Rasimu ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2014 kwa Lugha rahisi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,810
11,979
kitabu.PNG

Heshima kwenu wakuu,

Hiki ni Kijitabu kidogo kilichoandaliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kwa ajili ya Elimu ya Uraia kwa Watanzania wote. Kitabu hiki kinaelezea Rasimu ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2014 kwa lugha rahisi ili kutoa fursa kwa wananchi kuelewa mambo muhimu yaliyomo katika Rasimu. Tunatambua kuwa Rasimu ni kubwa sana maana ina Ibara 271 zilizo katika kurasa zaidi ya 100 ambapo sio kila mtu anaweza kupata Rasimu na kuisoma na hata akiwa nayo anaweza kushindwa kuisoma yote na kuielewa kwa urahisi kwa kuwa ni kubwa.

Kwa hiyo basi, madhumuni ya kuandika kitabu hiki ni kusaidia kuongeza uelewa wa mambo yaliyoandikwa katika Rasimu ya Katiba kwa wananchi na hata wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Tunategemea watapenda kusoma kitabu hiki. Wananchi wakielewa mambo yaliyomo katika Rasimu wataweza kushiriki vizuri zaidi katika mjadala wa utengenezaji wa Katiba mpya na pia wataweza kushiriki vema katika hatua ya mwisho ya upigaji kura ya maoni.

Chama cha Wanasheria Tanganyika kinafahamu kuwa Bunge Maalum la Katiba laweza kubadili, kurekebisha au kuboresha mambo yaliyotajwa katika Rasimu, lakini tunaamini kuwa kabla ya kupiga kura ya maoni, tunaweza kupata fursa ya kuwaelimisha wananchi tofauti itakayokuwepo kati ya mambo yaliyomo katika Rasimu kwa sasa na mambo yatakayokuwemo baada ya Bunge Maalum kumaliza kazi yake ya kuchambua na hatimaye kupata Katiba Mpya itakayokuwa inapendekezwa kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

Kitabu hiki kimeandaliwa na Kamati Maalum ya Katiba ya Chama cha Wanasheria Tanganyika ambayo ina wajumbe wafuatao:

i) Wakili Mpale Mpoki - Mwenyekiti

ii) Wakili James Jesse - Mjumbe

iii) Wakili Issa Miage - Mjumbe

iv) Wakili Godwin Musa - Mjumbe

v) Wakili Alex Mgongolwa - Mjumbe

vi) Stephen Msechu - Katibu wa Kamati

Kamati inapenda kutoa shukrani za dhati kwa uongozi wa TLS chini ya Rais wake Wakili Francis Stolla kwa kutoa support kubwa wakati Kamati ilipokuwa ikiendesha vikao na mikutano yake. Chama cha wanasheria pia kinatoa shukrani za dhati kwa mfadhli wetu mkuu, Ford Foundation, kwa kutuweza kifedha kufanikisha mradi wa Katiba na hata kuandika kitabu hiki.

Tunaamini kuwa kijitabu hiki kitasomwa na watu wengi na hatimaye malengo yetu yaweza
kufikiwa. Ndugu msomaji, tunakutakia usomaji mzuri!

Fungua kiambatanisho hapa chini.
 

Attachments

  • Rasimu-kwa-Lugha-Rahisi-Final.pdf
    514.9 KB · Views: 117
Back
Top Bottom