Safari yangu ya kwanza kwenda kuzimu ( 1 )

Chilojnr

JF-Expert Member
Jul 5, 2012
308
1,352
Mwandishi: Nyemo Chilongani
0718069269

Nilisimama juu ya mlima mmoja mkubwa, mawingu yalikuwa yametanda huku radi zikianza kupiga hali iliyoonyesha kwamba muda wowote ule mvua kubwa ingenyesha. Nilikuwa nikiogopa sana, pembeni ya mlima ule mkubwa ambao sikujua nilifikaje, kulikuwa na miti mingi iliyosababisha giza kuwa kubwa kitu kilichoniongezea hofu kubwa moyoni mwangu.

Sikuwa na msaada wowote mahali hapo, nilijaribu kuangalia huku na kule nikiamini kwamba ningeweza kupata msaada lakini hakukuwa na mtu yeyote. Wakati nikijiuliza nilifikaje mahali pale, ghafla nikaanza kusikia vishindo vikubwa vikija kule nilipokuwa. Sikujua vilikuwa vishindo vya nani, nikabaki nikitetemeka kwani nilijua kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa maisha yangu.

Mwili wangu ulikuwa ukinitetemeka sana, nilitamani kukimbia kutoka mlimani hapo, kitu cha ajabu, sikuweza kukimbia, miguu ilikuwa mizito kuinuka, hivyo nikabaki nikiwa nimesimama tu.

Ghafla, nikawaona watu zaidi ya ishirini wakija mbele yangu, walikuwa ni binadamu wa kawaida ila walikuwa na muonekano wenye kutisha sana. Walikuwa watupu, viunoni walivaa vitu kama ukili, nyuso zao hazikuwa zikionekana vizuri.

Walikuwa wakinisogelea huku wakicheza wimbo ambao sikujua ulitoka wapi. Walikuwa wakiniangalia huku wakichekacheka kama watu wasiokuwa na akili fulani. Walitisha, nilitamani kuyafumba macho ili nisiweze kuwatazama lakini nilipotaka kufanya hivyo, nilishindwa pia.

Nikabaki nikiwa nimesimama, dakika ziliendelea kwenda mbele, cha ajabu, idadi hiyo ya watu haikuishia ishirini tu bali iliendelea kuongezeka mpaka wakafika watu zaidi ya sitini.

Baada ya dakika kama thelathini hivi, nikawaona watu kadhaa wakija pale niliposimama huku wakiwa wameshika beseni kubwa, nilipochungulia ndani, niliona damu nzito za watu, zilikuwa mbichi kabisa na kila aliyekuwa akizingalia, alionekana kuzitamani.

“Umeshawahi kunywa damu wewe?” aliniuliza mwanamke mmoja, alikuwa na umri usiopungua miaka sabini, alikuwa hajiwezi lakini ndiye aliyeonekana kucheza kwa nguvu mahali hapo.
“Sijawahi kunywa damu, na siwezi kunywa,” nilisema kwa sauti tena kwa kujiamini sana.

“Hahaha....hahaha...hahaha...” niliwasikia watu wale wakicheka tena kwa nguvu kiasi kwamba nikahisi kwamba ngoma za masikio yangu zilitaka kupasuka.

“Utakunywa tu, tena hadi nyama utakula,” alisema mwanamke yule na hapohapo kuanza kuwaita watu wengine ambao walikuwa na sinia kubwa, lilikuwa limejaza nyama za watu na pia walikuwa na jagi kubwa, hilo lilikuwa na damu nyingi.

“Mlisheni naye ashibe manake ana njaa kali,” alisema mwanamke yule, hapohapo watu watatu wakanishika na kuanza kunilisha nyama zile na damu ile.

*****

Nilishtuka kutoka usingizini, jasho lilinitiririka mno, mapigo ya moyo yalikuwa yakidunda kupita kawaida huku mwili wangu ukisisimka sana. Niliangalia saa yangu ya ukutani, ilionyesha kwamba tayari ilikuwa saa tisa usiku, nilipochungulia nje, giza totoro lilikuwa limetawala.

Nikakaa kitandani, picha kamili ya ndoto ile ikaanza kunijia kichwani mwangu, nilikumbuka kila kitu kilichokuwa kikinitokea kuanzia wale watu walivyonifuata na kuanza kunilisha nyama zile.

Huku nikiwa sifahamu kilichokuwa kimetokea, mara macho yangu yakaanza kuwa mazito, sikuweza kufahamu nini kilitokea, lakini ghafla nikajikuta nikiwa pembeni ya bahari moja kubwa, sijui kama ilikuwa ni Hindi, Pacific au bahari gani.

Huku nikiwa ninajiuliza maswali hayo yote, kwa mbele nikaanza kumuona mwanamke mmoja aliyesimama juu ya maji, alivalia gauni kubwa jeupe, alikuwa na nywele ndefu mpaka mgongoni, miguu yake haikuwa kama yetu, ilikuwa ni kwato za ng’ombe, alininyooshea kidole na kuanza kuniita.

Kiukweli niliogopa, sikutaka kumfuata lakini ghafla nikajikuta nikianza kupiga hatua kumfuata huku nikiwa na hofu kubwa moyoni. Sikuzama kwenye maji yale, na mimi nilikuwa natembea juujuu mpaka nilipomfikia.

Alikuwa msichana mrembo mno, kwa kumwangalia harakaharaka ungeweza kusema kwamba alistahili kuwa mrembo wa dunia, alikuwa akitabasamu tu.

“Hujambo Michael,” alinisalimia.

“Sijambo, wewe nani?” nilimuuliza huku nikitetemeka, sikutaka hata aniguse.

“Ninatwa Yusnath.”

“Ndiye nani?”
“Mimi ni msichana mrembo kuliko wote duniani na kuzimu, nimekuleta kwa ajili ya kukuonyesha mambo fulani hivi,” aliniambia huku tukiwa tumesimama juu ya bahari.

“Mambo gani?” niliuliza kwa kuhamaki.

“Mambo yanayofanywa na watu kisiri. Upo tayari tuondoke?”
“Hapana, unataka twende wapi?”
“Kuzimu.”
“Kuna nini?”
“Kuna siri kubwa sana zimejificha, nataka nikuonyeshee watu wanaofanya mambo mabaya huku nyie mkiwaamini. Upo tayari?” aliniuliza.

Sikuwa tayari lakini kilichonishangaza, eti nikakubaliana naye bila tatizo lolote. Mara ghafla, kwa mbali likaanza kuja wimbi moja kubwa likija kule tulipokuwa, naweza kusema kwamba ukubwa wake ulikuwa ni sawa na jengo lililokuwa na ghorofa sita, niliogopa sana, nikataka kukimbia kuelekea ufukweni, mwanamke yule akanidaka mkono, akaning’ang’ania nisimkimbie, nikaanza kupiga kelele huku wimbi lile likiendelea kutufuata pale tulipokuwa.

Wala hazikuchukua dakika nyingi, wimbi lile likatupiga, tukaanza kuzama, nikaanza kupiga kelele za kuomba msaada mahali pale, ghafla nikajikuta nimetokea sehemu nyingine kabisa, ulikuwa mji mwingine ambao kwa kuuangalia harakaharaka, ulikuwa na majengo mengi yaliyonifanya kujiuliza, ilikuwaje kuhusu ile bahari? Mbona hatukuwa baharini tena?
“Karibu kuzimu tuanze kazi,” aliniambia mwanamke yule, nikapigwa na butwaa baada ya kusikia kwamba pale nilipokuwa palikuwa ni kuzimu.

*****

Nilipigwa na mshangao mkubwa, sikuamini kama pale nilipokuwa kulikuwa kuzimu. Hakukuwa na watu, eneo zima lilikuwa kimya kabisa hali iliyonifanya kuogopa sana. Mwanamke yule Yusnath akaniambia nimfuate, nikafanye hivyo.

Ardhi yao haikuwa kama hii yetu kwamba kuna mchanga, yao ilikuwa ni kama changarawe kwamba kama ukitembea pekupeku ni lazima uumie nyayo zako. Tulitembea huku nikiangalia huku na kule kana kwamba nilikuwa nikimtafuta mtu fulani.

Hakukuwa na mazingira mazuri hata kidogo na kila hatua niliyokuwa nikipiga, nilitamani kurudi duniani, yaani kwa jinsi mazingira ya kule yalivyokuwa, sikuwa na hamu ya kuendelea kukaa.

Tulitembea kwa mwendo wa taratibu na kuingia sehemu moja hivi. Ilikuwa ni sehemu yenye viumbe vingi mno. Kwa mbali walionekana kuwa kama binadamu lakini ukweli ni kwamba hawakuwa binadamu.
Maumbo yao yalitisha mno, hawakuwa na vichwa kama hivi vyetu, vichwa vyao vilikuwa ni vya wanyama. Kuna wengine walikuwa na vichwa vya paka, macho makubwa mithiri ya machungwa, vichwani walikuwa na mapembe lakini cha kushangaza, miguu yao ilikuwa kwato za ng’ombe.

Ukiachana na hao, kulikuwa na viumbe vingine vilivyokuwa na vichwa vya ng’ombe, walitembea huku miguu yao ikiwa mikubwa mno na mgongoni walikuwa na mabawa yaliyoonekana kuchoka.

Kila nilipokuwa nikiwaangalia, waliniogopesha mpaka kipindi kingine kuyapeleka macho yangu pembeni kabisa. Kila tulipokuwa tunapita, kulikuwa na majagi makubwa yaliyokuwa na damu ndani yake.

Duniani watu waliendelea kufa kwa ajali na kule kuzimu damu ziliendelea kukusanywa kama kawaida. Tulitembea mpaka kwenye jumba moja kubwa, lilionekana kuwa zuri lakini kwa nje kulisimikwa mafuvu ya watu na sehemu nyingine kuwa na miguu ya binadamu.

“Unaiona hii?” aliniuliza huku akiiangalia ile miguu ya watu.

“Naiona.”
“Hii ilikuwa miguu ya maiti, ngoja nikuonyeshee kitu,” aliniambia na kisha ghafla kukatokea kitu kama televisheni na kuanza kutazama kile alichotaka nikitazame.

Nililiona kundi kubwa la watu, ilikuwa ni usiku sana, walisimama sehemu moja ambayo kwa haraka sana niligundua kwamba ni makaburini. Kulikuwa na makaburi ya kila aina, sehemu nyingine majeneza yalikuwa nje huku sanda zikitundikwa juu ya makaburi, tena sanda nyingine zikiwa na damu mbichi kabisa.

Niligundua kwamba kulikuwa na maiti ambazo zilichukuliwa pindi tu zilipozikwa na ndiyo maana damu zile mbichi ziliendelea kuwepo. Hapo, katikati ya watu kulikuwa na mtoto mmoja, alionekana kuwa na sura ya kipole lakini Yusnath akaniambia kwamba huyo ndiye alikuwa malkia huko duniani, yaani wachawi wote wa Tanzania walikuwa wakimuabudu yeye.

Kazi kubwa iliyokuwa ikifanyika mahali hapo ni kufukua makaburi tu. Maiti zilikuwa zikihitajika kwa nguvu zote kwa ajili ya nyama ambayo huliwa kila inapofika siku ya alhamisi ambayo kwao kule kuzimu huwa ni siku ya sherehe.

Ufukuaji wa makaburi yale haukuwa wa kawaida, yaani kulikuwa na mwanamke anasimama juu ya kaburi huku akiwa mtupu, anacheza kwa kukatika viuno huku wakati mwingine akikaa juu ya kaburi na kuanza kuyasugua makalio yake hapo kaburini na ghafla kaburi linaanza kujifukua lenyewe.

Kuna maiti nyingine zilikuwa zikija juu huku zikiwa na sanda tu na nyingine zikiwa na suti. Zilikuwa maiti hizihizi ambazo zilikuwa zikizikwa hivi karibuni au kama hakukuwa na maiti mbichi, zoezi la kwenda mochwari huanza mara moja.

Zile maiti zinapotolewa na kuonekana zimeanza kukauka, zoezi la kwenda mochwari huanza mara moja. Siku hiyo, hakukuwa na maiti iliyokauka, nyingi zilionekana mbichi kabisa na hivyo kuzichukua na kuziweka juu ya kaburi.

Mambo yote yaliyokuwa yakitokea nilikuwa nayaangalia kwa macho yangu. Nilikuwa nikiogopa na kusisimka mwili lakini sikuwa na jinsi, kwa wakati huo nilitakiwa kuangalia kila kitu kilichokuwa kikitokea usiku huo.

“Unamuona yule mtoto?”

“Ndiyo! Amefanya nini?”
“Yule ndiye kiongozi wenu duniani, yeye ndiye anayepanga ratiba ya kuyashughulikia makanisa na misikiti, yeye ndiye mpangaji wa kila kitu,” aliniambia Yusnath.

“Anaishi wapi?”
“Duniani.”
“Sehemu gani?”

“Hahaha! Hahaha! Hahaha!” alicheka Yusnath, ghafla, na mimi nikajikuta nikiwa nimesimama katikati ya makaburi, nilikuwa nimezungukwa na watu wengi waliokuwa watupu kabisa, sijui kama waliniona au la, lakini niliwasikia wakianza kucheka kwa pamoja. Nilipogeuka na kuangalia pembeni yangu, kulikuwa na maiti moja ya mwanamke mjauzito, ghafla, ikafumbua macho na kuanza kuniangalia.

“Nisaidieeee....nisaidieeee....” ilisema maiti ya mwanamke yule, nilitamani kuzimia.

Nilibaki nikitetemeka tu, sikuamini kile nilichokuwa nikikiona, maiti kuongea, tena ikiniomba msaada makaburini, hakika niliogopa mno.

Maiti ile haikunyamaza, bado iliendelea kuniomba msaada mahali pale huku wachawi wengine wakibaki wakicheka tu. Sikujua ni msaada wa aina gani aliokuwa akiuomba kwani mimi nilikuwa mgeni mahali pale, hivyo sikujua ni kwa namna gani ningeweza kumsaidia.

Wala hazikupita sekunde nyingi, nikaanza kujisikia kuwa kwenye hali ya tofauti kabisa, baridi kali likaanza kunipiga makaburini pale. Sikuelewa ni kitu gani kilikuwa kikiendelea kwani hakukuwa na siku ambayo nilihisi baridi kali kama siku hiyo usiku.
Nilikwishawahi kukaa Mbeya, Iringa na hata Arusha lakini sikuwahi kusikia baridi kama nililokuwa nikilisikia Makaburini hapo kulijaa mauzauza mengi yaliyonifanya niogope mno na kujiona kama nilikuwa sehemu moja iliyonifanya nihisi kwamba muda wowote ule kuanzia sasa ningekufa.

Huku nikihisi baridi kali kiasi cha kujishika vilivyo kwa staili ya kuipitisha mikono kifuani mwangu, ghafla nikaanza kusikia sauti za watoto wakilia kwa sauti za juu kabisa. Sikujua watoto hao walikuwa wapi zaidi ya kusikia sauti hizo pale kaburini.

Nilianza kuangalia huku na kule ili kuona ni wapi watoto hao walipokuwa, baada ya sekunde kama ishirini nikawaona wanawake kama kumi wakisogea pale kaburini huku wakiwa wamewabeba watoto waliokuwa kwenye sanda, wanawake hao walikuwa kama walivyozaliwa.

“Hao ni watoto kutoka mahospitalini, wazazi wao waliwazaa lakini wameonekana kwamba wamekufa. Kiukweli, hawajafa bali tunawachukua hasa tunapokuwa na uhitaji wa kula nyama,” aliniambia mwanamke yule kwa sauti ya juu.

Hapa nikagundua kitu kwamba kwa kipindi chote nilichokuwa hapo makaburini, hakukuwa na mtu aliyekuwa akiniona zaidi ya ile maiti tu na ndiyo maana alipokuwa akisema kwamba anahitaji msaada, wale wachawi wengine walikuwa wakicheka tu kwa kuona kama alikuwa akiongea peke yake.

Niliwaonea huruma watoto wale waliokuwa wakilia tu, mbali na hao, nikawaonea huruma wanawake waliokuwa wakiwazaa watoto hao na kuona kwamba wamekufa na wakati ukweli wa mambo ni kwamba hawakufa zaidi ya kuchukuliwa na kupelekwa kwa ajili ya kuliwa nyama tu.

“Lete sinia,” alisema mwanamke mmoja, alionekana kuwa kiongozi chini ya yule mtoto mdogo. Sinia likaletwa.

Ndani ya sinia lile kulikuwa na kisu kikali kilichokuwa kimefungwa kitambaa chekundu. Hakikuwa kisafi, japokuwa ilikuwa ni usiku na mahali pale kulikuwa na giza lakini niliona damu zilizoganda zikiwa katika kisu kile hali iliyoonyesha kwamba kilitumika sana katika kukata nyama za watoto makaburini hapo.

Kwa macho yangu nikashuhudia watoto wale wakianza kuchinjwa na mwanamke yule. Hakuonekana kuwa na huruma hata mara moja, alianza kumchinja mtoto wa kwanza huku kila damu ilipokuwa ikitoka, alikinga mdomo wake na kuanza kunywa.

Niliumia zaidi, kitendo kilichokuwa kikiendelea makaburini hapo kilinitisha zaidi kiasi kwamba kuna kipindi sikutaka kabisa kuangalia zaidi ya kutaka kuyafumba macho yangu. Nilipojaribu kufanya hivyo, sikuweza, macho yangu yaliendelea kuangalia kile kilichokuwa kikiendelea.

“Imetosha, naomba unitoe hapa,” nilimwambia Yusnath.

“Bado, kuna mengi ningependa uyafahamu hapa makaburini na kuzimu, kuwa mvumilivu,” alisema mwanamke yule.

Ndugu yangu, makaburini kunatisha, usione kwamba unapita nyakati za mchana basi ukajua kwamba hata usiku huwa hivyohivyo tu. Huwa ninawashangaa hata wezi wanaokwenda makaburini nyakati za usiku na kufukua makaburi kwa ajili ya kuchukua vitu alivyozikwa navyo maiti.

Kwa kile nilichokuwa nikikiona usiku ule, kilikuwa ni cha kutisha mno. Baada ya kuhakikisha kwamba watoto wpote wamechinjwa, mwanamke yule akaanza kuwakatakata vipande.

Wachawi wengine wakaanza kuzigombania nyama zile kama tunavyogombania vitu fulani kwenye minada hasa masokoni. Kila aliyefanikiwa kuzipata nyama zile, alizitafuna harakaharaka kama mtu aliyeambiwa kwamba asiungefanya hivyo basi angepokonywa.

Ilikuwa kama sherehe kwao, wakaanza kuzila zile nyama huku wengine wakijilamba kuonyesha kwamba zilikuwa tamu mno. Niliendelea kusimama mahali pale mpaka walipomaliza na ndipo mwanamke yule aliyekuwa akicheza kama alivyozaliwa akalifuata kaburi moja na kuanza kucheza huku akiyasugua makalio yake katika kaburi lile.

Kama lilivyokuwa kaburi la kwanza, na lile likaanza kujifukua na baada ya dakika kadhaa, moshi mzito ukaanza kufuka na maiti moja kutoka huku ikiwa na sanda. Alipoifunua, ilikuwa maita ya mwanaume mmoja, alionekana kuwa mzee kama wa miaka sitini.

Wachawi wale wakaanza kucheka sana, walicheka huku vicheko vyao vikiwa kero masikioni mwangu kwani sikufurahia kabisa kile walichokuwa wakikifanya makaburini pale.

Walipoona kwamba maiti imetoka ndani ya lile kaburi, walichokifanya ni kuiweka pembeni na kisha mwanamke yule aliyekuwa na kisu kusogea na kuanza kumkata tumbo mpaka alipohakikisha utumbo unatoka, akauchukua na kuanza kuutafuna huku wenzake wakimwangalia kwa matamanio makubwa.

Katika hili ngoja nikwambie kitu kimoja jinsi ukweli wa mambo ulivyop. Si maiti zote zinazozikwa huwa na viungo vilivyokamilika, kwa mfano maiti hii ya huyu mzee, haikuwa na sehemu za siri, nahisi zilikuwa zimekatwa tangu ilipokuwa mochwari ambapo biashara ya viungo vya maiti hufanyika mara kwa mara.

Nilijiuliza kama wachawi wale walikuwa wakihitaji kuitafuna maiti yote au la kwani hawakuonekana kutosheka, yule mwanamke mchovumchovu alipokuwa akikata kipande na kula, kilichofuata alikikata na kuwapa wenzake ambao walivipokea kwa shangwe na kuanza kula.

“Nataka niondoke,” nilisema huku nikiwa sitaki kuendelea kuwa mahali hapo.

“Subiri kwanza,” aliniambiaYusnath.

“Nisubiri nini sasa? Sitaki kuangalia zaidi,” nilimwambia huku nikionekana kukasirika.

“Hutaki kumuona mkuu wa makaburini?”
“Mkuu wa makaburini?”
“Ndiyo! Kila sehemu huwa kuna mkuu wake, subiri, muda si mrefu atafika mahali hapa, usiogope,” aliniambia Yusnath.

Nikaanza kusubiria, nikashangaa nikiingiwa na hamu ya kumuona huyo mkuu wa makaburini.

Tukutane Siku ya Jumamosi.
 
Mwaka wa tano huu tunaingoja part two au kuna mitano tena!
 
Back
Top Bottom