Ridhiwan punguza kasi

Mallaba

JF-Expert Member
Jan 30, 2008
2,554
47
WAKATI mamilioni ya Watanzania wakiendelea kusubiri matokeo ya kura za urais, kuna mambo yameanza kujitokeza ambayo yanaonyesha kuwapo kwa kasoro kadhaa.
Moja ya kasoro ya kwanza kujitokeza kabla ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijatangaza matokeo hayo ni kile kinachoelezwa kuwa ‘uchakachuaji’ dhidi ya kura za mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.
Jana vyombo vya habari mbalimbali vilipambwa na habari za Dk. Slaa kuwa NEC imekuwa bingwa wa kuchakachua matokeo, tofauti na mategemeo ya wengi.
Dk. Slaa alitoa madai hayo mazito akiihusisha Idara ya Usalama wa Taifa, kuwa ni moja ya sehemu za serikali iliyohusika na wizi wa kura katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema anasikitishwa na tofauti zinazotangazwa na NEC, wakati matokeo ya vituoni yanaonekana kuwa tofauti kabisa, hali iliyosababisha kuiomba jumuia ya kimataifa kuingilia kati haraka.
Mbali ya kuitaka jumuia hiyo, Dk. Slaa ameitaka NEC kusitisha mara moja kuendelea kutangaza matokeo hayo ambayo yanaweza kuleta athari katika jamii.
Leo mada kuu katika makala hii, inamhusu mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwan, ambaye kwa siku za karibuni ameonekana kuwa mwiba kila kona ya nchi hii.
Juzi wakati Dk. Slaa anatoa kilio hicho, Ridhiwan bila aibu naye aliibuka na kudai kuwa Slaa ameonyesha dalili ya kushindwa kwenye kinyang’anyiro.
Nilisikitishwa na kauli ya Ridhiwan kwa sababu yeye si mmoja wa wagombea wa urais, bali ni mtoto wa mgombea, sasa iweje atoe kauli zisizokuwa na msingi?
Anasema Dk. Slaa ameanza kutapatapa kutokana na imani yake kwamba mikutano yake ilikuwa inajaza watu wengi ambao aliamini watampigia kura.
Naamini Ridhiwan katika umri mdogo aliona nao hivi sasa amegeuka kuwa mwiba mkali katika maeneo mbalimbali, si ya siasa tu, bali hata kwenye sekta ya michezo, amekuwa bingwa wa kuendesha propaganda kila kukicha.
Ridhiwa huyu huyu leo anaibuka na hoja mfu, anataka kuwafanya Watanzania ni mazezeta, nani asiyetambua yeye, baba na mama yake walivyopiga kampeni za kifamilia katika taifa hili? Hatuwezi kukubaliana na porojo zake hizi hata kidogo.
Ridhiwan amekuwa bingwa wa kuendesha siasa chafu dhidi ya watu ambao wanaonekana kuwa tishio ndani ya taifa, amekuwa akitumia vibaya kofia ya baba yake ya kuwa madarakani.
Jeuri ya aina hii tuliiona hata kwenye uchaguzi wa klabu ya Yanga jinsi alivyoweka mkono na kuendesha kampeni chafu za hadharani za kumwangusha mgombea uenyekiti wa klabu hiyo, Francis Kifukwe.
Alitumia jeuri yake kumkampenia Llyod Nchunga, ambaye aliibuka na ushindi, licha ya wanachama karibu wote walikuwa wanamtaka Kifukwe. Haya yote ni matokeo ya Ridhiwan, tunajua vizuri.
Kutokana na adha hiyo, Kifukwe aliamua kujitoa, kitendo ambacho Ridhiwan alikipokea kwa shangwe na kuona amefanikiwa na swahiba wake Nchunga akaibuka na ushindi, akaona malengo yake yametimia.
Lakini umefika wakati sasa Watanzania tuanze kuhoji kuhusu jeuri hii ya watoto wadogo wa viongozi kujifanya wao ndio wao katika jamii, hatutaki kumuonea mtu, bali kila mmoja atahukumiwa kwa matendo yake.
Nani asiyetambua jinsi Ridhiwan alivyofanya kampeni za ndani kwa ndani nchi nzima na kuwatolea maneno yasiyofaa baadhi ya viongozi wa CCM aliokutana nao mikoani?
Haya tunayaelewa wazi, tabia hii sasa inataka kugeuza uongozi wa nchi kuwa kama familia ya kifalme. Hatujafika huko. Punguza kasi mdogo wangu!
Mbona marais wastaafu; Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi wameondoka madarakani salama, hatukuona watoto wao wakiwa na mambo ya ajabu kama Ridhiwan.
Mzee Mwinyi ana mwanae ambaye ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, hata siku moja hatujawahi kuona anaendesha mikakati mikali ya siasa namna hii au kuwa na makundi ya ajabu ajabu. Hapa kinachotakiwa ni watoto wa viongozi kuwa na uadilifu.
Leo kama Watanzania wakiamua kuhoji ni nani aliyetoa mamilioni ya fedha kumfadhili yeye na wapambe wake kuzunguka nchi nzima, atawajibu nini? Tunasema, Waswahili wana msemo: ‘Kila jambo lina mwanzo na mwisho’. Hatutaki kuzalisha tawala za kibabe za kina Augusto Pinochet, marehemu Omari Bongo (Gabon) na wengine wengi.
Napenda kumshauri Ridhiwan aache kuingilia mambo makubwa ambayo si ‘saizi’ yake. Bado ni mwasiasa mchanga mno, angekuwa mgombea urais ningemwelewa.
Enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hatukuwa na wanasiasa ‘uchawara’ wa aina hii, ambao wanatanguliza masilahi yao badala ya taifa.
Namalizia kwa kusema, umefika wakati ngoma za wakubwa waachiwe wakubwa wacheze wenyewe, watoto wakae kando. Watanzania wamepiga kura ambazo zitaamua nani atakuwa kiongozi wao. Hatutaki kuona amani, umoja na mshikamano uliopo unaharibiwa na kikundi cha watu wachache, tena wasiokuwa wagombea urais kama Ridhiwan. source:freemedia:A S cry::sad::evil::cool:
 
Back
Top Bottom