Rais wangu Kikwete chagua bega au kwaheri ya kuonana

kkiwango

Senior Member
Aug 27, 2007
173
14
Paschally Mayega


RAIS wangu tumewafikisha wananchi wetu mahali wanapowaza zaidi ya nyuma kuliko ya mbele. Wananung’unikia yaliyopo na kuhofia yanayokuja.

Wamejaa woga. Wasiwasi umetanda. Tumewaondolea furaha na kuwafutia matumaini. Tanzania isiyo na matumaini inamnufaisha nani? Msiba wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hautaisha katika Awamu hii ya Nne.

Mwalimu alitamka “Mkiwachagua vijana hawa, watawapeni shida: Watanzania sasa wanayatafakari maneno ya Nyerere nukta kwa mkato.

Rais wangu imeandikwa: “Atawalae kwa upanga, atakufa kwa upanga.” Kama ni kweli tulipandia vyombo vya habari kufika hapa tulipo, basi ni kweli pia vyombo hivyo hivyo vitatushusha na kuturudisha kule tulikotokea.

Kuna mahali nikisoma nahisi mapigo ya moyo kutaka kusimama. Nguli wa maswali magumu aliandika, “Yawezekana Watanzania tulifanya makosa kukifungua kile kilichofungwa na Nyerere. Nguli Mwingine akaandika, “Watanzania tuliuziwa mbuzi kwenye gunia”.

Rais wangu, haya si maneno ya amani. Haya si maneno ya utulivu, haya ni maneno yanayoashiria vurugu na ghasia. Haya ni maneno yanayoashiria mapambano, mapigano, vita. Alaumiwe nani basi kwa maneno haya? Alaumiwe vikali yule aliyesababisha hawa wayaseme haya. Si wale waliyoyasema. Anayeleta matusi katika jamii ni yule anayekaa uchi si yule anayemwambia aliyekaa uchi kuwa “bwana ee umekaa uchi”. Tulisema kuwa kama mamlaka au watu wanaotakiwa kudhibiti vibaka wangechomwa moto, vibaka wasingechomwa moto.

Kama polisi wala rushwa, mahakimu wala rushwa na watendaji wengine wa serikali wala rushwa wangedhibitiwa, hakuna raia angechukua sheria mkononi kuwaadhibu wahalifu.

Rais wangu, nikiangalia wingi wa simu na aina na mahali zinakotokea meseji ninazotumiwa kila baada ya makala kuchapishwa, nashawishika kuamini kuwa haya magazeti yanasomwa kila tarafa ndani ya nchi yetu.

Ndiyo kusema hayo niliyoyasoma mimi na mengine, yanasomwa nchi nzima. Anayedhania kuwa wananchi bado in mabwege ni bwege.

Gazeti moja limewataarifu wananchi kuwa kuna genge limeundwa linalojulikana kwa jina la “Mtandao safisha Lowassa.” Habari hizi hazijakanushwa hadi sasa. Limesema genge hili linaongozwa na mbunge na mfanyabiashara maarufu.

Lengo kuu la genge hili ni kumsafisha Lowassa. Wenye akili timamu siku zote husafisha kitu kichafu. Mwendawazimu peke yake anaweza kumsafisha mtu msafi. Genge hili linawathibitishia wananchi kuwa Lowassa ni mchafu, lazima asafishwe. Basi na wamsafishe lakini wakae naye. Wasithubutu kuwapelekea wananchi. Mtu mchafu huwa hasafishwi na watu wengine. Watu wachafu hawawezi kumsafisha mchafu mwenzao.

Uchafu wa mtu uko ndani ya mtu. Nafsi ya mtu ndiyo inayomfanya mtu kuwa mchafu au mwenye dhambi. Bila kuachana na uchafu, bila kujutia uchafu na bila kudhamiria kutochafuka tena, uchafu kamwe hauwezi kumtoka mtu. Wanaomsafisha Lowassa kwa maana hii watamchubua hadi ngozi Lowassa atabaki mchafu, milele. Gazeti limetoa picha na majina ya vinara wa genge hili. Ni vizuri sasa kuwa Watanzania wote katika ujumla wetu tumewajua kwa sura zao na kwa kwa majina yao.

Kwa sababu wote walishiriki kupitisha mapendekezo kama yalivyotolewa na Tume Teule ya Bunge kuhusu Richmond na wananchi wakawashangilia na kuwapa heshima kubwa iliyokuwa imepotea, na kwa sababu sasa wanataka wananchi wawaelewe kuwa Bunge yaani pamoja na wao walifanya makosa kupitisha mapendekezo yale, wanachowaambia wananchi kwa maneno mengine ni kuwa - ama walifanya ujinga wakati ule wa kupitisha au wanafanya ujinga sasa. Neno ‘ujinga’ linabaki pale pale mara zote mbili.

Kama ulifanya ujinga mwanzo wewe ni mjinga. Kama unafanya ujinga sasa wewe ni mjinga - Mtu mjinga. Mtu hovyo hovyo tu akiwa mjinga tutamwacha akafie mbele. Mheshimiwa yeyote hasa mbunge anayewakilisha watu wenye akili timamu akithibitika kuwa ni mjinga, huyu ni wa kupigwa mawe. Unakwenda kuwarubuni wananchi wa jimbo lako kuwa una akili timamu na kwamba utawawakilisha bungeni, kumbe huwawakilishi badala yake unafanya mambo ambayo sasa yanathibitika kuwa ni ya kijinga.

Rais wangu, ukizitazama sura zao katika gazeti utagundua kitu kimoja cha ajabu sana. Wote wanafanana. Lakini Lowassa wanayetaka kumsafisha yuko tofauti nao. Inasikitisha kumwona Katibu Mkuu wa CCM kuwa miongoni mwao. Labda ni kweli, wengine kadiri wanavyozeeka, ndivyo wanavyopukutika kichwani. Lakini kimtazamo naye kunakuchwa anafanana nao. Watanzania watamwelewaje Waziri wa Mambo ya Ndani kuwako katika genge hili? Bila kukanusha habari hizi, atawafanya wananchi wayaamini yote yasiyopendeza wanayoyasikia juu yake.

Wizara ya Mambo ya Ndani ni moja ya wizara nzito za nchi yetu. Mtu wa kukaa kwenye magenge hastahili hata kidogo. Tunamwomba alitolee ufafanuzi hili, ili kuwajengea imani wananchi.

Rais wangu, ulikubali kujiuzulu kwa Lowassa katika nafasi yake ya uwaziri mkuu ukifahamu kuwa kwa kufanya hivyo ulikuwa sahihi na kwamba ndiyo iliyokuwa njia muafaka kukabiliana na hali iliyokuwa imejiri.

Watu wako walikupongeza na heshima ikarudi katika Serikali yako. Leo kati ya mawaziri wako wale wale uliowateua wewe na wengine uliowateua pia baada ya Lowassa, wanakwambia ulifanya makosa. Kina Yuda Iskariote wako wengi. Kama hawa nao ni maswahiba na unaendelea nao basi watakutoa kwa vipande thelathini vya fedha. Vyombo vya habari viliwakariri wananchi kukutaka utengue uteuzi wao, ‘baba’ hukuwajibu watu wako. Hawa ni kisiki. Utatakiwa kupambana nao au kuungana nao. Ungekuwa ndani ya daladala au kifodi au mzunguko, konda angekuambia ‘mzee chagua bega, nembo ya Konyagi haitakiwi humu ndani’.

Ndugu Rais kama ulikuwa unasafiri katika treni kutokea Mwanza au Kigoma hapa ulipofika ni Dar es Salaam. Treni huwa haivuki bahari.

Rais wangu, Mwalimu Nyerere atakumbukwa kwa mengi. Alipokuwa akimnadi Mwinyi alitamka, “Mwinyi hana vikundi!” Ukumbi mzima ulilipuka kwa vifijo, nderemo na hoi hoi.

Sasa Watanzania watapata kuelewa kwa nini Mwalimu aliona hiyo sifa ya kutokuwa na vikundi kuwa ni sifa kubwa na muhimu kwa mtu anayetaka kuwa rais wa nchi. Wananchi wengi walimuhusisha rais wao na kikundi kilichojiita Mtandao wakati wa kampeni. Kama Rais ataamua kuungana na Mtandao safisha Lowassa, basi nchi yetu itakuwa Kenya, nchi yetu itakuwa Zimbabwe. Lakini wananchi sasa wamekwishaamka hawana ubwege tena. Watailinda nchi yao isichukuliwe na mafisadi hata kwa damu. Watamwambia rais wao ‘kwa heri ya kuonana.’ Watapambana na watawashinda mafisadi kwa sababu Mungu atakuwa upande wao.

Rais wangu, ukiamua kuungana na wananchi katika hili, genge la mafisadi litayeyuka kama moshi uyeyukavyo hewani baada ya moto kuzimwa. Hupotea bila kuacha alama yoyote. Amani ya kweli itatamalaki. Ustawi wa watu wako utachomoza kama jua la alfajiri.

Hata wanyama wa mbugani na ndege wa angani wataifurahia nchi yao Tanzania. Thawabu zako mbele ya Mwenyezi Mungu zitaongezwa nawe utatawala nchi yako kwa baraka zake kama Mfalme Suleiman.

Rais wangu, usikae kimya katika hili, kukaa kimya sasa si sahihi hata kidogo. Wananchi watakapodhani kuwa huko pamoja nao, watakuchukia wewe zaidi ya mafisadi. Usijiombee laana ya kuchukiwa na watu wako. Usimkubalie mtu yeyote atakayekwambia katika hili usiwe na upande, kwa sababu ukimkubalia wananchi watakuchagulia upande usio wako. Wataweka uadui kati yako na wao.

Hapa ndipo kitakapoeleweka nani anamfanya nani. Ni rais anayewafanya watu wake kuwa wananchi au ni wananchi wanaomfanya mtu kuwa rais wao. Kumwelewesha zaidi mtu katika hili ni sawa na kumdhalilisha.

Rais wangu, jambo hili lingekemewa sasa wakati bado mapema lingemalizika bila kuleta madhara yoyote. Kungojea mwisho ni kungojea machafuko. Watu wanakuangalia wewe unavyongojea machafuko. Nchi yetu ina wasiwasi na mustakabali wake haueleweki, baba wewe uko kimya. Hatusikii tena vikao vya kujadili maendeleo ya nchi yetu. Hatuoni tena jitihada zozote za serikali za kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.

Hatusikii tena ‘ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya’. Vyote vimepauka haraka. Kila kikao sasa ni ufisadi, mafisadi, ufisadi na mafisadi. Viwe vikao vya chama au mkutano wa Bunge - hadithi ni moja tu. Kwa nini lakini? Jibu ni jepesi. Kwa sababu baba yupo kimya. Yupo kimya kwa sababu hajui cha kusema au yuko kimya kwa sababu anaifurahia hali hii? Hata kwa maswali haya nako yupo kimya! Watoto wanasema baba ukuta wa nyumba yetu unaporomoka, baba yuko kimya. Anangoja ghorofa zima liporomoke.

Rais wangu, Rais Mwinyi alipokaa kimya, Baba wa Taifa alisimama akakemea hali ikawa shwari. Mwanzoni Rais Benjamin Mkapa alipokaa kimya, Baba wa Taifa alisimama akakemea hali ikawa shwari. Nyerere amekufa. Leo Baba wa Taifa na Rais wetu ni wewe, unapokuwa kimya unawaza nini! taifa litamaliza kweli msiba wa Nyerere katika kipindi chako?

Kwa kuwa tumekosa wa kukemea hatari hii, basi tunalazimika kumwangukia Lowassa ainusuru nchi yetu. Kwa kuwa tuna shida ya amani na utulivu, tatalazimika kukubaliana na mengi.

Edward Ngoyai Lowassa wewe ni ndugu yetu. Umekuwa kiongozi wetu katika nchi hii kwa muda mrefu. Umeshika nyadhifa mbalimbali. Ulitukuka ulipokuwa Waziri wa Ardhi na hasa ulipovunja ukuta wa Baghdad.

Wakati ukiwa Maji, watu wako walikushuhudia ukihangaika hadi usiku wa manane mabomba yalipokorofisha. Ni mara ngapi uliwatimua kazini watumishi wabovu papo hapo bila kujali lawama lakini ukalinda maslahi ya wananchi? Ufuatiliaji wako katika kazi baada ya Edward Moringe Sokoine nani mwingine kama Waziri Mkuu wewe? Taifa linatambua mchango wako.

Lowassa ni Mtanzania gani ambaye hakuitambua kazi kubwa uliyoifanya wakati nchi yetu ilipoingiliwa na balaa la njaa? Ndugu yetu ulihaha utadhani njaa imeingia nyumbani mwako. Ni sehemu gani ya nchi ambayo wewe hukwenda kuhakikisha kuwa wananchi wako wako salama?

Hatujui ulikuwa unalala saa ngapi, lakini tunajua bila jitihada zako binafsi njaa ile ingechukua maisha ya Watanzania wengi. Wacha Mungu watakusahau vipi katika jambo jema kama hili, Edward!

Hujapumua likaja homa ya Bonde la Ufa. Nao ukawa ugonjwa tishio kwa maisha ya watu wako. Tuliambiwa ulikubali hata kupungua lakini maisha ya wananchi yabaki salama.

Kwa haya, uliandikiwa thawabu na Mwenyezi Mungu na thawabu hizo ndizo zinazopaswa kukusemea leo, si watu waovu, wazandiki wasio na hadhi yoyote katika nchi hii. Sasa tunasikia kuna genge. Habari ambazo hazijakanushwa. Mtandao Safisha Lowassa (MSALO). Ni habari za kusikitisha sana. Sisi tuliokuunga mkono kwa muda wa miaka mingi tunapokuona kiongozi wetu unaashiria kukata tamaa na kuishiwa na matumaini ya baadaye, tunahuzunika sana.

Watu wanaanza kusema hovyo tu eti hivyo ndivyo wanavyokusafisha. Bahati nzuri wote waliosema hovyo hawana heshima yoyote kitaifa. Kikubwa wanachokosea, wanaposema wanabwabwaja. Hawakupi heshima unayostahili. Edward, wewe ni kiongozi wa kitaifa. Tena kiongozi wa mfano. Taifa la Tanzania linatambua hivyo.

Taifa linatambua umahiri wako katika kufikiri na kusema. Unakubali vipi mtu ambaye hata elimu yake tu ina shaka ya kughushi vyeti, akusemee hadharani? Wote waliokwisha kukusemea hakuna hata mmoja mwenye uwezo wa kufikiri kama wewe. Ukweli ni kwamba wote walioko katika hilo genge, hakuna hata mmoja anayefanana na wewe. Una akili kubwa kuliko wao. Unajua kusema kuliko wao; umeshika wadhifa mkubwa na kwa muda mrefu kuliko wote. Hao si saizi yako. Ukiendelea nao Watanzania watakuona kama mfa maji anayeshika hata jani tu linaloelea kama yeye akidhani litamwokoa. Edward, warudie wananchi wako. Mbona wao bado wanakuthamini? Mimi si mshauri wako, lakini wewe ni kiongozi wangu mimi nisiyestahili. Achana na hao, nenda ukapate matumaini mapya Kyela.

Mchukue Mwakyembe ukaeleze kilichotokea. Kwetu sisi nyinyi wawili ni viongozi wetu. Waambie ni Rais waliyemchagua wao ndiye aliyekuteua wewe kuwa waziri mkuu wao.

Waambie ni wabunge pamoja na mbunge wao waliyemchagua ndio waliokuthibitisha kuwa waziri mkuu wao, na kwa hivyo wewe si mtu wa hovyo hovyo tu. Kwa hiyo, ni wao waliokuweka pale na kwa kuwa yametokea ya kutokea ni wajibu wako kuwaeleza ukweli ulivyo.

Ukweli utakuweka huru. Uwe mwangalifu katika kuzungumza, kwani kweli wananchi wa sasa si mabwege. Ukisema umeonewa, sema ulifukuzwa kazi. Anayejiuzulu huwa haonewi na mtu.

Anaonewa na nani na kajiuzulu mwenyewe? Huendelea kushirikiana na wananchi nao humwamini zaidi hata baadaye huweza kumpa wadhifa mkubwa zaidi. Mzee Mwinyi hakuunda genge. Kuunda genge ni kuunda kikosi cha mapambano. Rais wetu alituambia kuwa wewe ni rafiki yake kimaisha. Watanzania tulivyolelewa hatukuwahi kuambiwa na Rais wetu yeyote kuwa fulani ni rafiki yake. Alikwenda mbali zaidi akasema hata kikazi wewe ulikuwa rafiki yake.

Wale ambao hatukumwelewa siku ile tunamwelewa sasa wakati linaundwa genge la watu wasikuwa na muamana wowote katika nchi na kwamba mwelekeo ni kwenye machafuko na ghasia, lakini Rais wetu hakukemei. Huenda anahofu asije akauharibu huo urafiki wenu. Ndiyo maana tunakuangukia wewe. Ni wewe tu sasa unayeweza kuleta amani na utulivu au machafuko na ghasia katika nchi yetu.

Ndugu yetu Edward, wewe ni binadamu kama tulivyo sisi. Tumeumbwa na upungufu. Kukosa ni hulka ya mwanadamu. Kukubali kukosolewa ni kujijengea heshima katika jamii. Usisikie maneno yadanganyayo kuwa ufisadi unaweza kusafishwa.

Ufisadi utabaki kuwa haramu hadi mwisho wa nyakati. Kwa nini kuisumbukia dunia na mambo yake? Wewe unaejiweza unawatuma wasiojiweza. Imeandikwa: “Amtumaye mpumbavu hujikata miguu yake na kunywa hasara”.

Mipango na mikakati yote inayofanyika hivi sasa ni sawa kabisa na masumbuko ya bure ya yule aliyekosa radhi. Nayo baada ya kushindwa itaidhoofisha nafsi yako kiasi cha kukupunguzia siku zako.

Nyerere aliona mbali sana kusema hayo........ila ubishi wetu kujifanya kwetu wajuaji sasa twamkumbuka.
 
Paschally Mayega
Kwa kuwa tumekosa wa kukemea hatari hii, basi tunalazimika kumwangukia Lowassa ainusuru nchi yetu. Kwa kuwa tuna shida ya amani na utulivu, tatalazimika kukubaliana na mengi.

Edward Ngoyai Lowassa wewe ni ndugu yetu. Umekuwa kiongozi wetu katika nchi hii kwa muda mrefu. Umeshika nyadhifa mbalimbali. Ulitukuka ulipokuwa Waziri wa Ardhi na hasa ulipovunja ukuta wa Baghdad.

Mipango na mikakati yote inayofanyika hivi sasa ni sawa kabisa na masumbuko ya bure ya yule aliyekosa radhi. Nayo baada ya kushindwa itaidhoofisha nafsi yako kiasi cha kukupunguzia siku zako.

Nyerere aliona mbali sana kusema hayo........ila ubishi wetu kujifanya kwetu wajuaji sasa twamkumbuka.

Mwandishi umeanza vyema ila sijakuelewa kwamba sasa hivi tumuangukie fisadi Lowasa kwamba yeye ndo kashikilia amani ya nchi yetu? hapo umenikoroga, nilitegemea umalizie kumwambia Jk akamate huyu fisadi apelekwe segerea akapate adabu yake badala ya kumuacha aendelea kusumbua walala hoi kwa hela aliyo tuibia!
 
Hiki ni kielelezo tosha kuwa elimu ya fisadi bado haijatuuingia sawa sawa
 
Washwahili tunao msomo wetu kwamba MAJUTO NI MJUKUU. Mtu ukiachiwa radhi mara nyingi unakaa chini na kuwaza kile ambacho kilikufanya uwachiwe radhi.
Mafisadi ndio walioachiwa radhi na pia kulaaniwa kwa vile ule ufisadi uliotokea wa Richmond ulifanyika wakat wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Dua zetu nazo zilikubaliwa na mafisadi hatimaye wakafichuliwa. CCM iliwafuga hao wafisadi wote. Sasa itabidi CCM yenyewe iwapeleke mafisadi hao mahakamani ili wahukumiwe.
Na wale wengine waliomiliki mgodi wa Kiwira wakiwa ni rais wa Jamuhuri ya Tanzania. jambo ambalo ni kinyume ya katiba ya nchi pia wapelekwe mahakami.
Sisi watanzania hatutakuwa radhi na serikali yetu mpaka wale mafisadi wote wahukumiwe ipasavyo.
 
JK hasikii kabisa ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa tena siku hizi hata nchi kama vile ameihama hasikiki wala haonekani!
 
Back
Top Bottom