RIWAYA YA ANGAMIZO 7

Feb 5, 2016
16
4
RIWAYA: ANGAMIZO
MWANDISHI: HALFANI SUDY
SIMU 0674 395733
WHATSAPP 0757 633010

CHUKI ni kitu kibaya sana. Siku zote chuki ina matokeo mabaya kwa wote, anayechukia na anayechukiwa. Tuache kuikumbatia chuki moyoni mwetu, kuikumbatia chuki moyoni ni sawa na kulikumbatia kaa la moto katikati ya kiganja chako. Bila shaka utaumia mwenyewe mshikaji, na pengine utamuumiza unayemchukia. Utajitesa mwenywe bure, pengine usimtese unayemchukia. Tuache kuibeba dhambi ya chuki moyoni mwetu, Namaanisha tupendane. NA HII NI SEHEMU YA SABA....
***
Mayasa alikuwa Mtoto wa mkubwa Serikalini. Serikali ilituma wapelelezi mahiri watatu. Kwenda Arusha kumsaka muuaji ! Walienda wapelelezi watatu. Lakini kila mmoja alivuliwa ngozi kwa siku yake. Waliuwawa kwa maji yaleyale yaliyomuua Mayasa. Maji yaleyale yaliyomuuwa afande John ! Mmoja alikutwa amekufa hotelini kwake, akiwa amelala.Ngozi ikiwa imejitenga na mwili wake ! Wapili alikutwa amekufa akiwa kwenye gari lake. Aina ileile ya kifo alichouwawa mwenzake. Wa mwisho aliuwawa mgahawani. Akiwa anakula chakula cha usiku.
Hali sasa ilitisha !
Ndani ya selo hali Abdul Ilikuwa mbaya sana. Polisi hawakuwa wamempiga hata kidogo . Lakini alikuwa amechoka taabani. Alichoka kimwili. Alichoka kimawazo. Kifo cha Mayasa kilimuumiza sana kichwa. Akilini mwake alijua Raiya anahusika kwa asilimia zote. Aliukumbuka sana wema wa Mayasa. Mayasa alikuwa kama malaika kwa Abdul. Mayasa alikuwa mwanamke mwenye roho ya kipekee sana. Alimsaidia bila ya sharti lolote. Alimkumbuka kila dakika mle selo. Sasa alimchukia sana Raiya. Chuki kwa Raiya ilianza taratibu. Lakini sasa ilikuwa imeota mizizi. Alimwona ni adui yake namba moja duniani. Adui kwa kumuua Mayasa. Rafiki mwenye upendo wa kweli kwake.
Wazazi wake hawakuwa wanajua kama yuko jela. Na wala hakutaka kuwaambia, maana hata angewaambia isingesaidia lolote, maana hakuna atakayeenda Arusha. Wasingekuwa na nauli ya kwenda Arusha. Alikuwa anaijua hali ya uchumi ya nyumbani kwao. Aliacha kuwaambia akihofia kuwapa presha za bure. Wakati akiwa anawaza hayo, mlango wa selo ulifunguliwa. Aliingia askari mmoja wa kike. Alikuwa na sura ya huzuni. Alikuja kumpa taarifa mbaya ya kifo. Taarifa ya kifo cha Afande John !
"Inamaana Raiya kamuua na Afande John ?"
" Sidhani kama Raiya anahusika. Afande John amefariki wakati Raiya yuko selo"
"Unasema !"
"Ndio hivyo Abdul, hebu tuambie mtu mwengine unayehisi anaweza kuwa nyuma ya mauaji haya Abdul ?"
"Hakuna nilijualo Afande kweli sijui kitu afande" Alisema huku machozi yanamtoka .
Alirudishwa selo baada ya mahojiano mafupi na askari yule wa kike. Sasa akaona uzito na ugumu wa kesi hii iliyokuwa inamkabili. Akaamua kuwaeleza wazazi wake Bagamoyo kwa simu. Hakuwa na jinsi sasa. Alikuwa anahitaji hekima za wakubwa. Alikuwa anahitaji sana majaliwa ya Mungu. Kutoka katika mkasa huu mzito...!
Aliwaomba askari wampe simu ili awapigie wazazi wake. Awataarifu juu ya kukamatwa kwake.
Walimruhusu.
Alimueleza baba yake mzazi, Mzee Washiro juu ya kukamatwa kwake na Polisi na tuhuma za mauaji zinazomkabiri. Alisikitika sana baba yake. Kwa mara ya kwanza alimsikia baba yake akilia kwenye simu. Alipatwa na uchungu sana. Abdul alikuwa mtoto wake wa kwanza kati ya watoto saba. Alikuwa ndiye tumaini hai la familia yake. Mtoto aliyesoma zaidi ya wote katika familia yake. Habari ya kutuhumiwa kwake kwa kesi ya mauaji, kwa baba yake ilikuwa mithili ya kuzimika ghafla kwa mshumaa pekee akioutegemea gizani. Pamoja na yote alimuahidi kitu. Alim-ahidi lazima aende Arusha punde atakapopata pesa. Abdul alijua baba yake hatokukwenda Arusha karibuni. Na pengine hatokwenda kabisa. Na anaweza kuozea jela Arusha bila kumuona ndugu yake yeyote. Walikuwa mafukara sana nyumbani kwao. Lakini kidogo alipata imani. Kwakuwa nyumbani kwao walikuwa wanafahamu sasa kuwa mtoto wao yupo katika matatizo makubwa ugenini.
Kwa upande wa Polisi wa Arusha Ilikuwa hekaheka ndani ya Jiji. Walitafuta wachuna ngozi wale wasio na huruma bila mafanikio. Walimkamata kila waliyemuhisi, lakini hawakufanikiwa kumkamata muuaji halisi. Ilikuwa kama ametoweka ghafla Arusha. Jiji lilibaki likisubiri Muuaji yule katili ataibukia wapi?
Baada ya wiki mbili yalitokea mauaji!. Safari hii katika Jiji la Mwanza . Mauaji ya aina ileile kama yaliyotokea Arusha. Katika Chuo kikuu cha St Augustine cha huko jijini Mwanza kuna mwanafunzi aliuwawa kikatili. Alikuwa anatoka kujisomea usiku akielelekea Hosteli. Alinyang'anywa njiani roho yake!
Maiti yake iliokotwa asubuhi katika uwanja wa mpira wa chuo ikiwa haitamaniki! Ngozi iliokotwa upande wa goli la kaskazini. Kiwiliwili kisicho na ngozi kiliokotwa karibu na goli la kusini. Yalikuwa mauaji ya kinyama sana! Yaliowaacha na uwoga mkubwa sana wanafunzi wa Chuo hiko kikubwa jijini Mwanza. Mwanafunzi huyo alikuwa ni mtoto wa waziri wa ujenzi, Mheshimiwa Karimu Nduguga.

TUKUTANE TENA KESHO KUENDELEA NA MAMBO HAYA YA AJABU...JE KWELI KUNA MKONO WA RAIYA KATIKA MAUAJI HAYA
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom