RICH DAD, POOR DAD by Robert T. Kiyosaki

Konzo Ikweta

JF-Expert Member
Oct 3, 2013
735
1,464
UTANGULIZI unaendelea...

Kama mhasibu, niliona kucheza mchezo unaohitaji taarifa ya mapato (income statement) na mizania (balance sheet) ilikuwa rahisi sana. Kwa hiyo nilipata muda wa kumsaidia binti yangu na wengine kwenye ile meza yetu hasa yale maneno ya kihasibu ambayo hawakuwa wanayajua. Mimi pekee kwenye meza ndie niliyefanikiwa kutoka nje ya ' Rat Race' siku ile. Nilitoka ndani ya dakika 50 ingawa mchezo uliendelea kwa masaa 3.

Kwenye meza yangu kulikuwa na mkurugenzi wa benki, mmiliki wa biashara na anayehusika na programu za kompyuta. Kilichokuwa kinanisumbua hasa ni jinsi hawa wataalamu walivyokuwa na ufahamu mdogo sana kwenye masuala ya uhasibu na uwekezaji, wakati ni masomo muhimu sana maishani mwao. Nilikuwa nashangaa hivi wanawezaje kusimamia uchumi wao binafsi kwenye maisha yao halisi. Binti yangu (miaka 19) akisema sielewi, yeye namwelewa anachomaanisha, lakini hawa wengine sikuwaelewa kwani walikuwa wameshakuwa watu wazima kiumri.

Baada ya kukaa nje ya mchezo kwa masaa mawili huku nikiwaangalia binti yangu na wale watu wazima, nilikuwa nafurahia wanavyojifunza ila nilishindwa kuwaelewa wale watu wazima wanavyoshindwa kujua mambo hata ya msingi ya uhasibu na uwekezaji. Walishindwa kuona uhusiano iliopo kati ya taarifa ya mapato (income statement) na mizania (balance sheet). Waliponunua na kuuza vitu hawakuweza kukumbuka kwamba hayo manunuzi yangeweza kuathiri kipato chao. Nilitafakari hivi kuna mamilioni wangapi ambao wanapata hii tabu kifedha kwa sababu tu hawajawahi kufundishwa haya masomo?

Baada ya muda tulipewa mapumziko.

Kwenye like kundi, Mfanyabiashara hakuwa na furaha kabisa. Hakuupenda ule mchezo. " Sihitaji kujua mambo haya yote," alisema kwa sauti. "Ninaajiri wahasibu, wakurugenzi wa benki na mawakili kunielewesha mimi kuhusu haya mambo ya kifedha."

"Hujagundua ndio maana wako wahasibu wengi ambao sio matajiri?" Robert alimjibu. "Pia wakurugenzi wa benki, mawakala wa hisa na wale mawakala wa majumba. Wanajua vitu vingi na wako maridadi kabisa, lakini wengi wao sio matajiri. Kwa sababu shule zetu huwa hazifundishi kile matajiri wanachokijua, hivyo tunalazimika kuchukua ushauri wao hawa. Lakini siku moja ukiwa unaenda kazini ukakwama kwenye foleni na hujui utafika saa ngapi huko kazi ni na ukatupa macho kulia ukamwona mhasibu wako nae amekwama kwenye hiyo foleni, ukatupa macho kushoto ukamwona mkurugenzi wa benki nae kakwama. Hii inatakiwa ikupe ujumbe wa kufikirisha sana.

Mtaalamu wa programu za kompyuta nae hakuvutiwa kabisa na huu mchezo, akasema, " nitanunua programu ya kompyuta inifundishe haya yote."

Mkurugenzi wa benki yeye alivutiwa, akasema, "niliyasoma haya nikiwa shuleni, lakini sikuwahi kujua jinsi ya kuyatumia kwenye maisha halisi. Sasa nimejua. Natakiwa nitoke hapa kwenye 'Rat Race'."

Lakini niliguswa sana na maneno ya binti yangu, ambaye alisema, "nimefurahia kujifunza, nimejifunza sana jinsi pesa inavyofanya kazi na jinsi ya kuwekeza."

Akaongezea, "sasa najua naweza kuchagua fani ambayo itaniwezesha kufanya kazi ninayoipenda na sio kwa ajili ya usalama na maslahi au kiasi ninacholipwa kwenye ajira. Kama nikifanikiwa kujifunza kile kitu huu mchezo unachofundisha, basi nitakuwa huru kufanya na kusoma kile moyo wangu unachopenda na sio kusoma fani nyingine ambazo biashara inazihitaji. Nikijifunza hivi sitakuwa na hofu ya usalama wa ajira kama walivyo wanafunzi wenzangu."

Tulipata mapumziko na baadae tuliendelea na majadiliano.

Mimi na mume wangu tulipanga kuwa na chakula cha pamoja na Robert na mke wake. Ingawa tulikutana kwa mara ya kwanza, mazungumzo yetu yalikuwa kama tumejuana kwa miaka.

Tuligundua tunafanana vitu vingi. Tulijadiliana sana kuhusu jinsi waamerika wengi wanavyostaafu wakiwa hawana kitu au kama wanacho ni kidogo sana kwa ajili ya usalama kijamii na afya zao. Na tulijiuliza kama watu wengi wanafahamu kuwa ni hatari sana kutegemea mafao pekee.

Yeye Robert alikuwa na wasiwasi jinsi kulivyo na ufa mkubwa unaendelea kukua kati ya walio nacho na wasio nacho huko Marekani na duniani kote.

Robert, mjasiriamali aliyejifunza mwenyewe ambaye amesafiri duniani na kukusanya uwekezaji wake pamoja aliamua kustaafu akiwa na miaka 47. Alitoka kwenye kustaafu kwa sababu na yeye alikuwa anahitaji pia kujifunza kuhusu fedha kama Mimi nilivyokuwa nahitaji kwa ajili ya watoto wangu. Alifahamu kuwa dunia imebadilika lakini elimu bado haijabadilika. Kutokana na Robert, yeye anasema, watoto wanatumia miaka mingi kujifunza elimu kwa mfumo wa kizamani sana, wakijifunza masomo ambayo hawatakaa wayatumie kamwe, huku wakijiandaa kukabiliana na dunia ambayo haipo!

"Leo ushauri hatari sana unaoweza kumpa mtoto ni ' nenda shule, pata maksi nzuri za juu na utafute kazi nzuri yenye maslahi.'" anapenda kusema, "huo ni ushauri wa kizamani. Kama ungeona kinachotokea kule bara la Asia, Ulaya na Amerika kusini ungejali kama nilivyo Mimi."

Yeye anaamini ni ushauri mbaya, " kwa sababu kama unapenda mtoto wako awe na usalama kiuchumi hapo baadae, huwezi kucheza na hizo kanuni za kizamani. Ni hatari sana."

Nikamwuliza ana maana gani kuziita " kanuni za kizamani?"

"Watu kama mimi huwa tunacheza kwa kanuni tofauti na hizo mnazocheza nyie," alisema.

"Nini huwa kinatokeaga pale shirika linapotangaza kupunguza matumizi ili liwe imara kiuchumi?" Aliniuliza.

"Watu hupunguzwa," nilimjibu. "Familia zinaumizwa. Ukosefu wa ajira unaongezeka."

"Sawa lakini nini hutokea kwenye kampuni kwenye soko la hisa?"

"Bei ya hisa huongezeka pale kupunguza matumizi kwa kampuni kunapotangazwa," nilijibu. "Soko linapenda pale kampuni inapotaka kupunguza matumizi ya uendeshaji ama kwa kutumia mitambo inayojiendesha yenyewe au kwa kuimarisha nguvu kazi kwa ujumla."

"Hiyo ni sawa," alisema. "Na bei ya hisa inapopanda, watu kama mimi, wenyehisa, wanatajirika. Hiyo ndio naamaanisha ninapoongelea seti tofauti ya kanuni. Wafanyakazi wanapoteza/wanashindwa, wakati wamiliki na wawekezaji wanapata/wanashinda.

Robert alielezea sio tu tofauti ya mwajiriwa na mwajiri, bali pia na tofauti iliyopo pale unaposimamia hatma yako mwenyewe au unapoiachia kwa mwingine, yeye ndie akusimamie.

"Lakini ni ngumu kwa watu wengi kuelewa kwa nini hii hutokea," nilijibu. "
"Wengi huwa wanafikiri hii huwa haitendi haki."

"Na ndio maana ni ujinga kumwambia mtoto, 'pata elimu nzuri,' alisema. "Ni ujinga kudhani elimu inayotolewa mashuleni itawaandaa watoto wenu kukabiliana na ulimwengu watakaokutana nao siku ya kuhitimu. Kila mtoto anahitaji elimu zaidi. Elimu tofauti. Wanahitajika kuzijua kanuni. Seti tofauti ya kanuni.

"Kuna kanuni za pesa ambazo matajiri hucheza na kuna kanuni ambazo 95% ya watu duniani hucheza," alisema. "Hao asilimia 95 (95%) hujifunza hizo kanuni majumbani na shuleni. Na ndio maana ni hatari leo kumwambia mtoto, ' soma sana na utafute kazi nzuri." "Mtoto wa leo anahitaji elimu ya kisasa wakati mfumo wa sasa hauzalishi hiyo bidhaa. Wala sijali ni kompyuta ngapi zimewekwa madarasani na wala sijali wameingia gharama kiasi gani kama shule. Ninachojiuliza ni, mfumo wa elimu utafundishaje somo usilolijua?"

"Hivyo wazazi watafundishaje kitu ambacho shule haifundishi? Unamfundishaje mtoto uhasibu? Hivi hawataboreka kweli? Na unamfundishaje mtoto uwekezaji wakati wewe mzazi mwenyewe unapinga kuchukua hatua za hatari (taking risk)? Mimi, badala ya kuwafundisha watoto kucheza kwa usalama na maslahi (kutegemea ajira), nawafundisha kucheza kwa werevu."

"Sasa unawafundishaje watoto kuhusu pesa na mambo yote tuliyoyaongea hapa?" Nilimwuliza Robert. "Tunawezaje kuiweka kirahisi kwa wazazi hasa pale ambapo hata wao hawaielewi?"

"Nimeandika kitabu kuhusu hili somo," alijibu.

"Kiko wapi?"

"Kwenye kompyuta yangu. Kiko huko kwa miaka sasa, vikiwa vipande vipande. Nimekuwa naandika mara kwa mara ila sijazipangilia zote pamoja. Nilianza kuandika baada ya kitabu changu cha kwanza kushinda kwenye mauzo, lakini sijakimalizia. Kiko vipande vipande."

Baada ya kukipitia kitabu cha Robert, niliamua kitabu hiki kina faida na kinatakiwa kusambazwa hasa kwa nyakati hizo za mabadiliko. Tukakubaliana tushirikiane kwenye kukiandika.

Nilimwuliza anafikiri mtoto anahitaji taarifa za kifedha nyingi kiasi gani? Akajibu inategemea na mtoto. Anachojua yeye alipokuwa mtoto alitamani kuwa tajiri na akapata mzazi aliyemwongoza njia. Elimu ni msingi wa mafanikio, alisema Robert. Kama ambavyo mbinu za kisomi ni lazima na zina umuhimu, hivyo hivyo na mbinu za kifedha na za kimawasiliano zina umuhimu.


Hadithi za baba wawili wa Robert, mmoja tajiri na mmoja maskini zinaelezea ujuzi alioupata katika kukua kwake hapa duniani. Utofauti uliopo kati yao unaleta mtazamo muhimu. Kitabu kiliungwa mkono, kilihaririwa na kukusanywa pamoja na mimi. Kwa mhasibu yeyote atakayesoma hiki kitabu, simamisha vitabu vyako vya kitaaluma na fungua ufahamu wako kwenye nadharia zilizowasilishwa na Robert. Zinafungua macho jinsi wawekezaji wanavyochambua maamuzi yao ya kiuwekezaji.

Sisi wazazi tunapowaambia watoto wetu, " nenda shule, faulu vizuri na upate kazi nzuri," huwa tunawaambia kutokana na utamaduni tuliokulia. Siku zote ulikuwa ni ushauri nzuri kabisa. Nilipokutana na Robert kwanza mawazo yake yalinistaajabisha. Akiwa amelelewa na wazazi wawili alifundishwa kujitahidi kwenye malengo mawili. Mzazi wake aliyekuwa msomi na maskini, alimshauri kufanya kazi kwenye shirika. Mzazi wake yule tajiri alimshauri alimiliki shirika. Njia zote hizo za maisha zilihitaji elimu. Na masomo yalikuwa tofauti. Baba yake msomi alimwambia awe mwerevu. Lakini baba yake tajiri alimwambia aajiri watu werevu.

Kuwa na wazazi wawili ilisababisha matatizo sana. Baba yake mzazi alimtishia sana, "usiposoma vizuri, hutapata kazi nzuri." Na alipofikisha miaka 16 alikuwa ameshafahamu mambo mengi na hakuathirika sana na maneno hayo ya mzazi wake. Alishajua anaenda kumiliki mashirika na sio kuyafanyia kazi mashirika. Na kama sio kwa kushauriwa hakutaka hata kwenda chuoni, alitaka aanze kujenga mali zake mapema, lakini akakubali kuwa hata elimu ya chuoni itakuwa ya msaada sana baadae.

Kiukweli mawazo yaliyotolewa kwenye hiki kitabu yanaweza kuwa ya msimamo mkali kwa wazazi wa leo. Wazazi wengi bado wanawaweka watoto shuleni, lakini ni wakati sasa wa kupata mawazo mapya na ya kijasiri. Kuwahamasisha watoto wako kuajiriwa ni kuwashauri kulipa kodi zaidi kadri muda unavyoenda, kwa kupewa ahadi ndogo au ahadi hewa. Na ukweli usiopingika ni kwamba kodi ndio matumizi makubwa ya mtu. Familia nyingi zinafanyia kazi serikali kuanzia Januari mpaka Disemba ili waweze kulipa kodi. Kweli mawazo mapya yanahitajika na kitabu hiki kimeyatoa.

Robert anasema matajiri huwafundisha watoto wao tofauti. Wanawafundisha watoto wao nyumbani wakiwa mezani. Yanaweza kuwa ni mawazo ambayo hujawaza kuyajadili na watoto wako, lakini asante hata kwa kuyafuatilia. Ushauri wangu ni uendelee kutafiti zaidi. Mimi kama mama na mhasibu niliyethibitishwa (CPA), hili wazo la, 'nenda shule na upate kazi nzuri' ni la kizamani mno. Tunatakiwa kuwapa watoto wetu ushauri wa kisasa. Tunahitaji elimu mpya na ya kitofauti. Hata wazo la kuwashauri wajitahidi kuwa wafanyakazi bora wakati wakijitahidi kumiliki iwekezaji wao binafsi sio wazo baya.

Ni matumaini yangu kama mama hiki kitabu kiwasaidie wazazi wengine. Robert anataka watu wajue kila mtu anaweza kufanikiwa akitaka. Hata kama leo wewe ni mtunza bustani, unaweza kujifunza wewe na pia kuwafundisha wengine kujitegemea kiuchumi. Kumbuka kuwa akili ya kiuchumi ni mchakato wa kiakili unaotusaidia kutatua matatizo ya kiuchumi.

Leo tunakabiliana na mabadiliko ya kiulimwengu na kiteknolojia ambayo hayakuwepo huko nyuma. Ukweli ni kuwa mabadiliko makubwa zaidi ya uhalisia yanakuja. Nani ajuaye kitakachotokea kesho yake? Lakini kwa chochote kitakachotokea ni mawili, ama ucheze kwa kiusalama (kutegemea kuajiriwa) au ucheze kwa werevu kwa kujiandaa na kuamsha akili ya kiuchumi ndani yako na ndani ya watoto wako. - Sharon Letcher.

Asante
Rich Dad, Poor Dad

Mwisho wa UTANGULIZI...

Itaendelea sura ya KWANZA.

Uchambuzi huu umeandaliwa na
Edith K. Mbanzendole 2019
Ubunifuspring Pages
Mobile:+255 654 303 652
Email: info@ubunifuspring.co.tz
 
Back
Top Bottom