*NYUMA YAKO --- 01*
*Simulizi za series*
Hongkong, China. 2018.
Jana nilikuwa ufukweni mpaka majira ya saa tisa za usiku. Nilikunywa pombe nyingi na kula pia, vyakula vya kichina nadhani wavijua, vingi vya ajabu, kama isingelikuwa ni kwa ushawishi wa rafiki yangu, Jack Pyong, haki nisingetia mdomoni chochote kile kati ya nilivyokula.
Jack Pyong, jamaa mfupi wa kichina, ni rafiki yangu kwa muda mrefu sasa, takribani miaka nane. Amekuwa ni kiongozi wangu kila nijapo China, na zaidi mshawishi wangu mkubwa wa kuja huku China kila tupatapo likizo.
Ni mwanaume mcheshi sana. Ana asili ya China ila kiuraia yeye ni Mmarekani. Na kwasababu anapenda sana kushinda akitazama tarakilishi, macho yake yamekuwa mabovu, haoni vizuri pasipo msaada wa miwani, hivyo muda mwingine huwa namuita macho manne.
Jana hiyo usiku, kama nakumbuka vema na si akili ya pombe, Jack Pyong alinitambulisha pia kwa mwanamke fulani wa kizungu mkazi wa New Zealand. Mwanamke huyo alikuwa na macho yaliyojawa na haya, nywele nyeusi ndefu na gauni lake lilikuwa jekundu lenye dotidoti zinazong'aa.
Hivyo tu! ... ni hivyo tu ndivyo ninavyovikumbuka toka usiku wa jana, hamna kingine. Ni Jack, huyo mwanamke na kula na kunywa, basi! Mengine kichwa changu kimegoma kabisa kuyakumbuka.
Hapa niwapo kitandani, hata macho sijayafumbua, najaribu sana kukumbuka ila wapi! Nadhani sasa napaswa kuamka. Niamke na kumtafuta Jack, nadhani yeye atakuwa ana kumbukumbu nzuri kuliko mimi.
Lakini hayo ya jana ya nini? Sidhani kama yana umuhimu wowote. Nilisonya na kuminya lips, nikajigeuza upande mwingine wa kitanda na kuendelea kulala. Sikujali mwanga wa jua ulikuwa umeshaingia vya kutosha ndani ya chumba changu. Nilijisemea nipo likizo basi acha nilale mpaka usingizi ukate kabisa.
Sikujua hata nini kilikatisha usingizi wangu mpaka kuwaza yale ya jana. Nilipuuzia nikarudi kwenye jitihada zangu za kuutafuta usingizi ila punde zikakatishwa kiukatili na hodi mlangoni. Kabla huyo aliyegonga sijamsikia sauti yake, nikawa nimeshajua atakuwa ni Jack Pyong! Hakuna mtu ambaye angegonga mlango wangu kwanguvu zaidi ya mpuuzi huyu!
"Amka we zoba!" Alifoka Jack Pyong akibamiza mlango. Haki nilimchukia kwa dakika hizi. Nilijibandua kitandani, kiuzembe nikaujongea mlango na kuufungua nikiwa nimekunja ndita.
"Jack unaweza niacha nikakaa kwa amani, tafadhali?"
Alikuwa ameshika simu yake mkononi, amevalia pajama ya pinki! Hivi mwanaume unavaaje pajama ya pinki? Nikiwa namshangaa, kabla sijasema kitu, akan'tolea macho yake akinionyeshea kioo cha simu, "hivi we lofa, hujaona calls za general?"
"General? ... unamanisha inspector general?" Nikababaika. Hapa kidogo mawazo yangu yakatoka kwenye pajama ya Jack Pyong na macho yakakauka usingizi.
"Ndio, general!" Jack Pyong akanijibu akizama ndani. Akashusha pumzi ndefu akiketi kitandani, "Amenipigia mara nane! Mara nane, Tony," alisema huku mimi nikifunguafungua mashuka kutafuta simu yangu. "Nilivyopokea tu, kitu cha kwanza kuniuliza yu kwapi Marshall?"
"Ukamjibuje?" Hapa nikauliza huku nikiendelea na msako wangu. Kusema ukweli sikuwa najua wapi niliweka simu yangu. Nilikuwa natafuta hapa kitandani ila sina uhakika. Pombe ya jana ilikuwa imenivuruga akili. Nilikuwa natafuta huku kichwa kikiniwaka, nitakuwa nimeitupia wapi?
"Nikamjibu haupo karibu na mimi," akanguruma Jack Pyong, "akaniambia nikutafute haraka iwezekanavyo!"
Kumbe ndo' maana ulikuwa umevaa pajama ya kike? Nikajisemea mwenyewe kifuani huku nikiendelea kutafuta. Nikamaliza msako pasipo kuona.
"Jack, haukuona simu yangu?" Nikamuuliza nikiwa nimeshika kiuno, macho yanatazama huku na kule kusaka.
Akan'tazama,
"Simu yako mimi natolea wapi? ... Tony, au ulimhonga yule mwanamke?"
"Mwanamke yupi?"
"Si yule ... yulee ..."
"Unamaanisha yule m-new Zealand?"
"Hahah nilitaka nikuone tu, kumbe unamkumbuka enh?"
"Jack, huu si muda wa masikhara. Mbona mimi sikuhangaika na hiyo pajama yako ya kike?" Hapa Jack Pyong akajitazama kisha akaniangalia kwa hasira.
"Sioni simu yangu, Jack. Nisaidie kutafuta."
"Mie najua ilipo? ... sikia, Tony, chukua simu yangu uongee naye, acha kun'potezea muda."
Nikachukua simu hiyo na kuweka namba za simu, nilikuwa nimezihifadhi kichwani namba za General, nikapiga na kuweka simu sikioni.
"Tony, umefunguaje simu yangu?" Jack Pyong akaniuliza akininyooshea kidole. "Umejuaje password yangu? We mjinga, umejuaje password yangu?"
Sikumjibu, punde General akapokea.
"Mkuu, unaongea na Anthony Marshall hapa."
"Marshall," General akaita na kusema, "nataka ufike ofisini haraka iwezekanavyo!"
"Sawa."
Akarudia tena, "namaanisha haraka iwezekanavyo!" Kisha akakata simu. Nikamtazama Jack Pyong na kumuuliza, "Umesikia General alichosema?"
"Nitasikiaje na wewe ndo' ulikuwa unaongea naye?" Jack akateta akinipokonya simu yake.
**
Kabla sijaendelea nadhani kuna haja ya kujitambulisha. Kwa jina, nadhani hilo tayari ushalijua, acha niachane nalo. 'Anyway', naitwa Anthony Marshall, ndilo jina langu rasmi. Jack hufupisha kuniita Tony, ila kazini najulikana zaidi kwa jina la Marshall. Mimi ni mkazi wa New York, Marekani. Ni ajenti wa shirika la upelelezi la Marekani, CIA (Central Intelligence Agency).
Sina mke wala mtoto, wala mchumba. Ndio. Na si kwamba umri haujafikia, hapana. Nina miaka thelathini na tano hivi sasa. Pengine sijapata mwanamke sahihi, au ni kazi zinanibana sana. Ila hiyo sababu ya kwanza ndiyo yenye mantiki zaidi.
Kwa upande wa kazi, sasa ni takribani miaka nane tangu niwe katika shirika la CIA, nikihusika zaidi na kategoria jenzi ya watu waliopotea na kutekwa.
Mpaka sasa, kwa mkono wangu, nimeshasaidia uokozi wa wamarekani kumi na moja waliopotea na watano waliotekwa nchi mbalimbali haswa Somalia na uarabuni. Nimekwepa risasi zisizohesabika na kupata jeraha karibia kwenye kila sehemu ya mwili wangu.
Sina haja ya kukwambia nimepitia magumu kiasi gani. Hatari kiasi gani. Bila shaka mwajua ajenti wa taasisi ya siri ya upelelezi anayoweza kukumbana nayo anapokuwa kazini. Lakini ajabu ni kwamba nimekuwa nikiyafurahia hayo. Napenda kazi yangu. Napenda ninachokifanya.
Tatizo ni kwamba, nakaa muda mwingi sana mbali na nyumbani. Kuna muda mpaka naweza jisahau kama kwangu ni New York! Kukaa miaka mitano, mitatu, miwili au hata kumi ukiwa nchi ya ugenini ni jambo la kawaida kwa ajenti wa CIA. Kukutana na watu wageni machoni, kuzungumza lugha za kigeni kama mzawa, kubanwa kiuno na bunduki, ni mambo ya kila siku hayo, si ya kushangaza tena.
Kazi yangu kama ajenti, pasipo kujali ni wapi natumwa, ni kukusanya taarifa nyeti na muhimu kisha kuzituma nyumbani kwa ajili ya hatua zaidi. Na pale panapohitajika, kujiingiza kwenye kombati kwa ajili ya jambo fulani, haswa kujiokoa pumzi yako na wale ambao unawalinda.
Sababu hiyo basi, natakiwa kuwa mkufunzi wa mapambano pasi na silaha na nikiwa na silaha pia. Lakini zaidi, kuwa mwepesi mno kwenye kuchambua hali na kufanya maamuzi yenye tija. Ninaposema mwepesi mno, namaanisha kweli hivyo. Mimi na Jack Pyong, huwa tunasema kabla risasi haijakufikia, inabidi uwe umeshaamua cha kufanya.
Hivi hilo litawezekanaje? Kuna muda tunajazana ujinga sana na Jack! Ila tu ni kuonyesha namna gani ambavyo mtu inabidi uwe mwerevu na mwenye akili nyepesi sana. Na hivyo basi ndo' maana CIA huwa inaweka madaraja na kuwa wachaguzi sana kwa watu wanaowaajiri.
Wakikagua kuanzia GPA ya mtu awapo kozi, lakini pia namna anavyojieleza, kuchambua na kuhitimisha mijadala yenye mikanganyiko ndani ya muda mfupi. Mtu mwenye 'sense' zaidi ya tano za binadamu. Zaidi ya hapo, akiwa tena mwenye ujuzi wa lugha nyingi, haswa Kiarabu, Dari, kikorea, kituruki, kichina, kisomali, kiindonesia na kadhalika.
Kwa upande wa Jack Pyong, aaaahmmm, sijui kwanini walimchukua kwakweli. Hajui kupambana, hajui lugha yoyote zaidi ya kiingereza na kichina. Utumizi wake wa silaha ni hafifu haswa na ninapomsihi ajifunze zaidi huniambia hana muda huo kwani CIA hawakumchukua kwa ajili ya kupambana.
Labda anachojivunia ni utaalamu wake nyuma ya 'keyboard' na ujuzi wake kwenye mambo ya sayansi. Ni mwerevu sana kwenye hayo, na basi hataki mengine kabisa.
Lakini mbali na ubishi huo, ni rafiki mmoja mzuri sana, japo kuna muda huwa ananipotosha. Ni mtu wangu wa karibu sana na mara nyingi nakuwa naye kazini na mbali ya kazini.
Yeye pia hana mke wala mtoto, bali mchumba tu ambaye huitwa Violette. Mwanamke huyo ni Mmarekani na amekuja naye hapa Hong Kong kwaajili ya likizo hii.
Nadhani utambulisho huo unatosha. Mengine utayajulia kadiri nikusimuliapo yanayotukia kwenye kisa hiki cha kukuacha mdomo wazi. Kisa ambacho nimekipa jina la NYUMA YAKO kwa maana kwamba, si kwasababu unatazama mbele, ukadhani nyuma ya mgongo wako mambo yamesimama. Lah! Ukiwa unatazama mbele, nyuma pia kuna mambo yanaendelea, na mambo hayo yanaweza yakawa ya hatari kuliko uwazavyo.
Na kwasababu haujayapa kipaumbele kama yale ya mbele, mambo haya ya nyuma huwa ya ghafla na hatarishi zaidi, yakikuacha ukiwa umelala chini hujiwezi, damu zakububujika.
Tazama nyuma yako. Huenda kuna mchezo unaendelea ambao hauuoni.
***