RC: Hakuna ugaidi mapango ya Amboni Tanga

Bilionea Asigwa

JF-Expert Member
Sep 21, 2011
16,515
28,487
martine-shigela_210_120.jpg


MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela amewatoa wasiwasi wakazi wa mkoa huo kuhusu watu wanaodaiwa kufanya uhalifu katika baadhi ya maeneo, ikiwamo mapango ya Majimoto yaliyopo Amboni, nje kidogo ya mji.

Amesisitiza kwamba hakuna magaidi katika mapango hayo; na wahalifu wa eneo hilo, si magaidi wa kundi la Al- Shabaab, kama inavyodaiwa na baadhi ya watu mitaani.

Alifafanua kuwa wahalifu waliopo huko wamegundulika kuwa wahamiaji haramu kutoka Ethiopia, ambao wanaingia nchini kwa kutumia vichochoro vilivyoko kwenye mapori ya mpaka wa Kenya na Tanzania, wakielekea nchi jirani. Wamekuwa wakiingia nchini kupitia baadhi ya maeneo ya wilaya ya Mkinga.

Wahalifu hao hutumia mapango hayo, kujificha kwa muda wakati wakisubiri kuendelea na safari yao kuelekea nchi za Kusini mwa Afrika. Alitoa kauli hiyo jana katika mkutano maalumu na waandishi wa wa habari, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisini kwake.

“Napenda kuwajulisha wakazi wa Tanga na taifa kwa ujumla kwamba hapa mkoani hatuna vita dhidi ya kundi lolote la ugaidi wala kikosi cha Al-Shabaab, isipokuwa kuna operesheni maalumu ya kikosi kazi chetu cha ulinzi na usalama, kinachopambana na mambo makuu matatu; kubwa ni matukio ya uhalifu unaofanywa na wahamiaji haramu,” alisema Mkuu wa Mkoa.

Alisema kamati ya ulinzi na usalama mkoa, baada ya kutafakari mwenendo wa kiusalama kutokana na matukio ya uhalifu wa hapa na pale, imeunda kikosi kazi kukomesha vitendo hivyo, vinavyofanya mkoa kutumiwa kama uchochoro.

Shigela ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, aliyataja mambo yanayoshughulikiwa na kikosi kazi hicho ni kudhibiti uingizaji wa dawa za kulevya, magendo ya bidhaa zisizoruhusiwa au kuingizwa bila kufuata utaratibu pamoja na wahamiaji haramu.

“Wahamiaji haramu ndilo jambo hatarishi sana hapa kwa sasa, kwa sababu hao watu wakishaingia nchini kwa njia za panya na kufanikiwa kujificha, basi wanaposikia njaa hulazimika kujitokeza mitaani kutafuta chakula kwa kuvamia maduka, kama walivyofanya katika duka kuu la Central Bakery mwishoni mwa mwezi uliopita”, alisema.

Akizungumzia wakazi wa Kata ya Amboni yaliko mapango na mapori husika, aliwataka kuchukua tahadhari, hasa wale wanaofanya shughuli za kilimo jirani, kwa kuacha kuwenda kwa muda maeneo hayo, hasa kipindi hiki ambacho kikosi kazi kinaendeleza operesheni.

Source: Habari Leo
 
Back
Top Bottom