Njaa ni janga

Njaa ni janga

Mohamed Ismail

JF-Expert Member
Joined
Mar 16, 2014
Posts
228
Reaction score
249
WANITESA NJAA
____________________

Katika mihangaiko ya kuhakikisha angalau na mimi napata uhakika wa kuunganisha mahusiano mazuri kati ya mkono na mdomo. Nikiwa naishi kwenye jiji la hekaheka natoka kwenye mizunguko yangu na hapo jua tayari limeishaanza kurembua likilikaribisha kiza kwa mbali. Nipo zangu kituo cha Makumbusho nasubiri daladala zinazoelekea Tabata. Nimesimama nimechoka huku moka yangu iliyoishilia upande mmoja nasikia inachoma miguu yangu kwa joto kali kutokana na mwendo mrefu niliyotembea kuelekea kituoni.

Natumia zaidi ya nusu saa sioni gari nawaza au nimepata laana ya yule bibi ambaye asubuhi niligoma kumuachia seat akae wakati naenda kwenye mihangaiko. Ila moyoni najisemea hakuna laana za hivyo hapa ni mjini kila mtu na mama yake. Nataka kuuliza kama magari leo hayapo huku moyoni naogopa nitaonekana mimi wa kuja. Naamua kutulia nikijipa moyo kuwa yatakuwepo punde si punde basi linafika huku watu ni wengi sana kila mtu anampiga kikumbo mwenzie angalau aweze kuingia ndani. Ukiangalia unaona kabisa watu ni wengi basi halitoshi. Mlimwengu mimi natumia mbinu za kivita najichomeka chomeka hadi naingia kwenye basi na kupata siti ya kukaa.

Konda wa gari anazidi kupanga abiria kama magunia ya mkaa. Nikiwa nimekaa natoa simu yangu ya tecno iliyopasuka kioo na kuangalia yaliyojiri mjini. Nakutana na habari ya mfungwa anayeombwa arudishwe jela kisa maisha ya uraiani kwake anaona magumu, napata kutafakuri kuwa duniani kuna watu na viatu.

Nikiwa nimekaa pembeni yangu kasimama dada mmoja mzuri mwenye asili ya kimanga, konda anavyozidi kuwapanga watu yule dada anabanwa na kulalamika. Mlimwengu mimi naamua kujitoa muhanga kama askari wa kivetnam na kumuambia aje akae siti yangu mimi nitasimama. Najua hapo utasema mimi fala ila naamini kwa yule mtoto hata wewe usingegoma. Ile asante yake kwangu ilimaanisha mengi nikamuachia anishikie begi langu mimi nikashika bomba huku nakumbuka wahenga walishasema wanaume mateso.

Ndani ya masaa mawili nipo kwenye basi kutokana na foleni za jiji letu zinazochagizwa na ujenzi wa barabara unaoendelea kwa kazi nzuri ya serikali yetu.
Nikiwa na njaa napitia genge la kwa mpamba nakumbuka geto upo unga na mimi nimebakiwa na elfu mbili mfukoni. Nachukua nyanya kitunguu na nyanya chungu mfukoni nabaki na buku.
Nafika geto naanza na kutengeneza mboga inaiva vizuri naweka maji ya kusongea ugali. Nikiwa ndio naanza kusonga ugali mara naona moshi wa bluu ghafla gesi inakata na kuzima. Nikiangalia akiba yangu inasoma sh mia tano. Nawakumbuka wale wanasiasa wanaotuhumiza tutunze akiba wanazungumzia akiba ipi?. Kiukweli njaa inazid kusumbua ule ugali hauwezi kulika ndio kwanza unga ulikuwa umechanganyikana na maji. Asikwambie mtu njaa inauma naamua kula mboga na kunywa maji mengi.

Nilikuwa na kazi ya kufanya kabla sijalala hata nguvu inaniishia naona akili kabisa hazimo. Nabaki tu nabonyeza simu na ninachokibonyeza sikijui. Naingia kitandani ikiwa imelala napigiwa simu na my wangu ananiuliza baby umekula? Namuambia ndio. Ananiuliza umekula nini? Namuambia usiku napenda kula vitu laini nimekula chips na samaki. Ananiambia usiku mwema huku mwenzie njaa naisikia. Nalala nikiwa na mawazo mengi nakumbuka taabu ninazozipitia naapia moyoni siku nikipata hela kitu cha kwanza nanunua debe la unga na debe la mchele na gesi ya kutosha. Na nikipata zaidi kitu cha kwanza nitanunua gari maana kero ya usafiri ninayoipata nimechoka.

Nikamfikiria Baba wa Taifa Mwl J.K Nyerere ndio maana vitu vya kwanza kutaka kupambana navyo ni njaa. Kiukweli njaa haina adabu, na ukishakuwa na njaa automatically huwezi kuwa romantic, asilimia 90 ya mahusiano yetu ya mapenzi yanakufa kwa sababu ya njaa. Hakuna anayependa njaa jamani ndio maana njaa ni kama laana. Tumebaki kuwasema watu siyo waaminifu wametusaliti kumbe sisi ndio tumejisaliti tuliwekeza mioyo yetu kwao ila wengine wakajiwekeza kiuchumi na kuhakikisha njaa siyo shida kwao. Hatimaye tunakimbiwa tuliowekeza mioyo na wanakimbilia kwa wale waliojiwekeza kulinda tumbo.

Ukisoma kwenye riwaya ya Kuona Bin Safari mwandishi kajitahidi kuzungumzia njaa kuwa endapo tumbo likishalegea huwezi kuwa na maamuzi mazuri kichwani mwako lazima uwe bendera fuata upepo ilimradi mkono uende kinywani. Demokrasia kwenye njaa haiwezekani hiyo labda litakuwa domo tupu. Naamini hata wanasiasa wetu wakijiimarisha kwenye njaa tutakuwa na watu wenye misimamo.

Ile siku nimeamka na njaa nasikia Tanzania ya viwanda. Nikajiuliza moyoni hawa viwanda wanazungumzia vipi wakati mimi nina njaa. Niliona ni kitu ambacho hakiwezekani kutokana na njaa. Njaa inazalisha chuki, uvivu, husuda, roho mbaya na uchawi. Ninaamini tukishakitahidi kudhibiti njaa kwa kiasi kikubwa ndio tutakapoweza kuzungumza lugha moja. Wahenga walishasema shibe mwana malevya njaa mwana malegeza.

Mlimwengu mimi ngoja niishie hapa maana hii njaa siyo kitu kizuri. Imepeperusha wachumba wetu, imetupotezea kujiamini kwetu, imetuharibia mawazo yetu mazuri tuliyokuwa nayo na sasa hivi inanyongonyesha ufanisi wetu wa ufanyaji kazi.

Ni Mlimwengu mimi yuleyule uliyembiwa kuwa usipofunzwa na mama yako atakufunza.
#njaaninoma
#njaanimsiba

Imeandikwa na Mohamed Ismail Rwabukoba
Email: mohammedismail613@gmail.com
Phone no: 0762070361

16/12/2019
FB_IMG_1576569171039.jpeg


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Isee! Huwa sisomagi story ndefu ila hii imenishika nikaisoma mpaka mwisho! Nimefurahishwa sana na mahali pale ulipompa siti binti ili mradi tu akupe 'Asante'. Unajua katika maisha tunajimwambafai na kuleta dharau ni kwasababu hatujapitia changamoto. Ukipata changamoto utatafuta hata mtu wa kukusalimia atakosa
 
Nakuhakikishia story yako imegusa wengi sana.
Kweli kabisa mkuu, haya yashawah nitokea acha kabisa boss unaweza waza mengi mpaka kukufuru, ila hii ni mitihani tu mkuu katika maisha, one day historia yako itakuwa hamasa kwa wengine na kuamini nothing is impossible boss, inuka, jikung'ute vumbi kisha endelea kupambana mpaka maisha yajisalimishe kwako na siyo wewe kujisalimisha.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Isee! Huwa sisomagi story ndefu ila hii imenishika nikaisoma mpaka mwisho! Nimefurahishwa sana na mahali pale ulipompa siti binti ili mradi tu akupe 'Asante'. Unajua katika maisha tunajimwambafai na kuleta dharau ni kwasababu hatujapitia changamoto. Ukipata changamoto utatafuta hata mtu wa kukusalimia atakosa
Kabisa kuna wakati unahitaji tu mtu mmoja wa kukupa nguvu

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom