Rais Magufuli, 2020 usituletee wabunge washereheshaji na wapiga watu magongo

SANCTUS ANACLETUS

JF-Expert Member
Mar 5, 2016
3,010
2,000
Hili ni tatizo kubwa.Wengine wana macho lakini hawalioni.Matatizo ya Mikataba mibovu na hivi kuibiwa rasilimali asilia ni kwa sababu ya kuwa na watu tulioamini wana macho lakini kumbe hawaoni.Kuwa na rasilimali na fursa kibao lakini zilizoshindwa kutuletea ustawi katika maisha yetu chanzo chake ni kuwa na watu tuliowadhania wanafikiria kwa Kichwa na wanatembea kwa miguu kumbe sivyo.Tuna viongozi na rasilimali watu wanaofikiria kwa kutumia miguu na wanatembelea vichwa.Tukio la Dodoma ni kilele cha haya ninayoyasema.Huwezi kuwaweka kando kwa mwaka mzima watu ambao Mara zote wameonyesha kuwa wanatumia vichwa kufikiria namna ya kuimba Tanzania na Miguu yao Mara zote wametumia kuendea kwenye "karakana" hizo za uumbaji.

Ninafahamu kuwa mtoto umuleavyo ndivyo akuavyo.Kuna watu wengi Leo hapa Tanzania wanafanya mambo ya hovyo kuliko hata Nzi afanyavyo si kwa sababu wameumbwa hivyo Bali kutokana na aina ya malezi waliopokea.Kuna mahali katika malezi ya kimwili na kiakili tumemwachia "mungu". Tunazaa watoto tukimaliza tu kazi ya malezi mema inakuwa sio yetu tena.Binadamu sio kuku Wa kienyeji.Mazingira haya ndio yanapelekea tunakuwa Wabunge,Mawaziri na Viongozi wengine ambao wao wanafikiria kuwa kiongozi ni kujua kubwata.Wanajua kuwa kiongozi ni kuwa tu nguvu za kupanua Mdomo na kutapika maneno bila kuyachuja.Kwamba kuwa kiongozi ni kujifunza kupasha watu mipasho mithili ya mipasho ya Taarabu.

Kuumbwa kwa Binadamu na ulimwengu wote kulitumia akili kubwa na Mantiki kubwa.Nasi tulizawadiwa Akili na Mantiki ili tuweze kuendeleza uumbaji kwa nafasi zetu na mazingira yetu. Hatukuzawadiwa magongo ya kutwangia watu vichwani na migongoni ili wazimie.Kiongozi gani anajigamba kwamba anataka Polisi wepesi wa kutwanga watu na Virungu na Magongo ili washike adabu? Kiongozi wa akili ya kuzimisha watu kwa magongo na mateke hawezi kuwa na uwezo Wa kuwaongoza na kuwaelekeza Wabunge waone "devils" katika miswada na hoja za Bajeti zinazowasilishwa mbele ya Wabunge.

Kiongozi mwenye akili na mantiki inayomtuma kuona kuwa mtu mzima akipigwa na gongo ndio anafundishika ni kiongozi anayefikiria kwa miguu na kutembelea Kichwa.

Mbunge anayetumia akili na Mantiki kuona mawazo pinzani hayafai isipokuwa ya chama tawala huyo hana tofauti na ndege Mbuni anayeficha Kichwa chake huku akiacha makalio wazi.Ni ajabu kuwa Mbuni akiona hatari mbele yake husahau kuwa Kichwa pekee ndicho kitamsaidia kujiokoa na sio makalio anayoyaacha juu tena yenyewe yakigalagala tu bila msaada wowote.

Tunahitaji viongozi wanaotumia akili na mantiki mithili ya Nyoka aina ya Cobra.Kwamba akiona hatari kichwa ndio huchukua nafasi zaidi kuliko viungo vingine katika mwili wake.

Rais Magufuli pamoja na kwamba baadhi yetu tunakukubali kwa kazi nzuri unayoifanya lakini lazima tukuambie wazi wazi kuwa CCM yako chini ya viongozi kama hawa wanaota kutwanga watu magongo ndio walioifikisha nchi hapo ulipoikuta.Ni CCM chini ya Viongozi wapiga watu magongo ndio waliofanya nchi uikute sio donor country wala haiitwi Developing Partner(DP).

Pale baadhi ya Wapinzani walipotumia akili na mantiki kushauri mambo na jinsi ya kuendeleza uumbaji mujarabu Wa nchi yetu wana-CCM wenzio walitumia magongo kuwapiga na kuwafukuza Bungeni.Kwa sababu pengine wewe mwenzetu ulipozaliwa na kulelewa hukufundishwa utamaduni Wa kutwanga watu na magongo tunaomba mwaka 2020 usituletee tena Bungeni watu wenye akili na mantiki zilizojaa maono ya magongo kwa matumizi ya kutua katika vichwa vya wenzao bali magongo katika kugeuzwa na kuwa madawati mashuleni.Magongo kwa matumizi ya fanicha za wao kukalia Bungeni na maofisini.

Kama Mwenyekiti wa Chama chako usipitishe majina ya Wabunge watakaokuja kuwa washereheshaji.Usipoliona hili basi ujue hakutakuwa na viwanda.Wabunge wa aina hii wanakuona kuwa wewe ndiye unapaswa kuwa think tank ya nchi pekee na wao kazi yao kupiga mapambio na vigelegele.

Ulimwengu uliumbwa na unaongozwa na Mungu katika Utatu Mtakatifu tena ulioshikamana sana na wenye umoja. Je, wewe utaweza bila nguvu ya watanzania wengine? Utaweza kuumba nchi hii kwa kuambatana na kushikamana na watangwaji Wa watu wengine magongo? Tuletee watu wenye magongo ya hoja na si magongo ya miti.Usituletee washereheshaji.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom