Nyuki wavuruga karamu ya msiba

Jidu

JF-Expert Member
Mar 9, 2011
1,212
2,000
Details
Imechapishwa Ijumaa, 07 Desemba 2012
07:45
Imeandikwa na John Mhala, Kibosho
Imesomwa mara: 811
PAROKO wa Parokia ya Mkombole ya
Kanisa Katoliki, aliyetajwa kwa jina moja la
Ephraim amelazimika kutimua mbio baada
ya makundi matano ya nyuki kuvamia
waombolezaji mara baada ya kuzika.
Katika tukio hilo la aina yake, Paroko
Ephraim na Mwenyekiti wa Halmashauri
wa Wilaya ya Moshi Vijijini, Morris Makoi
walijikuta wakikimbia waombolezaji na
magari yao kwenda kujificha mashambani
kuepuka kudhuriwa na nyuki hao.
Kabla ya nyuki hao kuvamia msiba huo
juzi, Paroko Ephraim aliwaongoza
waombolezaji kumzika Agnes Malya (30)
katika Kijiji cha Osaki, Kibosho wilayani
Moshi Vijijini aliyefariki hivi karibuni kwa
maradhi.
Baada ya maziko, Paroko Ephraim, Makoi
walikaribishwa katika chakula
kilichoandaliwa kwa waombolezaji wote
kijijini hapo. Hata hivyo, wakati
waombolezaji wakijipanga kushiriki
chakula hicho, ghafla walijitokeza nyuki
wakiwa katika makundi matano na
kuvamia waombolezaji waliokuwa hata
hawajagusa chakula hicho.
Uvamizi huo ulisababisha Mwenyekiti wa
Halmashauri wa Wilaya ya Moshi Vijijini,
Makoi na Paroko Ephraim kutangulia
kutimua mbio kuokoa roho zao baada ya
kushambuliwa na kung'atwa na kundi la
nyuki walioibuka na kuvamia msiba huo
na kufuatwa na mamia ya waombolezaji
wengine.
Wosia wa marehemu “Marehemu aliacha
wosia kutokana na ndugu wa marehemu
mumewe kukataa kuchangia matibabu
yake wakati akiwa hospitali, basi wasije
wakajidai kuandaa sherehe wakati akifa
kwa kupika vyakula, pombe na vinywaji.
“Sasa si mnaona shughuli ya kumzika
imekwenda vizuri ila kabla watu hawajala
ndio nyuki wakajitokeza?” Alisema mmoja
wa ndugu wa marehemu ambaye
hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Muombolezaji mwingine, Gerad Temba
aliwalaumu ndugu wa marehemu kwa
kukiuka wosia wa dada huyo aliyeweka
bayana kwamba asingependa sherehe na
madoido ya aina yoyote katika msiba
wake.
“Kabla na wakati wa mazishi nilikuwa
nikikumbusha alichosema marehemu,
lakini hawakutaka kusikia sasa matokeo
yake ndio haya,“ alisisitiza Temba.
Mwenyekiti ashangaa Akizungumza na
gazeti hili lililoshuhudia kisa hicho, Makoi
ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ukaoni
alisema ni mara ya kwanza kuona tukio la
namna hiyo na limemshtua mno.
“Tulilazimika kukimbia mbio kuokoa
maisha yetu, ni tukio la kushangaza sana
nyuki wengi kiasi kile kutokea
kusikojulikana na kuanza kushambulia
waombolezaji kabla ya kumaliza shughuli
za mazishi.
“Kuna tetesi kuwa marehemu hakutaka
chakula wala pombe na vinywaji wakati wa
mazishi yake vitu ambavyo alisema
gharama zake zingetosha kumtibu
ugonjwa uliomwua, sasa sina hakika kama
ni kweli,” alidai Makoi. Baadhi ya
waombolezaji walikimbizwa katika vituo
vya afya vilivyopo karibu na kijiji hicho
akiwamo wifi wa marehemu ambaye ndiye
aliyeandaa chakula katika msiba huo, Mery
Sembeki.
Sembeki aliumwa na nyuki mwili mzima
na kulazimika kuvua nguo na baadaye
alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya
KCMC ambako alitundikiwa maji ya dawa.
Majeruhi wengine 8 walikimbizwa katika
Hospitali ya Misheni ya Kibosho ambako
walipatiwa huduma ya kwanza na
kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Pia kutokana na kizaazaa hicho, chakula na
vinywaji vyenye thamani ya zaidi ya Sh
milioni 5 vilimwagwa jana asubuhi kama
ishara ya kutimiza alichokisema
marehemu Agnes.
Waombolezaji wengine Wakizungumzia
tukio hilo, baadhi ya waombolezaji
walishauri jamii kubadili mtazamo wake
kwa kuchangia mambo ya msingi kama
wagonjwa katika matibabu badala ya kutoa
michango mikubwa wakati mgonjwa
anapofariki.
“Tutalazimika kubadilika, badala ya
kuchanga mamilioni kwenye mazishi
tuchange kumnusuru mgonjwa ili yeye
mwenyewe atambue mchango ule badala
ya kuchangia maiti” alisema mmoja wa
waombolezaji ambaye hakupenda jina lake
litajwe gazetini.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom