RIWAYA: Sitaisahau Facebook

RIWAYA: Sitaisahau Facebook

Respect kwako, Ila Isabela atawakomboa tu usiwe na shaka mkuu.
 
SITAISAHAU facebook
MTUNZI: Emmy John P.




SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI


Joka lilijinyanyua juu. Sote tukawa chini yake. Joka lenye rangi ya dhahabu!! Sasa ikawa patashika kila mtu analazimisha kujificha nyuma ya mwenzake. Hakuna aliyetaka kufa. Mimi, Jenipher na wale wengine waliokuwa wanatambua yule nyoka amekuja kufanya nini pale tulijiweka mbali na vile vipande vya zile nya
ma zenye namba 666.
Joka likavimba kama linataka kutema sumu. Likavimba zaidi kama linataka kupasuka. Hatimaye likautoa ulimi nje. Likatanua mdomo kama linataka kutumeza sote. Kisu chan gu bado kilikuwa mkononi.
Mara likajirusha na kujizungusha kama pangaboi. Hapa hakuna kitu kilichosalia. Kila mmoja wetu alirushwa mbali kabisa. Mimi sikuumia lakini wenzangu waliumizwa.
Nilipogeuka nilimwona kiumbe akiwa amelowa damu akiwa na jambia mkononi. Alikuwa akikimbia mahali ambapo joka lipo. Alikuwa ni Samson yule jasiri wa kisukuma.
Macho yako yalifumba kisha yalipofumbua alikuwa ameingia mzimamzima katika kinywa cha yule nyoka. Jambia na yeye wakawa wamemezwa.
Hali ya hatari!! Nilijitahadharisha.
Joka lilikuwa linameza vile vipande vya mabaki ya nyama yenye chapa ya 666. Ndipo hapa nilimuona tena yule Osmani aliyetambuliwa kama waziri wa miundombinu. Nikakumbuka kuwa ni huyu bwana nimeambiwa kuwa anazijua njia zote za kutoka katika mji huu wa kishetani. Nikamnyemelea huku nikiwa makini na yule joka na pia nikiwa makini asiweze kuhisi chochote kile.
Nikamfikia nikamkaba shingoni. Nilikuwa na nguvu za ajabu sana. Nikamvuta hadi katika kichaka nilichokuwa nimejihifadhi hapo.
Hakuwa ananiona!! Jambo hilo lilinipa nafasi nzuri ya kumtawala. Kwa ukombozi wa wengi na kujitoa katika adha ya kufia katika mji huo. Nikanyanyua kisu changu nikazamisha katika paja lake. Akatoa kilio kikubwa sana. Kilio kile kikasababisha lile joka linyanyuke mara moja. Likaanza kuangaza huku na huko. Nami nikatulia tulii kuangalia nini kinatokea. Joka likanyanyuka kisha likatanua midomo yake. Kisha likionekana dhahiri kuwa na hasira lilitapika. Maajabu!! Samson yule jasiri katika vita hiyo akatangulia kisha jambia lake likafuata.
"Njia ya kutoka hapa ni ipi?" nilimuuliza Osman huku bado akiwa katika himaya yangu.
"Sijui." Akanijibu kwa jeuri. Nikamchoma tena kisu katika sehemu ileile kilipopitia awali.
"Nasemaaaaa!" akapiga kelele.
"Dakika moja tu nakupa sema upesi."
Osman akaanza kutoa maelekezo ya namna gani ya kutoka katika kijiji hicho cha maajabu!!
Maelezo yalikuwa yamenyooka!! Japo yalikuwa na masharti. Sikuwa na budi kuendelea kumshikilia. Ni huyu angetuwezesha kutoka.
Joka lilizidi kuhangaika.
Sasa lilitazama mahali alipokuwa Osmani na mimi. Likatambaa kwa hasira kali sana likawa linatufuata. Nikajikuta namuiachia Osmani. Nikaanza kukimbia. Joka likawa linaufuata uelekeo wangu.
Mungu wangu!! Kumbe linaniona sasa hivi. Nimekwisha.
Nilizidi kutimua mbio. Hatimaye mbio za sakafuni zikaishia ukingoni! Nikaanguka chini. Joka nalo hilo likanifikia.
Likaachama mdomo wake mkubwa.
Sasa nakufa! Nilikubali yaishe.
Achaaaaaa!! Nilipiga kelele za mwisho za kutokwa na roho. Huku nikitegemea zitakuwa kelele za mwisho. Haikuwa hivyo. Niliweza kuwa hai tena. Joka lilikuwa limeufumba mdomo wake. Likatulia tuli.
Nikaduwaa kulikoni nyoka huyu hajanimeza. Au! Au! …nikakosa majibu.
Joka likaendelea kutulia kama lina urafiki na mimi. Kwa uoga nikasimama na kuanza kutambaa taratibu. Joka limetulia halina habari. Nikasimama. Bado tuli! Nikaanza kuondoka hadi nikatokomea! Nyoka ametulia.
Maajabu makubwa sana haya!!


*****


Nilirejea hadi kule walipokuwa wanakijiji wenzangu. Osmani alikuwa amehitisha mkutano tena. Alionekana mwenye furaha sana na ni kama alikuwa anatoa karipio kali.
Samson niliyedhani amekufa kumbe alikuwa amezimia tu baada ya kutemwa na yule nyoka. Nilimkuta akiwa amefungwa kamba nyingi sana. Bila shaka adhabu yake ilikuwa imewadia.
Nilimuona Jesca pia. Lakini John pekee ndio nilikuwa sijamuona.
Nilikuwa na hasira. Nikatumia ule mwanya wa joka kutulia. Nikamvamia Osmani. Nikamkaba tena. Safari hii sikutaka mambo mengi sana, nilihitaji njia ya kutokea.
"Wakati wa kuwa watumwa wa shetani umekwisha. Tunatakiwa kusihi maisha yetu tuliyoshi awali. Manyanyaso haya yote na yasiendelee. Tusikubali kabisa uonevu huu. Sasa tunatoka humu. Kila mwenye nia na aungane nami sasa. Tunatokaa!!" niliunguruma kwa sauti kuu. Wale wasiokuwa na Chapa walinisikia na kuniona. Wale waliokuwanayo waliduwaa wasijue kinachoendelea.
Samson alifunguliwa kamba alizokuwa amefungwa. Sasa Osmani akawa anatuongoza kuielekea njia ya kutokea.
Chapa ya 666 ilikuwa katika mkono wake wa kuume.
Kijiji kilikuwa kikubwa sana. Tulipenyeza njia hadi njia bado hatukufika tulipokuwa tunahitaji.
Sasa tulifika mahali palipokuwa na majani makavu lakini laini sana. Tulipokuwa pale. Osmani akaniponyoka. Kisha akapiga mluzi fulani hivi. Wakatokeza kenge wa ajabu. Wakubwa kama mamba. Walikuwa wanne. Na dhahiri walikuwa na njaa. Walishambulia katika namna yha ajabu na upesi sana.
Waliua! Watu kumi wakaanguka chini. Mamba wale badala ya kula nyama wakawa wananyonya damu.
Ilikuwa zamu yangu sasa. Osmani alikuwa pembeni akitucheka. Kuna unga fulani alijipaka usoni, sasa aliweza kuniona vizuri.
"Achaaaa!!" nilijikuta natamka neno lililoniokoa midomoni mwa joka lile kuu. Kenge hawa wa ajabu wakatulia palepale wakafunga vinywa vyao. Osmani akashangaa na mimi pia nikashangaa.
Samson ambaye naye alikuwa amekata tamaa alishangaa.
Nikawahi kuipoteza hali yangu ya kushangaa. Nikamwendea Osmani. Nikamkaba tena. Nikampiga makofi mawili akaanza kutema damu.
"Njia ya kutokea!!" niliamuru.
Akageuka, akatunyooshea mkono. Palikuwa na mlango mdogo wa mbao zilizooza. Nikawaamuru wanakijiji wsaliosalia wapite. Wakapita!!
Hadi walipomalizika ndipo mimi na Osmani tulipita. Kabla hatujamaliza kupitia nilisikia kilio kikubwa. Kuna mtu alikuwa akiniita.
Sauti ile ilikuwa ya John!
Nikasita kutoka. Nikarejea nyuma niweze kuchungulia.
John alikuwa anagalagazwa na lile joka kubwa.
Huruma ya mapenzi yangu kwa John ikanijia. Nikaweka kando yote aliyowahi kunitendea. Nikarudi kwa kasi. Neno acha likiwa mdomoni mwangu. N ilipofika nikaamuru kwa sauti kuu. Joka lile likatii kwa nidhamu. Nikaduwaa. Nikamchukua John na kuanza tena kuitafuta njia ya kutokea.
Kosa kubwa! Nilimuacha mbali waziri wa miundombinu!
Osmani akawa amepotea! Sikujua ni wapi pa kupita.
John hakuwa akiniona wala kunisikia. Nilitamani ajue ni mimi nipo naye. Lakini haikuwa hivyo.
Nilifanikiwa kukipata kisu. Nikaamini sasa nitaiondoa alama ya 666 katika mwili wake na ataweza tena kuona.\
Hofu! Na kukata tamaa. John alikuwa na alama ile shingoni mwake. Mwili ukafadhaika.
Siwezi kumchinja John!! Siwezi!! Niliapa.
Lakini nitafanya nini sasa.
Kitu kama tetemeko la ardhi likatwaa mawazo yangu. Nikamvuta John asiyejielewa nikamkumbatia. Tetemeko hilo lilivyopita hapakuwa tena na lile joka.
Lakini kitu kipya kikajitokeza. Ulikuwa mwanga mkali kama jua vile!! Nikatafakari ni kitu gani hicho. Sikuweza kutambua.
Mara ule mwanga ukapotea. Nikasja kushtuka nimepigwa kibao katika shavu langu. Nikaanguka.
Niliposimama nikapigwa tena, na sikumjuona kiumbe aliyekuwa ananifanyia hivyo.
Mapigo yakaongezeka. Nikawa navuja damu.
Sikuweza kusimama tena.


Sauti ya Jenipher ikanijia kichwani, "Ukinywa damu unakuwa kama wao!!"
Maneno hayo yakanifanya nipatwe na ari mpya. Nikatambaa nikamfikia John.
Badala ya kumchinja! Nitamnyonya damu walau kidogo tu.
Nikamfikia. Nikamkamata. Akaanguka chini, nikajirusha shingoni mwake. Nilipoifikia shingo yake nikamkumbuka yule mganga wa kinaijeria. Hapo sasa nikakumbuka sio mara yangu ya kwanza kunywa damu. Nikapenyeza meno yangu pale pale kwenye alama ya 666 aliyopigwa shingoni.
Damu ikaanza kutoka. Nikaimeza huku nikiwa nimeikunja sura yangu.
Nguvu za ajabu zikaniijia. Sasa niliweza kumuona adui yangu aliporejea tena. Alikuwa ni Dokta tuliyekutana katika mtandao, alikuwa ni Dokta Davis.


Alikuwa ananisogelea tena aweze kunipiga. Nikaudaka mkono wake. Akataka kujitoa hakuweza. Nikaweka sawa kisu changu nilichokuwa nimekificha kwa nyuma. Nikazamisha katika sehemu zake za siri huku nikipiga kelele.
Akaanguka chini na kuanza kujirusharusha.
Nikamkumbuka yule ninja wa kisukuma, Samson ambavyo hakuwa na huruma. Na mimi nikamuiga. Nikamrukia Davis na kuanza kumchoma visu.
Nilipoanza tu kumchoma kisu cha kwanza mambo yakawa tofauti na yule ninja wa kisukuma aliyekuwa akichoma kisu anaua hapo hapo...nikakumbwa na mfadhaiko mkubwa.
Oparesheni ukombozi ikaingia doa jingine!!


***ISABELA katika mapambano ana kwa ana na Davis. Je nini hatma!! na ni kipi kimetokea mbona amefadhaika


***Je? John ndio amekufa baada ya kung'atwa na Isabela.
Nyrum Mwadunda Ngoami Cyduu ram amina mabata Excel Khantwe binti kiziwi showtie miss neddy korino Nicas Mtei Angelicious
 
Last edited by a moderator:
SITAISAHAU facebook
MTUNZI: Emmy John P.




SEHEMU YA ISHIRINI NA TATU


Nikafadhaishwa baada ya yule Davis ambaye sasa niliamini naenda kummalizia alipogeuka kuwa joka kubwa la kijania. Haraka nikawahi kujitoa lakini nilikuwa nimechelewa sana. Joka lile likawahi kujiviringisha kuanzia kiunoni likawa linapanda juu. Sasa lilikuwa limenifunga hadi kifuani.
Ajabu!! Lilikuwa linawasha sana.nilitamani kujikuna lakini haikuwezekana na mikono ilikuwa imefungwa tayari.
Nililiamuru liniachie lakini halikuiheshimu amri yangu. Nikazidi kuwashwa, nikajaribu kujigalagaza, haikuwezekana. Sasa likaanza kujikaza, muwasho ukaenda likizo, maumivu yakaingia kati. Lilizidi kukaza, mara likaongeza kujiviringisha hadi likaniziba usoni. Kifo kikanukia harufu ya kukera.
Nikabaki jicho moja tu kuona nje!! Viungo vingine vyote vilikuwa vimefunikwa. Sikuwa na ujanja. Jicho langu likamuona John akiwa ameshangaa kama tahira. Nilijaribu kutoa sauti haikutoka, nilikuwa namwomba John kwa mara ya mwisho aweze kuniokoa. Hakuweza kunisikia.
Nikatazama juu nikakutana na mawingu yenye rangi inayoshabihiana na buluu, nikaikumbuka rangi ya mtandao wa kijamii. Ni huku nilikutana na Dokta Davis. Akanipa zawadi ya utajiri, akanipatia kazi nyepesi inayonipatia kipato kikubwa. Nikamuamini sana. Sasa alikuwa amegeuka joka kubwa na lilikuwa linaniua.
Hakika lazima nife!! Jitihada zangu zote hazikuwa na maana tena.
John hakuwa msaada wowote kwangu. Na hakuwepo mwingine wa kunipa msaada.
Nilipofikiria ni nani mwingine wa kunisaidia akili yangu ikaejea kwa mwalimu Nchimbi. Mama yangu mzazi. Nikajaribu kuita sauti haikutoka. Mama naye hakuwa na msaada katika hali hii.
Nikayakumbuka maneno ya mama. Miaka mingi sana nikiwa mdogo aliwahi kunikambia maneno.
"Yupo mtu anakusikia hata usipotoa sauti." Hili lilikuwa jibu alilonipa baada ya kumuuliza iwapo mabubu na viziwi wanaweza kuzungumza na Mungu. Jibu lake hadi ukubwani halikunitoka.
Nami sasa nilikuwa bubu. Jaribio la mwisho kabisa ni kuzungumza na yule anayesikia wakati wote. Ajuaye unachokiwaza. Kila wakati, mahali popote.
Mungu!
"Eeh! Baba sijui kama nilistahili adhabu hii. Na kama ilikuwa stahili yangu baba. Nichukue kwako sasa. Nimeumia na IMETOSHA." Nilizungumza katika nafsi yangu. Kisha nikasubiri kuiaga dunia hii chungu.
Nilitua chini kama mzigo mzito, bahati nzuri nilitua katika majani. Sikuumia. Nilipumua kwa fujo sana, nilikuwa nimerejewa na uhai tena.
Nikalishuhudia lile joka likihangaika huku na huko, hatimaye likatoweka.
Maajabu makubwa ambayo sijapata kuyaona na yalikuwa yanastahili kutolea ushuhuda.
Sikuwahi kuwa na imani katika miujiza lakini sasa ilinitokea ili niiamini. John naye alikuwa anashangaa kama awali. Na bado hakuweza kuniona. Sikupoteza muda nikamshika mkono. Tukaanza kuondoka. Sikukiacha kisu changu.
Nilijikuta naifuatilie ile njia tuliyopita awali hadi nikaufikia ule mlango. Nikamtanguliza John nami nikatoka.
Maajabu mengine. Niliwakuta wale waliotangulia wakiwa katika sintofahamu wasijue nini cha kufanya.
Kwa kukadiria muda ilikuwa saa sita mchana. Na tulikuwa katika ulimwengu halisi lakini hatukutambua ni wapi hapo tulipo.
Magu, Bariadi, Sumbawanga, Songea!! Kila mtgu alifanya utabiri wake.
Hatukuendelea kukaa pale. Tukaanza safari kuelekea tunapoelekea bila kutambua ni wapi.
Baada ya kilometa takribani sita tukaingia kijijini.
Mimi nikiwa na upande wa kanga pekee. Wenzangu wakiwa na nguo zilizochakaa sana. Tukakiona kijiji. Baadaye tukaanza kukutana na watu.
Kila mtu akiwa na lake la kufanya. Hakuna aliyetuuliza swali. Walikuwa weusi sana, wengine walifanana na nyani huku wanawake wengi wakiwa na maziwa makubwa.
Ni wapi sasa hapa? Nilijiuliza.
Tulitamani sana kuzungumza na watu hawa lakini hawakuwa wakarimu.
Njaa iliuvunja uamuzi wetu wa kusubiri watuanze. Njaa ilituuma na hatukuwa na chochote cha kuweka tumboni.
"Ha…habari.."
"Nkesuu…" asijui kama aliniuliza ama alinijibu salamu.
Lugha ya wapi hii!! Niliwahi kusikia mahali, ni wapi vile. Niliumiza kichwa. Kila mmoja alikuwa ananitazama mimi kama mwokozi katika mapambano haya.
"Me come great…" nilizungumza kiingereza kibovu ili nipate kujua wanazungumza lugha gani na ni watu wa wapi. Hakunijibu akanikazia jicho kwa shari. Ni hapo nikapata jawabu sura hizi nimewahi kuziona wapi. Ni kwenye basi. Siku ya safari yangu kuelekea Ndolla Zambia kwa Dokta Davis kusaini mkataba ule ulionifikisha hapa nilipo.
"Sam…it's either Congo or Ndolla….(Sam ni aidha Kongo ama Ndolla)" nilimnong'oneza yule msukuma.
"Ndolla??"
"Yes! Ndolla Zambia.." nikamjibu. Akashangaa. Yule bwana tuliyemuuliza akawa amesonya na kutoweka.
Watu hawa sio wazuri hata kidogo. Wameathiriwa na vita za wao kwa wao. Wakitugundua ni hatari. Naamuru!! Hakuna mtu kuzungumza na mgeni yeyote, I WILL!!! Nilitoa tamko kama amiri jeshi mkuu wa mapambano hayo.
Kila mmoja akanielewa.
Safari ikaendelea, tulikuwa tumechoka lakini tuliuhitaji sana ukombozi, tulihitaji uhuru wetu.
NDOLLA TOWN 40 KM AHEAD. Kilisoma hivyo kibao kigumu cha chuma. Nikajipongeza katika nafsi yangu kwa kuwa na kumbukumbu nzuri.
Jesca alikuwa mtu wa mawazo mazito. Hakuwa akiongea na ule urembo wake wa enzi zile haukuwa na nafasi hapa. Pia ugomvi wetu wa kumuwania John kimapenzi haukupewa nafasi pia. Kila mmoja alitazama anajikomboa vipi.
Tulitembea kimafungu mafungu. Jumla tulikuwa watgu ishirini na moja lakini, tulikuwa kama hatufahamiani. Kila mmoja na lake. Likitokea la kuzungumza nilikuwa nachukua nafasi hiyo.
Tulipoufikia mto, kila mmoja aliyatumia maji anavyoweza, wengi walikunywa na wachache walioga. Pumziko la dakika ishirini kisha tukaendelea mbele. Tukaufikia mti wa maembe. Hapa sasa kila mtu alikula kulingana na ukubwa wa tumbo lake. Angekuwa mjinga ambaye angeacha kubeba akiba ya maembe matamu ya Zambia.
Sasa kasi ikaongezeka na mazungumzo yakaibuka. Njaa kitu kibaya sana.
Mimi na John tulikuwa tumeambatana. Ile hali ya yeye kutoniona iliniumiza sana lakini sikuwa na namna.
Kilometa zikazidi kukatika, tulitembea hadi usiku, kwa kukadiria tulitumia masaa yanayozidi kumi. Kuzikamilisha zile kilometa.
Mji wa Ndolla ukatukaribisha. Ulikuwa mara yangu ya pili kuja katika mji huu na mara ya kwanza kufika nikiwa katika matatizo.
Nilijipongeza tena kwa tabia yangu niliyoionyesha siku ya kwanza. Tabia ya kushangaa shangaa. Hivyo kuna baadhi ya vitu nilivikumbuka. Hadi tukaipata stendi.
Kama nilivyoamuru kila mmoja alijitenga kama hatujuani. Kanga yangu ikiwa imefungwa vyema. Ni hiyo pekee ilikuwa ngao yangu. Nikaingia katika stendi ile ambayo ilikuwa inazidiwa hadhi na stendi ya Ubungo jijini Dar es salaam katika nchi yangu ya Tanzania.
Nilizunguka hapa na pale. Nikaiona ofisi ya magari amabyo nilikuwa naitaka.
"Mambo vi wewe…inakuwaje…mishemishe vipi…oya acha kuzingua…" maneno haya yalikuwa yanazungumzwa katika ofisi hizi.
Nikainama chini jicho langu la kulia likatangulia kumwaga chozi la kushoto nalo kwa uchungu likamwaga chozi. Nikajiinamia chini nikalia kwa uchungu mkubwa. Uchungu wa kuikumbuka nchi yangu Tanzania. Kilio hichohichoi kwa namna ya kipekee kilikuwa kilio cha furaha. Ndio lazima nifurahi. Sasa ningeweza kumvuta mtu na kuzungumza naye Kiswahili.
Ni hivyo nilifanya. Mwanaume kipande cha mtu akavutika kunisikiliza. Kwanza sikutaka kumuelezea kuwa tupo wengi. Niliitetea nafsi yangu. Nilikuwa natetemeka kwa baridi. Akanipatia sweta zito nikajistiri. Nikajielezea kuwa nimepotezana na bwana aliyenileta Zambia.
"Umesema wewe mwenyeji wa Makambako."
"Ndio kaka."
"Makambako sehemu gani hiyo?"
"Ni karibia na stendi kuu. Hapa Magegele ….."
"Alaa Magegele napafahamu sana huko…kabla ya kuhamia huku nilikuwa naenda na mabasi ya Dodoma Mbeya…sasa hapo Magegele kuna mgahawa tulikuwa tunakula tulimzoea sana yule mama kiukweli..hata wewe nikutajia lazima utakuwa unamjua.."
"Mama Kesho." Niliwahi kumjibu. Akacheka sana, hakuna mtu wa Makambako ambaye hakumjua mama huyu. Alikuwa mkarimu sana.
Tulizungumza mambo mengi usiku ule. Alizungumza nami kwa ukarimu. Ni nani alikwambia kuwa watanzania sio wakarimu.
Kuna tofauti kubwa kati ya mtanzania na mbongo!! Mtanzania ana utu lakini mbongo anajifanya mjanja mjanja. Huyu bwana alikuwa mtanzania haswaa.
Upesi nikapata chakula. Kisha akaingia ndani akatoka na nguo. Zilikuwa za kike.
Akanieleza abiria huwa wanasahau nguo zao na kamwe hawarudi tena kuzichukua. Nikamshukuru. Akanipatia na kiasi cha pesa. Akaniomba nirejee majira ya saa tano asubuhi aweze kunifanyia utaratibu wa kunisafirisha kurejea Mbeya kisha Makambako Iringa.
Ilikuwa bahati ya kipekee sana kupata msaada huu. Lakini hapo hapo ilikuwa bahati mbaya sana maana nisingeweza kusafiri peke yangu. Na yule bwana sikumueleza tupo wengi zaidi ya kikosi cha timu ya mpira wa miguu.
Ubarikiwe sana!! Nilimpa Baraka hizo.
Kisha nikiwa na mavazi kamili sasa. Nikapiga hatua kwa hatua. Kigiza giza kikanifanya nionekane kama kivuli. Mkono mmoja mfukoni kuzilinda Kwacha (Pesa halali kwa matumizi ya Zambia) nilizopewa, mkono mwingine ukiwa umeshika kiroba cha nguo nilizopewa na yule bwana. Isabela nikiwa na raba nyepesi miguuni. Nikatoweka huku nikiamini nina mzigo mkubwa wa kuwaokoa rafiki zangu ambao walinitazama kwa jicho la huruma.
Nilijihesabu kama mshindi wa vita ya 666. Lakini bado nilikuwa na vita nyingine ya kurejea nyumbani.
Mshindi akifia ugenini huyo ni mshindwa lakini akirejea nyumbani hata kama amejeruhiwa vipi bado ataitwa mshindi.
Mapambano yameanza rasmi!!! Nilikiri huku nikiwa nayatamani hayo mapambano ambayo niliamini hayawezi kuwa magumu kushinda vita ya joka kuu la msituni.






***HAYA SASA KAMANDA ISABELA OPARESHENI UKOMBOZI imefikia Ndolla Zambia. Nini kitaendelea katia nchi hii ya kigeni??


*** Je Davis amekufa?? Vipi kuhusu chata ya 666 katika shingo la John!!!!


Nyrum Mwadunda Ngoami Cyduu ram amina mabata Excel Khantwe binti kiziwi showtie miss neddy korino Nicas Mtei Angelicious munimuni Meljons aniceth mzahula
 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom