Roma akiwa Harare, mimi nitakuwa Gaborone

Roma akiwa Harare, mimi nitakuwa Gaborone

mwankuga

JF-Expert Member
Joined
Aug 30, 2010
Posts
334
Reaction score
120
ROMA AKIWA HARARE, MIMI NITAKUWA GABORONE.

Umbali kutoka Harare hadi Gaborone, Botswana ni kilomita 927, sawa na umbali kutoka Mwanza kwenda Mbeya, kupitia barabara ya Dodoma – Iringa. Huu ndio umbali utakaotutenganisha mimi na ROMA. Nimeona bora niende Gaborone Botswana kuliko kwenda Zimbabwe. Zimbabwe itakuwa ni sehemu ya mwisho kabisa kwa mimi kwenda. Namshauri hata ROMA, kuja Gaborone na kuondoka Zimbabwe mara moja.

Mji mkuu wa Zimbabwe ni Harare, mji ambao uko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Jiji la Harare lina wakazi wapatao 1.6m. Hapa ndipo kuna ikulu ya Zimbabwe, ambayo inamilikiwa na Robert Gabriel Mugabe na Mama Grace.

Wakati nikiwa kijana barubaru nilikuwa naipenda sana nchi ya Zimbabwe kupitia kwa mbabe wa vita, Robert Gabriel Mugabe. Ndani ya miaka kumi ya utawala wa kizalendo chini ya Robert Mugabe kulikuwa na mafanikio mengi sana ya kiuchumi na kijamii. Zimbabwe ilikuwa inaitwa gala la Afrika, kwa sababu ilikuwa inazalisha mazao ya chakula na biashara kuliko nchi yoyote chini ya Jangwa la Sahara. Uchumi ulikuwa unakua kwa kasi ya kuridhisha, maendeleo ya kuridhisha katika sekta ya elimu na nyinginezo.

Kwa bahati mbaya, Zimbabwe ikaingia kwenye mtego ambao umenasa nchi nyingi za Afrika. Matatizo ya Ardhi, utawala mbaya chini ya comrade Mugabe na kikundi kidogo cha marafiki (maveterani wa vita), yameifanya Zimbabwe kuwa sio sehemu nzuri ya kuishi. Uchumi umeanguka katika hali isiyosimulika ambayo imeweka rekodi ya dunia.
Siasa za Zimbabwe zimeshikiliwa na Mugabe na familia yake, huku chaguzi nyingi zikifanyika kama geresha tu. Ikulu ya Harare inashikiliwa na Grace Mugabe, kwani babu Mugabe hana nguvu tena ya kuhimili majukumu ya Urais.

Uhuru wa kushiriki kwenye siasa, na wananchi kutoa maoni upo kwa hisani ya Ikulu ya Harare. Viongozi wa vyama vya upinzani na waandishi wa habari wanaoikosoa serikali wanashikiliwa na polisi na kuwekwa rumande bila kupelekwa mahakamani. Mgawanyo wa maadaraka kati ya bunge, serikali na mahakama umevurugika kabisa. Serikali ya Mugabe ndio mahakama na ndio bunge. Kwa vigezo vyovyote vya uchumi, kisiasa na kijamii, Zimbabwe inabaki kuwa mfano mbaya kwa nchi za Afrika.

Hapa ndipo nashangaa kwanini ROMA ameamua kwenda Zimbabwe, wakati nchi hiyo haina mfano mzuri kwa Afrika. Wakati ROMA anaenda Harare, mimi naenda zangu Gaborone. Swali; kwanini nimechagua Gaborone na sio Harare?
Goborane ni mji mkuu wa Botswana ambao uko Kusini Mashariki mwa nchi hiyo. Mji huo uko kilomita 15 tu kutoka mpaka wa Botswana na Afrika Kusini. Ni mji ambao unakadiriwa kuwa na watu milioni 2, na miongoni mwa miji inayokuwa kwa haraka sana Barani Afrika. Gaborone ni makao makuu ya SADC, huku makampuni makubwa kama Hyundai, IBM, Daewoo, Volvo, Siemens yakiweka makazi ndani ya jiji hilo.

Hivyo si jambo la kushangaza kuona nchi ya Botswana ikiwa miongoni mwa nchi ambayo inaendelea kwa kasi kubwa sana. Miaka ya 1970s, Botswana ilikuwa miongoni mwa nchi masikini kabisa katika dunia hii. Lakini kwa sasa Botswana ni nchi ya uchumi wa kati. Wananchi wengi wa Botswana wanakimbia nchi yao na kujihifadhi Gaborone na miji mingine ya Botswana.
Mafanikio ya kiuchumi ya Botswana yamechangikiwa kwa kiasi kikubwa na uimara wa misingi ya demokrasia na utii wa sheria. Botswana ni miongoni mwa nchi ambazo rushwa iko chini sana. Demokrasia na utii wa sheria umepelekea nchi ya Botswana kuwa nchi ya amani, usalama na maendeleo. Kwa miaka minne mfululizo, taasisi ya Transparency International imeitaja Botswana kuwa miongoni mwa nchi ambazo rushwa iko chini sana.

Kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Botswana yamechangiwa na uongozi na utawala bora. Kipengele hiki ni muhimu sana ili nchi kupata maendeleo. Tangu Botswana imepata uhuru imekuwa na bahati ya kuwa na viongozi wenye maono na kujua wanachotaka wananchi. Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Seretse Khama (baba wa Ian Khama, rais wa sasa) aliweka misingi bora ya uongozi ambayo imefuatwa na viongozi waliofuatia; Quett Masire, Festus Mogae na Ian Khama.

Pamoja na kwamba Botswana ni nchi kame, lakini uwepo na madini, ufugaji na utalii, nchi hiyo ina sera nzuri za uchumi ambazo zinawavutia wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi. Madini yanachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa Botswana. Wakati hapa nyumbani tunajadili mambo ya makinikia na kodi zinazotokana na madini, Botswana imepiga hatua kubwa sana katika eneo hilo. Kampuni kubwa ya madini, iitwalo Debswana inamilikiwa kwa asilimia 50 na serikali, wakati asilimia 50 zinamilikiwa na kampuni binafsi. Sekta ya madini pekee inachangia asilimia 40 ya mapato yote ya nchi.

Demokrasia na uhuru wa maoni umenifanya kuchagua kuishi Gaborone. Moja kati ya matatizo ya nchi za afrika ni ukosefu wa demokrasia na uhuru wa kutoa maoni. Hakuna demokrasia iliyokamilika, wala uhuru uliopitiliza, lakini Botswana ni mfano wa kuigwa barani Afrika. Ni nadra sana kukuta watu wanakamatwa kwa kuikosoa serikali, na kushtakiwa kwa kutoa maoni yanayoendana tofauti na serikali. Serikali kwa kiasi kikubwa, imetambua kwamba ili maendeleo yapatikane, ni lazima wananchi washirikishwe.

Katiba na Vyama vingi. Kwa kiasi kikubwa wanasiasa na wananchi wanaheshimu utawala wa sheria na Katiba. Katiba ya Botswana imeweka misingi ya mgawanyo wa madaraka kati ya Serikali, Bunge na Mahakama. Kila muhimili unafanya kazi bila kuingiliwa na mhimili mwingine tofauti nan chi nyingi za Afrika. Vyama vya upinzani vinapewa nafasi ya kufanya kazi yao, licha ya kwamba chama tawala (Botswana Democratic Party) kimetawala siasa za Botswana. Nchi nyingi sana za afrika, vyama vya upinzani vinachukuliwa kama vikundi vya wahaini na watu waliokosa uzalendo.

Kwa mifano hiyo, ndio maana nimechagua kwenda Botswana, badala ya Zimbabwe ambako ROMA amechagua kwenda. Inawezekana ROMA amekata tiketi ya kwenda Zimbabwe kuungana na bingwa wa vita Robert Mugabe, lakini bado hajachelewa. Anaweza kuachana na tiketi hiyo, na kukata tiketi nyingine ya kwenda Zimbabwe. Haijalishi ataenda kwa njia gani, muhimu ni kwamba Botswana iko kwenye njia sahihi ya kujipatia maendeleo.

Kwa hali ilivyo Zimbabwe, uchumi kudorora, uongozi wa kiimla wa Mugabe, vyama vya siasa (upinzani) kuchukuliwa kama vikundi vya kihaini, uhuru wa maoni kuwa wa upande mmoja (ni serikali tu inayosema ukweli), sio sahihi kwa watanzania kwenda huko. Botswana ni mfano mzuri katika sera nzuri za uchumi, matumizi sahihi ya rasilimali, utawala bora n.k. Viongozi wa Botswana wanajenga taasisi imara badala ya kujijenga wenyewe, ni mfano wa kuigwa katika kutii sheria, kanuni na taratibu, wanatanguliza mbele masilahi ya nchi n.k.

Ewe ROMA kabla hujaenda Zimbawe, naomba pitia Botswana ili uweze kujifunza mambo mazuri ambayo yataisaidia nchi yetu. Zimbabwe sio nchi sahihi ya kujifunza. Kwa mambo utakayoyaona Botswaana, bila shaka utaachana na mpango wa kwenda Zimbabwe.

ROMA AKIENDA ZIMBABWE, MIMI NITAKUWA BOTSWANA- GABORONE.
 
Back
Top Bottom