Saa 48 kukata ngebe za CCM na Chadema | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Saa 48 kukata ngebe za CCM na Chadema

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MziziMkavu, Mar 29, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Mar 29, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,616
  Likes Received: 4,617
  Trophy Points: 280
  Nassari nataka nikalie kama paka
  [​IMG] Medeye amvaa Slaa kuhusu ardhi
  Kupigana vijembe na kurushiana tuhuma kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki ni matukio yaliyotawala kampeni hizo zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya kufanyika uchaguzi huo na kuamua nani mshindi kati ya wagombea wa vyama hivyo.

  Ingawa vyama vinane vimesimamisha wagombea, hadi sasa Chadema na CCM ndiwo wanaonekana kuchuana katika harakati za kunyakua jimbo hilo lililoachwa wazi na Jeremiah Sumari (CCM) aliyefariki Januari mwaka huu.

  Vyama vingine vinavyoonekana kama wasindikizaji ni pamoja na TLP, Sau, AFP, UPDP, DP na NRA, huku vingine vikishindwa kufanya mikutano ya kampeni.


  SUGU: UBUNGE SI WA KUFUTA MTU MACHOZI


  Miongoni na vijembe vilivyotawala jana ni pamoja na kauli ya Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr. Sugu dhidi ya ombi la makada wa CCM la kutaka mgombea wao, Sioi Sumari, apewe ubunge ili kumfuta machozi kutokana na kufiwa na baba yake, Jeremiah Sumari ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki.


  Akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nshapu Kata ya Nkoaranga, Sugu alikejeli ombi hilo na kusema kuwa ubunge hauwezi kumfuta mtu machozi.


  Alisema: “Kama ingekuwa hivyo basi, Rais wa Tanzania leo angekuwa Madaraka Nyerere au Makongoro, maana nao ni wafiwa, tena baba yao tunamheshimu kwa kuwa alikuwa Baba wa Taifa.”


  Sugu alirusha kijembe hicho kwa lengo la kumjibu Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, ambaye amekuwa akimwombea kura Sioi kwa kuwataka wananchi wamchague ili wamfute machozi kwa sababu amefiwa na baba yake.


  Sugu alisema ameshangaa kusikia kuwa mgombea wa Chadema, Joshua Nassari, hivi sasa anasomesha watoto kadhaa ambao ni yatima ilhali yeye (Sugu), ameanza kuwasaidia watoto wa namna hiyo baada ya kuwa mbunge.


  MBOWE: CHADEMA TULIENI, USHINDI WETU  Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliwataka wafuasi wa chama hicho kutulia na kutofanya fujo wala kuwazomea wafuasi wa CCM kwa kuwa anaamini kwamba Chadema imekwisha kushinda kwenye uchaguzi huo.


  Badala yake, aliwataka wananchi hao waombee uchaguzi huo pamoja na Nassari ili ushindi wa Chadema uwe ni wa haki ambao hauhitaji kumwaga damu.

  Alisema wananchi wa jimbo hilo wanapaswa kutumia mikutano ya chama hicho kutafakari changamoto zinazowakabili, badala ya kuichukulia kama burudani kwa kuwa inalenga kuamua mustakabali wa maisha yao.


  NASSARI AJIFANANISHA NA PAKA


  Mgombea wa Chadema, Nassari, amejifananisha na paka kwa kuwataka wananchi wa jimbo hilo wamchague ili akatawanye panya ambao wapo kwenye Halmashauri ya Meru.


  Akihutubia jana kwenye mikutano yake ya kampeni katika Kata za Leguruki, Nkoaranga, Akheri, Nkoarisambu, Songoro na Mbuguni, Nassari alisema Halmashauri ya Meru imekuwa ikitengewa mabilioni ya fedha za maendeleo kila mwaka, lakini hazijulikani zinakoelekea kwa kuwa huduma nyingi muhimu bado ni mbovu.  Alitoa mfano kwamba katika mwaka wa fedha wa 2011/12, halmashauri hiyo imetengewa Sh. bilioni 3.9 za miradi ya maendeleo, lakini hadi sasa mwaka unaelekea mwishoni na hakuna kilichofanyika.


  “
  Bado mama zetu wanajifungulia sakafuni, hakuna maji, hakuna barabara, shule zetu hazina madawati na hampati taarifa za matumizi ya fedha...nitumeni mimi kama panya katika halmashauri ili nikalie ‘nyau’ hawa panya wanaotafuna fedha zetu watawanyike,” alisema.  Nassari huku akishangiliwa na umati wa watu waliokuwa wanamsikiliza, alisema imekuwa kawaida kwa wananchi wa Meru kutopewa hesabu za mapato na matumizi ya fedha zao, huku wakilazimishwa kuchangia miradi mbalimbali ambayo hata hivyo haikamiliki.


  “Kila mwaka wadogo zangu wanapojiunga kidato cha kwanza wanaambiwa waende na madawati, mimi najiuliza kwani waliomaliza kidato

  cha nne wanaondoka na madawati yao?” alihoji na kuongeza “Wananchi wenzangu miradi mingi wala siyo ya kwenda kuidai Dar es Salaam, ni suala tu la kuingia Halmashauri na kuamua vipaumbele kwa sababu fedha zipo.”


  Wakati huo huo, viongozi kadhaa wa CCM wamehamia Chadema akiwemo Mwenyekiti wa Mahakama wa Ardhi Kata ya Nkoaranga, Richard Mungure, pamoja na mabalozi kadhaa.


  MEDEYE ASHAMBULIA SLAA


  Katika mwendelezo wa malumbano, jana Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Medeye ambaye pia ni Mbunge wa Arumeru Magharibi, alimshambulia Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod, Slaa na kumtaka aache kuwahadaa wananchi

  wa Arumeru Mashariki kuwa atayatwaa mashamba yanayomilikiwa na walowezi na kuwawagawia.


  Medeye alitoa kauli hiyo katika mikutano ya kampeni katika vijiji vya Sing’isi, Seela na Nkoanekoli katika kata ya Poli wakati akimnadi mgombea wa CCM, Sioi Sumari.


  Alisema kuwa Dk. Slaa amekuwa Mbunge wa Karatu kwa miaka 15, lakini hajaweza kuwasadia wananchi wa Karatu kupata mashamba.


  Alisema tayari serikali ya CCM inalishughulikia tatizo la uhaba wa ardhi na kuwa ni serikali pekee inayoweza kuyatwaa mashamba hayo kwa kufuata taratibu za kisheria.

  “Nataka niwaambie ukweli, nathubutu kumwita Dk. Slaa ni profesa wa uongo, anapita katika vijiji katika kampeni za chama chake na kuwadanganya kuhusu mashamba yanayomilikiwa kisheria na wawekezaji kwamba atawapa, hii ni ajabu atatumia njia ipi?” alihoji Medeye na kuongeza:

  “Huyu anayewaambia hayo maneno amekuwa Mbunge wa Karatu kwa miaka 15, naomba niwaambie hakuna wilaya yenye shida ya maji kama Kataru.”

  Akifafanua kuhusu tatizo la ardhi inayomilikiwa na wawekezaji katika jimbo hilo, alisema tayari kero hiyo ilishachukuliwa na kufanyiwa kazi, lakini anashangaa kuona bado wapinzani wachache wanaendelea kuzungumzia hoja hiyo.

  Medeye alidai kuwa Dk. Slaa kwa miaka yote 15 alishindwa nini kuyachukua mashamba 32 ya wawekezaji wa kigeni waliopo Karatu na kuongeza kuwa Karatu ina mashamba 32 makubwa ya wawekezaji na kuhoji ni kwanini hajawahi kwenda kuyachukua.

  Akifafanua kuhusu tatizo la maji kwa baadhi ya maeneo, Medeye, aliwaeleza wananchi hao kuwa tayari mchakato wa upatikanaji wa maji ya kutosha katika baadhi ya maeneo umekwisha kukamilika na kinachosubiriwa kwa sasa ni utekelezaji.

  Medeye aliwaomba wananchi kumchagua Sioi ili kupeleka maendeleo ya jimbo hilo.

  NCHEMBA: WAPINZANI NI WAROHO

  Meneja wa Kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba, amedai kuwa viongozi wengi wa vyama vya upinzani wana uchu wa madaraka.

  Alitoa kauli hiyo wakati akiwapokea wanachama waliodai kujitoa upinzani na kujiunga na CCM.

  Aliwaambia wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni kuwa wanachama hao wamefanya jambo jema kujiunga na CCM.

  Baadhi ya waliodai kujiunga na CCM ni kutoka TLP na Chadema.

  Viongozi hao ni Katibu Mwenezi wa TLP Wilaya ya Arumeru, Agustino Kiungay na mhamasishaji wa Chadema wa Kata ya Sing’isi, Anna Sillas na wanachama 20 wa vyama hivyo.

  MSIMAMIZI: SIJAPOTEA MALALAMIKO YA SHAHADA

  Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Arumeru Mashariki, Trasias Kagenzi, amesema hadi sasa hajapokea malalamiko yoyote kutoka vyama vya siasa, kuhusiana na tuhuma za ununuzi wa shahada za wapiga kura.

  Alisema kuwa kimsingi kuuza na kununua shahada ni kosa kisheria, hivyo wanaofanya hivyo wanapaswa kushitakiwa kwa mujibu wa sheria.

  Aidha, alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha uchaguzi unapita salama na vifaa vyote vya kupigia kura vipo tayari na vitasambazwa siku moja kabla ya kupiga kura.

  WANNE WASHIKILIWA

  Jeshi la Polisi linawashikilia vijana wanne wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema kwa madai ya kufanya vurugu katika mikutano ya CCM.

  Kijana mmoja alikamatwa kwa madai ya kushambulia kwa mawe msafara wa mgombea wa CCM, Sioi, wakati ukielekea Kata ya Seela Sing’isi.

  Vijana watatu ambao walikuwa wamevaa beji za Chadema waliupopoa kwa mawe msafara huo mita chache kutoka eneo la mkutano kabla ya mmoja wapo kushikiliwa kwa madai ya kuushambulia msafara huo kwa mawe ambayo yalikuwa yamehifadhiwa katika mfuko wa rambo.

  Tukio hilo lilitokea jana saa 6:30 mchana ambapo wakati msafara huo ukielekea eneo la mkutano ghafla walijitokeza mbele ya msafara huo na kuanza kushambulia magari yaliyokuwa yametangulia mbele.

  Tukio hilo lilizua purukushani wakati wa kushikiliwa kwa kijana huyo na baadaye wenzake wawili kukimbilia maeneo yasiyojulikana.

  Mara baada ya kushikiliwa na vijana wa ulinzi wa CCM walimkabidhi kwa Polisi na kishakupandishwa ndani ya gari la polisi lenye namba PT 2065.

  Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, alilaani kitendo hicho na kusema kwamba chama kilichowatuma kufanya kitendo hicho kimeishiwa sera za kuwaeleza wakazi wa jimbo hilo.

  Katika tukio lingine, vijana watatu ambao walikuwa wakinyoosha alama ya vidole viwili inayotumia na Chadema walishikiliwa wakati mkutano wa kumnadi mgombea wa CCM ukiendelea katika uwanja wa Chama eneo la Seela Sing’isi.

  Vijana hao waliokuwa wamesimama nyuma ya eneo la mkutano walishikiliwa na askari wa Jeshi la Polisi baada ya Medeye kutamka ya kwamba wanaoiunga mkono CCM wanyooshe mikono juu na ndipo wafuasi hao wakanyoosha alama ya vidole viwili.

  Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Thobias Andengenye, alisema ofisi yake haijapokea taarifa kuhusiana na matukio hayo na kuhaidi kufuatilia.

  Imeandikwa na Restuta James, Cynthia Mwilolezi na Charles Ole Ngereza, Arumeru.  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...