GE2025 Othman Masoud (OMO) azindua kampeni Pemba

GE2025 Othman Masoud (OMO) azindua kampeni Pemba

Matukio, Taarifa, Habari na Mijadala ya Wananchi WAKATI wa Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025

Parabolic

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2013
Posts
2,743
Reaction score
2,601
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman leo September 13 anazindua kampeni zake katika uwanja wa Tibirinzi, Chake Chake, Pemba kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza katika mkutano huo, Othman Masoud Othman, amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais, atahakikisha mipango ya maendeleo kwa wafanyakazi wa serikali na walimu itekelezwa mara moja, huku akisisitiza usawa na heshima kwa kila mtumishi wa Zanzibar.

Alisema moja ya hatua za haraka atakazochukua ni kuhakikisha askari wote wa Vikosi vya Usalama wa Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wanapata mshahara usiopungua milioni moja, hatua ambayo itaimarisha familia zao na kuongeza morali ya utumishi wa taifa.

Aidha, Othman aliahidi kuangalia upya hadhi na hali za walimu, ili kuwarejesha walimu kwenye heshima na mafao yanayofaa, kuondoa changamoto za kazi ya kupokea mwenge kila mwaka na kuhakikisha elimu Zanzibar inakuwa na misingi imara ya kitaaluma na kimaadili.

Othman alisema ameamua kugombea urais akiwa na dhamira ya dhati ya kutimiza kiu kubwa ya Wazanzibari ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa miaka mingi.

Alisema zama za subira zisizo na kikomo, ambazo ziliwahi kuhubiriwa na Almarhum Maalim Seif, zimepita na sasa ni wakati wa kusimama imara kudai haki ya Zanzibar.

"Tunataka kuiambia dunia kuwa tunachotaka sisi ni haki ya nchi yetu ambayo imeporwa muda mrefu. Wananchi wengi wa Zanzibar hawajanufaika na rasilimali zao, badala yake wachache wameendelea kunufaika kwa maslahi binafsi," alisema Othman huku akishangiliwa na wafuasi wake.

Othman alisisitiza kuwa Wazanzibari wanapaswa kushikamana zaidi katika uchaguzi huu ili kuiondoa Zanzibar kutoka kwenye hali ya kunyanyaswa na kudharauliwa kisiasa na kiuchumi. Alisema wananchi wamekuwa mstari wa mbele kwa miaka yote wakipigania mamlaka kamili ya Zanzibar na sasa ni wakati wa kuikomboa nchi.

Aidha, akigusia Muungano uliopo baina ya Zanzibar na Tanganyika, Othman alisema ni aibu kubwa kuona Zanzibar ikiendelea kunyanyasika. Alisema hata muasisi wa Muungano huo, Hayati Abeid Amani Karume, alipinga baadhi ya dosari zilizokuwamo, lakini hadi leo hakuna hatua zilizochukuliwa kuzirekebisha.

"Zanzibar inahitaji Muungano wa usawa, unaotoa fursa sawa kwa pande zote mbili, na si huu uliopo sasa unaonufaisha zaidi upande wa Tanganyika. Hili linawezekana tu iwapo Wazanzibari watanipa kura zao Oktoba 29, ili tuanze safari mpya ya heshima na usawa," alisema.

Othman pia aliwashutumu CCM kwa kutumia macho kufumbia matatizo ya msingi ya Zanzibar na badala yake kuruhusu nchi izidi kudidimia, huku wachache pekee wakinufaika kwa maslahi yao binafsi.

Akibainisha hatua atakazochukua endapo atachaguliwa Rais wa Zanzibar, Othman alisema atahakikisha changamoto hizo zinamalizika mara moja kwa kuweka msingi imara wa demokrasia na haki.

Aliahidi kusimamia mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya ya Zanzibar, itakayohakikisha uhuru wa kila mtu, tume huru ya uchaguzi, vyombo vya haki vinavyofanya kazi kwa uwazi, na uwajibikaji wa viongozi wote bila upendeleo.

"Katiba mpya itatoa nafasi ya kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza na kuwachukulia hatua wahalifu wote, ili hakuna mtu atakayejiona yuko juu ya sheria. Hii ndiyo Zanzibar mpya tunayoiandaa," alisema kwa msisitizo.

Kwa mujibu wa Othman, Katiba hiyo mpya pia itafungua njia ya Zanzibar kuwa na tume huru ya uchaguzi yenye heshima, ambayo itahakikisha kura ya kila mwananchi inalindwa na kuhesabiwa ipasavyo.

Viongozi mbalimbali wa chama hicho pia wamehudhuria, akiwemo aliyekuwa kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, pamoja na viongozi wengine wa kitaifa na kikanda. Pia wapo maelfu ya wanachama na wafuasi wa wamejitokeza kwa wingi kushiriki uzinduzi wa kampeni hizo.

0d84f607-92a4-4fc6-9efc-4c0d57e9031b.jpg

b58b4dbd-9b5f-46a6-95f9-61879dddc91b.jpg

fcb74b25-4cd2-4315-b620-96732096e9c7.jpg
Awali akizungumza kwenye mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa Timu ya Ushindi wa ACT Wazalendo, Mansour Yussuf Himid, amewataka watawala kujitafakari kwa kina, akisema misimamo ya Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, Othman Masoud Othman, ni mwendelezo wa dira na maono ya marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.

“Wananchi wako tayari kupambana ili kuhakikisha Othman Masoud anaingia Ikulu baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba. Kampeni hizi ni mwendelezo wa mapambano ya Maalim Seif kwa Zanzibar yenye heshima, haki na usawa.”

9b90658d-f794-4f4a-832d-c7711753701a.jpg

Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, amesema kwamba fursa pekee iliyobakia kwa Zanzibar kurudisha heshima na mamlaka yake ni kumchagua Othman Masoud Othman kuwa Rais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Amesema amemfahamu Othman Masoud kwa muda mrefu na anamtambua kama kiongozi mwenye msimamo wa kweli na aliye tayari kupigania maslahi ya Zanzibar bila kuyumba. Alikumbusha kuwa wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman hakusita kupambana hadharani akitetea mamlaka ya Zanzibar hata pale alipofukuzwa kazi, lakini alibaki imara na thabiti.

1e0d8da5-4d0b-4371-9645-cd2a83a1d874.jpg
 
Back
Top Bottom