peno hasegawa
JF-Expert Member
- Feb 24, 2016
- 18,310
- 31,567
Geita. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya siku mbili mkoani Geita ikiwa ni ziara yake ya kwanza ya kikazi toka achaguliwe kuongoza Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 13, Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema Rais atafanya ziara Oktoba 15 na 16 akitokea mkoani Kagera.
Amesema Rais Samia atatembelea Wilaya ya Chato na kupokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Kanda ya Chato pamoja na taarifa ya huduma za kibingwa za matibabu zinazotolewa hospitani hapo na baada ya hapo atatembelea kuona hatua zilizofikiwa.
Rais Pia atazungumza na wananchi katika eneo hilo la hospitali kisha kuanza safari ya kwenda Wilaya ya Geita ambapo akiwa njiani atazungumza na wananchi katika eneo la mji mdogo wa Katoro na kupokea taarifa za miradi ya maendeleo ya wilaya nzima ya Geita kisha kusalimia wananchi wa eneo hilo.
Siku hiyohiyo pia Rais atatembelea kituo cha kupoozea umeme cha Mpomvu kisha kuuzindua mradi huo ambao ni muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Geita hasa kwenye sekta ya madini.
Aidha amesema Rais atatembelea na kufungua kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Geita (GGR) kinachoongeza thamani ya madini ya dhahabu katika mkoa huo na baadae atafanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Kalangalala vilivyopo mjini Geita.
Septemba 16 Rais Samia atahitimisha ziara yake katika wilaya ya Bukombe kwa kuzungumza na wananchi wa Runzewe akiwa safarini kuelekea mkoa wa Kigoma.
Source: Mwananchi