Zilizokuwa ofisi za wabunge wa CUF Magomeni Dar es Salaam.
Wakati wanachama wa CUF wakiendelea kumfuata Maalim Seif Sharif Hamad aliyehamia ACT-Wazalendo, ofisi za wabunge wa CUF zilizopo Magomeni jijini Dar es Salaam zimebadilishwa na kuwa ofisi za chama hicho.
Akizungumzia mabadiliko hayo, mwanachama mpya wa ACT-Wazalendo Mbarara Maharagande amesema jengo hilo sasa ni ofisi ndogo za ACT -Wazalendo na zitafanya shughuli za chama hicho.
“Ofisi hizi zilipangishwa na wabunge wanane wa CUF ambao walitimuliwa, sasa wao pia wamehamia ACT-Wazalendo na wametoa kibali kwamba zitumike kwa chama hiki,” amesema Maharagande ambaye alikuwa naibu mkurugenzi wa habari wa CUF.
Amesema ofisi nyingi za matawi ya CUF ni nyumba za watu binafsi ambao walikuwa wanachama na baadhi yao wameamua kuhamia ACT-Wazalendo na kuzifanya nyumba zao kuwa ofisi za ACT-Wazalendo.
“Hii ni operesheni inayofanyika Dar es Salaam nzima, matawi yote ya CUF yatakuwa ya ACT-Wazalendo kwa sababu wananchi wameamua kumfuata Maalim Seif katika chama cha ACT- Wazalendo,” amesema Maharagande.
Kwa mwendo huu Lipumba na msajili watabaki wamiliki wa jina tu la CUF. Hawakutegemea itakuwa hivi.