Pamoja na hatua nzuri, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara inahitaji kuziba kabisa Pengo la Kijinsia

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,801
USAWA WA KIJINSIA KUSINI MWA JANGWA LA SAHARA.jpg


Kufikia usawa wa kijinsia ni lengo muhimu katika maeneo yote duniani kutokana na athari zake chanya kwa jamii, uchumi, na maendeleo kwa ujumla. Usawa wa kijinsia unahusu kutoa fursa sawa na haki kwa watu wa jinsia zote, bila kujali jinsia yao, ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi, kisiasa, na kitamaduni.

Global Gender Gap Report 2023 imeleta mwangaza kuhusu jinsi hali ya wanawake na wanaume inavyotofautiana katika maeneo mbalimbali ya dunia. Ripoti hii imegawanya nchi katika maeneo/kanda nane tofauti ili kuchunguza tofauti hizi. Maeneo hayo ni pamoja na: Eurasia na Asia ya Kati, Asia Mashariki na Pasifiki, Ulaya, Latini Amerika na Karibiani, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Amerika Kaskazini, Asia Kusini, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kwa upande wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ripoti inaonesha kwamba kuna utofauti mkubwa katika usawa wa jinsia. Ukanda huu unashika nafasi ya sita kati ya nane, ukiwa umefikia 68.2% ya usawa wa kijinsia. Hii inamaanisha kwamba maendeleo ya usawa wa kijinsia ni bora kuliko kanda za Asia Kusini na Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

Hata hivyo, maendeleo hayalingani miongoni mwa nchi zilizopo katika eneo hili. Nchi kama vile Namibia, Rwanda, na Afrika Kusini, pamoja na nyingine 13, zimefanikiwa kufunga zaidi ya 70% ya pengo la jinsia kwa ujumla. Lakini nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mali, na Chad, zimebaki nyuma sana na kuwa na alama chini ya 62%.

Kuhusu fursa za kiuchumi, eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara limefanikiwa kufunga 67.2% ya pengo la kijinsia. Nchi kama Liberia, Eswatini, na Burundi zimeshika nafasi za juu katika orodha ya usawa wa kiuchumi. Lakini Benin, Mali, na Senegal wamefikia kiwango cha chini zaidi cha usawa.

Kuhusu elimu, mkoa huu umekuwa na changamoto. Usawa wa kijinsia katika elimu ni asilimia 86%, na hii inauweka ukanda huu kwenye nafasi ya chini zaidi katika suala hili. Ni nchi chache tu kama Botswana, Lesotho, na Namibia zilizofikia usawa kamili. Nchi 16 zimefanikiwa kufikia usawa wa chini ya 90%, na nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Chad zimekuwa na utendaji duni zaidi.

Katika suala la afya na kuishi, eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara limepata mafanikio kwa kuwa na 97.2%. Hii inamaanisha kwamba tofauti za jinsia katika suala la afya na matarajio ya kuishi (life expectancy) yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Pengo_la_kijinsia_lililofungwa_hadi_sasa_Kusini_mwa_Jangwa_la_Sahara.jpg

Ripoti hiyo pia inaonesha pia kwamba kuna maboresho katika uwiano wa jinsia katika nyanja nyingine, kama vile uwiano wa kuzaliwa kwa jinsia, matarajio mazuri ya kuishi maisha yenye afya, na uwezeshaji wa kisiasa. Ingawa bado kuna changamoto, hatua kubwa zimepigwa katika kuboresha usawa wa jinsia katika maeneo mbalimbali.

Kuziba kabisa mapengo ya usawa wa kijinsia katika ukanda uliogubikwa na umaskini, kama vile Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni suala muhimu kwa sababu linachangia moja kwa moja katika kuleta maendeleo endelevu na kuinua hali ya maisha kwa watu wote. Hapa kuna sababu kadhaa zinazoonyesha umuhimu wa kufanikisha usawa wa kijinsia:

Wanawake ni sehemu kubwa ya nguvu kazi ya bara la Afrika, na kwa hivyo, kuziba mapengo ya usawa wa kijinsia kutawezesha kuchangia kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii. Wanawake wamekuwa wakishiriki katika shughuli za kilimo, biashara ndogo ndogo, na huduma za kijamii. Kwa kuwapatia wanawake fursa sawa na kuhakikisha hawakabiliwi na ubaguzi au vikwazo vya kijinsia, uwezo wao wa kuchangia katika ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini unaweza kuimarishwa.

Lakini pia, wanawake wakiwa na fursa sawa za elimu na ajira, wanaweza kutoa michango mikubwa katika uzalishaji na uchumi kwa ujumla. Wanawake pia ni watumiaji wakubwa wa rasilimali, na kuongezeka kwa ushiriki wao katika masoko na uzalishaji kunaweza kuchochea ukuaji wa uchumi.

Wanawake wakipata elimu bora na huduma za afya, wanaweza kuwa walezi bora kwa familia zao na jamii nzima. Wanawake wazima wakiwa na elimu wanaweza pia kuongoza katika kutoa elimu kwa kizazi kijacho, kusaidia kupunguza pengo la elimu.

Kubwa zaidi, Wanawake wanapaswa kuwa na uwakilishi katika ngazi zote za uongozi na maamuzi, ikiwa ni pamoja na serikali na mashirika ya kiraia. Usawa wa kijinsia katika uongozi husaidia kuleta mtazamo tofauti na kuongeza sauti za wanawake katika kutunga sera na kufanya maamuzi. Usawa wa kijinsia ni haki ya msingi ya binadamu. Kuhakikisha haki za wanawake zinaheshimiwa na kulindwa ni hatua muhimu kuelekea jamii yenye haki, yenye usawa, na maendeleo endelevu.
 
Back
Top Bottom