Waberoya
Platinum Member
- Aug 3, 2008
- 15,169
- 10,785
Source: Tanzania Daima: ijumaa, 19 septemba 2008HAKUNA shaka hata kidogo kwamba gazeti la uchambuzi wa masuala ya siasa la Rai, linalokuwa mitaani kila Alhamisi, kwa miaka mingi limejipambanua kuwa moja ya magazeti makini na yanayoheshimiwa na wasomaji wengi.
Hata hivyo ni ukweli ulio bayana kuwa, katika siku na miezi ya hivi karibuni, heshima ambayo gazeti hilo liliijenga kwa miaka mingi imekuwa ikiporomoka.
Miongoni mwa sababu ambazo zimechangia kuporomoka huko kwa Rai ni mwenendo usiofaa wa mhariri wake wa sasa, Deodatus Balile, ambaye amekuwa bingwa wa uandishi na uhariri unaoongozwa na misingi ya hisia, badala ya miiko na maadili ya uandishi wa habari.
Watu wanaomfahamu Balile vyema kama tulivyo sisi, ni mashahidi wa namna ambavyo mwanahabari huyo amekuwa akifanya kazi zake kwa kuwafurahisha mabwana zake ambao kwa bahati mbaya katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakikabiliwa na tuhuma nzito za ufisadi.
Katika kutimiza malengo yake hayo, Balile amekuwa akifanya kila linalowezekana kuwashambulia kwa hoja za kuzusha, kejeli na wakati mwingine matusi, watu wote ambao anadhani wamekuwa chanzo au msingi wa matatizo yanayowakabili wanasiasa wa kundi fulani, ambao amekuwa akiwaabudu kwa mfano wa miungu watu.
Ili kufanikisha kazi hiyo ambayo hakuna shaka amekuwa akiifanya kwa maelekezo mahususi yaliyojengwa katika misingi ya kulipa kisasi, kukomoa, kutukana na hata kuchafua watu, Balile amegeuka kibaraka wa hoja, sambamba na kuwa mtumwa wa ushawishi wa wanasiasa wa kundi hilo ambao wamejeruhiwa kimamlaka, kwa makosa ambayo ama waliyafanya wao moja kwa moja au yalifanywa na ofisi walizopewa dhamana ya kuziongoza.
Miongoni mwa wanasiasa ambao amekuwa akifanya juhudi kubwa za kujaribu kuwasafisha kutokana na majina yao kuchafuka baada ya kutajwa katika kashfa kadha wa kadha za kifisadi katika miezi ya hivi karibuni, ni pamoja na Rostam Aziz na Edward Lowassa.
Historia inaonyesha na kuthibitisha wazi kwamba, Balile amekuwa kinara na mmoja wa wanahabari ambao wamekuwa wakimpamba Lowassa tangu mwanasiasa huyo alipokuwa Waziri wa Maji na Mifugo, zama za Serikali ya Awamu ya Tatu na akaendelea na kazi hiyo, ama kwa kujipa mwenyewe au kwa maelekezo, hata alipokuwa waziri mkuu kabla hajalazimika kujiuzulu Februari mwaka huu, wakati jina lake lilipotajwa katika ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.
Katika kutimiza azima yake hiyo, Balile amekuwa akitumia vibaya mamlaka ya uhariri aliyonayo kuwapaka matope watu wote na taasisi ambazo amekuwa akiamini kuwa zilichangia katika kuwaangusha na kuwafikisha pale walipo leo wanasiasa hao wa kundi lake.
Ushahidi wa hili ni rahisi kabisa, kwani tangu akabidhiwe gazeti hilo akiwa mhariri, habari nyingi kubwa zinazoandikwa zimekuwa zikiwalenga kwa maana ya kuwashambulia kina Freeman Mbowe, Dk. Willibrod Slaa, Zitto Kabwe na John Mnyika, ambao ni viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kimekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi kwa takriban mwaka mmoja sasa.
Ni wazi kwamba kwa namna ya kishabiki, Balile amekuwa akishindwa kuficha hisia zake, hali iliyosababisha awe akikitaja chama hicho cha upinzani na viongozi wake kuwa watu walioshiriki katika kile anachokiita kuwazushia watu uongo, kuwapaka matope na hata kusababisha wangatuke.
Si hao tu, Balile amekuwa akilishutumu Bunge na akafikia hatua ya kumwandama waziwazi, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, si kwa hoja, bali kama ajenda zinazoonyesha hasira ya namna taasisi hiyo ilivyoshiriki kikamilifu katika kile anachokiona kuwa ni kuwaangusha, kuwanyamazisha na kuwahujumu wanasiasa wa kundi analoonekana kuliabudu.
Akitumia mwelekeo huo huo, Balile katika toleo la jana la gazeti la Rai, baada ya kuona juhudi zake za kuwashambulia wanasiasa hazitoshi na pengine zimeshindwa kuzaa matunda, akaamua kuliingiza gazeti hili la Tanzania Daima katika propaganda zake chafu za kuwasafisha wanasiasa wake hao na kuwachafua wale wanaoonekana kuwa wabaya wao.
Kwa namna ya kujidhalilisha na pengine kujikana mwenyewe, mhariri huyo wa Rai akaandika habari moja iliyoanzia ukurasa wa kwanza inayomshutumu Mbowe na CHADEMA, akiwatuhumu kulitumia Tanzania Daima kuwachafua wanasiasa na baadhi ya viongozi wa serikali ya Kikwete.
Katika kuonyesha kwamba ni mtu aliyechanganyikiwa, Balile ambaye kabla ya kujiunga na Rai akitokea masomoni Uingereza alikuwa Mhariri Mkuu wa kwanza wa Tanzania Daima, akafikia hatua ya kuliita gazeti hili kuwa ni la CHADEMA, ilhali akijua kuwa yeye mwenyewe alishiriki kikamilifu kulisajili.
Katika hali hiyo inayoonyesha hulka ya uongo iliyojengeka ndani mwake, akafanya hivyo akisahau kwamba, ni yeye mwenyewe ambaye wakati akiwa mhariri wa gazeti hili alipata kuandika kwa zaidi ya mara moja tahariri akipinga maneno ya watu waliokuwa wakijaribu kulihusisha gazeti hili na chama cha siasa ambacho leo anakihusisha na chombo alichoshiriki kukianzisha. Huu ni unafiki unaovuka mipaka.
Katika kujistawisha kiuongo, katika tahariri ya Rai ya jana, Balile alifikia hatua ya kulizushia uongo mwingine Tanzania Daima, akidai kuwa, ndilo lililohusika kumwangusha Lowassa, na kwamba limekuwa likiwatukana watu matusi ya nguoni.
Hakuna shaka kwamba, maandishi ya namna hii ni ya uzushi na kimsingi ni matusi, si kwa Tanzania Daima tu, bali hata kwa taasisi za umma ambazo tunaamini zinafanya kazi ya kuhakiki mwenendo na kazi za kila siku za vyombo vya habari nchini, na kuhakikisha vinaendesha shughuli zake kwa kuzingatia maadili ya kazi ya uandishi wa habari.
Sisi wa Tanzania Daima tunaamini kwamba, taasisi zinazosimamia maadili ya kazi ya uandishi wa habari hazitakaa kimya pasipo kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya gazeti la Rai, wamiliki wake na hususan mhariri wake, ambaye hakuna shaka, amejipambanua kuwa mwanahabari aliyechanganyikiwa, na mtu aliye tayari kugharamia kupoteza thamani ya utu wake kwa sababu tu ya kuangalia masilahi yake. Hakika huyu ni mchumia tumbo.
Wakati tukiamini kwamba kilio chetu dhidi ya Rai na hususan Balile kitakuwa kimefika mahali panapostahili, sisi wa Tanzania Daima tunapenda kueleza bayana kwamba, tumeamua kwa dhati kushughulika ipasavyo na umamluki wa aina hii wa uandishi wa habari kwa kufuata taratibu za kitaaluma na kisheria, ili jambo hili liwe fundisho kwa watu wengine wenye hulka za namna hii, ambazo hatuna shaka ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya taifa letu. Mungu ibariki Tanzania.
Waberoya: Mhariri wa Tanzania Daima Amenifurahisha!!Big Up Kibanda
Waberoya
I have come to the conclusion that politics are too serious a matter to be left to the politicians. Charles De Gaulle (1890 - 1970