Profesa Chachage: Mbegu itakayoota kesho

Profesa Chachage: Mbegu itakayoota kesho

Bujibuji Simba Nyamaume

Platinum Member
Joined
Feb 4, 2009
Posts
79,290
Reaction score
169,252
KWA binadamu wanaozaliwa na
mwanamke, wakaishi, wakafanya
mambo yao, wakifa inaleta kihoro
na msiba kwa watu wengi.
Lakini wapo wengine ambao
utamani kuamini walizaliwa na
mwanamke wakaishi katika jamii
ya binadamu wakifa japo si mila
njema kushangilia kifo, watu
ukaa na kusema afadhali shetani
kachukua mtu wake. Labda kila
binadamu upenda kujua lipi kati
ya haya mawili yatatokea siku ya
kifo chake.
Na Julai 12 mwaka jana, katika
Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, walikusanyika
watu wa matabaka yote, wenye
hadhi, makabila na jinsia zote
wakiongozwa na Rais Jakaya
Kikwete, walikuja kutoa heshima
za mwisho kwa msomi.
Ni nani huyo? Si mwingine ni
hayati Profesa Chachage
Chachage (51).Chachage ni
nani? Alifanya nini hata makundi
hayo yakaitwa na kifo chake?
Hakuna msomi mwingine ndani
ya nchi hii ambaye kifo chake
kilivuta wingi wa watu kama
hawa.
Nilimfahamu Profesa Chachage.
Naweza nikasema mimi nilikuwa
ni mwandishi wa mwisho
kuzungumza naye kuhusu fikra
zake wakati alipokaribia
kuhitimisha safari yake hapa
duniani.
Ilikuwa ni Jumamosi, siku moja
kabla ya kufa kwake, kiasi cha
saa 4:30 hivi usiku nikiwa
sebuleni nyumbani kwetu Sinza
‘C’. Nilipatwa na mshawasha wa
kuzungumza kwa njia ya simu
yangu ya mkononi na Profesa
Chachage, ambaye alikuwa ni
miongoni mwa vyanzo vyangu
vya habari nyeti.
Ambaye kabla ya kukumbwa na
mauti alikuwa akiniambia ataki
katu katu kuitwa mwanaharakati,
akitaka aitwe Mwanamapinduzi,
kwa maelezo kwamba
wanaharakati wengi ni wanafki
na wasanii. Na kweli nikazoea
kumwita jina hilo.
Kwa nini nilipata mshawasha wa
kuzungumza naye siku hiyo?
Mezani kwake, kulikuwa na
maswali kadhaa ambayo
nilikuwa nimemwandikia, nikitaka
kupata ufafanuzi wa masuala
mbalimbali kwa ajili ya habari na
makala, ambavyo nilitarajia
kuchapisha katika gazeti.
Nilizungumza naye kwa takriban
dakika tano, kabla ya kuniambia
kwamba muda huo alikuwa
Kibaha, mkoani Pwani, kikazi.
Baada ya kuniambia yuko
Kibaha , nilipata hamu ya kutaka
kujua kazi anayoifanya huko.
Hata hivyo, hakutaka kuweka
wazi juu ya shughuli iliyokuwa
imempeleka huko. Hata hivyo
kabla ya kumaliza mazungumzo
yetu, alinidokeza kwamba katika
safari hiyo alikuwa ameongozana
na rafiki yake mkubwa, na
ambaye pia alikuwa mtu muhimu
kwangu katika kazi yangu ya
uandishi wa habari, Dk. Abuu
Mvungi.
Bila hiana, nilimwomba Profesa
Chachage kunipatia simu yake ili
naye nimsalimie. Alifanya hivyo,
tukaanza kutupiana ‘madongo’
ya utani kama ilivyokuwa ada
yetu pindi tunapokutana katika
mihangaiko mbalimbali.
Baada ya kumalizana na Dk.
Mvungi, Profesa Chachage
alirudisha simu yake katika
masikio yake, huku nikiendelea
kumdadisi ni nini hasa
kilichokuwa kimewafanya
wanamapinduzi hao wawe Kibaha
muda huo.
“Happiness, Jumanne nitakuwa
ofisini. Usijali, njoo nakuahidi,
kisha nitajibu maswali yako
ambayo uliniletea wiki tatu
zilizopita, usijali, ” aliserma.
Hiyo ndiyo ilikuwa kauli ya
mwisho ya Profesa Chachage.
Wapo waliomfahamu marehemu
kama mwandishi wa vitabu,
mwanafalsafa na mpenzi wa
muziku wa Bongo Flavor.
Mimi nilimfahamu kama mtu
mwenye fikra za kimapinduzi,
mwandishi wa vitabu na
mpigania haki na masilahi ya
umma, mkweli.
Leo Watanzania wa kada
mbalimbali hususan jumuiya ya
wasomi, tunaadhimisha mwaka
mmoja tangu kufariki kwake,
Professa Chachage Seith
Chachage.
Professa Chachage alifariki dunia
ghafla Julai 9 mwaka jana, saa
5:00 usiku, akiwa katika ukumbi
wa mikutano Kibaha, ambako
alikuwa ameongozana na jopo la
wasomi wanne waliopewa kazi
mahususi, ya kuandika ripoti
kuhusu hali ya Muungano na
migogoro ya kisiasa Zanzibar na
namna serikali inavyoweza
kuitatua.
Kazi hiyo walikuwa wametumwa
na serikali zote mbili, ya
Muungano na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar.
Kabla ya kifo chake, habari
zilisema Profesa Chachage
alianza kulalamika kuhusu hali
ya joto iliyokuwa katika chumba
hicho cha mikutano, ingawa
inaelezwa kwamba wasomi
wenzake hao walimwona kama
anatania kutokana na ukweli
kwamba chumba hicho kilikuwa
na ubaridi unaotokana na
viyoyozi vilivyomo ndani ya
chumba hicho, na vyote vikiwa
vinafanya kazi barabara kiasi cha
baadhi ya waliokuwamo kuhisi
baridi kali.
Katika malalamiko hayo,
ilielezwa kwamba Professa
Chachage alichukua chupa ya
maji, baada ya kunywa maji,
habari zinasema aliendelea
kutokwa jasho jingi, hali
iliyomfanya asimame kitini
kwake, akijaribu kujikongoja ili
atoke nje kupata upepo.
Hata hivyo, kabla hajafika nje,
ghafla alianguka na kupoteza
fahamu. Hapo ndipo wenzake
walizinduka na kuanza kushika
hiki na kile kwa nia ya kunusuru
uhai wake.
Kama wasemavyo wahenga, ‘siku
ya kufa nyani miti yote huteleza’.
Siku na muda ambao Mwenyezi
Mungu amepanga kuchukua roho
ya mja wake, binadamu hawezi
kuukwepa.
Akiwa njiani akipelekwa katika
Hospitali ya Tumbi, Kibaha,
alikata roho.
Huo ndio ukawa mwisho wa
safari ya maisha yake duniani,
Profesa Chachage, kipenzi si cha
jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam na wanafunzi wa Idara
ya Sosiolojia waliopo na
waliopita.
Nikiri kwamba pamoja na
kulisikia jina la Profesa
Chachage tangu nikiwa katika
Shule ya Msingi Mugabe, jijini
Dar es Salaam, kwa mara ya
kwanza nilishikana mikono na
profesa huyo mwaka jana kabla
ya kifo chake.
Ilikuwa Jumamosi moja, Januari
mwaka jana, saa moja jioni, pale
UDASA Club. Aliyenikutanisha
ana kwa ana na bingwa huyu wa
sosiolojia ni aliyekuwa Mkuu wa
Kitivo cha Sheria wakati huo, Dk.
Sengondo Mvungi.
Tangu siku hiyo, hadi kifo chake,
Profesa Chachage na mimi,
tuliishi kama chanda na pete.
Katika mambo ambayo
sitayasahau, ni msimamo wake
kuhusu kuanzishwa kwa Chuo
Kikuu cha Uhandisi ndani ya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
ambapo Rais Kikwete alikifungua
mwaka jana.
Enzi ya uhai wake, alitaka kuwe
na utaratibu mzuri unaolinda
masilahi ya wasomi kwa maana
kwamba wasomi walipwe vizuri
ili waweze kuishi kutoka na
utaalamu wao badala ya hali
ilivyo hivi sasa, ambapo wasomi
wanajikuta wakiwa wabangaiza
mitaani, wakifanya biashara ya
kuuza machungwa, mchicha au
kufuga kuku, ng’ombe na
nguruwe ili waweze kujikimu.
Kwa hiyo, ndiyo maana hayati
Profesa Chachage alisimamia
kidete suala la mishahara na
masurufi ya wahadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam.
Tunaweza kusema kwamba
wasomi wa UDSM walimtambua
kwa hilo na walimuunga mkono,
na hadi sasa wameshapata
awamu ya kwanza ya nyongeza
ya mishahara waliyoahidiwa na
serikali.
Kuhusu suala la wasomi
kulitumikia taifa lao kizalendo,
huo ndio ulikuwa msimamo wake
kiitikadi kwamba katika kila taifa
wasomi lazima wawe wana
mageuzi wanaotetea haki za
walio wengi.
Hilo hata yeye mwenyewe katika
uhai wake hakuweza
kulifanikisha, japo aliandika
mengi akilipigania hilo.
Hakulifanikisha kwa sababu
linahitaji pawepo idadi ya
kutosha ya wasomi wenye
msimamo huo ili waweze
kulitekeleza.
Hivi sasa wasomi walio wengi
wanapendelea kujiunga ama na
CCM, kuunga mkono sera zake,
au kukaa kimya ili kutetea
masilahi yao binafsi na
kushibisha matumbo yao na
familia zao.
Wasomi wengi hivi sasa
wanadhalilisha taaluma zao kwa
kuunga mkono au kutumika
kubuni miradi ya kifisadi na ya
kuuza nchi, na wanafahamika.
Nitaendelea kumkumbuka na
kuheshimu mchango wa Profesa
Chachage kwa vitendo, kwani
nakumbuka katika uhai wake
alijaribu kutetea nafasi ya vyuo
vikuu kuhusu mfumo wa elimu.
Yeye alisimama kidete
kupambana na mrengo wa
kibwanyenye unaotaka kugeuza
vyuo vikuu kuwa taasisi za
kufanyia miradi ya kiuchumi.
Na katika hili, alipambana na
katiba mpya ya chuo iliyokuwa
ikipendekezwa na enzi za
uongozi wa Makamu Mkuu wa
UDSM, Profesa Methew Luhanga,
ambayo ingekigeuza chuo kuwa
taasisi ya kibiashara badala ya
wajibu wake wa kutoa elimu ya
juu na kufanya utafiti.
Katika harakati zake hizo
aliwaongoza na kuwashawishi
wasomi katika chama chao cha
(UDASA) na katika chama cha
wafanyakazi wa (RAAWU)
kupinga katiba hiyo.
Hata hivyo katiba mpya ya chuo
hicho imepatikana baada ya yeye
kufariki.
Wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam walionyesha dhahiri
kumkubali na kumuenzi
mwanamapinduzi huyu kwa
sababu walikubali kuanzisha
Mfuko wa Profesa Chachage,
kwakukatwa mishahara yao.
Wasomi wa UDSM wana haki ya
kumuenzi marehemu Chachage,
labda enzi za uhai wake
alifahamika kwa watu wengi
lakini mambo yalivyo,
mwanamapinduzi huyu
atapendwa zaidi na Watanzania
baada ya kifo chake.
Yale aliyoyapigania na
hayakupatikana katika uhai wake
na wala Tanzania ya leo haitapa
faida ya mchango wake.
Hata hivyo kesho watapatikana
kina Profesa Chachage wengine
watakao chukua kurunzi
aliyoiwasha kuwaangazia
Watanzania wa kizazi chao
kuona njia ya kufika kwenye
maendeleo.
Profesa Chachage, sasa
marehemu ametoka wapi?
Alizaliwa Januari 8, mwaka 1955
katika Kijiji cha Mtwango,
wilayani Njombe, Iringa.
Kwa asili, yeye ni kutoka kabila
la Wabena, ambalo ni moja ya
makabila makubwa mkoani
humo, ukiacha Wahehe.
Si siri, marehemu alikuwa ni
mwanamapinduzi wa kweli na
asiye na woga katika kutetea
haki na masilahi ya umma na
itachukua muda mrefu kumpata
msomi mwenye sifa kama za
marehemu.
Pia kifo chake ni pigo kwa
jumuiya ya wanachuo, duru za
wasomi ndani na nje ya nchi.
Profesa Chachage, ambaye
ameacha mjane na watoto
wanne, kwa mara ya kwanza
alitunukiwa shahada ya kwanza
ya Sosiolojia ya Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam mwaka 1982.
Baada ya ya kuhitimu, na kuwa
miongoni mwa wanafunzi bora
alipewa kazi ya kufundisha
shuleni hapo akiwa kama
Mkufunzi Msaidizi, kabla ya
kuendelea na masomo ya
shahada ya pili na ya uzamili
chuoni hapo katika fani yake
hiyo mwaka uliofuata.
Mwaka huo wa 2000, akiwa na
cheo chake hicho cha Profesa
Mshiriki, Chachage alijiunga na
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
na akakabidhiwa dhamana ya
kuongoza kitengo cha Utafiti na
Uchapishaji cha chuo kikuu hicho
hadi 2003.
Kuanzia mwaka 2003 hadi
anafariki dunia, Profesa
Chachage alikuwa ni Mkuu wa
Kitivo cha Sosiolojia na pia
Mwenyekiti wa UDASA.
Lakini pia, Profesa Chachage
ameandika mada na vitabu
kadhaa, ambavyo vitatumika
katika vyuo vikuu na vyuo
vingine vya elimu ya juu nchini.
Moja ya vitabu na mada zake
zilizotia fora katika ulimwengu
wa mazingira ya Tanzania, ni
Makuadi wa soko huria,
ambacho, pamoja na mambo
mengine, Profesa Chachage
anayaangalia madhira ya
wakulima wa korosho
wanayoyapata kutokana na sera
mbovu za nchi, dhidi ya
wanunuzi wa zao hilo.
Vitabu vingine ni pamoja na
Honourable Teacher
(Mheshimiwa Mwalimu), Dhima
ya Fasihi na Sudi ya Yohana,
ambavyo amevitunga katika
mfumo wa hadithi. Pia vipo
Fasihi na sanaa na uhusiano
wake na Kiswahili, Kivuli na
almasi za bandia.
Profesa Chachage, binafsi
nakutakia mapumziko mema
huko uliko. Najua utakutana na
wana mapinduzi magwiji, kama
Mwalimu Julius Nyerere, Kwame
Nkrumah, Patrice Lumumba na
wengine wengi.
Usisahau kuwaeleza mbinu mpya
ya ukoloni unaolinyemelea Bara
la Afrika.
Pia umweleze Mwalimu Nyerere
kile chama chake alichokiasisi
cha CCM, kimejaa makundi
madogo na makubwa,
lililoyafunika kwa sasa ni kundi
la ‘wanamtandao’ na si tena
chama cha wakulima na
wafanyakazi, bali hivi sasa
chama hicho ni cha
wafanyabiasha na matajiri.
Aidha, umweleze kwamba
makada wa chama chake wengi
wao hawawezi kugombea nafasi
za uongozi bila kupewa baraka
na ‘sangoma’.
Pia hivi sasa ni nadra sana kuwa
kiongozi kama si
mwanamtandao, mpika majungu,
mfitini na bingwa wa kutumia
vyombo vya habari ili vikupambe.
Nilazima pia uwe hodari na
mahiri wa kujikomba kwa
wakubwa na kuwasifia hata kama
utendaji wao ni mbovu.Tafadhari
usisahau kumweleza haya.
Umweleze ile migomo ya vyuo
vikuu inaendelea kama kawaida
na ubinafsishaji na uingiaji wa
mikataba yenye utata imeshika
kasi.
Pia umweleze hivi sasa tofauti
kati ya maskini na wenye nacho,
ambayo alikuwa akiipinga kila
siku hivi sasa imeanza kuota
mizizi.
Najua umekutana na wasomi
wenzako kutoka pande nne za
dunia pamoja na walalahoi
kadhaa waliopoteza maisha
kutokana na taabu walizozipata
katika harakati zao za kutetea
mazingira mazuri na bora ya
elimu, ambayo sasa yameanza
kuharibiwa na mitazamo pamoja
na sera mbovu za wanasiasa na
watunga sheria.
Mwisho kabisa, pamoja na pengo
kubwa uliloliacha kwa Jumuiya
ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
na familia yako, lakini kumbuka
kwamba wale marafiki zako
tuliokuwa tukikata karibu usiku
mzima kutakiana heri kwa
kugongeana bilauri, nasi
umetuacha taabani.
Mimi nitaendelea kukuenzi daima
kwa kuandika ukweli na kukemea
maovu kama ulivyokuwa
ukiniusia kila mara.
Naahidi kuwa jasiri kwa kusema
na kuandika ukweli katika
kutetea masilahi ya wanyonge wa
nchi yetu.
Profesa Chachage ambaye
alizikwa kijijini kwake Mtwango,
Njombe, mkoani Iringa,
atakumbukwa pia na wale
aliokuwa akichangia nao katika
‘upigaji pafu’ wa sigara.
Hao nao wataendelea kukulia na
kuuenzi mchango wako,
umewaacha bila mlezi wala
mshauri. Watakukumbuka daima.
Mungu alikuumba na akakutwaa.
Jina la Bwana lihimidiwe na
aipumzishe roho yako mahala
pema peponi.
Amina.
 
Duu huu mtu alikuwa shupavu saana kwa kweli. Hata darasani alikuwa akifundisha na kutetea kile anachokiamini kwa mifano iliyothabiti kabisaa na ukweli ndani yake hasa katika kuutetea uafrika na imani za kiafrika. Daima tutakukumbuka na utakumbukwa na vizazi vingi sana nyuma yako. Ila utachukiwa sana na wapinga uadilifu na wasaliti hasa Makuwadi wa Ufisadi wanaoingia mikataba mibovu kwa niaba ya familia zao, marafiki katika biashara na si wananchi ambao waliwapa dhamana kufanya hivyo..MUNGU AKUREHEMU NA KUKUANGAZIA MWANGA WA MILELE.........AAMEEN
 
Rest in Peace Prof Seith Chachage (The meek shall inherit the earth but not mining rights) Madini yamekwisha sasa tumebaki na mahandaki na umasikini unazidi kujizatiti miongoni mwa watanzania. wamehamia kwenye gesi!!!!!!!!!!!!!
 
Rest In Peace Prof. Chachage.

Sent from my BlackBerry 9300 using JamiiForums
 
Back
Top Bottom