Saratani ya matiti (breast cancer)

Dr. Wansegamila

JF-Expert Member
Feb 3, 2012
2,954
8,093
Saratani ya matiti ni aina ya kansa inayojitokeza toka tishu za matiti hasa mirija myembamba inayopitisha maziwa. Ugonjwa huu (Saratani ya matiti) hutokea kwa binadamu na mamalia wengine. Idadi ya wanaume wanaopatwa na kansa ya matiti ni ndogo sana ikilinganishwa na ya wanawake(1 kati ya wagonjwa 100).

Ulimwenguni pote, saratani ya matiti hubeba asilimia 30 ya saratani zote kwa wanawake.

Licha ya maendeleo ya kitiba, bado kansa ya matiti ndiyo saratani inayosababisha vifo vingi zaidi vya wanawake.

Nchi zilizoendelea za Amerika Kaskazini na Ulaya Magharibi ndizo zenye idadi kubwa zaidi ya watu walio na saratani, lakini idadi ya wanawake walio na saratani ya matiti inaongezeka katika bara la Asia na Afrika ambako kwa kawaida kumekuwa na idadi ndogo.

Idadi ya wanaokufa kati ya wale wanaogundulika kuwa na ugonjwa huo huko Asia na Afrika ni ya juu kwasababu saratani hiyo haigunduliwi mapema. Wagonjwa wengi huja ikiwa tayari imeenea sana.

Saratani ya matiti huanza wakati ambapo chembe moja inajigawanya haraka sana isivyo kawaida na bila utaratibu, na hatua kwa hatua inafanyiza uvimbe.

Uvimbe unakuwa ksaratani wakati chembe zake zinapovamia tishu nyingine. Uvimbe fulani unaweza kuchukua miaka kumi hivi kabla ya kugunduliwa.

VIHATARISHI/VISABABISHI

Hatari ya kupatwa na saratani hiyo huongezeka dadiri umri unavyosonga. Asilimia 80 hivi ya wanawake wenye saratani ya matiti wana umri unaozidi miaka 50.

Lakini jambo linalofariji ni kwamba saratani ya matiti ni mojawapo ya kansa zinazoweza kutibiwa kwa urahisi.

Watakaotibiwa kabla ya saratani hiyo kuenea wanaweza kuishi muda mrefu kwa ukawaida.

Visababishi vya saratani ya matiti bado ni fumbo.

Baadhi ya wanasayansi wanaamini kwamba saratani ya matiti hutokana na hatua nyingi tata ambazo huanza wakati ambapo chembe fulani ya urithi yenye kasoro inapofanya chembe zitende kwa njia isiyo ya kawaida, yaani, zigawanyike kwa kasi sana, zishambulie tishu nyingine na kuepuka kuharibiwa na mfumo wa kinga, kisha pole pole chembe hizo zinashambulia na kuharibu viungo muhimu vya mwili.

Jambo lingine linalohusishwa na saratani ya matiti ni homoni ya estrojeni ambayo huenda inachochea aina fulani za kansa hiyo.

Kwa hiyo, mwanamke anaweza kupatwa na saratani hiyo ikiwa alianza kupata hedhi mapema maishani au ikiwa aliacha kupata hedhi akiwa amechelewa isivyo kawaida, ikiwa alipata mimba ya kwanza umri wake ukiwa umesonga au ikiwa hakuwahi kupata mimba, au ikiwa alipata matibabu ya kurudisha homoni fulani mwilini.

Kwa kuwa chembe za mafuta hutokeza estrojeni, huenda wanawake walionenepa kupita kiasi waliofika umri wa kuacha kupata hedhi na hivyo ovari zao hazitokezi tena homoni, wakawa katika hatari ya kupatwa na saratani hiyo.

Pia watu walio na viwango vya juu vya insulin na watu walio na viwango vya chini vya homoni ya usingizi inayoitwa melatoniakama vile watu wanaofanya kazi usiku, wako pia katika hatari ya kupatwa na saratani hiyo.

Uvutaji wa tumbaku umeonekana kuongeza hatari zaidi ya kupata saratani ya matiti, kiwango kikubwa cha tumbaku iliyovutwa na kuanza kuvuta tumbaku katika umri mdogo hufanya hatari kuongezeka zaidi.

Mionzi na kemikali za viwandani huongeza hatari ya kansa ya matiti. Kemikali kama polychlorinated biphenyls, polycyclic aromatic hydrocarbons na dawa za kuulia wadudu huchangia kutokea saratani hiyo.

DALILI

– Uvimbe wowote au kuongezeka kwa unene wa ngozi kwenye makwapa au titi.

– Umajimaji wowote unaotoka kwenye chuchu ambao si maziwa.

– Mabadiriko yoyote ya rangi au ngozi ya titi.

– Chuchu iliyodidimia kwa njia isiyo ya kawaida au inayowasha.



JINSI YA KUJIFANYIA UCHUNGUZI KUFAHAMU KAMA UNA UVIMBE KWENYE TITI (BREAST SELF EXAMINATION)

Inashauriwa kuwa, muda bora wa kufanya breast self examination ni siku 3 hadi 5 baada ya kuanza hedhi. Namna ya kujichunguza matiti au breast self exam ni kama ifuatavyo. Kwanza kabisa ni vizuri zaidi uchunguzi huo ukifanywa wakati mtu akiwa amelala kwenye kitanda au akiwa mbele ya kioo kinachoweza kuonesha vizuri kiwiliwili hasa upande wa juu. Kama umesimama nyoosha mkono wako na kuukunja hadi kiganja cha mkono wa upande unaotaka kupima kiwe nyuma ya kisogo. Kwa kutumia kiganja cha mkono mwingine papasa na kubonyeza sehemu zote za titi kwa mduara, tokea pembeni huku ukibonyeza taratibu kuelekea kwenye chuchu hadi karibu na ndani ya kwapa. Baada ya hapo papasa na kubonyesha ziwa upande wa chini. Angalia iwapo utahisi tezi au uvimbe wowote, ngozi kuwa ngumu au mabadiliko ya aina yoyote. Kama umelala nyoosha mkono na kuulaza ili nao ulale kwenye kitanda pia. Baada ya hapo papasa na kubonyeza taratibu ziwa upande wa juu halafu papasa au bonyeza ziwa kwa pembeni karibu na ndani ya kwapa. Baada ya hapo papasa na kubonyesa ziwa upande wa chini na chuchu pia.

1433305290177.jpeg


MATIBABU

Uvimbe ukiwa na saratani hufanyiwa upasuaji ili kuondoa uvimbe huo na tishu zinazozunguka titi. Upasuaji husaidia kuonyesha uvimbe ulipofikia (ukubwa, aina na kuenea kwake) na kuchunguza uvimbe unakua upesi kadiri gani.

Chembe zenye saratani zinaweza kutoka kwenye uvimbe na kusafiri kupitia mfumo wa damu au mfumo wa limfu na kuanza kukua tena mahali pengine mwilini.

Kuenea kwa saratani hadi kwenye viungo na tishu muhimu kama vile ubongo, ini, uboho wa mfupa au mapafu ndio hufanya ugonjwa huo uwe hatari.

Hivyo baada ya upasuaji, wagonjwa wengi hupata matibabu mengine ambayo yatazuia saratani isirudi na kuenea (mionzi na dawa za saratani).
 
Asante kwa elimu nzuri. Kuna uvumi kuwa kunyonywa sana chuchu kunapunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti,je hii ni kweli?
Sina uhakika sana na hilo ila nliwahi kukutana na article moja ikiwa inaeleza hvyo ila katika vitabu hawajaeleza sana nahisi ni utafiti mpya ulioleta hayo majibu
 
Sina uhakika sana na hilo ila nliwahi kukutana na article moja ikiwa inaeleza hvyo ila katika vitabu hawajaeleza sana nahisi ni utafiti mpya ulioleta hayo majibu
Ni utafiti ndio mana wakina mama wameambiwa wanyonyoshe sana kwa faida kuu hizi
1. Kumpa afya mtoto
2. Kujikinga na saratani ya matiti

With a clean ♥
 
Mkuu Ahsante sana kwa ushauri mzuri...

Ila Nina Dada Yangu ana sumbuliwa na ziwa, Hiyo picha No.6 hivyo viganja vya mikono mahali vilipo chini ya chuchu pametokea uvimbe/kinyama some time kinauma.
Akaenda Hospital Amana wakampima na kusema hakuna kitu ila wakakikata hiko kinyama.

Sasa Mkuu hapo sijui ndio huo ugonjwa...?
 
Back
Top Bottom