Raia Mwema; Rostam, Lowassa wakatwa miguu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Raia Mwema; Rostam, Lowassa wakatwa miguu

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Apr 14, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Apr 14, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 61
  Trophy Points: 145
  [​IMG][​IMG]

  Waandishi Wetu, Dodoma
  Aprili 13, 2011

  [​IMG]Yumo pia Chenge, sasa watakiwa kujiuzulu

  [​IMG]Werema, Malecela, Meghji wawamaliza

  [​IMG]Richmond, Kagoda na Rada zawaponza


  UNAWEZA kusema kwamba huu ni mwisho wa zama kwa Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge ambao, juzi Jumatatu, chama chao kiliwatosa kwa kuwapa siku 90 kujiondoa katika nafasi walizonazo kwa vile wamekuwa wakichafua haiba ya chama hicho.

  Taarifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), iliyotolewa juzi usiku kwa vyombo vya habari, mjini Dodoma, imeeleza kwamba vikao vya juu vya chama hicho vinataka wanasiasa hao watatu wajiuzulu nafasi zao zote za uongozi katika Chama.

  Vikao hivyo vya Sekretariati, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu (NEC), vilivyokuwa vimeanza Jumatano ya wiki iliyopita na kukamilika juzi usiku, vililenga kutekeleza dhamira ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ya chama hicho ‘kujivua gamba'.

  Dhana ya CCM kujivua gamba inahusishwa na matokeo mabaya ya chama hicho katika uchaguzi wa 2010 ambapo kilipata upinzani mkali kutoka Chadema.

  Chenge, Rostam, Lowassa wapime wenyewe
  "Kama mlivyomsikia Mwenyekiti (Jakaya Kkwete) wale wote ambao wamekuwa wakituhumiwa kukichafua Chama, NEC imeamua watupishe.

  "Uamuzi ni kwamba katika miezi mitatu wapime wenyewe, wajiondoe katika nafasi zao. Kama watakuwa hawajafanya hivyo katika miezi mitatu ijayo, hadi tutakapokutana hapa, basi chama kitawaondoa," alisema John Chiligati, Katibu wa uenezi katika sekretariati iliyopita ambaye mabadiliko yaliyotangazwa juzi yamempa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara).

  Kuanguka kwa Lowassa, Waziri Mkuu aliyejiuzulu mwaka 2008 ambaye pia ni Mbunge wa Monduli na mjumbe wa NEC, Rostam Aziz ambaye ni mfanyabiashara, Mbunge wa Igunga na mjumbe wa NEC na Chenge, mwanasheria aliyechafuka baada ya kutumikia nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kipindi chote cha awamu ya Benjamin Mkapa, Mbunge wa Bariadi Magharibi na mjumbe wa NEC, ni jambo lililotarajiwa.

  Wanasiasa hao watatu wamekuwa wakitajwa katika tuhuma mbalimbali za ufisadi lakini uongozi wa CCM umekuwa ukitetea ukidai kutokuwapo kwa ushahidi wa kisheria dhidi yao.

  Mwanasheria Mkuu achochea ‘moto'
  Pengine aliyeharakisha kuanguka kwao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye alikuwa ameitwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mwenyekiti Kikwete, kutoa ufafanuzi kwa Kamati Kuu juu ya mambo kadhaa, likiwamo suala la mchakato wa Katiba mpya.

  "Kifo cha kina Lowassa, Rostam na Chenge kimeharakishwa na Werema. Aliletwa na Mwenyekiti kuja kufafanua mambo kadhaa kama mchakato wa Katiba mpya.

  "Katika mchango wake kama mtu aliyeko nje ya Chama, alizungumzia mambo ambayo yeye alisema hayaendi sawa ndani ya CCM. Kwanza alianza kwa kusema yeye si mwana CCM; japo huko nyuma, kama walivyokuwa wengi, alipata kuwa mwanachama.

  "Akasema kwao anakotoka (Jaji Werema anatoka Mkoa wa Mara) mwanamume anapaswa kusema ukweli hata kama ukweli huo unauma kiasi gani.

  " Akasema kwamba alikuwa anaona tatizo kwamba taarifa nyingi za vikao kama hicho alichokuwa ameitwa kuzungumza, zilikuwa zinavuja sana.

  " Akasema hata hayo ambayo angeyasema, jioni yangekuwa yamewafikia watu wa nje, na wahusika wakubwa wa kuvujisha taarifa hizo walikuwa ndani ya Kamati Kuu hiyo hiyo.

  " Akiachana na hilo, akahoji kwa nini, chama hicho kinalialia kuwa haiba yake imeshuka na wakati huo huo kikikumbatia vitu kama Richmond na Dowans ambavyo vinaichefua jamii na ambavyo wahusika wake wakuu wamo katika uongozi wa juu wa chama," anasema mjumbe mmoja wa Kamati Kuu aliyezungumza na Raia Mwema.

  Chiligati, Malecela wapigilia msumari
  Ni kana kwamba moto aliokuwa ameuwasha Jaji Werema jana yake ulirejewa na Chiligati ambaye akiwasilisha ripoti ya Sekretariati kuhusu tathmini ya hali ya siasa nchini na uchaguzi uliopita kwa Kamati Kuu, aliendeleza mwanzo wa mwisho wa safari ya Lowassa, Rostam na Chenge.

  Akizungumza katika kikao cha Kamati Kuu cha kuandaa ajenda za NEC, Chiligati alieleza kwamba haiba ya chama hicho ilikuwa imechafuliwa kwa kiasi kikubwa na viongozi waliokuwa wakitajwa katika tuhuma za ufisadi.

  Bila kutaja majina, Chiligati alisema kwamba tuhuma za kampuni ya kufua umeme ya Richmond ambayo baadaye ilizaa kampuni nyingine tata ya Dowans na kashfa ya ununuzi wa rada, wizi katika Benki Kuu wa kampuni hewa ya Kagoda ni kati ya mambo yaliyochangia sana katika kukinyima kura chama chao katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana na hivyo Sekretariati inapendekeza wahusika na tuhuma hizo wawajibike.

  Taarifa zinasema wajumbe kadhaa walichangia katika ripoti hiyo. Waziri Mkuu wa zamani John Malecela akisema kwa maoni yake isingekuwa muafaka watoswe Lowassa, Rostam na Chenge tu huku ikijulikana kuwa Sekretariti, na hasa Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, akiwa anahusika kwa matendo na kauli zake kukinyima chama kura.

  Mwingine ambaye alipigilia msumari katika ‘jeneza' la wanasiasa hao, ni Zakhia Meghji ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na yeye alimrushia makombora waziwazi Rostam akimtaja kuwa ni mhusika wa kampuni ya Kagoda na kwamba amekuwa akimchafua katika vyombo vya habari; huku akijua kufanya hivyo anaichafua CCM.

  Meghji, ambaye ameingia tena katika Kamati Kuu, anaelezwa kueleza wazi kwamba Rostam anastahili kuchukuliwa hatua bila kuchelewa.

  Sofia Simba awatetea, Kikwete amkejeli
  Na kama kawaida, Lowassa, Rostam na Chenge safari hii pia hawakukosa watetezi. Alisimama Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Sophia Simba ambaye akiungwa mkono na mjumbe mmoja kutoka Zanzibar, walitaka uletwe ushahidi wa tuhuma hizo, vinginevyo hayo yalikuwa ni maneno ambayo yasingeweza kufanyiwa kazi.

  Hatua hiyo ya kina Sophia Simba kwa namna ilikejeliwa na Mwenyekiti Kikwete aliyechomekea ya kuwa ushahidi ulikuwa ni ushindi wake wa asilimia 61 mwaka 2010 badala ya asilimia 82 za mwaka 2005.

  Msekwa, Kinana waongeza nguvu hoja
  Hatua hiyo ya Mwenyekiti Kikwete ilimsimamisha Makamu Mwenyekiti Pius Msekwa, ambaye pamoja na Abdulrahman Kinana walishiriki katika tume ya usuluhishi wa wabunge na viongozi wa CCM mwaka jana ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa umechangiwa na tuhuma za vigogo katika masuala kama Richmond, Dowans, Kagoda na ununuzi wa rada.

  Bila kutafuna maneno, Msekwa alisema katika maoni yote waliyokusanya wakati wa usuluhishi, majina matatu yalikuwa yakipata maksi za juu. Na hayo ni ya Lowassa, Rostam na Chenge.

  Wakati akitaja majina hayo, Chenge na Rostam ambao walikuwa wajumbe wa Kamati Kuu, walikuwa katika kikao hicho na walionekana kuduwaa.

  Msekwa akasema hapakuhitajika ushahidi wa kipolisi kubaini kwamba watatu hao sasa walikuwa ni mzigo kwa chama na hoja za kila mara kwa Upinzani na wakosoaji wa CCM, na kwa ajili hiyo wakitakiwa kuwajibika.

  Taarifa zinasema kwamba huku upepo ukivuma vibaya kwa Lowassa, Rostam, Chenge na Makamba ndani ya Kamati Kuu, alisimama Kinana. Akasema kwamba matendo yote yaliyokuwa yakihusishwa na tuhuma za ufisadi yalifanyika mbele ya macho ya wajumbe wa Kamati Kuu.

  Naye, kama Msekwa, akasema hakukuwa na haja ya kutafuta ushahidi kwa vile tayari nguvu ya umma ilikuwa inataka CCM ichukue hatua dhidi ya ufisadi na watuhumiwa wa ufisadi. Akasema, kwa maoni yake, Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri, ana vyombo vikuu vya kumshauri viwili, Baraza la Mawaziri na Kamati Kuu.

  Taarifa zinasema ni Kinana aliyependekeza Kamati Kuu ijiuzulu kwa kushindwa kumshauri vyema Mwenyekiti, uamuzi ambao kwa muda, ulionekana kuwa ulikuwa unawapunguzia joto na kuwalindia heshima Rostam na Chenge, lakini ambao ungewasilishwa kwenye NEC kupata baraka.

  Makongoro Nyerere mwiba mkali
  Lakini la kuvunda halina ubani, juzi ikiwa tayari Sekretariati na Kamati Kuu za zamani zikiwa zimejiuzulu, akichangia katika tathmini na mapendekezo ya Kamati Kuu ya kutaka Lowassa, Rostam na Chenge wawajibike, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa Mara, Makongoro Nyerere, alizungumza kwa hisia za mguso mkubwa akisema isingewezekana Lowassa, Rostam na Chenge kuendelea kuwa na nafasi za uongozi ndani ya chama.

  Anasema mtoa habari wetu: "Kwanza alianza kwa kumwambia Mwenyekiti kwamba japo yeye ni Mwenyekiti wa Taifa, yeye (Makongoro) naye ni Mwenyekiti wa Mara na kwamba NEC ndio waajiri wa Mwenyekiti Taifa.

  "Akasema anapokaa Mwenyekiti wa Taifa ni mahala patakatifu, na kwa ajili hiyo pasingeweza kusogelewa na shetani, hata kama siku moja Mungu alipata kukutana na shetani barabarani.

  "Akasema kule site (kwenye eneo la ujenzi ambako yeye ndiko anakoshinda akichanganya zege na kupiga bati) wanasema na wanataka watuhumiwa wote wa ufisadi watoke kwenye nafasi zao.

  "Lowassa ni ndugu yangu. Sina matatizo naye. Najua ananipenda, nami nampenda. Lakini kule site wanasema hapana. Atoke. Tena nawe Mweyekiti ulipokwenda Monduli, ukainua mkono wake juu, ukasema hujapata kuona kama yeye (Lowassa), kule site wakauliza, sasa hii ndiyo nini?

  "Rostam simfahamu vizuri. Ninakotembelea yeye hawezi kuja na mimi siwezi kwenda anakotembelea. Sina ugomvi naye. Lakini kule site wanasema naye hapana. Ulipokwenda Igunga ukamuamsha mkono ukasema ni kama timu ya mpira iliyokamilika watu kwenye site wakauliza sasa hii ndiyo nini?

  "Nasikia Chenge wanamwita Mzee wa Vijisenti. Ni ndugu yangu. Sina hakika kama anavyo vijisenti kiasi hicho. Lakini kwenye site, si mimi, watu wanasema naye hapana.

  "Ulikwenda pia Rombo, ukamuamsha mkono Mramba, kule kwenye site watu wakatuuliza hii ni nini?, " alikaririwa akisema Makongoro. Mifano aliyoitaja Makongoro kwa kumhusisha Kikwete ilijitokeza wakati akiwa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010, katika majimbo ya Igunga alikokuwa akigombea ubunge Rostam, Rombo alikokuwa akigombea ubunge Basili Mramba na Monduli alikogombea ubunge Lowassa.

  Akiwa katika majimbo hayo, Kikwete aliwanadi viongozi hao waliokuwa wamepitishwa na chama chake kuwania ubunge, licha ya tuhuma za ufisadi zilizokuwa zikielekezwa kwao.

  Kutokana na hatua hiyo ya Kikwete, makundi mbalimbali ya kijamii nchini yalikosoa hatua hiyo ya Rais kuwanadi watuhumiwa wa ufisadi, akitumia lugha ya "watu hao ni safi" huku Mramba akijinadi kuwa yeye ni panga la zamani lisiloisha makali.

  Habari zinaeleza kwamba wajumbe kutoka Zanzibar walizidi kuwakandamiza Rostam, Lowassa na Chenge, wakisema Visiwani hakuna watuhumiwa wa ufisadi na kwamba hawawezi kuwa chama kimoja na watuhumiwa wa ufisadi wanaokichafua chama, huku wakionyesha kuwa ni kauli ya pamoja kutoka CCM Zanzibar.

  Wajumbe wengi wa NEC-CCM wamelieleza gazeti hili kwamba, mbele ya macho yao, kwa mara ya kwanza Kikwete ameonyesha ni Mwenyekiti wa Chama tangu achukue madaraka hayo.

  Wanaeleza kuwa ameongoza vikao vyote kwa ujasiri mkubwa bila ubabaishaji pengine kama walivyokuwa wamemzoea na wameanza kujenga matumaini juu yake.

  Hata hivyo, wameeleza kuwa uamuzi mgumu uliochukuliwa na chama hicho ni lazima uambatane na juhudi za kubadili hali za uchumi kwa wananchi wa kawaida, vinginevyo itakuwa kazi bure.

  Katika uamuzi wake huo ambao unapaswa sasa kwenda sambamba na juhudi za kubadili hali za uchumi za wananchi, mabadiliko mengine yaliyofanywa yanalazimu Katiba ya chama hicho kubadilishwa.

  Pendekezo Baraza la Wazee liundwe
  Mabadiliko yanayolazimu Katiba kubadilishwa na mkutano mkuu wa CCM ni pamoja na kuanzishwa kwa Baraza la Wazee litakalokuwa na vikao na uamuzi huru na wakati wowote watakuwa na uwezo wa kutaka kuwasilisha mawazo yao katika vikao vikuu vya chama hicho.

  Mbali na baraza hilo, katiba pia itabadilishwa kuruhusu wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama hicho kuchaguliwa kutoka ngazi ya wilaya badala ya ngazi ya mkoa ya sasa.

  Inaelezwa pia kuwa itabidi chama hicho kifanye mabadiliko makubwa ya uongozi katika ngazi nyingine za mikoa na wilaya, ikitajwa bayana kuwa Makamba alikuwa amepachika watu wake wasiokitetea chama hicho kwa mujibu wa katiba yake na badala yake wamekuwa wakitumia madaraka yao kujifaidisha.

  Kejeli za Yusuf Makamba
  Wakati akitoa hotuba ya kuaga mbele ya wajumbe wa NEC, katika hali inayoweza kutafsiriwa kuwa amefurahia kung'oka kwa baadhi ya viongozi wenzake, Makamba alisema ameondoka lakini hakuondoka peke yake.

  Hata hivyo, kati ya watu ambao wameondoka wakiacha alama ya kutafsiriwa kuwa ni viongozi waliokigharimu chama hicho ni pamoja na yeye.

  Mara baada ya Makamba kung'oka watumishi mbalimbali wa CCM, Makao Makuu walishangiliwa, wengine wakijumuika katika tafrija ndogo ikiwa dhahiri kuwa hawakuwa katika utumishi wenye utulivu wakati wa kiongozi huyo.

  Raia Mwema ilimshuhudia mmoja wa wafanyakazi hao akiwa amevalia fulana ya njano, ikionekana imepauka kwa umri, yenye picha ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na maandishi yaliyoanza kufifia yaliyosomeka: "Bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba".
  Raia Mwema ilimuuliza mfanyakazi huyo, kwa nini umevaa fulana hii leo? (siku ambayo habari zilikuwa zinavuma za Sekretariati na Kamati Kuu kujiuzulu).

  Alijibu: " Tena tangu asubuhi nimevaa hivihivi, na nilikaa kwenye lango kubwa ili kila mjumbe wa NEC anayepita hapa asome ujumbe huu," alisema mfanyakazi huyo wa siku nyingi wa CCM. Maneno hayo ya Mwalimu, ya Agosti 1990, yameandikwa pia kwa herufi za mkolezo ndani ya ukumbi wa NEC Dodoma.

  Makamba pia amewahi kutoa kauli mbalimbali zilizopata kutajwa kuudhi baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hicho, hasa wastaafu.

  Katika kongamo la miaka 10 baada ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, baadhi ya viongozi na wadau wengine nchini walijadili na kupendekeza Rais Jakaya Kikwete kuchukua uamuzi mgumu kwa kuwafukuza baadhi ya viongozi wa chama na serikali waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi, na akishindwa ang'olewe yeye.

  Makamba alijitokeza na kujibu kuwa wanaofikiri hivyo ni wendawazimu na kwamba Kikwete hawezi kutoswa kwa sababu ndiye mtaji wa chama hicho.

  Mgawo wa fedha kwa watetezi
  Taarifa zaidi za kiuchunguzi zinabainisha kuwa baada ya upepo kwenda mrama dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi, baadhi ya wajumbe inaodaiwa walipewa fedha kwa ajili ya kuwatetea watuhumiwa hao, walibaki kimya.

  "Kuna wajumbe fulani walipewa fedha kwa ajili ya kuwatetea kama ilivyo kawaida yao na hawa wanajulikana, lakini safari hii walikwama. Walisoma upepo wa kikao na ukali wa Mwenyekiti Kikwete, ilibidi wakae kimya wasije wakahatarisha nafasi zao pia," anaeleza mjumbe mmoja.

  Mbali na hali hiyo, inaelezwa kuwa baadhi ya wajumbe sasa wamekuwa na wasiwasi juu ya hatima yao kisiasa na hasa wale ambao walikuwa wakitumia madaraka yao ndani ya chama hicho kukomoa wanachama wenzao; hasa waliokuwa wakiomba nafasi za uongozi ukiwamo ubunge.

  Imeelezwa kwamba baada ya uamuzi wa ‘kujivua gamba' ngazi ya taifa, CCM sasa itahamishia kazi hiyo katika ngazi ya mikoa na kwamba tayari kuna taarifa za kuchukuliwa hatua kwa viongozi kadhaa wa mikoa wakiwamo Wenyeviti na Makatibu kadhaa.
   
Loading...