Rais Magufuli, usikubali kupakwa mafuta na Bunge la 12

MSOLOPAA

Member
Dec 10, 2016
82
107
MHE RAIS MAGUFULI USIKUBALI KUPAKWA MAFUTA NA BUNGE LA 12

Na Emmanuel M. Makalla
+255716605949


Bwana Yesu asifiwe, As-salamu Alaykum!
Naomba kuchukua fursa hii kukupongeza mhe Rais John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa tena kutangazwa mshindi katika uchaguzi mkuu wa tarehe 28 October 2020 uchaguzi ambao uliifanya Tume ya Taifa ya uchaguzi ikutangaze mshindi kwa ushindi wa kishindo wa asilimia 84(%). Bila shaka ni ushindi wa kihistoria pamoja na mambo mengine yote lakini tuamini kwamba uchaguzi umeisha na sasa maisha mengine lazima yaendelee. Na hii ndio itakuwa maana halisi ya msemo wa "KUNA MAISHA BAADA YA UCHAGUZI".

Mhe Rais, natambua kwamba nia yako ya kuijenga Tanzania bado iko pale pale kama ambavyo ilikuwa katika kipindi chako cha kwanza cha awamu ya 5 ambapo ulifanya maamuzi mengi magumu na kubadilisha kabisa mfumo wa maisha ya watanzania kuanzia utendaji kazi wetu maofisini, kwa wafanyabiashara, machinga, mashuleni, hospitalini, machimboni, kwa wavuvi, wafugaji, wakulima na kila kona ya nchi hii, hakuna sehemu ambayo mkono wako haukufika.

Mhe Rais, kutokana na maamuzi yako ya kugusa kila kona ya kitanda cha mtanzania awe masikini au tajiri, awe mtumishi au mfanyabiashara, mzazi au mtoto, mwalimu au mwanafunzi hakuna shaka kwamba katika kipindi hicho cha miaka mitano ya awamu ya tano kuna wale ambao walinufaika moja kwa moja na mfumo wako wa uongozi lakini kuna kundi lingine la watanzania hawakunufaika na huo mfumo badala yake waliumia. Nakushauri Rais wa nchi yangu uketi kitako uone namna gani utaweza kujenga Taifa lenye usawa🙏🙏

Mhe Rais, tunapoingia katika kipindi cha pili cha uongozi wako, napenda kumuomba Mwenyezi Mungu akujalie hekima na busara, akujaze afya njema ili uwatumikie watanzania kwa moyo, nguvu na upendo.

Mhe Rais, umeingia madarakani awamu ya sita na kuwa na Bunge ambalo halitakuwa na kambi rasmi ya upinzani, ni Bunge ambalo muda wote litakuwa tayari kupigia makofi hoja zote za Serikali bila kujali athali zake kwa watanzania kwani kwa jinsi hali ilivyo ni Bunge ambalo litakuwa la kukusifia badala ya kukushauri. Kwa upendo wa dhati kabisa ili ubaki kuwa kiongozi ambaye utakumbukwa kwa kujenga nchi yenye usawa nakushauri Mhe Rais usiyakubali makofi ya wabunge badala yake wasikilize wananchi wanasema nini maana naamini wabunge wengi watakuwa tayari kukupigia makofi ili wakufurahishe wewe ambaye ni Mwenyekiti wa CHAMA CHA MAPINDUZI huku wakiwaza kuteuliwa tena kugombea Ubunge mwaka 2025.

Mhe Rais, usiwaone wabunge wote wa CCM ukafikiri wanapendana kuna wengine walikuwa tayari kuwaangusha wenzao katika uchaguzi mkuu, hapa namaanisha kwamba Mbunge wa Jimbo A alishiriki kumuangusha au alishiriki kutaka kumuangusha Mbunge wa Jimbo B ambao wote walikuwa wabunge wa katika Bunge la 11. Hivyo utambue kwamba wapo wabunge watakaoona uovu na kuuacha ili wewe uanguke na huu ndio mfumo wa maisha ya mwanadamu.

Mhe Rais, katika kujenga Taifa lenye haki, usawa na Maendeleo ya kweli ya kiuchumi nakushauri uimarishe ulinzi na usalama wa Taifa letu, hakikisha unadumisha umoja na mshikamano kwa watanzania wote ili tusiwe na maumivu kama yale tuliyoyashuhudia katika kipindi cha awamu ya tano ambapo tuliona chuki ikiongezeka katika jamii huku chuki kubwa ikiwa kwa wanasiasa hasa wale wa chama tawala na vyama vya upinzani hasa CHADEMA kilichokuwa chama kikuu cha upinzani. Katika awamu ya tano tulishuhudia mwana CCM akifurahia kifo cha mwana CHADEMA, hivyo hivyo mwana CHADEMA alifurahia kifo au matatizo ya mwana CCM. Hii sio Tanzania ambayo tuliachiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Natamani kusikia neno kutoka kwako Nahodha Mkuu wa Meli yetu ya MV MAENDELEO TANZANIA.

Mhe Rais katika kuzijua na kuzitatua kero za watanzania ni vyema ukaimarisha kitengo cha usalama wa Taifa ambacho kitakuwa msaada wa kuchukua taarifa njema kutoka kwa wananchi kuja kwako ili uweze kujua watanzania wanahitaji nini maana ukiwategemea wabunge wa Bunge la 12 kamwe hawatakuwa na msaada kwako. Kazi ya usalama wa Taifa isiwe kuchukua taarifa za wafanyabiashara wanaosafiri na pesa mkononi kwenda Kenya kununua vyombo vya Plastiki na sahani za mfupa badala yake waje mtaani wasikilize watanzania wanasemaje juu ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Mhe Rais, naomba utazame video yako wakati ukitoa hotuba ya kuzindua Bunge la 12 utagundua kwamba makofi yalikuwa mengi zaidi ulipowataja wabunge kwamba unataka nao wawe sehemu ya mabilionea wa nchi hii. Hiyo pekee itoshe kukuonyesha kwamba katika Bunge la 12 utasifiwa zaidi badala ya kushauriwa. Kazi ya Bunge sio kusifia Serikali bali ni kutunga sheria na kuisimamia Serikali.

Mhe Rais, natambua matamanio yako makubwa ya kutaka kuiona Tanzania ikiwa nchi ambayo imekamilika kwa kuwa na miundombinu inayochochea maendeleo ya kiuchumi, afya, elimu na Maendeleo watanzania kwa ujumla. Mhe Rais napenda kukushauri kwamba katika kujenga nchi yenye maendeleo thabiti lazima kuwe na usawa katika maendeleo ya miundombinu na Maendeleo ya watu. Unaweza kujenga shule, hospital, barabara, kujenga meli na kila aina ya miundombinu lakini ukashindwa kuwajengea uwezo watu waweze kutumia vyema hiyo miundombinu na matokeo yake uzalishaji utashuka.

Mhe Rais, una Bunge ambalo halitaweza kukukosoa wala kuibua hoja ambayo itaonyesha udhaifu wa Serikali, hutokuwa na wabunge ambao watakuwa tayari kuibua Sakata lolote kama lile TEGETA ESCROW badala yake watakushangilia kwa kila jambo na kamwe hawatakutendea haki katika kukushauri hivyo nakushauri Mhe Rais utafute njia mbadala ya kushauriwa na sio kutegemea Bunge.

Mhe Rais, Bunge la 12 lina sura mbili kwa Chama Cha Mapinduzi, sura ya kwanza ni ile ya mafanikio ambayo itaifanya CCM kuchaguliwa tena mwaka 2025 iwapo matarajio ya watanzania yatafikiwa japo kwa asilimia 70 lakini sura ya pili ni ile ya Chama Cha Mapinduzi kuwa na mazingira magumu katika uchaguzi wa mwaka 2025 endapo matarajio ya watanzania hayatafikiwa hata kwa asilimia 50. Iwapo watanzania hawataona nafuu katika maisha yao ya kila siku wataamini kwamba tatizo ni CCM na sio upinzani hivyo katika uchaguzi wa mwaka 2025 watatafuta mbadala wa CCM.

Mhe Rais, nakushauri rudi chini zungumza na wafanyabiashara ambao ndio walipa kodi wakubwa katika Taifa hili uweze kuwasikiliza vilio vyao maana leo hii biashara inakufa, biashara imeshuka, kila mfanyabiashara analia kilio chake na siku zote hakuna kilio kisicho na sababu na hakuna kilio kisicho na maumivu. Naamini kwamba wanalia sio kwa sababu wanakuchukia bali kuna sehemu umewagusa na wanaumia.

Mhe Rais, katika awamu ya tano Serikali yako kupitia Bunge ilibadilisha sheria ya mafao ambayo awali ilikuwa inamruhusu mwajiriwa anaeacha kazi kuchukua mafao yake na kwenda kufanya biashara zake ambazo ziliweza kuzaa hata viwanda vidogo vifogo lakini leo hii sheria imebadilika ambapo mwajiriwa akiacha kazi anatakiwa kusubiri mpaka afikishe miaka 60 ndipo apate mafao yake. Hii ni hatari sana Mhe Rais kwani imepunguza kiwango cha watu kujiajiri na kutengeneza ajira kwa watu wengine na hatimaye kuisaidia Serikali katika kutengeneza ajira. Nakushauri Mhe Rais kupitia Serikali yako utakayoiunda ipitie tena sheria hii ya mafao. Watanzania wanalia kila kukicha tangu Bunge la 11 lilipobadilisha hii sheria.

Mhe Rais, Tanzania sio kisiwa kwamba kimejitenga peke yake katika Bahari au ziwa bali Tanzania ni Taifa huru lenye mamlaka yake hivyo tunayo kila sababu ya kulinda na kuheshimu haki na Uhuru wa kila mmoja. Vyombo vya ulinzi na usalama hasa jeshi la Polisi lisifanye kazi kwa uoga badala yake lifanye kazi ya kulinda watanzania na mali zao kwa weledi mkubwa. Hofu ni kubwa kwa wananchi wengi hawana imani na jeshi la Polisi wanaamini linafanya kazi ya kuilinda Serikali badala ya kuwalinda watanzania na mali zao. Ipo haja ya kukaa na vyombo hivi vya ulinzi na usalama ili kuona namna gani ya kuondoa huu mtazamo kwa wananchi.

Mhe Rais, wewe ni mpambanaji haswa na katika uongozi wako awamu ya tano umetufundisha jinsi ya kujiamini, kumtegemea Mungu, kutumia kile tulichonacho kujiletea maendeleo lakini nakuomba Mhe Rais utufundishe pia namna ya kuishi kwa UPENDO sisi watanzania tuna imani na wewe na ndio maana wakati wa CORONA uliposema tufanye maombi ya siku tatu tulikusikiliza na baada ya hapo ukatuomba tumshukuru Mungu na pia tukakusikiliza. Hivyo Mhe Rais katika kipindi hiki cha miaka mingine mitano ya awamu ya sita nakuomba Mhe Rais wetu utufundishe kuishi kwa UPENDO.

Mwisho Mhe Rais, nakutakia kila la kheri katika uongozi wako na Mwenyezi Mungu akulinde sawa na mapenzi yake na hatimaye utufikishe katika nchi ya AHADI.

Ndimi,
Emmanuel M. Makalla
 
Mmmhh, yaani wabunge waache kumsifia wakati wameeingia bungeni kupitia madaraka yake? Hakuna bunge linatunga sheria, sheria zote zinatungwa na serikali, huko bungeni ni rubber stamp tu. Kwa maneno marahisi hilo ni bunge kibogoyo, na liko hapo kula hela za wananchi kisheria.
 
Mmmhh, yaani wabunge waache kumsifia wakati wameeingia bungeni kupitia madaraka yake? Hakuna bunge linatunga sheria, sheria zote zinatungwa na serikali, huko bungeni ni rubber stamp tu. Kwa maneno marahisi hilo ni bunge kibogoyo, na liko hapo kula hela za wananchi kisheria.
Kwa hiyo Chadema ingepata wabunge 70+ ndio lingekuwa bunge lenye meno?
 
Mhe Rais utufundishe pia namna ya kuishi kwa UPENDO sisi watanzania tuna imani na wewe na ndio maana wakati wa CORONA uliposema tufanye maombi ya siku tatu tulikusikiliza na baada ya hapo ukatuomba tumshukuru Mungu na pia tukakusikiliza. Hivyo Mhe Rais katika kipindi hiki cha miaka mingine mitano ya awamu ya sita nakuomba Mhe
Mimi humo kwenye kundi la watu walio na imani na yeye usiniweke! Siwezi kuwa na imani na mtu aliyekuwa amakataliwa na watu akaingia Ikulu kwa mgongo wa TISS! Mimi simo kabisaaaa!
 
Mtoa mada anahoja za msingi wenye maamlaka dola mpeni summary JPM.
 
Umeongea bahadhi mazuri,ila tu nikubali neno moja tu na nakuhuu
MH, USIKUBALI PAKAWA MAFUTA KWA MGONGO WA CHUPA, hili neno dogo but Ina maana kubwa sana
 
Back
Top Bottom