Salamu za mwaka mpya 2014

Noor

Senior Member
Feb 5, 2012
146
225
Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na kutuwezesha kufika siku ya leo ya kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014. Wapo wenzetu wengi tulioanza nao mwaka lakini hawakujaaliwa kuwa nasi siku hii ya leo kwa kuwa wametutangulia mbele ya haki. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape mapumziko mema. Kwa wenzetu wanaougua tuwaombee awape nafuu ya haraka ili waendelee kutoa mchango wao katika maendeleo yao, jamii zao na taifa zima kwa jumla. Aidha, tuendelee kuomba rehema za Mola wetu atujaalie afya njema na umri mrefu ili tuweze kuushuhudia mwaka wote wa 2014 na miaka mingine mingi ijayo.

Kama wote mlivyosikia, siku ya mwisho ya mwaka 2013, Taifa letu lilipata muelekeo mpya wa maisha ya watanzania hapo jana baada ya kupata Rasimu Mpya ya Katiba na mchakato wa Kupata Katiba mpya ndio kwanza umepamba moto na katika mwaka unaoanza kesho ni imani yangu kuwa wahusika watatumia busara zao kutengeneza Katiba inayoangalia maisha halisi ya Mtanzania na si kundi la watu au chama Fulani au watu Fulani.

Ni jambo la faraja na kuonea fahari kwamba tunaumaliza mwaka 2013 taifa letu likiwa salama na kwamba amani na utulivu viliendelea kutawala. Aidha, taifa letu limeendelea kuwa moja na watu wake wameendelea kuwa wamoja, licha ya kuwepo kwa changamoto za hapa na pale zilizotokana na harakati za vyama vya siasa na kauli za baadhi ya wanasiasa na viongozi wa kijamii wakiwemo wale wa dini. Wakati mwingine, matendo na kauli zao zimekuwa na mwelekeo wa kuwagawa Watanzania katika makundi yenye mifarakano na uhasama.

Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru kwa dhati Watanzania wenzangu kwa ukomavu wa kisiasa, moyo wao wa uzalendo na busara waliyotumia ya kukataa kuwa wahanga wa njama hizo ovu. Badala yake mmechagua kufuata na kufanya mambo yenye maslahi kwa umoja, maendeleo na usalama wa taifa letu. Hakika ni moyo huo na ufahamu huo ndiyo umeliweka taifa letu kuwa moja na lenye amani na utulivu tulionao tangu uhuru wa Tanganyika, mapinduzi ya Zanzibar na baadae Muungano mpaka leo. Nawaomba ndugu zangu tushikilie msimamo huo hasa katika mwaka ujao wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo haya yaliyofanywa mwaka huu yanaweza kufanywa maradufu.

Kuhusu Elimu

Ndugu Watanzania; huku kwenye Elimu sipendi kuongelea maana wote mnajua kilichotokea baada ya daraja la tano kurudishwa kwa maana ya kuweka wigo mpana wa sifuri kuongezeka. Ni matumaini yangu kuwa mwaka 2014 Wizara kwa kushirikiana na wadau wa elimu wataliona hili na kulipa kipaumbele kwa ajili ya kuokoa Taifa hili maana hakuna Taifa lililopiga hatua bila Elimu.

Kuhusu Umeme

Kwa upande wa umeme, mwaka huu mikoa, wilaya, miji na vijiji vinavyopata umeme wa gridi vilikabiliwa na tatizo la mgao wa umeme. Tatizo hili lilitokana na ukarabati wa mitambo ya Songas. Tatizo hilo limesisitiza haja ya kuongeza uzalishaji wa umeme na kuwa na akiba ya kutosha. Kwa sasa hatuna uwezo huo ndiyo maana hitilafu ndogo ikitokea inakuwa ni tatizo kubwa. Naishauri Serikali ya CCM kuongeza uzalishaji wa umeme mwaka ujao na mingine ijayo na pia Serikali iangalie njia mbadala ya kutunusuru na giza. Nashauri waachane na njia ya mwaka moja ya kutegemea shirika moja, kuanzia kuzalisha umeme, kusafirisha umeme na kusambaza umeme. Zianzishe Taasisi zingine na kugawa madaraka ili kuona ufanisi. Nawafananisha Tanesco na Filamu ambayo kuanzia, Story, Script, Kupiga picha, Muongozaji na hadi kushiriki anakua ni mtu mmoja (Samahani ndugu watanzania wenzangu ila uchungu wangu nimeona nitumie mfano huo ili Serikali ya CCM iamke iachane na mawazo ya mwaka moja.

Kuhusu Ushirikiano wa Kimataifa

Katika mwaka huu unaoishia leo, nchi yetu imefanikiwa kuimarisha uhusiano na mataifa mengine duniani na mashirika ya kimataifa. Tanzania imeendelea kuheshimiwa katika medani za kimataifa. Kwa ajili hiyo, tumeshirikishwa katika masuala mengi makubwa ya kimataifa. Tumetembelewa na viongozi mashuhuri wengi waikiwa Wakuu wa Nchi kadhaa akiwamo Rais wa Marekani, Rais wa China na wengine wengi). Viongozi wakuu wa nchi yetu nao wamealikwa na kutembelea nchi nyingine duniani hasa mkuu wan chi Bwana Rais Mzee wangu Daktari Kikwete. Mahusiano hayo yanaweza kua na manufaa ya kusaidia maendeleo na ustawi wa nchi yetu kama viongozi wetu watasimamia rasilimali za Taifa kwa uadilifu.

Pengine katika heshima kubwa na muhimu tuliyoipata mwaka huu ni ile ya Mzee Wangu Daktari Kikwete kuhutubia Bunge na kutoa ya moyoni juu ya ushiriki wa Taifa letu ndani ya Jumuia ya Afrika Mashariki. Kwa mara ya Kwanza siku hiyo ndio niligundua nina kiongozi anayethubutu. Ni heshima kubwa kwa Tanzania, hivyo nawaomba Watanzania wenzangu pale unapoona Daktari Kikwete mpe salamu zangu kua namuamini kupitia hotuba yake kwa Bunge japo naona bado anakabiliwa na changamoto za hapa na pale hasa anapochelewesha kunitangazia baraza jipya la mawaziri na kuniondolewa mawaziri mizigo wanaoligharimu Taifa.

Hitimisho

Watanzania Wenzangu; Napenda kumalizia salamu zangu za mwaka mpya kwa kumshukuru tena Mwenyezi Mungu kwa rehema zake alizotujalia mwaka huu 2013. Tumuombe atuzidishie maradufu yale yaliyo mema na kutunyooshea yasiyokuwa na maslahi mema kwetu katika mwaka ujao 2014.

Kesho, tunapouanza mwaka mpya, tuhakikishe kuwa tunashirikiana bila kujali dini, kabila, wala rangi ili tujenge Tanzania iliyo njema na pale kiongozi wako anapoonekana kutotenda inavyopaswa ni wajibu wetu kumuwajibisha kwa nguvu zetu zote. Naamini kwa umoja wetu, juhudi na maarifa tutafanikiwa.

Nawatakieni nyote heri na fanaka tele katika mwaka mpya 2014.

Mungu Ibariki Afrika,
Mungu Ibariki Tanzania!!

Noor
www.abdulnoorblog.wordpress.com
 

KABERWA2013

JF-Expert Member
Feb 5, 2013
304
195
Poa mkuu tumekusoma na umetusaidia sana kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa niaba yetu.Amani kwako 2014
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom