ilijibiwa na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Dkt. Sospeter Muhongo kwa kutumia msingi uleule wa Ripoti ya CAG.
Sayansi ya hoja inahitajika kupima uzito wa hoja za pande mbili kwa kutumia ripoti ileile moja ili kubaini ukweli ulikuwa wapi kwani bado kuna kiporo cha maamuzi ya Rais baada ya ule wa kumuachisha kazi Prof. Dkt. Anna Tibaijuka.
Kisha sayansi ya hoja itahamia katika majibu ya Rais. Kwa nafasi yake katika muktadha wa sakata hili, Rais alisimama kama Hakimu ambaye kwanza alisikiliza pande zote, na kisha kufanyia kazi maelezo ya kila upande. Hata hivyo, kabla ya kuhukumu, Rais naye alipata nafasi ya kulizungumzia Sakata hilo.
Halikadhalika na yeye alisimamia ripoti ileile ya CAG. Na hata kabla, alikwishaagiza isambazwe ili kila mtu aisome. Upungufu kwa upande wa Ripoti ya PAC ni kwamba, wananchi hawakutangulia kupewa nakala ya ripoti ya CGA ili pale walipomsikiliza Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto Kabwe, nao wapate kuhakiki kila alichokisoma.
Angalau jitihada zilifanyika kwa Waziri wa Nishati na Madini kusambaza kile alichokisoma. Tuikumbushe PAC kwamba Watanzania, yawezekana wengi si wasomi sana, lakini kwa elimu ya kujua kusoma na kuandika, ni matajiri kabisa!
Wangeliweza kusambaziwa nakala ya ripoti ya CAG kabla ya ripoti ya PAC kusomwa Bungeni. Vinginevyo, ingekuwa au ilikuwa rahisi kuwadanganya kwa kuwasomea kitu wasichokijua. Kwa hiyo, alichofanya Rais kilikuwa na umuhimu mkubwa katika kuwashirikisha wananchi katika maamuzi yake magumu.
Sayansi ya hoja mtiririko (syllogism) ambayo huanza na premisia itaonesha namna gani baadhi wamekubaliana na maamuzi ya Rais na namna gani wengine wameyatilia shaka maamuzi hayo.
Sasa ni vema tukatumia premisia kama mawe au matofali ya kujengea hoja ili kupata mahitimisho ya kimantiki katika maelezo ya kila upande. Pale inapolazimu tutatumia idadi ya premisia tatu, lakini zaidi tutatumia premisia nne.
A. Kamati ya Zitto au PAC imeelezea wizi katika Akaunti ya Escrow
B. Ripoti ya CAG haikutaja kabisa wizi wa Fedha za Escrow
C. Ripoti ya PAC ilitegemea Ripoti ya CAG
D. Ripoti ya PAC imepingana na ripoti ya CAG
Hitimisho la kimantiki linatulazimu kusema kuwa Ripoti ya PAC haikusema ukweli kuhusu wizi kwani aliyepaswa kutoa ripoti ya wizi ni CAG!
PAC imepata wapi uhakika kuwa fedha zimeibwa ilihali CAG hakuonesha wizi huo katika ripoti yake? Taifa linaweza kutanabahi kuwa kama nakala za ripoti ya CAG zingelisambazwa mapema kabla ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kusoma taarifa yake Bungeni, kila mtu angeanza kuujua ukweli yeye mwenyewe kabla ya kuambiwa.
Kwa sababu ya wananchi kutojua chochote kuhusu kitu kinachoitwa Akaunti ya Escrow, ikawa rahisi kwao kukubaliana na ufafanuzi wowote wa PAC kwani tangu hapo ndio mara yao ya kwanza kukisikia kitu hicho.
Ilikuwa ni fursa muhimu kwa PAC kwani ilikuwa na uchaguzi wa kusema ukweli au uongo na bado ungeaminika. Wananchi walikuwa sawa na watoto wa darasa la kwanza ambao huhitaji ukweli wa mwalimu. Mwalimu akiita A kuwa ni B mwanafunzi huyu mgeni ataamini hivyo hivyo!
Kwa bahati nzuri, kanuni za kitaaluma haziruhusu uongo huo. Lakini katika siasa hilo linawezekana. Mtu anaweza kutumia nafasi ya kwanza kuchafua hali ya hewa. Hadi ukweli uje kubainika tayari gharama itakuwa kubwa.
Kuliweka wazi hili ni kwamba, kwa kutosambaza ripoti ya CAG hata kupitia vyombo vya habari, PAC inaweza kutuhumiwa kuwa ilipanga kutumia uongo kama hoja ya kuhalalisha madai ya wizi wa fedha ambayo hayamo katika ripoti ya CAG.
Ni kweli Taifa limezugika. Hadi Rais alipokuja kutoa agizo la kusambaza ripoti ya CAG, tayari athari za uongo zilishasambaa. Matokeo yake, wananchi wakaamini kuwa Taifa limeibiwa mapesa mengi takribani Dola milioni 300. Na hivi sasa wananchi wanadai fedha hizo zirudishwe!
Tuendelee kujenga hoja kwa kutumia ripoti ya CAG dhidi ya madai ya Wizi huo wa fedha za Escrow.
A. Akaunti ya Escrow ilifunguliwa na IPTL na Tanesco
B. Tanesco ilikuwa inalipa deni la IPTL kupitia Akaunti hiyo
C. Tanesco ni Shirika la Umma
D. Umma wa Watanzania uliweka fedha za malipo katika Akaunti ya Escrow
Hitimisho la kimantiki hapo linatwambia wazi kuwa kilichokuwa kinawekwa kwenye Akaunti ya Escrow ni Fedha ambazo Tanesco ilikuwa inalipa kwa IPTL ambayo ni kampuni iliyoliuzia Umeme Shirika hili la Umma.
Mtu au taasisi inapolipa deni kwenye Akaunti maana yake haina chake au haihifadhi akiba yake. Kwa kuwa Tanesco ni Shirika la Umma ambalo linanunua umeme kwa IPTL kwa matumizi ya umma, Umma huu unapodai fedha za Escrow ni zake, una maana gani?
Hata kama Wataalamu ambao binafsi nawaheshimu kwa taaluma watasema kuwa kulikuwa na kodi katika fedha hizo bado, kisheria, hakuna uhalali wa kuiita mali ya Umma. Ni suala la TRA kukabana koo na Mkwepa kodi, lakini si suala la kuyageuza mapato ya mtu au kampuni kuwa mali ya Umma.
Hatuwezi kuigeuza mali ya Bakhresa au Reginald Mengi kuwa mali ya Umma eti kwa sababu hawajalipa kodi. Tukianza kugeuza mali za watu kuwa mali za Umma kwa misingi ya kodi, tutahalalisha ujambazi kwani mali za watu wengi itabidi zifanywe za Umma. Inaingia kweli akilini kuwa kama ITV haijalipa kodi, tuigeuze kuwa TBC yaani mali ya Umma?!
Lakini si Umma uliozusha madai hayo, bali ni Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliyozusha madai hayo na kuwahemsha wananchi! Ni nani mwizi kati ya IPTL na Umma wa Watanzania kwa muktadha huu wa sayansi ya hoja na mantiki? Tuweke tena matofali ya premisia ili kujenga hoja ya kuzaa mantiki ya kumkamata mwizi halisi wa Fedha za Escrow.
A. IPTL imeuuzia Umeme Umma wa Watanzania kupitia Tanesco
B. Umma wa Watanzania umelipa deni la Umeme kwa IPTL kupitia Tanesco
C. Fedha zote za malipo zimewekwa kwenye Akaunti ya Escrow
D. Fedha za Akaunti ya Escrow ni za IPTL
Hitimisho la kimantiki hapo "linaukamata wizi" Umma wa Watanzania ambao unataka kuhesabu fedha za malipo ya Umeme kwa IPTL kuwa ni fedha za Umma!
Ni sawa na mteja aliyelipa bili ya umeme Tanesco baada ya kutumia nishati hiyo halafu aende Tanesco kudai fedha zake ilihali umeme ameshatumia!
Sasa Umma wa Watanzania usikubali kukamatwa wizi bali umrudi yule aliyewaambia kuwa fedha za Escrow ni zao! Huyo si Mwingine bali ni Zitto Zuberi Kabwe, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali.
Lakini ajabu ni kwamba badala ya yeye kuitwa mwizi, yeye ndiye kawaita wenziwe wezi. Hebu tujenge hoja ya kuona kichekesho cha hali ya juu cha mwizi kuwaita wenziwe wezi, na kisha watu kumuamini!
A. IPTL ndiyo Mmiliki wa fedha za Akaunti ya Escrow
B. IPTL haijalia na wizi au uchotaji wa fedha za Akaunti ya Escrow
C. Kamati ya Bunge ndiyo inayolia na Fedha za IPTL
D. Kamati ya Bunge inalilia fedha za wizi?
Ajabu hapa ni kwamba, Mwenye fedha zake katika Akaunti ya Escrow ambaye ni IPTL hajasikika kulia na wizi au uchotaji wa fedha zake. Herbinder Singh Sethi, Mmiliki (Mkurugenzi) wa Kampuni ya IPTL ndiye aliyepaswa kulilia fedha kama kweli zilichotwa au kuibwa.
Lakini hakuna kilio chochote kutoka kwake. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ndiye aliyezuka na kilio cha fedha ambazo Umma wa Watanzania hauzihusu!
Sasa inaposemwa fedha za Umma zimechotwa au kuibwa, ni nani Mwizi hapa? Sayansi ya hoja na mantiki hapa inaikamata wizi Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali. Kwa maana nyingine, Kamati hii imewafundisha wizi wa fedha za watu Watanzania.
Leo hii Watanzania wanadai eti warudishiwe fedha zao za Escrow! Kwamba PAC imewageuza Watanzania mazuzu! Kibaya zaidi ni pale Kamati hii inapofanya kazi ya kukamata watu wizi bila kutumwa na IPTL yenye fedha zake.
Imewaita "wezi" Maprofesa wetu wa kuheshimika duniani, Muhongo na Tibaijuka. Sasa tujenge hoja kuona kama kweli kuna huo wizi unaodaiwa, na nani wa kuwakamata wezi.
A. Prof. Muhongo kasema fedha za Akaunti ya Escrow si za Umma
B. Akaunti ya Tegeta Escrow ilipokea malipo ya Tanesco kwa IPTL
C. Prof. Muhongo ndiye aliyesema kweli kuhusu fedha za Escrow
Kama fedha zingeibwa kabla ya kuingia kwenye Akaunti ya Escrow, basi, kwa namna moja au nyingine, tungeweza kuutilia shaka uadilifu wa wale waliopewa dhamana ya kulipa deni la IPTL.
Kama IPTL ingelalamika kuwa fedha za malipo hazijaingizwa kwenye Akaunti ya Essrow, hapo CAG angetukamatia wezi wetu, na hapo PAC ingekuwa na haki ya kuwakamata watu kwa wizi wa fedha za Umma.
Nje ya Akaunti ya escrow, ni kweli fedha zilikuwa za Umma lakini baada ya kuingia kwenye Akaunti hiyo fedha si za umma tena, ni za IPTL. Laiti zingepotelea njiani kabla ya kuingizwa kwenye Akaunti ya Escrow, tungekuwa na haki ya kusema fedha za Umma zimeibwa!
Lakini kwa pamoja, CAG na PAC zimekubali kuwa fedha zimeingia kwenye Akaunti ya Escrow. Hii maana yake ni Kwamba Wizara ya Nishati na Madini kupitia Tanesco, imesimamia kwa uadilifu malipo ya deni la IPTL.
Baada ya fedha kuingia kwenye Akaunti, mwenye dhamana nazo ni Mwenyewe IPTL, sio Wizara ya Nishati na Madini wala Tanesco. Sasa ukisema Waziri kaiba au kachota fedha za Escrow, wa kukamata mwizi ni IPTL, sio Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali. Lakini IPTL haijamtuhumu Muhongo wala Tibaijuka kwamba kachota au kuiba fedha zake.
Hivyo, hitimisho letu katika hoja za hapo juu ni sahihi kwamba Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini ndiye aliyesema ukweli kuhusu Fedha za Akaunti ya Escrow kwamba si za Umma.
Na kwamba hakuna wizi wala uchotaji wowote kama ilivyodaiwa na PAC! Wachotaji au wezi wa fedha za Escrow, kama kweli wangekuwepo, basi wa kuwakamata na kuwashitaki angelikuwa ni IPTL.
Kwa kuwa IPTL haijalalamika wala kumwita mtu yoyote mwizi, na badala yake imefungua shitaka dhidi ya Bunge lililothubutu kuwaita watu wezi kwa niaba yake, hakuna "Mwizi" wala "Mchotaji" wa Fedha za Akaunti ya Escrow! Kwa vile hakukuwa na mwizi, hoja ya msingi ya Ripoti ya Kamati ya Zitto pamoja na mapendekezo na maazimio ya Bunge haikuwa na mashiko.
yaliyopoteza muda wa Kamati kuchunguza, na baadae muda wa Bunge kujadili, ni madai ya wizi wa Fedha za Akaunti ya Escrow. Laiti hoja isingelikuwa hii, Taifa lisingelikuwa na sababu ya kushituka au kutikisika! Kazi nzima iliyofanywa na Kamati ilikuwa ni ya "kukamata wezi", na wengine wakaita "Majizi".
Lakini kumbe wezi au majizi hawakuwepo! Labda tujenge hoja ili ieleweke vizuri. Tuzingatie kuwa popote ambapo pana nguvu za hoja, pana ushindi. Hata, Mahakamani ukijenga hoja vizuri lazima ushinde kesi.
Tunaweza kuifikisha Mahakamani na kuishinda Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa kutushirikisha kukamata wezi wasiokuwepo! Kosa la kulidanganya Taifa ni baya kwani linaweza kuzaa fujo za kuhatarisha amani ya nchi. Tungeliweza kuumizana na hata kuuana kwa vurugu za kudai fedha ambazo, kumbe, si zetu!
Kama Nchi inafuata kikwelikweli Utawala wa sheria, basi hoja hizi zinaweza kuisaidia kuwawajibisha Viongozi na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kinidhamu na kisheria.
Kinidhamu, Kamati hii ivunjwe, na kisheria wahusika wanaweza kufikishwa Mahakamani kujibu shitaka la kuhatarisha usalama wa Taifa. Tuendelee na hoja.
A. Msingi wa Ripoti ya PAC ni "Wizi" wa Fedha za Escrow
B. Fedha za Escrow ni za IPTL
C. IPTL haijalalamika kuibiwa fedha zake za Akaunti ya Escrow
D. Ripoti ya PAC haikuwa na msingi!
Hitimisho hapo linaipunguzia kama si kuiondoshea thamani kazi ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali. Kwani wahusika waliliambia Taifa kuwa Kamati hiyo ilikuwa inashughulikia wizi au uchotaji wa fedha za Escrow wakati kumbe hakukuwa na cha umma kilichoibwa au kuchotwa. Sasa ile hamkani yote ilikuwa ya nini?
Kwa sababu ya kukosekana kwa msingi wa ripoti, mapendekezo yote ya PAC na maazimio ya Bunge yalipoteza thamani. PAC ilimsakama Prof. Muhongo, ikamsakama Prof. Tibaijuka, ikamkaba Katibu Mkuu Maswi, na ilithubutu hata kumkaba Waziri Mkuu na kutaka ajiuzulu kwa sababu ya ule ulioitwa "wizi" au "uchotaji" wa fedha za Umma katika Akaunti ya Escrow!
Lakini kumbe, kama tulivyoona, hakukuwa na fedha ya Umma kwenye Akaunti ya Escrow, bali kulikuwa na fedha za IPTL. Kulikuwa na thamani gani tena ya mapendeklezo na maazimio ya Bunge? Hili tuliweke katika mfumo wa sayansi ya hoja ili lieleweke vizuri.
A. Ili kumpata Mwizi lazima kiwepo cha kuiba
B. Mawaziri wameitwa wezi wa Fedha za Umma katika Akaunti ya Escrow
C. Akaunti ya Escrow haikuwa na fedha za Umma, bali za IPTL
D. Hakukuwa na mwizi wa fedha za Umma.
Hitimisho la hoja hapo juu sio tu linaikosesha msingi ripoti ya Kamati ya Zitto, bali inaacha swali gumu la nani aliiba nini ambalo linaweza kabisa kuzaa jinai mahakamani ya kuwataka wale waliochafua wenzao wajibu kesi kwa nini walitunga uwongo kinyume na taarifa za CAG?
Sasa Sayansi ya hoja inahamia kwa Rais ambaye kwa muktadha huu tunamwita Hakimu wa kesi ya fedha za Escrow. Bunge lilimtaka Rais aharakishe kufanya maamuzi lakini naye akajipa muda.
Kusema kweli hoja ya msingi kwa Rais ambayo ilikuwa mwanzo na mwisho wa kila kitu ilikuwa ni, je, Fedha za Escrow ni za Umma au za IPTL? Jawabu la swali hili ndilo lingezaa hukumu ya Rais.
Na hukumu hii ama ingetofautiana au ingelingana na Azimio la Bunge la kuwaondosha Madarakani Mawaziri waliotuhumiwa kwa "wizi". Tulihitaji jibu moja kati ya mawili; fedha za Escrow ni za Umma au za IPTL.
Kama fedha zingelikuwa za Umma, basi kusingelikuwa na namna kwa Rais isipokuwa kulikubali Azimio hilo la Bunge. Na hapa ndipo pia mapendekezo na maazimio yaliyosalia yangekuwa na nguvu na maana kwani msingi wa tatizo lililozaa maazimio hayo ni wizi wa fedha za Umma.
Lakini kama jibu lingelikuwa hapana fedha si Umma, bali ni za IPTL, basi Rais angehitaji kuhukumu kesi kinyume na Azimio la Bunge. Na baada ya hapo yale mapendekezo na maazimio yaliyosalia yangekosa au yangepoteza thamani. Sasa hebu tujenge hoja kuona hukumu ingekuwaje.
A. Rais alisema Fedha za Escrow ni za IPTL
B. Mapendekezo ya PAC yalijengwa kwa msingi wa tuhuma za wizi wa fedha za Umma
C. Maazimio ya Bunge yalijengwa kwa msingi wa mapendekezo ya PAC
D. Azimio la kuwavua Madaraka Mawaziri halikuwa na msingi
Hitimisho hapo linawaondosha hatiani wale wote waliotuhumiwa kwa wizi au uchotaji wa Fedha za Umma za Akaunti ya Escrow kwani Rais ambaye ni hakimu wa Kesi amethibitisha kuwa fedha hizo si za Umma bali ni za Kampuni ya IPTL.
Taifa zima lingeelewa mantiki ya hukumu hiyo kwani lenyewe lilidanganywa kuwa fedha zilizoibwa ni za Umma. Bila shaka, Mawaziri wenyewe walitarajia hukumu hii.
Na ndio sababu aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka alijitokeza mbele ya wanahabari kuondosha uwezekano wa yeye kujiuzulu. Hatua yake ilikuwa ni ya kimantiki kwa sababu hakukuwa na kosa kimsingi.
Tangu hapo saikolojia ya Taifa zima haikuandaliwa kupokea hukumu ya mgao wa Rugamarila, bali iliandaliwa kupokea hukumu ya wizi au uchotaji wa Fedha za Umma kwenye Akaunti ya Escrow. Kwa kuwa saikolojia ilikuwa hii, Watu pia walitaka kuwa, baada ya hukumu kutolewa, fedha zirudishwe! Tuliweke hili katika mtiririko wa hoja ili lieleweke vizuri.
A. Watanzania walisubiri hukumu ya wizi wa Fedha za Umma
B. Rais amesema fedha za Escrow si za Umma
C. Hukumu waliyoisubiri Watanzania haikuwa sahihi
Msomi yoyote wa sayansi ya hoja na mantiki alitatanishwa na hukumu ya kuwavua madaraka na kuwaweka viporo Mawaziri kwani msingi wa hukumu hiyo haukuwepo tena baada ya kubainika kuwa Fedha za Escrow si za Umma. Na kweli hivyo ndivyo alivyofanya Rais. Alitoa sababu nyingine kabisa ya kutengua uteuzi wa Waziri Tibaijuka.
Ndio maana baadhi ya watu waliamini kuwa Mawaziri wamepona baada ya Rais kusema fedha za Escrow ni za IPTL. Hili ndilo lilikuwa hitimisho la kimantiki. Kinyume chake kutoa hukumu iliyosubiriwa na wananchi kungelikuwa na tafsiri mbili; mosi, kweli Akaunti ya Escrow ilikuwa na fedha za Umma, na pili, kweli Mawaziri ‘wameiba au kuchota fedha hizo.
Kwa kuwa saikolojia ilishaathiriwa na dhana kuwa fedha zimeibwa ndiyo maana baada ya hukumu kwa Prof. Tibaijuka, baadhi ya watoa maoni walibaki na mawazo yaleyale ya wizi na hivyo kutaka isiishie kumuondoa Waziri tu bali na fedha zirudi.
Hawa walishaathirika kisaikolojia na kwa hali hiyo hawakuweza hata kuelewa kuwa Tibaijuka hakuhukumiwa kwa wizi bali maadili. Ukichanganya na utambuzi mdogo wa suala lenyewe, ikawa rahisi kwa watu kuamini kuwa kile kilichosemwa na akina Zitto kilikuwa sahihi.
Hii nayo tuiweke katika mtindo wa hoja ili ieleweke wazi. Kama Rais angewahukumu Mawaziri kama walivyotaka watu fulani, kungekuwa na mgongano mbaya sana wa hoja. Hebu tuone ingekuwaje.
A. Tibaijuka katuhumiwa kwa uchotaji wa Fedha za Umma katika Akaunti ya Escrow
B. Rais kamuhukumu Tibaijuka
C. Fedha za Akaunti ya Escrow ni za Umma!
Huu ni mgongano au mgogoro wa hoja katika sayansi ya hoja. Na matokeo ya mgogoro huu ni wananchi kudai warejeshewe fedha zao.
A. Wananchi waliamini fedha za Umma zimechotwa na Tibaijuka
B. Tibaijuka kahukumiwa
C. Wananchi wana haki ya kudai fedha zao zirudi.
Kwa kuwa hukumu isingezingatia ukweli kuwa baadhi ya waliodanganywa na kudanganyika walikuwa wakisubiri Tibaijuka ahukumiwe, na ndio maana walishangilia alipohukumiwa, wananchi hawa wasingetazama sababu nyingine iliyomtoa madarakani Tibaijuka ila ileile waliyopewa na Kamati ya Bunge,
Tangu hapo, wao hawakuwa na jingine walilolijua zaidi ya fedha za Escrow kuwa ni za Umma, lazima hawa wangeendelea kudai fedha zirudi huku wakichochewa na Wapinzani wa kisiasa wa serikali ya CCM.
Lakini kama wangeulizwa mara kadhaa kuwa wananchi mmesikia kuwa fedha si za Umma bali za IPTL, na wao wangeitikia ndio, wao wenyewe wasingeona tena sababu ya kushikilia lile wazo kuwa Tibaijuka ahukumiwe. Hebu tuiweke hoja hii katika mtiririko wa hoja ili mantiki yake ieleweke.
A.Umma ulidanganywa kuwa Tibaijuka kachota fedha za Umma
B. Rais kasahihisha kuwa Fedha za Escrow si za Umma
C.Umma ungehukumu wenyewe kuwa Tibaijuka hakuchota fedha za Umma
Hitimisho lina maana kuwa baada ya kufahamishwa kuwa Fedha za Escrow si za Umma, basi Umma ungeafiki hatua ya kumwacha na hata kumsafisha Tibaijuka.
Lakini yaliyotokea yametokea, wapo walioyatarajia na wapo ambao hawakuyatarajia lakini undani wa waliozusha ya kuzusha haukuwa na dhamira ya kweli katika kile walichokizusha. Ndio maana haishangazi leo kuona hawaridhiki na hatua iliyochukuliwa na Rais. Ni mbinu tu za kujijenga kisiasa kuelekea 2015.
Tukihamishia sayansi ya hoja katika mgao wa fedha za Rugemarila, kwanza tunashukuru kuwa Rais amesema fedha ya Rugemarila ni halali na ililipiwa kodi. Kuhusu mgao aliofanya hiyo ilikuwa ni juu yake. Ila tatizo ni Tibaijuka kupewa fedha hizo kupitia akaunti yake.
A. Fedha ya Rugemarila ni halali
B. Tibaijuka ni mmoja wa waliopewa fedha za kusaidia maendeleo ya elimu Jimboni
C. Tibaijuka kapokea fedha halali
Hitimisho hapo juu linamuondosha Tibaijuka katika zile tuhuma kuwa alipokea fedha za kutakatisha kutoka Benki ya Mkombozi. Fedha aliyopewa, naye kuipokea kwa ajili ya maendeleo ya elimu Jimboni kwake, ilikuwa ya halali.
Kama ripoti ya PAC ingesomwa tena vizuri, wala isingeonekana kuwa ilitaka Tibaijuka aondoke madarakani kwa sababu za kukiuka maadili ya utumishi wa Umma. Ripoti ilisema fedha za Rugemarila zilikuwa ni chafu, kwamba Bwana huyu ni tapeli, na kwamba benki ya mkombozi ni benki ya kitapeli.
Hivi ndivyo ripoti ilivyotaka watu waelewe. Hivyo serikali ingeiachia tu Takukuru itazame uhusiano au urafiki wa Tibaijuka na Rugemarila. Hapo sasa ingebainika kama ni rafiki, ndugu, jamaa, wa nyumbani, mshirika wa maendeleo ya elimu wa Tibaijuka Muleba, na kadhalika.
Kazi ya pili ya Takukuru ya kuchunguza uhalali wa fedha za Rugemarila ingelikuwa nyepesi tu kwani tayari ilishaelezwa na Rais kuwa fedha ni halali na zilipiwa kodi. Kwa kuwa ni jambo la kibinafsi nje ya mipaka ya utumishi wa Umma, yumkini lisingelikuwa tatizo.
Maoni tuma 0712578455