Polisi lawamani kuomba wananchi mafuta

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,850
34,300
ASKARI Polisi wa kituo cha Ulyankulu wilaya ya Kaliua mkoani Tabora wamelalamikiwa kwa kudai malipo ya Sh 300,000 kutoka kwa wananchi kama gharama ya mafuta ya kuwafikisha kwenye matukio ya kihalifu.

Akizungumza na askari hao, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, John Kadutu alisema hivi karibuni askari hao walidai wapewe kiasi hicho cha fedha ili waweze kufika kijiji cha Sasu kulipotokea uhalifu.

Alisema kitendo cha kudai fedha kutoka kwa wananchi ili watekeleze majukumu yao ni miongoni mwa kero walizonazo wananchi na kuwataka askari hao kuacha kuwaomba fedha wananchi kwa kuwa ni ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza shughuli za utekelezaji wa majukumu yao.

Mbunge huyo alisema endapo askari hao watatenda haki na kuacha kuwaomba wananchi fedha za mafuta, kupokea rushwa na kuwabambika kesi hawataingiliwa katika majukumu yao na kazi yao itakuwa nyepesi kwani watapata ushirikiano mkubwa.

“Kumekuwa na malalamiko mengi juu yenu jambo ambalo linapaswa kuangaliwa… Tekelezeni majukumu yenu kwa mujibu wa taratibu zenu badala ya kutanguliza tamaa ili kujinufaisha,” alisema.

Mbunge huyo wa Ulyankulu aliwahimiza askari hao kuacha vitendo vya kukiuka haki za binadamu kwa kuwapiga watuhumiwa au kuwanyanyasa kwa namna yoyote hata kama wametii kuwa chini ya ulinzi.

Kadutu alibainisha kuwa vitendo hivyo vinazidi kuchochea chuki kutoka kwa wananchi, hali ambayo inadhoofisha dhana nzima ya polisi jamii, ulinzi shirikishi na utii wa sheria pasipo shuruti.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kaliua, Haruna Kasele, alikemea tabia ya baadhi ya askari hao kuvujisha siri wanazopewa na raia wema kuhusu uhalifu au wahusika wa uhalifu kwa nia ya kujinufaisha.

Mbunge wa Ulyankulu alifanya ziara ya siku ya tatu ya kutembelea taasisi za umma na binafsi kwa lengo la kupokea ushauri, kero na maoni kabla ya kuanza kwa vikao vya bunge Januari 26 mwaka huu.

chanzo.Polisi lawamani kuomba wananchi mafuta
 
Back
Top Bottom