Nyumba Salama kwa Mtoto Wako

Nyumba Salama kwa Mtoto Wako

Sema Tanzania

JF-Expert Member
Joined
May 18, 2016
Posts
251
Reaction score
466
Kila mzazi hufurahia mtoto anapofikia umri wa kutambaa na hatimaye kusimama na kutembea. Mtoto anakuwa amepata uhuru mpya unaomuwezesha kutoka sehemu moja kwenda nyingine mwenyewe. Pamoja na kufurahia hatua hii ya makuzi, mzazi pia huingiwa na wasiwasi maana sasa mtoto anakua na uhuru wa kufikia sehemu nyingi za nyumba na kuna namna nyingi ambazo anaweza kuumia.



Katika umri huu, mtoto wako ana hamu ya kujifunza jinsi ulimwengu unavyofanya kazi, na kwa sasa nyumba yako ndio dunia ya mtoto wako. Ni muhimu mtoto awe na uwezo wa kuchunguza vitu ili ubongo wake uweze kukua vizuri na wigo wa uelewa upanuke. Wajibu wako kama mzazi sio kumkataza kila kitu anachojaribu kugusa au kufanya bali kuhakikisha kwamba nyumba yako ni salama iwezekanavyo kwa mtoto wako kuzunguka na kujifunza.



Kuna mambo kadhaa unayoweza kufanya ili kuhakikisha nyumba yako ina usalama kwaajili ya mtoto wako. Ni muhimu kuzingatia kuwa baadhi ya vitu tunavyotumia katika shughuli za nyumbani kila siku huweza kumdhuru mtoto wako na hivyo vinatakiwa vihifadhiwe sehemu ambapo sio rahisi kwa mtoto kufikia.



Vitu vyenye ncha kali kama visu, nyembe na mikasi vinatakiwa viwekwe sehemu iliyojificha ambapo mtoto wako hataweza kufikia. Watoto hupenda kuiga kile tunachokifanya hivyo wanapotuona tunakata mboga jikoni, wanatamani kutusaidia. Bila shaka, utawakataza kushika visu lakini usipoviweka sehemu salama, wanaweza kurudi baadae na kujaribu kuvitumia wenyewe.



Nyumba zetu zimejaa sumu mbalimbali kuanzia sabuni, sumu za kuulia wadudu, dawa na hata vipodozi! Hakikisha vyote hivi vimehifadhiwa sehemu salama ambapo mtoto mdogo hawezi kufikia. Baadhi ya watoto hufarahia kumeza dawa na huweza kutafuna vidonge bila hata maji. Kuwa makini na mikoba ambayo mara nyingi huwa na dawa au vipodozi vinavyoweza kumdhuru mtoto endapo atavila.



Watoto wanapenda kuchezea soketi na vifaa vya umeme ambavyo ni hatari. Si ajabu kukuta mtoto mdogo akicheka kwa furaha huku akiwa anazima na kuwasha swichi. Wakati mwingine, watoto huingiza vidole kwenye matundu ya soketi au huingiza nyaya za umeme mdomoni. Ili kuepuka mtoto kuumia na umeme, jaribu kufunika soketi zote za umeme au uweke samani mbele ya soketi ili mtoto asiweze kuzifikia. Nyaya za umeme, pasi na vifaa vingine vya umeme viwekwe sehemu ambapo watoto wadogo hawafikii.



Hakikisha unaweka vyombo vizito na vinavyovunjika sehemu ambapo mtoto atashindwa kuvivuta ili visimdondokee na kumuumiza. Mara nyingi, watu hupenda kuweka vitambaa kwenye meza na vitu vizito kwa juu. Endapo mtoto atavuta kitambaa kile iwe kakusudia au kwa bahati mbaya, vyombo vitamdondokea na vinaweza kumuumiza.



Epuka mtoto wako kuungua jikoni kwa kuhakikisha anakaa mbali na sufuria za moto na uwe makini zaidi unapoandaa vyakula vya kukaanga kama vile samaki ambapo mafuta yanaweza kumrukia mtoto. Vilivile, mpini wa sufuria unatakiwa ugeuziwe upande ambapo mtoto hatoweza kuuvuta. Mueleze mwanao kuwa hatakiwi kugusa masufuria yakiwa jikoni maana yanakuwa ya moto na ataungua. Aidha, vitu kama viberiti na mishumaa vifichwe mbali.



Kuwa makini na maji bafuni na sehemu nyingine nyumbani. Watoto wengi hupenda kuchezea maji; iwe ni kuoga, majaribio ya kudeki, kufua nguo au kunawa tu mikono. Mtoto mdogo hapaswi kuachwa mwenyewe na maji maana kuna hatari ya kuzama au anaweza akanywa maji machafu. Vivyohivyo, maji na vimiminika vingine vikimwagika sakafuni huweza kusababisha mtoto akateleza na kaunguka vibaya.



Muhimu kuliko yote ni kuhakikisha mtoto wako haachwi mwenyewe hasa akiwa katika hatua za kujifunza kutambaa na kutembea. Hakikisha mtoto anakua na mtu makini ambaye ataweza kumsaidia mtoto kuepukana na ajali zinazotokana na utundu na kutaka kujifunza. Sio kwamba mtoto anyimwe kila kitu na kusimamiwa kama yupo jela, ila uangalizi ni muhimu. Iwapo mtoto atakua ameshashika kitu cha hatari kama vile kisu, muombe akupe na kisha muelezee matumizi ya kisu na kwanini kina hatari ili awe muangalifu.



Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia kurasa zetu za Facebook, Instagram na JamiiForums: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na
www.sematanzania.org.
 
Wangu alikua anafata visu mara kwa mara kilipomkata hataki kukiona kabisa
 
Back
Top Bottom