Padri Tetzel Vs Padri Martin Luther

Aaron Arsenal

JF-Expert Member
Jul 24, 2014
24,504
28,692
Soma kisa hiki cha kusisimua, ambacho ndicho msingi wa uhuru wa dini na chimbuko la Uprotestant mnamo october 31, 1517, na kisa hichi kitakutia moyo katika jitihada zako za kutafuta ukweli wa Kristo hata kama upo mwenyewe tu, hata kama unapingwa na watu maelfu. Karibu

Kanisa la Rumi lilifanya biashara ya neema ya Mungu. Chini ya ombi la kukusanya fedha za kujengea kanisa la Petro mtakatifu huko Rumi, vyeti vya msamaha wa dhambi vilitolewa kwa kuuzwa, kwa agizo la Papa. Kwa bei ya makosa kanisa lilijengwa ili kumwabudu Mungu. Jambo la namna hii ndilo lililochochea adui za papa wakaanzisha vita, vilivyotetemesha utawala wa Papa, na kuiondoa taji kichwani mwa papa.

Tetzel, ambaye aliwekwa huko Ujerumani ili auze vyeti hivyo vya msamaha wa dhambi, alipatikana na hatia ya kudhulumu watu na kuasi sheria ya Mungu. Lakini aliwekwa kuajiri mradi wa askari wa kukodiwa na papa katika Ujerumani. Alijulikana kwa ulaghai wake wa kudanganya watu wajinga kwa hadithi za ajabu ajabu na kuwahadaa. Kama wangelipokea neno la Mungu wasingalidangayika lakini Biblia iliondolewa kwao, kwa hiyo wakabaki tu katika hali ya ushirikina.

Tetzel alipokuwa akiingia mji fulani mjumbe humtangulia na kutangaza “Neema ya Mungu na ya Baba mtakatifu imewafikieni”. Basi watu humkaribisha mwenye kufuru huyu kama kwamba ndiye Mungu hasa. Tetzel akipanda mimbarani, katika kanisa husifu sana vyeti vya msamaha na kusema kuwa hivyo ndivyo karama ya Mungu ya thamani kwa wanadamu. Husema kuwa kwa njia ya vyeti hivyo dhambi zote ambazo mtu atatenda baadaye husamehewa wala hakuna haja ya kutubu. Cheti kimekamilisha mambo yote. Aliwahakikishia wasikilizaji wake kwamba cheti hicho kina uwezo wa kuokoa mtu aliyekufa; mara ile fedha inapotumbukizwa katika kisanduku. Roho ya marehemu hupita moja kwa moja bila kuingia matesoni kwanza mpaka mbinguni.

Hivyo fedha na dhahabu vikamiminika katika sanduku la Tetzel. Wokovu ulipatikana kwa njia ya kuununua ulikuwa rahisi kuliko wokovu unaopatikana kwa njia ya kutubu. Imani na juhudi ya kupinga majaribu ya dhambi, mpaka upate mtu ushindi.
Luther alijazwa na hofu mno. Wengi hata katika watu wake walikuwa wamenunua vyeti vya msamaha. Mara wakaanza kumjia mchungaji wakiungama dhambi huku wakitazamia kupata ondoleo la dhambi kwa njia hiyo, wala si kwa njia ya kujuta na kuziacha, wakitumaini vyeti kwamba vitawakamilisha. Luther alikataa mambo hayo na kuwaonya kuwa wasipotubu kamili na kugeuka moyo, wataagamia katika dhambi zao. Wakamwendea Tetzel wakilalamika kwamba yeye waliyekwenda kumwungamia, amekataa vyeti vyao, hata wengine wakadai warudishiwe fedha yao. Yule mtawa Tetzel akatoa matusi mazito kwa hasira nyingi, akaagiza moto uwashwe uwanjani, na akasema kuwa ameagizwa na papa kumchoma mtu yoyote atakayeupinga mpango huo mtakatifu.

Sasa sauti ya Luther ikawa ikisikika mimbarani, akitoa maonyo. Aliwaonya watu waziwazi ubaya wa tabia ya kutenda dhambi na ya kwamba mtu hawezi kwa bidii yake kujiondolea hatia ya dhambi, na kuondokana na adhabu yake. Hakuna njia nyingine ya kuondokana na hayo na kutuokoa ila tu ni toba ya kweli na imani kamili kwa Mwokozi aliyetufia. Neema ya Kristo haiwezi kununuliwa, ni kipawachabure. Akawashauri watu wasinunue vyeti vya msamaha ila wamtazame mwokozi aliyesulubishwa kwa imani. Aliwasimulia jinsi alivyojitaabisha ili apate amani, lakini ikawa kazi bure, mpaka alipomwamini Kristo, ndipo akawa na amani na furaha.

Kadri Tetzel alivyoendelea na majivuno yake, Luther alikusudia kumpinga dhahiri. Kanisa la Wittenberg lilikuwa na vitu vya ukumbusho, ambavyo katika siku za sikukuuu huonyesha. Msamaha kamili wa dhambi ulitolewa kwa wote waliofika kanisani, na kuungama. Mojawapo ya sikukuu za namna hiyo ilikuwa karibu kutokea. Luther pia akiungana na msafara huo wa kwenda kanisani, alikwenda akatundika katika mlango wa kanisa maneno tisini na matano yanayopinga uzaji wa vyeti vya msamaha.

Maneno hayo aliyoyatundika liwavutia watu wote. Waliosomwa na kukaririwa kila upande. Mji mzima ukataharuki. Ikaonekana wazi kuwa uwezo wa kusamehe makosa na kuondolea adhabu ya dhambi, haukutolewa kwa papa kamwe, au kwa mtu mwingine yeyote. Ikafahamika kuwa neema ya Mungu na msamaha wa dhambi ni bure kwa wote wanaotubu na kuamini.
Maneno ya Luther yalienea katika nchi yote ya Ujerumani na kwa muda wa majuma machache yalienea Ulaya yote. Watu wengi waliokuwa wafuasi kamili wa Rumi waliyasoma maneno hayo ya Luther kwa furaha kubwa. Wakatambua kuwa hiyo ni sauti ya Mungu. Wakaona kuwa Bwana amenyosha mkono wake ili awatoe watu katika upotovu unaoendeshwa na kanisa la Rumi. Wakuu wa nchi na mahakimu walifurahia kisirisiri kwamba kumetokea kigingi cha kusimamisha majivuno ya upotovu wa Rumi.

Makasisi wenye hila walipoona kuwa pato lao linahatarishwa, walichukizwa mno. Hivyo Luther akakabiliwa na washitaki wenye uchungu sana. Aliposhitakiwa alisema “nani hajui kuwa ni mara chache mno, mtu kuweka kitu kipya bila... kushitakiwa kuwa mchafuzi? Kwa sababu walifanya mambo mapya bila kwanza kujinyenyekeza na kupata idhini ya wakubwa”.
Maalum ya adui za Luther, na kumwelewa kwao vibaya na chuki yao juu yake, vilimfurikia kama gharika. Yeye alitumaini kuwa viongozi watamwunga mkono, kwa hiyo alitulia tu. Katika jaribio lake, aliona matumaini mema na kuamsha kanisa.

Lakini sasa matumaini mema yamegeuka kuwa maalum. Wakuu na viongozi wengi wa kanisa waliona kuwa maneno hayo ya kweli waliyapokea yatadhoofisha mamlaka ya Rumi maana yatakomesha mafuriko ya fedha zinazokuja kwa hazina yake, na hivyo utukufu wa Rumi utafifia.

Kufundisha watu wamtazame Kristo pekee yake kutaangusha utawala wa papa na mwishowe kuangamiza mamlaka yake. Kwa hiyo wakakataa ukweli huu wa kumtazama Kristo kwa kumpinga mtu aliyetumwa na kuwaleta nuru.

Luther alitetemeka alipojifikiria. Mtu mmoja kupingana na uwezo mkuu katika nchi. Aliandika na kusema: “Mimi ni nani nishindane uwezo mkuu wa papa… ambaye wafalme wa nchi na ulimwengu wote humtetemekea?”... Hakuna ajuaye jinsi moyo wangu ulivyofadhaika katika muda wa miaka miwili hii, na jinsi nilivyokata tamaa na kuzama. Lakini msaada wa kibinadamu uliposhindwa alitazama kwa Mungu peke yake. Aliweza kutulia kwa amani katika mkono wa Mungu mwenye nguvu zote.

Akimwandikia rafiki yake Luther alisema, “Wajibu wako wa mwanzo ni kuanza na maombi... usitumaini kitu chochote kutoka kwako, kwa uwezo wako, au kwa akili zako. Mtumaini Mungu kamili, katika mvuto wa Roho wake”. Hilo ndilo fundisho kwa watu wote wanaojisikia kuwa wameitwa na Mungu kutoa ujumbe wa kweli kwa wakati huu. Katika mashindano na maovu kunahitajika uwezo zaidi ya ule wa kibinadamu na hekima zaidi ya kibinadamu.

My take

Katika watu waliotumiwa na Mungu kulitoa kanisa katika giza la upapa, na kuwaleta katika nuru ya kweli ya Biblia na imani halisi, Martin Luther ni mmoja wa hao katika mstari wa mbele. Hakujua kuogopa kitu kingine ila Mungu tu, wala hakujua msingi mwingine wa imani, ila ule uliomo katika Biblia. Alikuwa shujaa kwa wakati wake

Inasikitisha kazi ile ya Martin Luther ya jasho la damu, ilikomeshwa october 31, 2017, na kufunga kipindi cha miaka 500 ya uprotestant kwa muungano baina ya KKKT NA ROMANI CATHOLIKI. Je Katholiki wameshajibu hoja zile 95 za Martin Luther? tafakari na chukua hatua maana game bado linaendelea, unapaswa kusimama peke yako, katika ile kweli iliyopo kwa jinsi ya Kristo pekee na si kwa jinsi ya ulimwengu na maridhiano ya kidini.
 
Back
Top Bottom