Othman Masoud: Sisi sote ni Wazanzibari licha ya tofauti zetu, na hapa ndiyo kwetu

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
613
1,541
Sisi sote ni Wazanzibari licha ya tofauti zetu, na hapa ndiyo kwetu – Othman Masoud


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, mheshimiwa Othman Masoud Othman, amewataka Wazanzibari kutokubali kubaguana au kufitinishwa na watu wenye maslahi binafsi,kwani umoja wao ndiyo utambulisho wao.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo katika ziara yake huko Bububu, mkoa wa Magharib 'A' kichama. Mkutano huo ni muendelezo wa ziara yake ya kukutana na wanachama wa Chama cha ACT Wazalendo wa ngazi ya mkoa, jimbo na matawi.

Kiongozi huyo amesema kuwa ziara za kisiasa zinazoendelea kisiwani Unguja zimeamsha hamasa na kuleta matumaini mapya ya ukombozi.

"Hamasa ile ile, na ari ile ile ambayo ipo ndani ya nyoyo za wanachama hawa kwa lengo la kufikia mafanikio, binafsi zimezalisha matumaini zaidi katika nafsi yangu" alisema mjumbe huyo wa Kamati kuu.

Kiongozi huyo amewanasihi wanachama wa ACT Wazalendo wa mkoa huo kwamba siku zote mapambano ya kiukombozi yanakuwa na gharama kubwa hivyo waendelee kuwa na subira na kuongeza nguvu na ari zaidi. Aidha amewataka kujidhatiti katika kuongeza idadi ya wanachama wapya ili kukiimarisha zaidi chama chao na kuweza kuyafikia matarajio yao.

Naye Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar,Ndugu Juma Duni Haji, ambaye aliongozana na mheshimiwa Othman katika ziara hiyo alisema “kinachotuunganisha ni dhamira na dhamira ni umoja wetu. Na lengo letu ni ukombozi wa Zanzibar.”

Wakati huo huo mjumbe mwingine wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo Ndugu. Ismail Jussa alisema kuwa licha ya changamoto zote za kisiasa walizokumbana nazo tangu kuundwa kwa mfumo wa vyama vingi Zanzibar, bado imani na dhamira ya ukombozi haijapungua katika nyoyo zao.

"Tutaendelea kuwa pamoja katika mapambano haya mpaka tuhakikishe dola ya Zanzibar inasimama na tunapata mamlaka kamili ya Zanzibar”, alisema Jussa. Jussa ni miongoni mwa wanachama wa chama hicho wanaoshiriki ziara hiyo ya utambulisho wa mheshimiwa Othman Masoud.

Akitoa taarifa fupi ya chama mbele ya mgeni rasmi, Katibu wa Oganaizesheni na Wanachama, ndugu Omar Ali Shehe alisema kuwa Mkoa wa Magharibi 'A' kichama ni miongoni mwa ngome za ACT Wazalendo pamoja na kuwataka wanachama kuendelea kuidhibiti.

Katika hali ya kuboresha chama na kulinda hadhi na mustakbali wake ACT Wazalendo imezindua rasmi mpango mpya wa kulipia kadi na kuorodhesha wanachama wao, uliopewa jina la "LIPIA KADI YAKO, REJEA MATAWINI".

Mara baada ya kukamilisha ziara katika mkoa huo wa Magharib 'A', Mjumbe huyo wa kamati kuu, ambaepia ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameendelea na ziara yake katika mkoa wa Magharib 'B' kichama, yenye lengo la kutambuana na kufanya mazungumzo na wanachama wa chama chake katika mkoa huo.

Kesho (Mei 31) ziara itaendelea katika mkoa wa kusini pamoja na mkoa wa Kati Unguja kichama.​

IMG-20210530-WA0072.jpg
 
Safi sana. Tunataka siasa za kistaarabu hapa Zanzibar, CCM wafanye yao kistaarabu na ACT wafanye yao kistaarabu.

Sote tunajenga nyumba moja.

Tofauti hazikosekani
 
Back
Top Bottom