Nusura wanawake waniadhiri kwenye ‘Bustani ya Ibilisi’

Hamid Rubawa

Member
May 23, 2018
72
202
Nusura wanawake waniadhiri kwenye ‘Bustani ya Ibilisi’

Ahmed Rajab

Picha: Mwandishi wa makala haya, Ahmed Rajab (kushoto), akiwa na mwandishi mwenzake wa Tanzania, Salim Kikeke, wakiwa na tuzo zao zilizoenzi mchango wao katika kukuza lugha ya Kiswahili. Tukio hilo lilifanyika London, Uingereza, hivi karibuni.

Na Ahmed Rajab

DUH! Ningefedheheka nikashika adabu yangu. Na wanawake ndio wangeliniponza kwani mti huponzwa na tundale. Sijui uso wangu ningeutundika wapi.

Safari moja nikiwa ninatembea Tindouf, mji wa jangwani Magharibi mwa Algeria, niliwaona waandishi wa habari wa kimataifa wakiwazunguka viongozi wawili wa chama cha Polisario chenye kupigania ukombozi wa nchi hiyo kutoka ukoloni wa Morocco.

Viongozi hao, Bashir na Mouloud, walizungukwa na waandishi kama saba au wanane hivi kutoka Marekani, Ufaransa, Algeria na Uingereza. Sita kati yao walikuwa wanawake, wawili wao walitokea Uingereza pamoja nami.

Nilipowasogelea niliwasikia waandishi hao wakibishana vikali na wenyeji wetu. Kila upande ukitoa hoja zake. Niliwasikia wenzetu wa kike wakiwabembeleza akina Bashir waturuhusu twende mpakani ndani ya Sahara ya Magharibi kwenye eneo la mapigano baina ya wapiganaji wa Polisario na wanajeshi wa Morocco.

Huko mpakani kuna ukuta mrefu uitwao ‘Ukuta wa Morocco’. Ulijengwa na Morocco na unayatenga yale maeneo yanayoshikiliwa na Morocco na yale yanayodhibitiwa na Polisario na yenye kuunda Jamhuri ya Sahara ya Magharibi.
Wale waandishi wa kike waliponiona, nyuso zao na macho yao yalinigeukia mimi. Mmojawao akaniuliza: “Wewe unasemaje?”

Nilimjibu kwa kusema: “Bila ya shaka, lazima twende.”

Hayo ndiyo matamshi yaliyodondoka mdomoni mwangu lakini moyoni mwangu mlikuwa na matamshi mengine: “Balaa gani tena hili?” Nilijiuliza.

Kusema kweli sikuwa na hamu ya kwenda kwenye eneo la mapigano ndani ya Sahara ya Magharibi. Nilihisi tunakwenda kujitolea mhanga, bilashi.

Kwanza, eneo lenyewe lilikuwa mbali na tulipokuwako; pili, nilishawahi katika ziara yangu iliyopita ya Sahara ya Magharibi kusafiri jangwani na nilijuwa kwamba hiyo itakuwa safari isiyotegemea ramani wala dira ya kawaida.

Nyakati za usiku safari za huko hutegemea nyota zinazomeremeta katika anga lililogubikwa na giza. Saa za mchana hutegemea alama kama vile za miti na mijiwe. Joto lilikuwa sababu nyingine iliyoufanya moyo wangu usitamani kusafiri jangwani kwa muda mrefu. Safari ya jasho ya kutegemea nyota, miti na mawe.



Tindouf ni mji wenye historia ya vita. Mwaka 1963, mwaka mmoja baada ya Algeria kupata uhuru wake kutoka Ufaransa, mji huo ulishuhudia mapigano makali baina ya majeshi ya Algeria na ya Morocco. Kila upande ukisema kuwa sehemu hiyo ni yake. Mapigano hayo yalibandikwa jina la “Vita vya Mchanga”.



Tindouf uko kwenye hammada, uwanda tambarare wa jangwa la Sahara unaoitwa “Bustani ya Ibilisi.” Joto la huko halishikiki na si la kuchezewa. Tena mara kwa mara eneo hilo hupigwa na dhoruba za mchanga zenye kuyaparaganya maisha.



Mji huo ulijengwa na watu wa kabila la Tajakant, mabedui wa Sahara. Katika karne ya 19 Watajakant walikuwa haweshi kupigana na mabedui wa makabila mingine ya Reguibat na Kunta.



Tangu 1975 Tindouf umekuwa mji wa kambi za wakimbizi wa Sahrawi. Siku za vita kati ya wapiganaji wa Polisario na majeshi ya Morocco (1975-1991) kambi hizo zikiendeshwa na wanawake wakati wanaume wao walipokuwa wakipigana vitani. Kwa hakika, mambo mawili ya kupigiwa mfano waliyoyafanya wapiganaji wa Polisario katika kambi hizo ni kuwakomboa wanawake na kuufyeka ukabila.



Ingawa wapo wanawake waliotoroka kutoka kambi hizo na wanaodai kwamba wamekuwa wakidhalilishwa hata hivyo, kwa jumla, wanawake wanaoishi chini ya utawala wa Polisario wameendelea sana kifikra. Kwa vile wanawake ndio wenye kuziendesha kambi nyingi za Polisario wao pia ndio wenye kuongoza utawala wa Sahara ya Magharibi.



Waandishi wa kike niliokuwa nao walivutiwa sana na wanawake wa Kisahrawi waliowaona. Mimi kwa upande wangu nilivutiwa na wote — wanawake wa Kisahrawi pamoja na hao waandishi wa kike kwa namna walivyojitolea kufanikisha tasnia yao.



Walipokuwa wakishikilia turuhusiwe twende kwenye eneo la mapigano sikutaka kubishana nao. Nilichelea nisije baadaye nikatiwa hewani na wale waliotoka Uingereza kwamba nikiogopa. Kwa hivyo, nami pia bila ya kutaka nikajikuta nimeingia ngomani.



Bashir na Mouloud waliondoka wakisema wanakwenda kushauriana na wenzao. Waliporudi walirudi na nakala za waraka waliompa kila mmoja wetu na walitaka tuutie saini. Kwa ufupi, waraka huo ulisema kwamba tumeamua kwa hiyari zetu wenyewe kwenda kwenye mapigano na kwamba mauti yakitufika hakuna wa kulaumiwa.



Kichwa upande, huku moyo wangu ukianza kuwa mzito, niliishika kalamu na kutia saini yangu. Fikra za aina kwa aina zikaanza kunijia. Wenzetu wa kike walikuwa katika shangwe; walijaribu, bila ya mafanikio, kuviiga vigelele vya wanawake wa kisahrawi.



Wapiganaji wa Polisario wakaanza kutupa mafunzo ya nini tufanye tukifika kwenye eneo la mapigano. Mwanzo kabisa walitufunza namna ya kutembea kwa kugaragara na kwenda kwa tumbo.



Halafu wakatueleza kwamba mmoja wetu akipigwa risasi akaanguka basi wengine wamuache nyuma na wasonge mbele.
Baada ya hapo tukachukua virago vyetu kuelekea kwenye medani ya vita. Usiku katika giza la jangwani madereva wetu wakifuata njia kwa kuangalia nyota na mchana kwa kuangalia miti waijuayo na vifusi vya mawe. Mara mojamoja wakisimama kuwinda sungura ambao ndio tuliokuwa tukila.



Siku ya pili yake tulipofika karibu na ‘Ukuta wa Morocco’ nililiona jabali ambalo wapiganaji wa Polisario walilichimba na kulifanya pango. Tukaingizwa ndani ya pango hilo tukisubiri jua litue ili tukaribie kwenye mpaka wa mapigano. Wapiganaji wa Polisario walipiga mizinga dhidi ya vituo vya jeshi la Morocco.



Muda si muda wanajeshi wa Morocco nao wakarusha bomu lililoanguka mahala tulipokuwako kama dakika tatu kabla. Jasho jembamba lilinitiririka.



Giza lilipoanza kuingia tukaambiwa tunapelekwa kwenye ‘Ukuta wa Morocco’. Tuliamrishwa tusizungumze na amri tulizokuwa tukipewa tulikuwa tunapewa kwa minong’ono.



Kisha tukaambiwa tuanze kwenda kwa kutumia matumbo yetu. Polepole tukausogelea ‘Ukuta wa Morocco’. Upande wa pili tukisikia sauti za wanajeshi wa Morocco. Baada ya kitambo tukafika katika vituo ambavyo muda si mrefu vikishikwa na wanajeshi wa Morocco.



Tulivyoingia katika mahandaki yao tulikuta vipande vya sigara, mikebe ya samaki iliyokuwa mitupu na risasi walizokwishazipiga. Nilizichukuwa sita, ambazo ninazo hadi leo, kuwa kumbukumbu yangu.



Kwa bahati mbaya au nzuri, usiku ule hakujazuka mapigano. Hata hivyo, waandishi wenzangu wa kike walikikata kiu chao cha kuwa katika medani ya vita. Kwa upande wangu, nilifurahi kwamba na miye pia nilikuwako na sikuadhirika mbele yao.



Nilimshukuru Mungu kwamba hakuna miongoni mwetu aliyedhurika. La kusikitisha ni kwamba wiki kadhaa baadaye mwenzetu mmoja mwanamume wa Kimarekani aliyekuwa mwandishi wa gazeti moja maarufu la Marekani alikutikana ameuliwa nyumbani kwake mjini Algiers. Alinusurika vitani akaja kuuliwa chumbani.



Swali ambalo mara nyingi hujiuliza ni: kwa nini waandishi habari na maripota wa kike wanakuwa na shauku kubwa sana ya kuripoti katika maeneo ya hatari? Kila penye mapigano na vita utawakuta wamekwishafika. Nini kinachowavutia?



Pengine hili si swali zuri la kuuliza, kwamba labda lina harufu ya kibaguzi. Pengine utahoji kwamba ripota ni ripota tu na suala la jinsia yake halihusiki na kazi yake. Lakini nahisi ni halali kuuliza swali hili.



Nilipokuwa nikihariri jarida la Africa Analysis, London, nikishangazwa kwa idadi ya waandishi wa kike wa kujitegemea waliokuwa wakijitolea kuripoti katika maeneo yaliyokuwa na vita. Nikiwaruhusu wende ingawa siku zote nikiwatahadharisha na kuwanasihi kwamba hakuna taarifa yoyote ya habari iliyo adhimu kushinda maisha yao. Ni nasaha ninayopenda kuitoa kwa waandishi wote, wake kwa waume, wanaojitosa kwenda kuripoti katika maeneo ya mapigano.



Nilijikuta nikiitoa nasaha hiyohiyo miaka michache iliyopita nilipokuwa ninalisimamia Shirika la Habari la Umoja wa Mataifa la IRIN huko Dubai. Ofisi yetu ikishughulika na habari za nchi zilizokumbwa na vita na mizozo mbalimbali ya kijamii katika Mashariki ya Kati na Asia. Takriban asilimia 90 ya waandishi wangu walikuwa wanawake wakiripoti kutoka Iraq, Palestina, Israel, Yemen, Syria, Afghanistan, Lebanon, Misri na Pakistan. Wakiripoti katika hali ngumu na za hatari.



Mara kwa mara ikinibidi nende kuwazuru na nikiona namna walivyokuwa wakiishi katika mazingira ya shida kama, kwa mfano, katika eneo la Gaza baada ya kushambuliwa na Israel. Niliona jinsi wanavyozishika roho zao mikononi mwao katika nchi kama Afghanistan ambako hujui bomu litafyetuka wapi au washambulizi wa kujitoa mhanga watashambulia wapi na wakati gani.



Nakumbuka jinsi malaika yalivyonisimama niliposikia kwamba wapiganaji wa Taliban waliishambulia Hoteli ya Serena mjini Kabul siku chache tu baada ya mimi na wenzangu kula chakula hotelini humo. Tena saa hizohizo za usiku. Au niliposikia kwamba hoteli niliyoshukia mjini Peshawar, Pakistan, ililazwa kabisa kwa bomu wiki chache baadaye.



Ni nadra kumpata mwandishi mahiri na aliye shujaa. Linalonishangaza ni kwamba siku hizi wanawake wanazidi kuwa miongoni mwa waandishi wa aina hiyo. Ninaona mtindo huu unaanza kutia fora hata miongoni mwa waandishi wa kike wa Kiafrika.



Mmoja wao na aliye maarufu nchini Tanzania ni Valerie Msoka, Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa TAMWA, niliyeanza kumjuwa tangu akiwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha City University, London. Baadaye Valerie alifanya kazi na Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, pamoja na Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Iraq na sasa Somalia. Akiwa na BBC aliripoti kutoka Rwanda, Burundi, Congo na Uganda.



Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; X:mad:ahmedrajab



Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.



Makala haya yalichapishwa mwanzo kwenye gazeti la Raia Mwema la tarehe 25 Machi, 2015.







Gazeti la Dunia ni Jukwaa Huru la Fikra kwa wasomaji wa lugha ya Kiswahili lenye lengo la kuchapa makala za kichambuzi kuhusu masuala mbalimbali muhimu kwa Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla. Waandishi wa kwenye jukwaa hili ni maveterani na wabobezi kwenye maeneo watakayokuwa wanaandikia. Kama unajua unachokiandika, hili ni jukwaa lako.

Screenshot_20230928-213848_Chrome.jpg
 
Back
Top Bottom