SEHEMU YA KWANZA:
Jack Reacher alimuona mwanaume mmoja akiingia baani hapo kupitia mlango ambao haukuwa mlango, bali ukuta ulio wazi tu. Baa ilikuwa ikitazamana na barabara wanapopita watembea kwa miguu. Nje na ndani kulikuwa na meza na viti vilivyofunikwa na mwamvuli mkubwa uliolipa eneo lote kivuli na utulivu wa kutosha.
Yule mwanaume alisimama kwa dakika kadhaa ili kuyaruhusu macho yake yazoee giza lililokuwemo mule ndani baada ya kutoka kwenye mwanga mkali wa jua huko nje ya mitaa ya Key West. Ilikuwa ni mwezi wa sita, saa kumi kamili alasiri kusini kabisa mwa Amerika. Jua kali na joto lisilozoeleka. Reacher alikiegemea kiti chake vizuri na kupiga funda moja la maji halafu akatulia kuona nini kitafuata.
Yule mwanaume alianza kuzungusha macho yake kupakagua mule ndani. Baa yenyewe ilikuwa imetengenezwa kwa kutumia bodi zilizoonekana ni kama zimetolewa kwenye meli iliyokufa. Kwenye pembe moja kulikuwa na mkusanyiko wa vitu kama neti zilizochoka. Vifaa vya kuvulia, Reacher alihisi ingawa katika maisha yake yote hakuwahi kuvua samaki achilia mbali kupanda hata mtumbwi.
Yule mwanaume alianza kupiga hatua kuelekea ilipokuwa kaunta. Alikuwa mzee pengine wa miaka sitini. Urefu wa wastani na unene kidogo. Daktari angeweza kumuweka kundi la waliopitiliza uzito wa kawaida.
Alikuwa amevaa kama mtu wa kaskazini aliyeshtuliwa na safari ya ghafla. Suruali laini ya kijivu - Juu pana, chini nyembamba, Shati jeupe na koti la kijivu juu yake. Chini alikuwa na soksi nyeusi na viatu vya kimjinimjini. Mtu wa New York au Chicago, Reacher aliwaza. Pengine mtu wa Boston aliyekulia maisha ya kiyoyozi na nguo kama hizi huzivaa mara mojamoja pale inapobidi.
Yule mwanaume alifika kaunta na kutoa waleti kwenye mfuko wa koti lake. Reacher alikuwa bado anamtazama akiifungua waleti na kuigeuzia kwa mhudumu huku akiuliza swali. Mhudumu aliangalia pembeni bila kujali kama aliyetukanwa. Yule mwanaume akairudisha waleti yake mfukoni na kuongea jambo na mhudumu akainama akaibuka na kinywaji kutoka kwenye dumu la barafu. Yule mwanaume akakipokea na kukitazama huku akitabasamu.
Reacher akapiga fundo lingine la maji. Yeye alikuwa amekutana na watu wengi waliokuwa fiti na imara, lakini hakuwahi kukutana na mtu imara kama mwanajeshi mmoja wa kiBelgiji aliyeapa kuwa fanya chochote kile unachotaka kufanya alimradi unakunywa lita tano za maji ya madini kila siku, basi utakuwa fiti na imara. Reacher akagundua lita tano ni sawa na kigaloni kidogo na kwa kuwa yule mwanajeshi alikuwa na mwili mdogo yeye ilimfaa. Lakini yeye alihitaji lita kumi za hayo maji kila siku. Na tangu alipofika mitaa ya Keys alikuwa akiifuata hiyo ibada na ilikuwa ikimpa matokeo mazuri. Kila siku ilipohitimu saa kumi kamili angeitembelea baa hii na kukaa kwenye kona akinywa maji. Na alikuwa amejenga uraibu wa maji kama ilivyo pombe kwa mlevi.
Yule mwanaume alikuwa bado amesimama akishushia kinywaji chake kukata kiu huku akizungusha macho kama kutafuta uamuzi akae wapi. Ukitoa mhudumu, Reacher tu ndiye aliyekuwemo baani humo. Yule mwanaume akainua bia yake kama ishara ya kumwomba Reacher wakae pamoja. Reacher alitikisa kichwa. Yule mwanaume alisogea kuketi. Alipokaa akaanzisha mazungumzo.
"Wewe ndiyo Jack Reacher?" Aliuliza.
Hakuwa mtu wa Chicago. Alikuwa ni mtu wa New York. Sauti na lafudhi yake vilimfanya Reacher agundue hilo.
"Jack Reacher?" Aliuliza tena.
Kwa ukaribu, macho yake yalionesha ana maswali mengi. Reacher hakujibu baadala yake alichukua chupa yake na kupiga funda la maji.
"Wewe ni Jack Reacher?" Yule mwanaume aliuliza tena kwa mara ya tatu.
Reacher aliishusha chupa yake mezani halafu akatingisha kichwa chake.
"Hapana." Alidanganya.
Mabega ya yule mwanaume yakashuka chini. Akanyanyua mkono wake kutazama muda halafu akanyanyuka, lakini akarudi kukaa kama vile muda ulikuwa umemwambia aendelee kukaa.
"Saa kumi na moja tayari." Alisema.
Reacher akatikisa kichwa kukubali. Yule mwanaume akamuoneshea mhudumu chupa kama ishara ya kuomba aongezewe kinywaji.
"Joto," Alisema baada ya mhudumu kuondoka. "Kuna joto sana."
Reacher akatikisa kichwa chake kukubali halafu akapiga fundo lingine la maji.
"Unaweza ukawa unamfahamu mtu anaitwa Jack Reacher mitaa hii?" Yule mwanaume aliuliza.
Reacher akaguna. "Unaweza ukamwelezea muonekano wake labda nitamjua kwa kumuona ila sio kwa jina."
Yule mwanaume alikuwa anapiga funda refu la bia yake. Alipoishusha chupa akajifuta mdomo wake.
"Sina kwa hakika," Alianza kuongea. "Ninachofahamu ana mwili mkubwa na ndiyo maana nikahisi ni wewe."
Reacher alitikisa kichwa na kuongea, "Kuna watu wengi wenye miili mikubwa kuliko hata mimi kila sehemu."
"Lakini hata jina hujawahi kulisikia?"
"Ni lazima niwe nimelisikia?" Reacher aliuliza.
Yule mwanaume akaguna.
"Naitwa Costello," alijitambulisha kama kukwepa swali aliloulizwa kuepusha makubwa. "Nafurahi kukutana na wewe."
Reacher alitikisa kichwa na kuinua chupa yake na kuonesha alama ya cheers na kuanza kuongea, "Unafanya kazi ya kutafuta watu wanaotoroka?"
"Hapana, Mimi ni mpelelezi wa kujitegemea." Costello alisema.
"Na unamtafuta mtu anaitwa Reacher?" Reacher aliuliza. "Amefanya nini?"
Costello akainua mabega, "Hakuna alichokifanya. Nimepewa tu maelekezo ya kumtafuta."
"Na unahisi yupo huku?"
"Wiki iliyopita alikuwepo huku," Costello alianza kuelezea. "Anayo akaunti ya benki Virginia na amekuwa akituma hela huko."
"Kutokea huku Key West?"
Costello akatingisha kichwa kukubali, "Kila wiki kwa muda wa miezi mitatu sasa."
"Kwahiyo?"
"Kwahiyo anafanya kazi huku," Costello alisema. "Amekuwa akifanya kazi huku kwa miezi mitatu. Unahisi kuna mtu anaweza akawa anamfahamu?"
"Sidhani." Reacher alijibu.
Costello akatikisa kichwa kukataa, "Nimeuliza kuanzia Duval, ambako ndiyo pamechangamka na kwa bahati nzuri nikakutana na msichana mmoja kwenye bar f'lani akaniambia kuna mtu mwenye sifa hizo nilizokuambia na huwa anakunywa maji hapa kwenye baa hii kila saa kumi." Halafu akakaa kimya huku akimuangalia Reacher machoni kama anayetangaza pambano. Reacher akapiga funda lingine la maji halafu akamtazama Costello machoni pia.
"Sadfa." Reacher alisema.
Costello akatikisa kichwa na kuongeza, "Nadhani."
"Unajua kuna idadi kubwa ya watu wanaoingia na kutoka hapa Keys kila leo. Ni ngumu kujua nani ni nani." Reacher alisema.
"Nadhani." Costello alijibu.
"Lakini nitakuwa macho na masikio wazi." Reacher alisema.
"Nitashukuru sana."
"Kwani anatafutwa na nani?"
"Mteja wangu," Costello alisema. "Mwanamke mmoja anaitwa Mrs Jacob."
Reacher akapiga fundo la maji. Jina la Mrs. Jacob halikuwa na maana yeyote kwake. Jacob? Hakuwahi kusikia au kukutana na mtu mwenye jina hilo.
"OK, Kama nitapata fununu au kukutana naye nitamwambia, lakini usinitegemee sana kwasababu sikutani na watu wengi." Reacher alisema.
"Unafanya kazi gani?"
"Nachimba bwawa za kuogelea." Reacher alijibu.
Costello akawa kama anayetafakari kama mtu aliyejua bwawa za kuogelea ni nini lakini hakujua kwanini watu wa huku waliyahitaji.
"Unaendesha mitambo ya kuchimbia, sio?"
Reacher akatabasamu na kutingisha kichwa kukataa. "Huku tunachimba kwa mikono."
"Kwa mikono?" Costello aliuliza kwa mshangao. "Na koleo au?"
"Ndiyo." Reacher alijibu.
Costello akatikisa kichwa kama aliyeridhika na majibu na kuongeza, "Basi kwa hakika huwezi kumfahamu huyu Reacher. Kwa mujibu wa maelezo ya mteja wangu, Jamaa alikuwa ni mwanajeshi na nimeangalia nikakuta ni kweli. Medani za kutosha tena polisi wa wanajeshi mkubwamkubwa. Mtu kama huyo huwezi kumkuta anachimba mabwawa ya kuogelea tena kwa mikono."
Reacher akapiga funda lingine la maji ili kuficha msisimko wake. "Kwahivyo utamkuta anafanya nini?"
"Kwa huku?" Costello alianza kueleza. "Sina uhakika. Pengine atakuwa mkuu wa ulinzi kwenye hoteli kubwa au anafanya biashara."
"Wewe unahisi kwanini kati ya sehemu zote achague kuja huku?"
"Inashangaza," Costello alijibu. "Huku ni kuzimu, lakini ndiko aliko. Hilo halina ubishi. Aliachana na jeshi miaka miwili iliyopita akaweka pesa zake karibu na Pentagon halafu akapotea. Kuanzia hapo akawa anatoa hela karibu kila sehemu unayoijua halafu ghafla miezi mitatu iliyopita ameanza kuweka pesa kutokea huku. Hiyo inamaanisha amezunguka sana ameamua atulie hapa. Nitampata tu."
Reacher akatikisha kichwa. "Unahitaji msaada wangu kumtafuta?"
Costello akatingisha kichwa. "Usijali," Alisema halafu akanyanyuka kutoka kwenye kiti. Akawekwa pesa ya bili inayodaiwa mezani na kuanza kuondoka.
Reacher alimtazama akiondoka. Maongezi yao yalikuwa yametumia dakika 15.
Lisaa limoja baadae Reacher alikuwa anakatisha mitaa ya Duval huku maswali matatu yakiwa kichwani mwake. Kwanza ni atumie mkakati upi ili kuondoa taarifa zake za benki kupatikana kwa urahisi. Pili alikuwa anajiuliza ni wapi atapata chakula cha jioni mapema na akikipata atakula nini. Na tatu alikuwa akijiuliza ni kwanini alimuongopea Costello. Haikumchukua muda akapata majibu ya maswali yake. Kwanza kuanzia muda ule na kuendelea asingetumia tena benki kuhifadhi pesa hata kama iwe nyingi kiasi gani. Pili ni kwamba angeenda kwenye mgahawa wake wa kila siku na kufuata ushauri wa mwanajeshi mmoja kuhusu chakula kwa jioni hiyo. Swali la tatu jibu lake lilikuwa rahisi: Alimdanganya Costello kwa sababu hakukuwa na sababu ya kuacha kumdanganya.
Pia hakuwa na sababu kwanini mpelelezi kutoka New York awe anamtafuta. Hakuwahi kuishi New York. Au miji yeyote ya kaskazini. Au kuiweka sahihi, hakuwahi kuishi mahali popote. Hiyo ndiyo ilikuwa moja ya maana ya maisha yake. Ndiyo sababu mojawapo kati ya nyingi iliyomfanya awe alivyo. Alikuwa amezaliwa kwa Afisa wa jeshi la maji na alikuwa ametembea sehemu tofautitofauti tangu siku ambayo alitoka kwenye tumbo la mama yake katika hospitali moja huko Berlin. Hivyo maisha yake yote yalikuwa ni ya kwenye kambi tofautitofauti za jeshi. Alipokuwa akajiunga na jeshi hadi kuwa polisi wa wanajeshi na akaishi na kuhudumu kwenye kambi zilezile hadi mkataba wa amani uliposainiwa na jeshi likapunguza idadi ya watu ikiwemo yeye mwenyewe. Akaamua kurudi Amerika kuzungukazunguka kama mtalii asiye na hela za kutosha hadi alipofika chini kusini huku hela alizotegemea zikiwa zinaenda kuishi. Akaamua atafanya kazi kwa siku chache. Siku chache zikawa wiki na wiki ikawa miezi na bado alikuwa yupo hadi alipotokea Costello.
Hakuwa na ndugu wala jamaa mahala popote. Hakuwa akidaiwa na mtu yeyote. Hakuwahi kuiba, au kusema uongo. Alikuwa ni kama kiumbe kisichoonekana. Na kwenye maisha yake hakuwahi kufahamiana na mtu anaitwa Jacob. Hilo alikuwa na uhakika nalo. Hivyo alichohitaji Costello yeye kilikuwa hakimhusu.
Yote hii ilikuwa ni kwa sababu kutokutambulika ilikuwa imekuwa kama jadi yake na ilikuwa imemkaa kwenye ubongo wake wa mbele. Miaka miwili iliyopita kila kitu kiligeuka chini juu. Alibadilika kutoka kuwa papa hadi kuwa si chochote kwenye bahari. Kutoka kuwa kiongozi mkubwa na aliyeheshimika kwenye jamii ya wanajeshi hadi kuwa mmoja kati ya raia milioni miambili na sabini wasiojulikana. Hisia zake zilimwambia ni jambo la ajabu lakini kuna muda nafsi yake ilifurahia hio hali. Alipenda kutokujulikana. Ilimpa kujiamini na uhakika f'lani kama bima. Kila alipokutana na watu aliweka ucheshi na urafiki nao bila kusema mengi kuhusu yeye mwenyewe. Alikuwa ni mtu wa kulipa Cash na usafiri wake ulikuwa ni barabarani. Hakuna ndege wala cheki. Hakuwahi kumwambia mtu yeyote jina lake. Hata alipofika West Key alijitambulisha kama Harry Truman kwenye nyumba ya kulala wageni alipopanga chumba. Na kwavile West Key hawakujali nani ni nani alivutiwa napo. Akavutiwa kiasi cha kusahau alikuwa anatakiwa aondoke.
Alizunguka mtaani kwa muda wa lisaa limoja hadi akafika kwenye mgahawa alipozoea kula chakula.
Sahani ya chakula chake ililetwa na mhudumu ikiwa na nyama, mayai na mchanganyiko wa mboga za majani. Baadae ililetwa Ice cream ya chocolate na karanga. Alipomaliza kuila akanywa vikombe viwili vya kahawa kama kitindamlo na kushushia maji chupa mbili za lita mojamoja.
"Hapo safi?" Aliuliza mhudumu huku akitabasamu aina la tabasamu wanalotoa wafanyabiashara pale unapowapa hela.
"Imenishuka kunako kabisa." Reacher alijibu.
"Naona."
"Ndiyo. Najisikia vizuri sasa."
Na ilikuwa ni kweli. Siku yake ya kuzaliwa iliyokuwa inafuata ingemfanya awe na miaka 39, lakini bado alikuwa imara na mwenye nguvu. Hili lilimfanya ajisikie vizuri.
"Usiku unaenda kazini?" Yule mhudumu aliuliza.
Reacher akatabasamu. Alikuwa anafanya kazi nyingi. Ukitoa kuchimba bwawa za kuogelea, aliwafundisha watu pia mazoezi na usiku alifanya kazi ambayo wanaume wengi wangefurahi kuifanya bure kabisa. Alikuwa ni mlinzi kwenye baa moja ya maonesho ya utupu wa wanawake. Kazi yake ilikuwa ni kusimama akiwa kifua wazi, akinywa vinywaji vya ofa vya bure huku akihakikisha wanawake waliokuwa watupu hawabugudhiwi na mtu yeyote. Na mwisho wa siku angepewa dola hamsini.
"Ndiyo," Reacher alijibu. "Ninaenda."
Yule mhudumu akacheka. Reacher alinyanyuka akalipa hela yake na kuingia mtaani tena kuelekea bar alikokuwa akifanyia kazi ambako kuna jambo lilikuwa linamsubiria.
SEHEMU YA PILI BOFYA HAPA