Sababu 10 wazee Mbeya kumuunga mkono JPM

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
“KAULIMBIU ya Hapa Kazi Tu inatukumbusha kaulimbiu za huko nyuma kama vile Uhuru na Kazi, Uhuru ni Kazi na Heshima ya Mtu Kazi,” Ni kauli ya Mwenyekiti wa Wazee Wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mbeya, Isakwisa Mwambulukutu wakati wazee hao walipotoa tamko la kupongeza utendaji kazi wa Rais John Magufuli.

Wazee wengine wanachama wa umoja huo wanaounga mkono juhudi za Magufuli ni Edward Ndonde, Daniel Fussi, Kikeke A Kikeke, Rogate Masuba, John Mushi, Bujo Mwakatumbula, George Nyirenda, Boniface Kasyunguti, Philimon Mwansasu na mmoja wa waasisi wa TANU mkoani Mbeya, Helena Mwaipasi.

“Sisi wazee tunaounda umoja wa Wazee wa CCM tunaoishi jijini Mbeya kwa niaba ya wazee wenzetu tunapenda kutoa tamko rasmi la kumpongeza Rais John Magufuli kwa utekelezaji wake mzuri wa Ilani yetu ya CCM ya uchaguzi ya mwaka 2015 pamoja na utendaji wake mzuri wa kazi katika Awamu hii ya Tano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tunapotoa tamko la kumpongeza Dk Magufuli isieleweke kuwa tunaziona awamu nyingine zilizotangulia hazikufanya mazuri, la hasha. Kama alivyosema aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi kuwa kila zama na Kitabu chake. Viongozi wa awamu zilizotangulia kila mmoja alifanya mambo kwa kadiri ya karama aliyojaliwa na Mwenyezi Mungu kulingana na hali halisi ya wakati wake huo. Hata Dk Magufuli ni moja ya matunda ya awamu hizo zilizotangulia,” anasema Mzee Mwambulukutu.

Mwenyekiti huyo wa wazee wastaafu anasema ni ukweli usiopingika kuwa maendeleo ya mtu au taifa kwa ujumla hayawezi kupatikana kama watu hawataki kufanya kazi. “Hivyo ni jambo la kumpongeza rais kwa kuhimiza hilo na anapaswa alisimamie kwa nguvu zote ili nchi iweze kujikwamua kutokana na lindi la umasikini,” anasema. Wazee hawa wanasema sababu ya pili ya kumpongeza Rais Magufuli ni kuimarisha nidhamu na uwajibikaji wa watumishi wa umma.

Wanasema watumishi wengi wa umma walifikia mahali ambapo walifanya kazi kwa kadiri ya matakwa yao bila kujali taratibu na kanuni za kazi, ikiwa ni pamoja na kumheshimu mwananchi.

“Walisahau ile kaulimbiu aliyotoa Rais Ally Hassan Mwinyi isemayo, ‘Usipowajibika, utakumbana na fagio la chuma’. Sisi wazee tunaamini Magufuli ni fagio la chuma, kwani matokeo tumeanza kuyaona kwenye sehemu ambazo huduma hutolewa kama vile hospitali, ofisi za serikali na sehemu nyinginezo,” anasema Mzee Mwambulukutu kwa niaba ya wenzake. Sababu ya tatu ya kumpongeza Rais, wazee hao wanasema ni jinsi anavyopambana na ufisadi kwa maana ya rushwa, ukwepaji kodi na ubadhirifu wa mali za umma.

Anasema hatua ya kutumbua majipu, Dk Magufuli anawakumbusha enzi za Hayati Edward Moringe Sokoine alipopambana na wahujumu uchumi. “Sisi wazee tunamwombea Rais Magufuli kwa Mungu amlinde, ili atumbue majipu yote, vipele, chunusi na kukwangua kabisa ukurutu ili Tanzania yetu ibaki safi na yenye afya njema kiuchumi na yenye jamii iliyostawi vyema,” anasema.

Kuboresha huduma za jamii ili kuleta hali nafuu ya maisha ya Watanzania ni sababu ya nne wanayoitaja wazee hawa hadi kuwasukuma kutoa pongezi zao. Hii wanasema ni pamoja na kuboresha huduma hospitalini, kutoa elimu bure toka chekechea hadi kidato cha nne na kuhakikisha mikopo inapatikana kirahisi kwa vijana wa elimu ya juu.

“Kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara, reli, umeme, maji na mingine mingi hapa anatukumbusha usemi wa It can be done play your part (inawezakana kama kila mmoja atatekeleza wajibu wake). Hivyo tunatoa wito kwa Watanzania wenzetu kutimiza wajibu wao pale walipo ili huduma za kijamii ziweze kuwa bora na kutufanya wote tuwe na maisha nafuu,” anasema.

Kufufua na kuhimiza ujenzi wa viwanda ili kuongeza ajira,kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na kilimo, uvuvi na Ufugaji na kuinua uchumi wa Taifa pia limewakosha wazee hawa kama sababu yao na tano. Wanasema wameanza kuona matunda kwani mkoni Mbeya tayari kiwanda cha Zana Za Kilimo (ZZK) kimeanza kufanya kazi na baadhi ya vijana wamepata ajira.

“Hapa tukizingatia ile kaulimbiu ya ‘Kupanga ni Kuchagua’ hakuna kitakachoshindikana. Hivyo tunaomba juhudi ziendelee ili kufufua viwanda vingine kama vile HISoap, kiwanda cha nguo na kiwanda cha kusindika nyama,” anasema. Jambo jingine la sita lililowakuna wazee hao ni kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kuanza na kupunguza kodi inayokatwa kwenye mishahara yao kutoka asilimia 11 hadi asilimia tisa.

Wanasema wanaamini kutokana na kutumbua majipu, kudhibiti wafanyakazi hewa na madeni hewa hali ya kiuchumi itakuwa bora na hivyo kuwezesha kuongezeka kwa mishahara ya wafanyakazi na huduma bora kwa umma zitapatikana.

“Jambo jingine la saba ni kuhimiza ujenzi wa Taifa linalojitegemea. Ile kauli ya rais Magufuli ya Bora kushindia muhogo, kuliko mkate wa siagi wa masimango unatukumbusha kauli ya Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere ya ‘Heri kuwa masikini huru, kuliko kuwa tajiri mtumwa. “Sisi wazee tunamwomba rais wetu akaze uzi wala asijali vitisho vya wafadhili wanafiki na maneno ya wanasiasa uchwara. Tunaamini pia kwa kubana matumizi ya serikali kwa kupunguza safari za nje ya nchi, posho za vikao visivyo na tija kwa taifa letu na kupunguza sherehe zinazomaliza fedha nyingi nchi yetu itaweza kujikwamua kiuchumi na hatimaye kuweza kujitegemea,” anasema.

Wazee hawa wanasema unyenyekevu aliouonesha Dk Magufuli wakati wa kuzindua Daraja la Kigamboni ni wa kipekee na ni jambo la nane linalowavutia. Pamoja na kwamba usimamizi wa ujenzi wa daraja hilo ulikuwa chini yake tangu alipokuwa Waziri wa Ujenzi, alikataa daraja hilo kuitwa jina lake na badala yake aliamua liitwe Daraja la Nyerere ili kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuimarisha umoja wa kitaifa na kupigania Uhuru wa Bara la Afrika.

Mzee Mwambulukutu anasema kudhibiti uagizwaji holela wa sukari toka nje ya nchi ili kuhakikisha Watanzania wanapata sukari iliyo salama na kwa bei nafuu na pia kulinda viwanda vya sukari vya hapa nchini ni jambo linastahili pongezi. Pamoja na purukushani za hapa na pale zinazofanywa na wafanyabiashara wasio na uzalendo wanaamini juhudi za Rais zitashinda kwa kuwa palipo na mwanga, giza hujitenga. Hilo anasema ni sababu yao ya tisa ya kumuunga mkono.

“Jambo la mwisho (sababu ya 10) ni kudhibiti hali ya ulinzi na usalama visiwani Zanzibar na hivyo kufanikisha uchaguzi wa marudio bila fujo. Akiwa Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliweza kuhakikisha ulinzi na usalama katika visiwa vya Zanzibar unakuwepo na hivyo kuwezesha uchaguzi wa marudio kufanyika hapo Machi 20 mwaka huu bila vurugu zozote.” “Sisi wazee tunampongeza kwa hilo na tunapongeza ushindi wa kishindo wa CCM katika uchaguzi huo, uliofanyika kwa amani na utulivu,” alisema Mzee Mwambulukutu.

Wazee wengine akiwemo Kikeke A Kikeke, wanasema juhudi na ushirikiano wa pamoja baina ya Watanzania wote pasipokujali nafasi waliyonayo ndiyo utakaowezesha mikakati mbalimbali ya Dk Magufuli kufanikiwa. Anasema iwapo kutakuwa na makundi ya watu wanaojitenga na kukwamisha juhudi hizo itakuwa vigumu kwake kuwezesha Watanzania kupiga hatua kimaendeleo.

Kwa upande wa Katibu wa umoja huo, Philimon Mwansasu, anasema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa maisha bora hayawezi kupatikana kama taifa litabakia mikononi mwa matajiri wachache wenye kupenda kulimbikiza mali kwa ajili yao na familia zao na kuwaacha masikini wakiwa watumwa ndani ya taifa lao.

“Tunachopaswa kufanya Watanzania wote ni kushiriki na kuunga mkono mipango ya Rais, kuhakikisha tunafichua maovu yote yanayofanywa na watendaji wabovu. Kuchukuliwa kwao hatua ndiyo mwanzo wa walalahoi kupata unafuu wa ugumu wa maisha. Tukisema tushirikiane na wahalifu kwa madai kuwa tunawaonea huruma tutakuwa tunazidi kujikwamisha wenyewe,” anasema Mwansasu.
 
Back
Top Bottom