Riwaya: Muuza Mihogo

Riwaya: Muuza Mihogo

asanteelimu2016

JF-Expert Member
Joined
Sep 23, 2016
Posts
248
Reaction score
147
14th October 2007
Dar es salaam, Tanzania

Haikuwa ligi ya mbuzi au bata ili uuone ni mpira wa nguvu kama ule wa ujerumani. Ila ilikuwa ni mechi ambayo bila vigingi, upaja na basi nguvu huna, utaishia kupitwa na wachezaji wa timu pinzani huku ukizidi kuwalainishia timu hiyo kupata ushindi.
Hiyo ndiyo mechi pekee iliyoweza kumtoa waziri wa michezo na utamaduni Jerome Kazara ofisini kwake, na kwenda nyumbani kabla ya kuelekea uwanjani kushuhudia nyasi za uwanja wa taifa zikiwaka moto kila mara timu hizi mbili za watani wa jadi zinapokutana.

Haikuwa mara ya kwanza kwenda kushuhudia timu hizi zikimenyana, ila ni mara ya kwanza kwenda katika uwanja wa taifa akiwa kama mbunge wa jimbo la kinondoni, na pia alibahatika kuchaguliwa na raisi kama waziri wa michezo na utamaduni.
Alijisikia fahari alipokuwa akipita katika barabara zile, jirani na uwanja wa taifa. Akisindikizwa na pikipiki yenye askari, ndani ya landcruiser v8 nyeusi, huku upepo wa kiyoyozi ukisaidia jezi yake ya timu ya taifa kuendelea kutoa Ile harufu nzuri ya marhamu. Marhamu maridhawa kutoka visiwa vya zanzibar aliyojifukiza punde wakati alipokuwa akitoka nyumbani kwake mikocheni.

Magari yaliegeshwa pembeni na watu walikaa mbali wakati ambao Jerome alipokuwa akiingia katika viunga vya uwanja wa Taifa.
Baadhi ya mashabiki waliovalia jezi za kijani walisikika wakipaza sauti zao
"Mchaka Mchaka chinja, alinselema kashindwa" Wao waliimba hivyo wakiwa na imani Jerome ni shabiki damu wa timu hiyo, yenye maskani yake pale Jangwani. Ila wale waliovalia jezi nyekundu wao waliendelea kuimba huku sauti za ngoma ya asili zikisikika
"Anaipenda simba shabiki wa damu"

Ukiachana na sauti za shabiki hao waliokuwa wakileta burudani mbalimbali nje ya uwanja huo ambao ulifurika watu wengi hata kuleta shida kiasi kwa gari ya Jerome kuingia, ilisikika sauti ya binti mdogo mwenye sinia la Mihogo mibichi kichwani mwake.
Jerome Kazara alimuona binti yule akijitahidi kujipenyeza katikati ya watu kulifuata gari lake. Alipomtazama binti yule alishusha zaidi kioo cha gari yake na binti yule aliisogelea gari ya Jerome. Ni hapo binti yule alipopigwa kikumbo na askari wa eneo hilo, mwenye farasi mkubwa aliyekuwa akimtembeza.

Jerome Kazara, waziri kijana katika serikali mpya ya awamu ya tano ya Raisi Joshua Bagenzi; waziri mwenye roho ya ujamaa na urafiki, alishuka kutoka katika gari yake na kumzuia askari yule asimfanye chochote binti yule; hiyo ikiwa ni kuonesha uzalendo wake.
Wakati kitendo hicho kikiendelea eneo lile likapigwa na ububu wa butwaa. Kila mmoja aliyekuwa amekusanyika hapo, alinyamaza akimtazama waziri yule aliyechutama mbele ya binti aliyekuwa akiokota vipande viwili vya mihogo yake iliyodondoka, huku Jerome akichukua pande kubwa la muhogo kutoka katika sinia lile la binti.

"Pole" Jerome Kazara alitoa noti ya shilingi elfu tano na kumkabidhi binti yule na kurudi ndani ya gari "Yote ni yako!" Mara watu wote waliokuwepo hapo, wakalipukwa na nderemo na vifijo vya furaha kwa kitendo alichokifanya waziri Jerome.
Wakati ambao alikuwa akitazama mtanange ule baada ya kuingia uwanjani, huku muhogo alionunua kwa binti ukiwa umeoshwa vizuri kisha kukatwa vipande huku kipande kimoja kikiwa kimekatwa vipande vinne na kumenywa maganda yake, kipande kimojawapo kati ya hivyo vinne ndicho alichokuwa akikitafuna taratibu.
Hakuutazama mpira ule mpaka mwisho kama alivyodhani na ni kipande kimoja tu cha muhogo alichoweza kukimaliza kwani ni wakati huo alipoanza kutokwa na jasho jingi akahisi ni kutokana na jua kuwa kali.

Akamnong'oneza kijana wake ambaye ni Lucas
"Siwezi kumaliza nisaidie" akanyanyuka kisha akatoka uwanjani na kumuomba msaidizi wake huyo kurudi katika vyumba vya watu muhimu au maarufu(V.I.P) Ni yeye pekee aliyejua kuwa anatembea kwa shida licha ya kujitahidi asioneshe kupepesuka au hali yoyote ya kushitusha. Akili ilimuuma kuwaza ni kitu gani kimemkuta. Hakuweza kupiga hatua nyingine kuufikia mlango akataka kudondoka, akashikwa kushoto na kulia kisha kuingizwa ndani na vijana wake. Alipowekwa kwenye kochi, ghafla Jerome alitokwa na damu puani mdomoni na masikioni, jambo Hilo liliwashitua sana wale vijana waliomuingiza ndani mkuu huyo.

Chumba kile cha watu maarufu, kilitembelewa na wageni wanne baada ya simu ya Lucas kuwa busy kwa kipindi kifupi cha tukio lile la Jerome Kazara. wawili wakiwa askari wa ngazi ya juu ambapo mmoja ni kamishina wa polisi Juma Faki na inspekta wa polisi Jimmy Francis; huku wageni wengine wawili waliobaki ni meneja wa uwanja wa taifa huyu akiwa ni mwanaume mmoja mfupi mwenye nywele chache kichwani, huku kitambi chake kikubwa Kikiwa kimeathiri uvaaji nadhifu wa mkanda ulioshuka chini kidogo ambapo suruali yake bwanga kuwa kama kanyea humo humo. Mmwera wa Ruangwa almarufu kwa jina la Maliyatabu na mgeni mwingine ni mwanamke mrefu mwembamba mwenye mwanya mpana ambaye ni daktari aliyevalia koti jeupe, huyu yeye huitwa Ladysubira.

Wote kwa pamoja waliwakuta Lucas na Muhime, ambaye ndiye dereva wa Jerome, wakihangaika kuyalaza maiti ya Jerome kwenye kiti kikubwa kinachofaa kukaliwa hata na watu watatu.
"Yamemfika yapi mheshimiwa?" Ladysubira alihoji akiwa anazivaa gloves zake
"Ajabu" Lucas ambaye ni msaidizi wake Jerome, akajibu huku akitazama viganja vyake vilivyojaa damu "Mwili ni baridi, cha ajabu zaidi mzee amefariki lakini bado ngozi au niseme mwili wake unaendelea kutoa jasho lenye damu"
 
Hakuna ambaye aliweza kuacha kutoa mguno wa kushituka, kwani mastaajabu hayo hayakubaki katika masimulizi ya Lucas tu hata macho yao yaliweza kuwathibitishia mabonge ya damu yaliyoganda katika tundu za pua za Jerome, damu zilizochuruzika masikioni na pia machoni zilizotoka kama machozi mazito.

Ladysubira aliinama kuyakagua maiti yale baada ya kuyatazama alisimama na kuwatazama Lucas na Muhime kisha akageuka kwa inspekta wa polisi Jimmy Fransic
"Huu sio ugonjwa wa kawaida kama mnavyofikiri?" akatoa kichupa kidogo cha kioo kilichofungwa vizuri na mfuniko mwekundu katika moja ya koti lake na kisha kuyainamia tena maiti yale na kuchota kiasi kidogo cha damu kwa ajili ya kuipima
"Mmefanya makosa makubwa kuishika maiti hii" Alipoyazungumza hayo alimtazama Lucas na Muhime huku akifunga kichupa kile na kutoka nje.

Baada ya Ladysubira kutoka nje, Lucas alikwishajikwaa baada ya kuanguka alipokuwa akikimbilia bafuni ambako alikuwa akiwahi kwenda kunawa kwa maji na sabuni, Muhime alitazama mikono yake iliyochafuka kwa damu kidogo, hakuna alichoweza kufanya lakini woga ulitosha kumuadhibu asisikie hata kiyoyozi kilichokuwa kikipuliza ndani ya chumba hicho, kwani jasho jingi lilimtoka.

Kamishina wa polisi Juma Faki, aliwakaribisha vijana wawili wauguzi waliokuja pamoja baada ya kupewa taarifa na uongozi wa uwanja wa taifa kutoka katika amri ya meneja wa uwanja huo.

"Vijana hawa pia wawe chini ya uangalizi wenu kulinda afya za wengine kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu" ilikuwa ni sauti ya amri aliyotamka Juma Faki baada ya ujumbe ule aliouacha Ladysubira wakati anatoka, kumtia hofu kisha na yeye alitoka huku akimuachia Inspekta Jimmy Fransic kusimamia zoezi hilo la Muhime na Lucas kuwekwa katika uangalizi wa kunusuru afya za wengine.

Maiti ya Jerome yalitolewa ndani ya chumba kile na kisha wakiwa wamevalia nguo maalumu, wauguzi wale waliwatoa Lucas na Muhime katika chumba katika uangalizi maalumu kama ilivyoamriwa

.....

Jimmy Francis inspekta katika jeshi la polisi, hakuweza kulala siku mbili mfululizo baada ya matukio ya ujambazi wa kutumia silaha kushamiri Dar es salaam katika benki mbili tofauti, huko ilala na tandika sokoni. Simu za mkuu wake wa kazi, mrakibu wa polisi Nundu Pembe, zilipokuwa zikiingia, ziliichefua nafsi yake na kuichukia nafasi hiyo ya mkaguzi wa polisi aliyoihenyea kwa muda mrefu mpaka kuipata.

Ni vipi alale ikiwa walinzi wazee waliopaswa kupumzika, wamekabidhiwa virungu kulinda benki wakipigwa risasi na kufa kama kuku huko nje? Je askari wake wawili waliokuwa wameuwawa katika majibizano ya risasi walipokuwa wakisafirisha kiasi kikubwa cha pesa?
Alipokuwa ameelemewa na maswali ya matukio hayo aliyopaswa kuwasilisha taarifa yake masaa kumi na mbili baadaye, simu ya Lucas akiwa na wahka ikamchanganya zaidi
"Tupo uwanjani"

Ni neno la mwisho alilosikia, kisha simu ilikatwa na alipotaka kuipuuza taarifa hiyo, simu yake iliita tena. Akasonya kwa uchovu, alipoangalia juu ya kioo cha simu yake, simu iliyokuwa ikipigwa ilitoka kwa Nundu Pembe. Sauti ya Sp (Mrakibu wa polisi) ambayo inakwaruza na kukera kutokana na amri zake za kuchosha, ilikoroma katika sikio la kushoto la Jimmy Fransic ambaye kutokana na mikiki mikiki ya kazi nzito mchana na usiku, alipitiwa na wazo la kuikacha kazi hiyo ya upolisi.

"Unanyoosha miguu ofisini inspekta mzima wa polisi na waziri wako anakufa uwanjani?"
"Unasema!? kufa? waz.." alipigwa na butwaa kwani ni jambo hilo hilo ambalo lilimkatishia usingizi baada ya simu ya Lucas kuingia alipokuwa amejiegemeza katika kiti chake ofisini.
Akajitetea

"Bado nilikuwa naandika ripoti ya vifo vya wale askari wawili vilivyotokea kule tandika sokoni mkuu" alijibu kwa sauti iliyopwaya na kukata tama
"Iache hiyo kazi mara moja, nimepokea ujumbe kamishina wa polisi ametangulia katika eneo la tukio ni aibu bosi wako kutangulia katika eneo la kazi wewe ukinywa kahawa kwa starehe halafu unanidanganya unaandika ripoti isiyo na ushahidi wa wauwaji kukamatwa"
Hivyo ndivyo taarifa ya kifo cha waziri Jerome Kazara ilivyomkuta akiwa na uchovu mwingi na mlundikano wa mawazo uliomfanya kukata tamaa kabisa. Alirudi ofisini kwake Osterbay police na kupokelewa na waandishi wa habari katika benchi nje ya ofisi yake.
"Mheshimiwa sisi ni.."

Hakumaliza kuongea yule aliyejitia ni kimbelembele, sauti ya Jimmy Fransic iliwatosha kuwajibu kuwa hakuhitaji usumbufu wowote kwa wakati huo
"Sipo tayari kuzungumza chochote kwa sasa na wala msiniulize kitu kingine chochote" Aliingia ofisini kwake na kumpita katibu muhtasi wake kama vile hakumuona, na kufunga kwa ufunguo ikiwa ni ishara haitaji usumbufu wowote.

Rhoda Mbusule alimfahamu vyema bosi wake baada ya kuona hivyo hakujisumbua kumuaga hata muda wake wa ofisi ulipoishi alijikung'uta na kuondoka zake kimya kimya.
Ndani ya ofisi yake, Inspekta Jimmy alijitengenezea kahawa chungu kwenye kikombe chake kikubwa na kukiweka mbele ya meza yake pana iliyojaa karatasi mbalimbali. Baada ya kupiga funda moja la kahawa ile, alitazama juu kuangalia pangaboi iliyozunguka kivivu na kuzama kwenye tafakuri ya mambo mbali mbali aliyopata kuzungumza na Lucas wakati ambao alikuwa amepelekwa hospitali chini ya uangalizi wa Ladysubira.

"Ghafla tu mheshimiwa aliniambia anajisikia vibaya kwani hata mimi nilimuona akiwa anatokwa na jasho jingi sana wakati ule ambao tulipokuwa uwanjani na baadaye nilipokuwa nikimpeleka chumba cha VIP ndipo alishindwa kutembea kutokana na kutembea akiwa anapepesuka mpaka tulipomuingiza katika chumba kile akiwa hajitambui na damu zinamtoka katika Kila tundu la mwili wake. Kutokana na hali ile ndipo nilimpigia mzee Faki kutokana na ukaribu wa kirafiki alionao na mheshimiwa".

Kwa kuwa hakuna alichokipata kutoka kwa Lucas, Jimmy alitoka na kwenda kwa Ladysubira aliyekuwa akimfanyia uchunguzi Jerome
"Kuna chochote cha kutilia shaka ulichoweza kugundua kutoka katika mwili wake?"
"Hakuna jeraha lolote wala hakuna kitobo chochote lakini kikubwa ninachoweza kukuambia, mheshimiwa alilishwa Sumu"
"Sumu?"
 
Cjaipenda kabisa..
Haijakaa ki Engineer...

[HASHTAG]#Chief[/HASHTAG] Eng
 
Back
Top Bottom