RAIS SAMIA: KIONGOZI WA MABADILIKO NA MAENDELEO YA KWELI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuthibitisha kuwa uongozi wake ni wa vitendo, uwajibikaji na matokeo chanya kwa Taifa. Tangu aingie madarakani mwaka 2021, ameweka msisitizo mkubwa katika kukuza uchumi, kuboresha maisha ya wananchi na kulinda amani na mshikamano wa kitaifa.
Katika kipindi cha uongozi wake, Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta za elimu, afya, nishati, maji, kilimo, miundombinu na ushirikiano wa kimataifa. Kupitia falsafa ya
“Kazi Iendelee”, Rais Samia ameonyesha uthubutu wa kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo
Reli ya Kisasa (SGR), Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Julius Nyerere, ujenzi wa barabara na madaraja makubwa, upanuzi wa shule na hospitali, sambamba na kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.
Aidha, sera zake zimeimarisha uchumi kwa kuongeza mapato ya ndani, kupunguza utegemezi, na kuvutia wawekezaji wakubwa kutoka ndani na nje ya nchi. Kupitia ziara zake za kidiplomasia, Tanzania sasa imeimarika kimataifa, ikiheshimika kama nchi ya amani, fursa na mshirika thabiti katika maendeleo ya kikanda na kimataifa.
Zaidi ya yote, Rais Samia Suluhu Hassan amejipambanua kama kiongozi anayejali wananchi, hasa wanawake na vijana, akihamasisha ushiriki wao katika uchumi, siasa na uongozi. Hii imemfanya kuwa mfano wa kuigwa Afrika na duniani kote, akiweka historia kama mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Tanzania na kuongoza nchi kwa ufanisi mkubwa.