Rais Magufuli; Dhahabu ni nzito kuliko damu? PART 1

mwankuga

JF-Expert Member
Aug 30, 2010
334
120
DHAHABU NI NZITO KULIKO DAMU?

Kuna msemo wa Kiswahili unaosema “damu mzito kuliko maji”. Kwa ufahamu wangu, hakuna binadamu anayeweza kuishi bila kuwa na damu. Hivyo damu ni uhai. Lakini umuhimu wa maji hauwezi kupuzwa kwa namna yoyote! Hivyo damu na maji vyote ni muhimu. Lakini damu ni “nzito” zaidi.

Siku 81 zilitosha kuondoa uhai wa Patrice Emery Lumbumba, waziri mkuu wa kwanza wa DR Congo (zamani ikijulikana kama Zaire). Patrice Lumumba, mwana wa Afrika, mzalendo na mwana mageuzi, aliondolewa uhai wake kikatili na kinyama sana, na mataifa ya Ubelgiji na Marekani wakisaidiwa na Waafrika wenye uchu wa madaraka kama vile Joseph – Desire Mobutu Sese Seko. Uhai wa Lumumba uliondolewa kwa sababu aliamua kwa dhati kabisa kupigania rasilimali za nchi yake kwa masilahi ya watu wake. Hakuna asiyefahamu kwamba, Congo ni miongoni mwa nchi tajiri sana kwa rasilimali kama vile dhahabu ,lakini dhahabu hiyo imegeuka kuwa laana , badala ya Baraka.

Hakuna aliyejali sana uhai na maisha ya Patrice Lumumba. Ndio maana, sio kwamba aliuawa, bali aliondolewa utu na uhai wake kikatili mno katika historia ya dunia. Uhai wake haukuwa kitu, mbele ya dhahabu. Tangu kifo cha Lumumba, Congo bado iko kwenye ukingo wa mauti.

Nimemtumia Lumumba kama mfano tu, kuonyesha jinsi ambavyo mataifa ya Magharibi na Marekani yalivyo tayari kutoa uhai wa mtu kwa ajili ya kupata dhahabu na mafuta. Damu ya watu kumwagika kwao sio kitu kikubwa. Hivyo dhahabu na mafuta, ni zaidi ya uhai.

Tanzania, nchi nzuri, imebarikiwa sana na Mwenyezi Mungu. Tuna kila kitu ambacho kinaweza kutufanya Taifa lenye neema. Lakini kwa bahati mbaya bado taifa, linazidiwa vita na maadui watatu; umasiki, ujinga, njaa na maradhi. Bado tuko kwenye fungate la uhuru. Ni bahati nzuri sana, kwamba Mwalimu Nyerere hakuondolewa kikatili kama wapigania uhuru wengine. Alituachia misingi mzuri, ushauri na maono ya namna ya kutumia rasilimali zetu kwa manufaa ya watanzania wote. Moja ya ushauri aliotuachia, ni kutokukimbilia kuchimba madini kabla hatujajiimarisha hasa kwa upande wa rasilimali watu na teknolojia.

Lakini kwa sababu ya masilahi binafsi, tumeamua kuchimba dhahabu na madini mengine, bila kujali masilahi kwa wananchi. Tumeingia mikataba tata. Walioingia mikataba hiyo ni watanzania wenzetu. Wamekulia Namachumu, Mgumu, Isenyi, Nanjirinji, Kidonge Chekundu, Makongorosi na kwingineko. Wanafahamu maisha ya watanzania. Kwa bahati mbaya sana, watu wanaoishi kwenye ardhi iliyojaa madini wako kwenye umasikini mkubwa zaidi. Mambo ni kinyume. Sasa tuko njia panda. Hakuna mjadala kwamba hatufaidiki na rasilimali zetu.

Hakuna anayebisha kwamba kama Taifa tumepotea. Tumekosea. Tumepotoka. Tumeingia mikataba ya kinyonyaji. Sasa tuko njia panda. Hatuelewi njia ya kufuata. Hakuna wa kutushika mkono. Tumepotea njia. Hii ni habari njema sana kwa mataifa ya Ulaya na Marekani. Wamekaa pembeni wanatucheka. Bila shaka kuna makuhadi wao, kama ambavyo walifanya kwa Patrice Lumumba. Japo wanafanya tofauti na enzi hizo. Katika hali hii nani atatusaidia?

John Pombe Magufuli amejitokeza katika mkwamo huu. Itakuwa ni jambo la ajabu sana kama hatutaona juhudi za Rais kuona rasilimali za Taifa hili zinawanufaisha watanzania. Kuna na nia tu inapaswa kumpongeza Rais. Kama nilivyosema hapo juu, ni hatari sana kupigana vita inayohusisha madini na mafuta. Hatari mno. Tunaweza kutofautiana njia zinazotumika kupigana vita hii. Hii vita ni ngumu sana, kama ilivyo vita ya madawa ya kulevya.
Aidha hakuna ubishi kwamba, viongozi wanaotokana na chama chake ndio walioleta balaa, kwa kuingia mikataba ya kilaghai.

Katika hali kama hii, lazima tukiri kwamba tumewakosea sana watanzania katika hili. Baada ya hapo, tukubali kuanza upya. Magufuli sio lazima asimame hadharani na kuutangazia umma kwamba viongozi wa chama anachokiongoza wamehusika kulihujumu taifa hili. Hatua anazochukua ni uthibitisho tosha kwamba amekiri kuwepo na tatizo.

Ripoti ya iliyotolewa wiki iliyopita, kuhusu kiasi cha madini kinachokuwepo kwenye mchanga unaosafirishwa na makampuni yanayochimba, haikushtua sana, kwa sababu hata wananchi wa kawaida wanajua kwamba tunaibiwa. Bila kujali uhalali wa takwimu na kamati yenyewe ya uchunguzi, hakuna mashaka hata chembe kwamba tumeibiwa sana. Na wakati wote huo tumekuwa tukilalamika kuibiwa.

Anapojitokeza mtu kukemea wizi huo, shurti tumuunge mkono. Aidha tuna jukumu la kuishauri serikali kuchukua hatua dhabiti ili kuhakikisha rasilimali zetu zinawanufaisha watanzania. Kukosoa sio dhambi kabisa, lakini ni vema tukosoe kwa nia ya kuboresha juhudi za serikali. Vinginevyo kupinga kabisa nia njema anayoionyesha Rais, tutakuwa tunashiriki dhambi.

Ni muhimu sana wananchi kumuunga mkono Rais JPM katika hili, kwani mataifa ya Ulaya na Magharibi hawako na furaha, na hawaishiwi mbinu. Thomas Sankara, alijitokeza kama Che Guavara wa Afrika kutetea rasilimali za nchi yake na Afrika, lakini kilichompata imebaki kuwa simulizi tu.

Tumuunge mkono Rais JPM, vita anayopigana ni ngumu sana na ni aghalabu kushinda. Rais mwenyewe lazima awe makini sana kwa kila hatua anayochukua. Muhimu sana, ni kwamba wachimbaji wa madini hayo, wapo kisheria. Wanatuibia ndani ya sheria. Hivyo ni muhimu sana, kuchukua hatua zilizo ndani ya sheria. Kujua tatizo ni njia mojawapo ya kutatua tatizo. Sote tunatambua kwamba, ni kweli tunaibiwa. Sasa sio muda wa kulialia. Tujifute machozi na kufunga vizuri mikwiji. Wananchi tumuunge mkono Rais.

Wabunge watimize wajibu wao. Kilio chao cha muda mrefu kudai mikataba ya madini iwekwe wazi, huu ni muda mwafaka. Wasiishie tu kupongeza au kuponda. Bila kujali itikadi za vyama vyao (mara nyingi sana wanasimamia masilahi ya vyama vyao), mara hii wasimame pamoja. Waibane serikali kuweka wazi mikataba yote ya uchimbaji wa madini, baada ya hapo mikataba hiyo ipitiwe upya.Tuanze upya. Bahati nzuri madini hayaozi. Sasa kama serikali itakataa kuweka wazi mikataba hiyo, vita anayopigana Magufuli itakuwa kiini macho.

Kwa upande mwingine serikali ikubali kupokea maoni kutoka kwa watu mbalimbali. Nchi hii ni ya kwetu sote. Wote tunawajibika kujenga Taifa hili, kwa faida ya wote. Serikali ikubali kukosolewa hata kwa watu isiowapenda. Upinzani sio vita. Tupingane kwa hoja. Serikali iwasikilize wananchi wake. Isiweke pamba masikioni.
 
Hapo uliposema ccm watoke waombe radhi kwani wao ndio walituletea balaa hili.........ndio pagumu!
Hawataki kukubali ukweli, ila wanalazimisha kila MTU amuunge mkono raisi hata kama njia ya mapambano tunaona sio sahihi!
 
Ccm uwasikilize ukawa? Nyie tusubilini tuu miujiza ilihili taifa lionekane halina laana. Vingne nikujiburudisha tuu ili siku ziende hakuna la maana hapo.
 
Mkuu umeshauri vyema Sana Kama yule mwingine. Watu wakishamaliza kucoment nitakuambia umeshauri Kama nani. Hongera Sana kwa busara hizi
 
Hoja zinapokwisha vinakujaga vitisho jiandaeni kurudisha miamala miliyochukua kwa sababu kazi miliyopewa aitafanikiwa
 
Sasa wanafanya kinyume na wewe!

Huku wakikuterm ulikuwa dikteta kwa kuziba mianya ya rushwa na wizi katika awamu yako.

Waliobaki hawana uchungu na mali za Taifi hili, watu wanachota na kuzoa mali za Taifa hili Day & Night.
 
Back
Top Bottom