GE2025 Salaam za Shukrani 🙏 Kutoka kwa Habibu Mchange

GE2025 Salaam za Shukrani 🙏 Kutoka kwa Habibu Mchange

Matukio, Taarifa, Habari na Mijadala ya Wananchi WAKATI wa Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025

KIJICHO PEVU

Member
Joined
May 4, 2024
Posts
69
Reaction score
49
Salaam za Shukrani 🙏

Kwa unyenyekevu mkubwa, mimi Habibu Mchange ninakishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kunipitisha kuwa miongoni mwa majina sita yaliyopendekezwa—ambapo mmoja wetu, ikimpendeza Mungu, atakuwa mwakilishi wa wananchi wa Kigamboni kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Moyo wangu umejawa na furaha kubwa, furaha inayotokana na shauku ya kuona chama kikubwa kama CCM kikiniamini mimi—mtu ambaye miaka michache iliyopita sikuwa na mbele wala nyuma.

Uteuzi huu unanikumbusha kuwa ndani ya chama chetu kuna nafasi kwa kila mwenye nia njema, juhudi, na uaminifu. Ninajiona kuwa mmoja wa watu waliobarikiwa sana, kwa kuwa Kamati Kuu ya CCM, chini ya uongozi wa Rais na Mwenyekiti wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeamua kuyaacha majina makubwa na kuniweka miongoni mwa walioteuliwa kuomba ridhaa ya chama.

Kwa hili, nasema sina deni na CCM, sina deni na Kamati Kuu, wala sina deni na Rais na Mwenyekiti wangu mpendwa, Dkt. Samia. Deni langu ni kwa wananchi, kwa walio na matumaini mapya kupitia mgombea kama mimi.

Natoa shukrani za dhati kwa wote mnaoendelea kunitumia salamu za pongezi. Pongezi zenu zinanipa nguvu, moyo na matumaini makubwa sana.

Kwa wana CCM wa Kigamboni, nawaomba tuendelee kushirikiana kwa mshikamano kama ambavyo tumekuwa tukifanya. Sisi wanachama wa Chama cha Mapinduzi, katika ngazi mbalimbali, tumekabidhiwa jukumu la kuiongoza nchi kwa kutengeneza kesho iliyo bora kwa ajili yetu na kwa vizazi vyetu.

Nikiwa mkazi wa kudumu wa Kigamboni, nimeona na kushuhudia changamoto kadhaa ambazo tunaweza kuzitatua kwa ushirikiano wetu na chama chetu kwa maslahi mapana ya wananchi wa wilaya yetu.

Kadiri tunavyokaribia chaguzi za ndani ya chama, nawaomba tuimarishe mshikamano wetu, tuendelee kuwa wamoja, ili uchaguzi upite kwa amani na utulivu, ukituacha salama sisi na chama chetu.

Narudia tena kuwashukuru kwa dhati kwa salamu zenu za pongezi, huku nikiamini kwamba CCM imara ndicho chama pekee chenye uwezo wa kuwaongoza na kuwavusha Watanzania wa ngazi zote.

Mungu ibariki Tanzania.
Mungu ibariki Kigamboni.
Ndimi,
Habibu Mchange
Mgombea wa kura za maoni, Ubunge – Kigamboni
 

Attachments

  • IMG-20250729-WA0592(1).jpg
    IMG-20250729-WA0592(1).jpg
    80.6 KB · Views: 15
Back
Top Bottom