Profesa Kahyarara: Mwl Nyerere, uchumi na maendeleo

Profesa Kahyarara: Mwl Nyerere, uchumi na maendeleo

SautiYaMnyonge

JF-Expert Member
Joined
May 13, 2018
Posts
439
Reaction score
742
Taarifa hii inamuelezea Mwalimu Nyerere katika tasnia ya uchumi. Tathmini yake inazingatia:-
i) Mtazamo na Msimamo wake katika uchumi

ii) Mafanikio yake

iii) Changamoto alizozipitia na

iv) Mambo ya kujifunza.

~Mwalimu aliamini katika ujamaa wa kidemokrasia, uhuru wa kiuchumi, kujitegemea, usawa haki na fursa ya kumiliki na kunufaika na uchumi wa kitaifa.

~Alichukia mfumo wa kinyonyaji wa uchumi wa dunia na umuhimu wa nchi kusimamia uchumi kuitosheleza kwa kujenga viwanda na kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje. Alikataa masharti ya IMF na World Bank, Madhara ya masharti hayo yameonekana na kulazimisha mashirika haya kubadili mtazamo na kuanzisha Poverty Reduction Strategies na Debt relief mambo ambayo Mwalimu aliyatabiri mwaka 1979.

~Kitaaluma Mwalimu Nyerere alikuwa msomi wa kiwango cha juu na katika shahada yake ya uzamili alisoma Uchumi, Siasa, Social Anthropology, constitutional law na moral philosophy hivyo alikuwa na uwezo mkubwa wa kimataifa katika kufuatilia na kushiriki katika mijadala na mipango ya uchumi wa kimataifa na ule wa Tanzania.

~Mtazamo wake kiuchumi, Mwalimu Nyerere aliamini katika ujamaa wa kidemokrasia. Ujamaa huu ni tofauti ule wa Urusi, China au Cuba ambao ni wa kimapinduzi. Ujamaa huu wa kidemokrasia Fabian system chimbuko lake ni Uingereza na nchi za ulaya. Ni ujamaa wa hiari, na umekuwapo kwa muda mrefu na bado unaishi.

~Mwalimu aliamini kuwa kutokana na muundo wa maisha ya waafrika ikiwemo wa Tanzania maisha ya kuishi katika jamii na ushirikiano, kusikilizana na kujadiliana, mfumo sahihi wa maendelea ungekuwa huu wa ujamaa wa kidemokrasia.

~Msimamo wa Mwalimu katika uchumi
Msimamo wake ulikuwa ni Uhuru wa kiuchumi ambao unashirikisha wananchi katika kupanga na kumiliki uchumi wa nchi yao, umma kumiliki rasimilali za taifa kwa maendeleo ya kitaifa. Kwa bara la Afrika alisimamia nguvu ya pamoja ili Bara zima lijitawale kiuchumi, liheshimike na kuwa na sauti katika mfumo wa uchumi wa dunia kwa kuondoa unyonyaji hasa katika uuzaji bidhaa nchi za viwanda pamoja na upangaji bei. Mwalimu alisimamia biashara baina ya nchi za kiafrika kupitia OAU, kundi la mataifa 77 masikini na ushiriki katika mikataba kama ya Lome

¤ Uchumi wa Tanzania chini ya Uongozi wa Mwalimu Nyerere;

~Aliwaongoza wa Tanzania kuanzisha ujenzi wa uchumi wa kijamaa wa kidemokrasia. Msingi mkuu ulikuwa ni Uchumi uliojikita katika usawa na kuheshimiana, kuwapa haki raia wa Tanzania kumiliki uchumi wao wenyewe, kutoa haki ya kupata hifadhi ya maisha na mali aliyonayo kwa mujibu wa sheria, kuhakikisha haki ya malipo halali ya kazi bila unyonyaji umiliki wa rasilimali za nchi kama dhamana kwa vizazi vijavyo, na wajibu wa serikali kuhakikisha inasimamia ukuaji wa uchumi. Njia kuu za kiuchumi ikiwemo viwanda, mabenki, mashamba makubwa majumba ya kupangisha, migodi na rasilimali nyingine vilitaifishwa na kumilikiwa na umma.

¤Mipango ya Maendeleo na Mwelekeo wake

~Katika kuhakikisha maendeleo ya uchumi yanatekelezwa kwa ufasaha Mwalimu alianzisha Tume ya Maendeleo ya uchumi ambayo mwaka 1964 aliibadilisha na kuwa Idara ya mipango ya maendeleo.

~Kazi ya IDARA hii nyeti ilikuwa kusimamia Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano (1965-1969), Mpango wa piili wa maendeleo (1969-1974) na Mpango wa tatu wa maendeleo (1976-1981). Katika mipango ya maendeleo Mwalimu Nyerere aliweka msisitizo wa ujenzi wa uchumi unaojitegemea kwa kutumia rasilimali zake na kuongeza mauzo ya nje ya bidhaa zilizo chakatwa.

~Mipango iliweka mkakati wa ujenzi wa uchumi wa Viwanda lengo likiwa kuchakata asilimia 85 ya mazao kama pamba. Hii ilipelekea serikali kujenga viwanda vya nguo 12. Sungura textile, kiltex Arusha, Kiltex Dar es salaam, Mwatex, Mutex, Tabora Textile, Ubungo Spining, Urafiki, Mbeya Textile, Morogoro Ployster na vinginevyo.

~Licha ya nguo mwalimu alihimiza ujenzi wa viwanda kama karatasi, vinywaji, vyakula, vifaa vya ujenzi, vifungashio, uungganishaji mitambo na magari, madawa na vinginevyo. Tanzania iliweza kuwa na viwanda vikubwa katika Bara la Afrika kikiwemo kiwanda cha karatasi SPM Mgololo kikiwa na thamani ya dola milioni 300. Viwanda vingine vikubwa vilikuwa ni General Tyre, Mangula Machine tools, Kilimanjaro Machine tools.

¤Matokeo na Mafanikio

~Katika kutekeleza mipago na mtazamo wa uchumi chini ya Mwalimu Nyerere Mafanikio makubwa ya viwanda yalipatikana hasa kufikia katikati ya miaka ya sabini ambapo Tanzania ilikua inajitosheleza kwa bidhaa za viwanda ikiwemo vifaa vya ujenzi, radio, umeme, nguo, vyakula, vinywaji, madawa na pembejeo. Mchango wa sekta ya viwanda kwa Pato la taifa uliongezeka kwa asilimia 400. Mchango wa sekta ya viwanda katika ajira uliongezeka kwa asilimia mia tano.

~Uwekezaji katika sekta ya viwanda nao uliongezeka sana mauzo ya nje yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia 100 kutoka asilimia 9.9 mwaka 1966 hadi kufikia asilimia 22.3 ilipofika miaka ya 1980. Tanzania ilifanikiwa kupunguza utegemezi wa bidhaa zilizoagizwa kutoka nje hasa vifaa vya shule, nguo, vyakula, vyombo vya nyumbani, mbolea na maeneo mengine.

~Maendeleo katika sekta ya kilimo Mwalimu alihimiza kilimo katika ngazi ya vijiji na mashamba makubwa kupitia sera na maelekezo kama vile Siasa ni Kilimo, Kilimo cha kufa na kupona, kilimo ni uti wa mgongo.

~Tanzania iliendelea kuwa mzalishaji mkubwa wa zao la mkonge duniani na mengine kama vile Korosho, Chai, Pareto, Tumbaku, Kahawa na Karafuu. Tanzania iliwekeza sana katika utafiti na vituo vya mbegu bora kama vile Ukiriguru, Uyole, Ilonga, Maruku, Nalindere pamoja na kuimarishwa kwa chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine.

~Mafanikio mengine yalikuwa ni Tanzania kuwa na ujazo zaidi wa fedha za kigeni kuliko matumizi yake (Positive Trade Balance) na ndio maana iliweza kuwa na shilingi yenye thamani kubwa. Dola moja ilikuwa sawa na shilingi tano na ndio ilizaa mabasi ya daladala wakimaanisha shilingi tano tano kwa miaka ile.

~Paundi ya Uingereza ilikuwa shilingi 20. Hata wale waliosema shilingi ilikuwa over valued (World Bank na IMF) walikuwa wakibishana kuwa shilingi ya Tanzania ilikuwa overvalued kwa asilimia 57%.

¤Mafanikio katika maeneo mengine ya kiuchumi ni:-

~Kwa kutambua utajiri mkubwa wa nishati na madini Mwalimu aliahidi kuwa ipo siku Tanzania ingejitosheleza katika mafuta ya petrol na kuchimba madini yake kutumia wataalamu wake. Alisimamia uanzishwaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli TPDC, na kupeleka vijana wengi kusomea fani ya utafiti, utawala, mipango, fedha, biashara na uchimbaji wa mafuta na gesi. Mwaka 1972 alianzisha shirika la madini STAMICO kutekeleza jukumu kama hilo kwa upamde wa madini na uanzishwaji wa migodi. Itakumbukwa Kiwira, Mchucmuma, Liganga, Nyakabanga.

~Aidha Mwalimu aliwekeza katika ukataji almasi TanCut Almasi. Lengo lilikuwa kuongeza thamani ya almasi iliyouzwa nje.

¤Matatizo makubwa ya uchumi yaliikumba Tanzania wakati wa Mwalimu kuanzia katikati ya miaka ya 1970 mpaka miaka ya 1980 mwanzoni.Taarifa inasisitiza kuwa matatizo haya hayakutokana na sera za uchumi za Mwalimu, bali yalitokea wakati Mwalimu akiwa Rais wa Tanzania. Matatizo haya yalikuwa ni:-

~Kupanda sana kwa bei ya mafuta kwa asilimia 400, hatimaye Serikali ilijikuta ikitumia asilimia 60 ya fedha zote kigeni kuagiza mafuta peke yake.

~Kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika mwaka 1977 kulilazimisha Tanzania kuwekeza katika mashirika ya Reli, Ndege, Posta na Bandari ili kunusuru huduma hizo.

~Ukame uliathiri sehemu kubwa ya nchi.

~Soko la mazao ya mkonge Duniani lilianguka.

~Mwaka 1978 Tanzania ililazimika kuingia katika vita na Uganda

~Kusambaratika kwa nchi za Ulaya Mashariki hasa USSR na Ujerumani Mashariki.

¤Katika kutafuta ufumbuzi mijadala ya mageuzi iliibuka. Msimamo wa Mwalimu Nyerere katika mageuzi:-

~Mwaka 1979 Mwalimu Nyerere alikataa masharti yote ya shirika la fedha duniani na kuwafukuza wataalamu hao.

~Aliwashangaa kutokubaliana na sababu za msingi za uchumi kuyumba na kung'ang'ania imani kuwa mfumo wa uliberali ni muarobaini wa matatizo yote ya uchumi masharti ambayo hayakuendana na mtazamo na sera za nchi za kujenga uchumi wa kitaifa, unaosimamiwa na kulinda thamani ya sarafu. Mwaka 1981 Tanzania iliandaa mkakati wake wa kufufua uchumi-National Economic Survival Program (NESP) na mkakati wa miaka mitatu wa Structural adjustment program (1982 mpaka 1985).

~Mwaka 1983 serikali ya Mwalimu nyerere chini ya Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine iliongeza usimamizi wa utekelezaji wa vita ya uhujumu uchumi, nidhamu katika matumizi ya fedha za umma na ufuatiliaji wa utendaji katika mashirika ya UMMA na taasisi za serikali. Kwa mshangao takwimu znaonesha kuwa licha ya matatizo makubwa ya uchumi wakati ule palianza kujitokeza dalili za kufufuka kwa uchumi.

~Mwaka 1984 mashirika yaliyokuwa yanapata faida yaliongezeka sana na kufikia 213 kati ya mashirimambo 384. Serikali ilianzisha utaratubu wa kushirikisha sekta binafsi katika baadhi ya shughuli za umma ikiwemo kuanzishwa kwa daladala kwa kusimamiwa na UDA jijini Dar es Salaam.

~Mwalimu Nyerere aling'atuka mwaka 1985 baadaye Tanzania ikaingia makubaliano ya kurekebisha uchumi na kukubaliana na baadhi ya masharti ya IMF ikiwemo kushusha thamani ya shilingi na kubinafsisha mashirika ya umma. Mwalimu Nyerere kwa wakati tofauti aliweka wazi kuwa hakupinga mageuzi ya uchumi lakini alitilia shaka kasi ya kukubaliana na matakwa ya wataalamu wa nje ikiwemo suala la ubinafsishaji.

~Matokeo ya utekelezaji wa mageuzi
baada ya Tanzania na nchi nyingi zinazoendelea kukubali kutekeleza mageuzi ya uchumi matokeo yake yalikuja na sura tofauti. Kubwa umasikini uliongezeka sana, baadhi ya watu walishindwa kupeleka watoto mashuleni, madeni yaliongezeka sana, sekta hasa ya kilimo ilikumbana na changamoto ya kukosa ugani. Bei ya pembejeo ilipanda, thamani ya shilingi iliporomoka sana, riba zikaingezeka na ukosefu wa ajira kwani viwanda vingi vilifungwa ili kujiandaa kuvibinafsisha.

~Aidha zoezi la ubinafsishaji lilipelekea kuuzwa kwa viwanda ambavyo vingine mpaka leo havijawahi kufanya kazi, sehemu nyingine mashine zimeondolewa. Kufuatia mkanganyiko huu mchumi nguli duniani Professor Joseph Stiglitz aliandika kitabu Globalization and its disconents ambapo aliyoyazungumza kwa asilimia kubwa ni yale aliyoyasema mwalimu mwaka 1979 wakati akiwakatalia kutekeleza masharti hayo.

~Katika kuweka mambo sawa Debt Relief Program na Poverty Reduction Programs ni mambo yaliyoongezwa sasa katika mageuzi ya World Bank na IMF ingawa Mwalimu Nyerere aliyasimamia katika taarifa yake ya tume ya nchi za kusini yaani South-South Commission na aliyatabiri haya mwaka 1979 na aliwauliza je mnataka Tanzania iue biashara zake ianze kuagiza kila kitu kutoka nje? Hawa watanzania maskini wataweza kulipia huduma za kijamii?. Yote hata ni shuhuda kuwa Mwalimu Nyerere alijua alichokuwa anakisimamia katika uchumi na dunia ilikwisha tubu na nchi masikini zimeendelea kumuenzi na kumheshimu.

¤Mambo makubwa ya kujifunza kutoka kwa Mwalimu:-

~Umuhimu wa kujitegemea ili kuwa huru kiuchumi

~Viwanda ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo na hatimaye nchi kwa ujumla

~Mkakati wa kuchataka angalau asilimia 85 ya pamba kujitosheleza wenyewe

~Ni vema serikali ikaendelea kusimamia uchumi ikiwemo viwango vya riba, kulinda thamani ya shilingi na

~Usimamizi wa uzalishaji kuanzia ugani, pembejeo, bei na upatikanaji wa masoko.

~Nchi masikini kuendelea kuwa na sauti ya pamoja katika kupigania usawa katika uchumi wa dunia.

~Nchi za kiafrika zina fursa ya kukuza biashara miongoni mwao zenyewe na kubadilishana uzoefu katika uchumi.

~Mshirika ya umma yakisimamiwa vizuri yanafaida zaidi kwani serikali inapata kodi pamoja na gawio tofauti na biashara binafsi ambazo zinatoa kodi peke yake.

~Sera ya ujamaa na kujitegemea bado haijapitwa na wakati na ni tofauti za kimtazamo kwani ujamaa wa kidemokrasia una fursa ya kuamua aina ya mfumo wa uchumi na si kweli kuwa mfumo wa kiuchumi ndio inaamua mfumo wa itikadi. Ndio maana bado tuna bodi ya Mikopo, bodi ya nafaka, bima ya afya, hifadhi ya jamii, huduma za ugani kwa wakulima nk yote haya yanategemea ruzuku kubwa ya serikali.

Huyu ndiye Mwalimu Julius Kambarage Nyerere niliyemfahamu. Hakika ni urithi wa thamani kwetu kama Taifa.
IMG-20191004-WA0034.jpeg
 
Back
Top Bottom