Primus Inter Pares - Jenerali Ulimwengu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Primus Inter Pares - Jenerali Ulimwengu

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Nsololi, Sep 2, 2009.

 1. N

  Nsololi JF-Expert Member

  #1
  Sep 2, 2009
  Joined: Mar 8, 2007
  Messages: 290
  Likes Received: 34
  Trophy Points: 45
  BWANA ULIMWENGU ANAENDELEA KUELEZEA HOJA YA RAIS KIKWETE YA KUDAI KUWA ETI 'URAIS WAKE HAUNA UBIA NA MTU YEYOTE'.


  Rai ya Jenerali

  Primus Inter Pares


  Na Jenerali Ulimwengu
  Agosti 26, 2009

  WIKI hii nataka kujadili dhana ya Primus Inter Pares. Kwa Kiingereza ni First Among Equals. Kwa Kiswahili tunaweza kusema, Kiongozi wa Viongozi, au Mkuu wa Wakuu, au Kiranja wa Viranja, ingawaje naona ugumu katika majina yote hayo. Muhimu ni kujua kwamba kinachozungumziwa hapa ni “Wa Kwanza Miongoni mwa Walio Sawa.”

  Dhana hii inatokana na mfumo wa uongozi ambao unatambua kwamba ili kufanikisha shughuli yo yote kubwa ya kitaifa au kijamii ni lazima watu walioazimia kufanya jambo hilo wanawekeana yamini inayowafanya wabia katika azima yao hiyo.


  Hii ndiyo dhana ya ubia ambayo nimekuwa nikiijadili katika safu hii. Huu ni ubia wa raia wenye maono yanayofanana, wenye mwelekeo unaoshabihiana na wenye utashi unaoendana, ambao baada ya muda wa kuishi na kufanya kazi pamoja, baada ya kuwa wamekutana utotoni na katika ujana wao, au shuleni na chuoni, na kuelewana kifikra, wanajiona kama watu wanaoweza kuunganisha nguvu zao ili kufikia malengo fulani ya kibinafsi, kijamii na kitaifa.

  Baada ya muda wanaweza kuamua kujiunga na siasa ama harakati za utetezi wa masuala ya kijamii na kufanya kazi kama wabia katika suala wanalolisimamia. Iwapo eneo waliloliteua ni siasa, ubia wao huo utawapeleka katika siasa zinazofanana na hicho walichodhamiria kukifanya.

  Iwapo wataona ni vyema kujiunga na chama cha siasa kinachoongozwa na falsafa inayofanana na dhamira yao watakichagua chama hicho miongoni mwa vyama vilivyopo nchini na watajiunga nacho, si kwa sababu nyingine isipokuwa kwamba chama hicho na wao wanafanana katika malengo yao. Siyo kwamba chama hicho kinawahakikishia kupanda haraka haraka katika kushika madaraka ya dola.

  Kama hawaoni chama chenye mtazamo kama wao miongoni mwa vyote vilivyomo nchini wataanzisha chama chao, na watakitangaza kama chama kinachoongozwa na falsafa mahsusi na kitakachofuata siasa zinazofanana na falsafa hiyo.

  Chama walichoanzisha kinaweza kikahangaika kwa muda mrefu bila kupata kushika madaraka ya dola, lakini wabia hao hawahamaniki kutaka kuhama kutoka chama hadi chama mithili ya watalii wakitafuta ni njia gani ya kuingia madarakani kwa urahisi zaidi.

  Watakijenga chama chao; wataimarisha misingi yake ya kifalsafa na tafisri yake katika siasa na sera; watatafuta kuungwa mkono na wengine wenye mtazamo kama wao; watajifunza zaidi kuhusu matatizo ya watu wao na nchi yao kwa lengo la kuyatafutia utatuzi mwafaka….

  Sasa, watu hawa walioingia aina fulani ya yamini, wanapofanikiwa kuingia, wao na chama chao, katika madaraka, wanakuwa na hamu ya kuanza kutekeleza kwa vitendo yale yote waliyokuwa wameyapanga kwa muda mrefu, na ambayo kwayo wamepata ridhaa ya wananchi kuiongoza nchi.

  Hapa ndipo dhana ya Primus Inter Pares inakuwa na umuhimu. Kama watu hawa, ambao tuseme hadi wanafikia hatua ya kutafuta uongozi wa nchi wamefikia idadi ya hamsini au sitini wamekuwa na dhamira ya kweli ya kuchukua madaraka na kuiongoza nchi kwa mujibu wa misingi kadhaa wanayoiamini, ni vipi watachagua kiongozi wao na wasaidizi wake?

  Kama ni watu makini, na hiyo dhamira waliyoitangaza ni ya kweli, watakachofanya ni kukutana tena (kwa sababu wanakutana kila siku hata hivyo) na kwa pamoja watafanya kazi ya kupanga nafasi za uwajibikaji na watu wa kuzishika.

  Anayeonyesha kuwa mkali kwa masuala ya elimu atakuwa waziri wa sekta hiyo; anayeonyesha weledi mkubwa katika masuala ya fedha atakwenda Hazina; anayedhihirisha ushawishi mkubwa anapohusiana na mataifa ya kigeni atakwenda Mambo ya Nje, na kadhalika.

  Lakini, pamoja na kwamba hili ni kundi la wabia na lao ni moja, inabidi kundi hilo liamue ni nani atakuwa kiongozi wao, mtu ambaye ataunganisha nishati zao na mawazo yao kwa uwezo mkubwa, lakini pia atakuwa ndiyo sura na ndiyo sauti, ndiyo nembo ya kundi zima hilo linapowasiliana na umma na dunia, tangu wanapokuwa wanasaka madaraka hadi wanapokuwa wameingia serikalini.

  Huyo wanayemchagua si lazima awe na uwezo wa kufikiri kuliko wenzake (ingawa inasaidia ikiwa hivyo); si lazima awe yule wanayemsema kwamba “ana akili nyingi sana.” Anaweza kuchaguliwa miongoni mwa wenzake, kwa mfano, kwa sababu ni mwanadiplomasia bora kuliko wenzake, na hiyo inamfanya mpatanishi na muunganishi wa wenzake kila maslahi yanayokinzana (hayaishi haya) yanapocharukiana.

  Vile vile anaweza kuchaguliwa kwa sababu ni mwana-mawasiliano mzuri: anajua nini kinatakiwa kisemwe, kwa nani, wakati gani, na vipi. Kwa sababu kama mkuu mtangulizi wa wenzake itambidi ayasemee masuala yote ya serikali yake yote kuliko wenzake waliokasimiwa idara moja moja, uwezo wa kimawasiliano ni nyenzo muhimu sana.

  Anaweza kuwa na sifa nyingi nyingine, lakini mojawapo si kwamba yeye ndiye mwenye chama ama serikali, na wale wote wanaomzunguka ni watumishi wake, anaoweza kuwafukuza au kuwapandisha vyeo kama anavyotaka. Yeye na hao wenzake ni sawa, ila kwa sababu mahsusi yeye kakubalika achukue nafasi ya mbele kwa manufaa ya kundi zima lililomchagua kushika nafasi hiyo. Si bosi, bali ni Primus Inter Pare.

  Huyu anawaongoza wenzake kwa ridhaa yao, na ikifikia wakati ridhaa hiyo ikatoweka, watamuomba aondoka na watamchagua mwingine miongoni mwao asogee mbele kuchukua nafasi yake.

  Bila shaka katika mchakato kama huu kutakuwako na ushindani miongoni mwa wabia, hata kama wamekuwa pamoja kwa muda wa miongo kadhaa. Lakini huu unakuwa ni ushindani baina ya watu wanaopambanisha maoni juu ya njia iliyo bora ya kufanya walichokusudia kukifanya, ushindani unaotokana na dinamiki inayokataa mawazo yaliyotuama, na daima inasonga mbele. Si ushindani wa mahasimu, hata kama kwa muda watakasirikiana.

  Katika ubia wa aina hii, kiongozi wetu huyo, Primus Inter Pares, anafanya kazi kila siku kama sehemu ya timu na anasikiliza wanatimu wenzake wanamwambia nini. Hata angekuwa na ushawishi mkubwa sana miongoni mwao na miongoni mwa raia, atajizuia kuchukua maamuzi ya mara kwa mara ambayo yanakinzana na fikra za wenzake.

  Faida kubwa ya utaratibu huu ni kwamba unaondoa kabisa dhana ya kiongozi kama bosi.
  Kiongozi mkuu wa nchi yo yote ni bosi wa watumishi wa serikali walio katika utumishi wa umma, kutoka makatibu wa kuu hadi chini.
  Lakini tatizo linajitokeza pale anapoanza kuwa bosi wa watu wanaotakiwa kuwa wabia wake.

  Nimesema mapema kwamba kundi la watu lililokula yamini (hii pia ni namna fulani ya njama) ya kutafuta madaraka ya nchi ili kufanya mambo kadhaa (mema kwa wananchi) ni kundi la wabia. Haiingii akilini kwamba wabia hao, ambao wanatakiwa kuunganishwa na fikra ya aina fulani ya usawa, watajikuta wakimwachia mmoja wao awe ndiye mwenye fikra tukufu na wengine wawe ni matarishi wa kwenda kutekeleza fikra hizo.

  Haiyumkiniki kwamba kiongozi aliyetangulizwa mbele na wenzake, tena kwa kushawishiwa dhidi ya utashi wake wa awali, sasa, baada ya kuonja tamu ya madaraka, ajifanye kamaba yeye ndiye anayejua kila kitu na wale waliomtanguliza mbele ni watu wa kupewa amri na kuzitekeleza.

  Makala zangu za nyuma zinaeleza hali tuliyokuwa nayo wakati wa Uhuru na miongo miwili iliyofuata, wakati wa Baba wa Taifa, mmoja , peke yake, mwenye busara kuliko wengine. Labda kwa wakati huo dhana hiyo ilikuwa inavumilika, lakini tukumbuke kwamba haikukubalika kirahisi hivyo, hata wakati ule, kwani walikuwako watu, wazalendo na watu wema kabisa, walioipinga dhana hiyo wakati huo.

  Kama walikuwapo wazalendo wachache walioikataa dhana hiyo zama za Mwalimu, pamoja na kwamba Taifa lilikuwa changa na halikuwa na watu walioerevuka sana na mchango binafsi wa Julius Nyerere hatika harakati nzima ya kutetea Uhuru haikupingika, na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alijipambanua kwa njia nyingi kama mtu mwenye sifa za kipekee ambazo hadi leo zinatambulika nchini hapa na kote duniani, ni nini kinatufanya tuendelee kuikumbatia dhana ambayo hata kwa macho tu inaonekana kwamba haifui dafu hata kidogo?

  Itaendelea

  Chanzo: Raia Mwema
   

  Attached Files:

Loading...