riwaya mpya; BALAA


holygrail

holygrail

JF-Expert Member
Joined
Mar 24, 2012
Messages
1,238
Likes
166
Points
160
holygrail

holygrail

JF-Expert Member
Joined Mar 24, 2012
1,238 166 160
RIWAYA:BALAA
MTUNZI: Ibrahim GAMA SEHEMU YA KWANZA “Mahabusu na
Wafungwa simamaaaaa,
kofiaaaaaa towaa! Selo
salama kabisa Bwana
mkubwa , tupo tayari
kwa mafungio. Tunafungiwa mahabusu
mia mbili , na
wafungwa watano,
jumla miambili na tano,
Selo namba Mbili mkuu”
Ilikuwa ni sauti ya Nyapala wa
Kimahabusu, katika
Gereza la Mahabusu la
Segerea, akiwainua
mahabusu waliokuwa
wamekaa kitako, wakiwa katika mistari
ya watu kumikumi,
huku wakiwa vidari
wazi, yaani wamevua
shati na fulana zao,
tayari kwa kufungiwa ndani ya Selo, muda huo
ikiwa ni saa kumi alasiri
juu ya alama!!!
Askari Magereza,
mwenye zamu yake ya
kufungia, akiwa na askari wenzake wengine
wapatao kumi, alikuwa
makini na kifimbo
chake, akiwahesabu
wale mahabusu,
waliokuwa wakiingia ndani ya Selo, kwa
mwendo wa mbio,
mmoja baada ya
mwengine, hadi mtu wa
mwisho kuingia ndani
ya Selo ile, ambae ni Nyapala wa Kifungwa
aliposema kwa sauti,
akithibitisha ile hesabu,
aliyoitoa Nyapala wa
Kimahabusu! “Hapa
salama kabisa bwana mkubwa, tunafungiwa
wafungwa watano, na
mahabusu mia mbili,
jumla mia mbili na tano,
selo namba mbili bwana
mkubwa!” Baada ya kuingia ndani,
ya Selo ile, ambayo
imepewa uwezo wa
kulala watu wasiyozidi
hamsini, lakini
wanalazwa Mahabusu hadi mia tatu,
kutegemea na wingi wa
wahalifu, hasa kipindi
cha sikukuu, na mwisho
wa mwaka!
Askari magereza, aliifunga kufuli nje ya
mlango wa Selo ile,
kisha akaja askari
mwingine kuhakikisha ,
kama kufuli ile
imefungwa sawasawa! Askari wale walifungia
kwa utaratibu ule, hadi
walipomaliza kufungia
Selo namba tisa, ambayo
ndiyo ya mwisho
kufungiwa katika upande ule wa Rumande
wing, katika Gereza lile.
Ndani ya Selo ile namba
mbili, maarufu kwa jina
la ‘Spear’, ambayo ndiyo
imepangwa mahususi kwa ajili ya kuchukua
Mahabusu wageni,
ambao kwamba huwa
ndiyo mara yao ya
kwanza, kuingia
gerezani. Hivyo Selo ile ndiyo pekee iliyoteuliwa
na Afisa usalama, ili
wageni wa jela kupewa
maelekezo na taratibu
za kuishi ndani ya
Gereza! Alisimama kijana
mmoja, aliekuwa na
cheo cha askari Selo, na
kupiga makofi. (ASKARI
SELO NI MSAIDIZI WA
NYAPALA NDANI YA SELO ) Na mara kimya
kikatawala Selo nzima!
Hiyo ndiyo taratibu ya
kutaka utulivu, watu
wanyamaze ili itolewe
taarifa ndani ya Selo. Na baada ya utulivu
kupatikana, Yule Askari
Selo akasema. “Oyaa
sikia hiyoo. Kama wewe
unajijuwa umeingia leo
ndani ya Gereza, au uliwahi kuingia ukatoka
na leo umerudi tena,
twende mbele kule
ukapate maelekezo. Sasa
wewe kaa usitoke
mbele, halafu uyakanyage uone hapa
unapigwa Salala, kisha
kwa Meja nakupigisha
Rungu nyingi! Na humu
utaita taa hadi ishuke
chini ikufate” (SALALA) alikuwa anamaanisha
kofi la mgongo,
linalopigwa kwa mikono
miwili, kwa Mahabusu
aliekosa kufata taratibu!.
(Kuita taa, ni kusimama wima kisha unanyoosha
mikono yako juu usawa
wa taa ilipo unafumba
na kufumbua vidole
vyako mithili unamwita
mtu kwa ishara ya mkono!)
Mahabusu arubaini
waliinuka, na kuenda
mbele, ili kupata
maelekezo kwa Yule
msaidizi wa Nyapala au Askari Selo, kama
anavyopenda kuitwa
hivyo!
Walipokuwa wote
wamekaa na Selo, ikiwa
katika utulivu, yule askari Selo, alianza kwa
kuwajulia hali wale
wageni! “Habari zenu
wezi?!” Na wale wageni
ambao siyo wote
walioingizwa gerezani kwa kosa la wizi, lakini
waliitikia kwa pamoja
“Poa Mwizi!”
Kisha Yule Askari Selo,
akaendelea. “Sema nini,
humu ndani ya Selo tunataka heshima,
tuwaheshimu viongozi
wetu kwani wao ndiyo
jicho la askari Magereza.
Askari wao wamelala
majumbani kwao, sisi tumefungiwa humu
ndani kama kuku!” Yule
Askari Selo alikuwa
akizungumza huku
akiwatazama, wale
Mahabusu wenzake waliokuwa wamekaa
mbele yake ili kutambua
kama walikuwa
wanamuelewa
sawasawa! Baada ya
kuridhika kuwa wanamsikiliza
akaendelea. “Humu
ndani ya Selo yetu
namba mbili, tuna
viongozi ambao
mnatakiwa muwafahamu, ambao
wanastahili heshima!
Ambao ni Nyapala wa
kimaabusu, na Nyapala
wa Kifungwa. Mkisha
pewa maelekezo mtaoneshwa mahali
walipo ili
muwatambue.”
Yule askari Selo
alisimama kidogo, kisha
akaendelea. “Pia tuna kiongozi mwengine
mwenye cheo cha
Bwana Afya humu ndani
ya Selo. Yeye ndiye
anaetugawia maji ya
kunywa humu. Kwani bila ya yeye kuwepo na
kugawa maji katika
utaratibu, tungeweza
kugombea na asiye na
nguvu asingeweza
kudiriki kunywa maji! Pia yupo kiongozi
mwengine mwenye
cheo cha Kilina, yeye
anahakikisha vyoo
vinakuwa safi, na kwa
kuwa maji ni tatizo katika Gereza letu la
Segerea, ukisha kwenda
haja kubwa, kuna fimbo
pale pembeni tunaiita
mchokocho. Unatakiwa
baada ya kwenda haja kubwa, utapiga
mchokocho, kwa maana
ya kuponda kinyesi
chako, hadi kilainike
kiwe uji, ili uweze
kutumia maji machache kuondosha kinyesi. Sasa
wewe nenda kanye
kisha usipige
mchokocho uone
utakachofanywa! Humu
ndiyo mwana ukome jeuri uache kwenu!”
Yule askari Selo
alisimama kidogo
kuzungumza, kwani
alisikia minong’ono
ikizidi na kufanya kelele kutoka kwa baadhi ya
mahabusu wenyeji,
waliokuwa hawana
habari kabisa kama
wapo jela, walikuwa
wakiongea na kucheka kama hawana kesi
zinazowakabili! Mara
makofi yalipigwa na
Nyapala wa Selo, na
ghafla Selo yote ikawa
kimya kama hakukuwa na watu mle ndani ya
Selo! Kisha Yule Nyapala
akazungumza kwa ukali.
“Oyaa sema nini
mnazingua bwana,
wenzenu wanaelekezwa kaeni kimya, nyie
mmeshakuwa vijelajela,
mnakwenda na kurudi
humu nje hamna maisha
hamkai, siyo mnatupigia
kelele bwana, sasa nateuwa Kihelehele
akamate kesi, sasa
wewe kaidi, halafu
ukamatwe na Kihelehele
unapiga kelele uletwe
kwangu uone, wewe ndiyo utakuwa funzo
kwa wenzako mimi
nimeletwa na kesi
yangu humu, sikuja na
mtu!”
Nyapala baada ya kusema maneno yale,
akamteuwa mtu mmoja
wakuitwa Dubwi
Santana, ambae katika
jela na Selo ile,
aliaminika kuwa mnaa sana! Akapewa kazi
yakuwa Kihelehele
akamate kesi! Dubwi
Santana alisimama
akazungumza.
“Santana hapa, nishapewa rungu na
Nyapala, kuanzia sasa
hakuna kuzungumza
hakuna kumokee!
(KUMOKEE NI KUVUTA
IWE BANGE AU SIGARA) Hapa ni mwendo wa
kimya hadi Nyapala
atengue cheo changu,
bwanabwana wewe
unaejifanya unanijua,
ukataka kuniletea shobo, mbona nitakuzingua,
mie nuksi halafu
sijasingiziwa! Mie ni
mwizi na nje naiba
kweli yaani wazazi
wangu wenyewe hivi mie kuwa huku wao
wanaombea nisitoke
sasa wewe zingua uone
mbona nitakukomesha,
kwanza mie sina ndugu
humu nimekuja peke yangu na kesi zangu!
Askari Selo endelea
kuwapa maelekezo hao
mafresh huku hakuna
Briman wala Blue yeyote
atakaezingua hawa ni wanyonge tu,
wanaranda nje siyo
humu hawa wachumba
tu!!!”
Baada ya Dubwi Santana
kupiga mikwala mingi, Selo ikarejea katika
utulivu mkubwa. Na yule
askari Selo Baada
yakuona wale mahabusu
wageni walikuwa wapo
makini kumsikiliza, akawataka wale
mahabusu kila mmoja
akifika kwa Nyapala wa
Selo ataje kesi yake
kama alivyosomewa
mahakamani, pia ataje mahakama ilipo kesi
yake, na jina la
Muheshimiwa Hakimu
wake, aliemsomea
shitaka.
“Oyaa hapa usiseme nimesingiziwa, taja kesi
yako kama
ulivyosomewa
mahakamani, kesho
mtapoitwa kwa ajili ya
kuandikisha urithi, utaulizwa kesi yako na
askari magereza. Sasa
wewe ukisema
umesingiziwa kesi,
utachezea rungu hadi
magoti yajae maji hayo tumeelewana?”
Yule askari Selo,
alizungumza huku
akimalizia kwa swali. Na
wale mahabusu wageni
‘Fresh case’ wote kwa pamoja wakaitikia kwa
pamoja “ndiyooo.”
Yule askari Selo, alimfata
Nyapala wa
Kimahabusu, na
kumwambia. “Kiongozi wezi wapo tayari kwa
kukuona, nimeshawapa
maelekezo, hivyo
nawaleta waje
wakutambue na wewe
uwatambue!” Yule Nyapala wa Selo namba
mbili, alimuashiria
askari Selo wake,
awalete wale wageni ili
azungumze nao. Na
mara moja ikatendeka hivyo wale Mahabusu
wageni, wakawa
wanatazamana uso kwa
uso na Nyapala wa Selo.
“Habari zenu?” Nyapala
wa Selo aliwasalimia wale wageni wa Jela, na
baada yakuitikiwa
akaendelea kusema.
“Poleni sana ndugu
zangu, nawasihi mfate
taratibu za gereza, mtatoka salama bila
kupigwa hata kofi, lakini
kama mtakaidi yale
mliyoelekezwa,
mtaumia kwa vipigo na
kupata ulemavu wa Rungu za askari
Magereza. Mkiwa humu
ndani gerezani,
ondoweni kabisa
mawazo ya wake na
wachumba wenu mliowaacha nje! Hao
mkiwafikiria sana
mtaumiza nafsi zenu
bure. Kwani huku
unatakiwa ufikirie kesi
yako iliyokuleta humu tu acheni kabisa kuwaza
vitu ambavyo
vitawaletea msongo wa
mawazo. Jela
kajengewa binaadam na
hata wale ambao sasa hivi wapo nje wakiwa
raia wema na huru, nao
pia ni mahabusu na
wafungwa watarajiwa!
Kwani wanaweza siku
yoyote wakaletwa gerezani bila kukusudia!
Kwani siyo wote
tuliyopo humu kama ni
waalifu kweli, wengine
wameletwa kwa bahati
mbaya tu!” Alinyamaza kusema yule
Nyapala akitaka
kufahamu kama
anaeleweka. Baada
yakuona anasikilizwa
barabara, akawataka wale Mahabusu wataje
kesi zinazowakabili
kama walivyosomewa
mahakamani na Hakimu.
“Nataka mnitajie majina
yenu kamili, kesi zinazowakabili na
mahakama
uliyosomewa kesi hiyo.”
Wale mahabusu wageni,
mmoja baada ya
mwengine, walikuwa wakitekeleza agizo lile,
hadi kufikia kwa mtu
wa Arobaini
alipojitambulisha.
“Mimi naitwa Athumani
Dobe, Mahakama yangu ni mahakama ya mkoa
Kisutu, Kesi yangu ni
Mauaji, Nashitakiwa
kwa kumuua Mauwa
binti Simba Makupa,
hakimu wangu ni ……..!!!” Athumani Dobe
hakuweza kutaja jina la
Hakimu wake, kwani
uchungu ulimjaa
moyoni, donge
likamsugua na machozi yakamtiririka
mashavuni mwake, kilio
cha kwikwi kikamshika
hatimae akalia kwa
sauti iliyohuzunisha
kuisikiliza! Akazama katika lindi la mawazo.
Ama kweli mtu mzima
ukimuona analia, basi
ujue kuna jambo! Ni
kweli. *******
ZANZIBAR MWAKA 2006.
Upepo mkali ulikuwa
ukivuma kutoka kusini
kuelekea kaskazini,
watu wa pwani huita pepo za Kusi. Mji wa
Unguja ulikuwa safi na
upepo ule ulikuwa ni
burudani kwa watalii
wengi waliokuwa katika
Bandari ya Unguja kuelekea katika mji wa
Dar es salaam. Wasafiri
wengi walikuwa katika
hekaheka za kusafiri,
katika muda ule wa
Alasiri. Boti ya Sea Express,
ilikuwa inapakia mizigo
kabla ya kupakia abiria
waliokuwa
wamesheheni pale
Bandarini, wakiwa na wahaka wa safari.
“Wale abiria wenye
tiketi wanaosafiri na
boti yetu ya Sea Express,
kuelekea D’salaam
mnaombwa kupanda chomboni, muda wa
safari umekaribia.” Sauti
ya kike ya mfanyakazi
wa Boti ya Sea Xpress,
ilisikika katika kipaza
sauti na msururu wa abiria ulielekea katika
boti ile kwa ukaguzi na
kupanda chomboni.
Saa kumi kamili boti ile
ilifunga milango yake,
na safari ya kuelekea katika Jiji la Dar es
salaam ikaanza.
“Kaka yangu samahani,
naomba hilo jarida
nisome, kwani kuna
hadithi naifatilia humo yaani sitaki kuikosa.”
Ilikuwa ni sauti ya Abiria
mmoja mwanamke,
aliekuwa amekaa karibu
kabisa na Abiria
mwenzake mwanaume, huku boti ikiwa imeanza
safari, ikiitafuta Chumbe
kuelekea bandari
salama!
“Ohoo haina shida soma
tu mimi nitaangalia filamu katika video pale,
kwani hii filamu ya
KABIKUSH KABIGHAM,
naipenda sana hilo jarida
mie nitasoma
nyumbani.” Alijibu Yule abiria wa kiume huku
akimkabidhi lile jarida la
Ndoto.
Muhudumu wa Boti ile,
alikuwa akipita na
mifuko ya plastiki akigawa ndani ya boti
ile, kwani bahari
ilichafuka na wale abiria
ambao siyo wenyeji wa
bahari, wanaweza
kutapika sana! Hivyo ilikuwa rasmi mifuko ile
kwa kutapikia. Alipofika
katika usawa wa Yule
dada aliekuwa akisoma
lile jarida la Ndoto, Yule
abiria wa kiume alimchukulia Yule dada
mfuko, yaani alichukua
mifuko miwili! Kwani
yule dada alikuwa
amekazana macho yake
katika jarida lile, hakuwa na habari ya
mifuko.
Boti ile ilishika kasi,
kuitafuta bandari ya jiji
la Dar es salaam maarufu
ikijulikana kwa jina la Bandari salama.
Mwendo kasi wa boti,
wimbi kali na upepo wa
Kusi uliokuwa ukivuma
kwa kasi kubwa, uliitesa
sana Boti ile, kiasi ilisukwasukwa na
wimbi kubwa, kiasi
ikatibua matumbo ya
wasafiri, na wale
wageni wa bahari, mara
wakaanza kuhisi kichefuchefu, vilio kwa
watoto vikasikika. Yule
dada aliekuwa akisoma
jarida aliacha kusoma,
akawa amejiinamia
hasemi, mdomo wake ulijaa mate, tumbo
lilitibuka na akahisi
kutapika. Yule abiria wa
kiume alimpa mfuko
mmoja wa plastiki ili
atapikie mle, na kweli alitapika hadi nyongo!
Ule mfuko ulijaa, na Yule
abiria wa kiume akampa
ule mfuko mwengine,
nayeye akaenda kuutupa
chooni ule mfuko uliojaa matapishi ya Yule dada!
Baada ya kama saa moja
na nusu, wakiwa
wamebakisha nusu saa
kufunga gati, katika
Bandari salama, Jiji la Dar es salaam lilikuwa
linaonekana kwa karibu,
wakiwa maeneo ya
kunduchi. Yule dada sasa
akiwa ametulia na
bahari ikiwa imetulia, akamuomba Yule kaka
simu yake ya mkononi.
“Kaka yangu samahani,
naomba niazime simu
yako nitume ujumbe
sehemu.” Yule kaka bila kinyongo, alimkabidhi
simu ile huku nae
akimwambia. “Piga
kabisa tu, kwani simu
hiyo ina pesa za kutosha
humo!” Yule dada huku akitabasamu akamjibu.
“Asante sana ila ujumbe
tu mimi unanitosha.”
Baada yakusema
maneno yale aliandika
ujumbe wake, kisha akautuma
alipoukusudia, majibu
yakarudi kuwa ujumbe
ule umefika
ulipokusudiwa, kisha
akaufuta ujumbe ule katika simu ile, kule
kwenye sehemu ya
kutuma ujumbe, pia
akafuta na ule ujumbe
uluorudi kuonesha kuwa
ujumbe ule umefika, na alipomrejeshea simu
yake Yule kaka, kukawa
hakuna ujumbe
uliobakia katika simu ile!
“Samahani dada naomba
tufahamiane, Mimi naitwa Athumani Dobe,
nakaa Mwananyamala
Komakoma,
mwenzangu unaitwa
nani?” Yule dada huku
akitabasamu kwa aibu, nae akajitambulisha.
Mimi naitwa Mauwa
Bint Simba Makupa,
nakaa Mtaa wa Swahili
Kariakoo, upande ule wa
pili kama unaelekea Muhimbili.” Alijibu
Mauwa huku akiwa
hamtizami usomi
Athumani Dobe.
“Ahaa asante sana bi
Mauwa, Unguja kwa nani wako?” Athumani
Dobe, alimuuliza swali
lingine na Mauwa
akamjibu.
“Kule ni Kwa Baba yangu
Mdogo anaeitwa Haruna Makupa, nimekwenda
kuna kitu kuchukua, na
nilienda juzi leo ndiyo
narudi, mimi makazi
yangu ya kudumu ni Dar
es salaam.” Alizungumza Mauwa katika utulivu
mkubwa. “Je nikitaka
kukutafuta nakupataje?”
Athumani Dobe alianza
kurusha ndoana yake,
akakutana na Samaki mbishi! “Mmmh mimi
kwetu geti kali, yaani
mimi ni ndani, ndani na
mie sina muda hata wa
kwenda sokoni! Mungu
akipenda kama hivi tulivyoonana, basi
naamini tutakutana
tena!” Mauwa alimjibu
Athumani, huku
akimkabidhi lile jarida
lake la Ndoto, pia akitoa shukurani kwa kusoma. ITAENDELEA KESHO……
USIKOSE!!!
 

Forum statistics

Threads 1,250,604
Members 481,419
Posts 29,738,564