Nisikupende kwa nini, Nawe Umenikirimu

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,809
Ukiyaonja mapenzi utaujuwa utamu
Ndipo utapoyaenzi ukayaona adhimu
Nakupenda Mwenye enzi Ilahi Mola Karimu

Nisikupende kwa nini Nawe Umenikirimu


Nisikupende kwa nini Ya Ilahi ya Karimu
Nawe umenithamini kuniumba mwanadamu
Ukaniongeza shani Kwa dini ya Isilamu

Nisikupende kwa nini Nawe Umenikirimu


Meniumba insani Mwanadamu alo huru
Ukanipa Qur ani Ili iwe yangu nuru
Sasa nina kheri gani Kama sijakushukuru

Kwa nini nisikupende Nawe Umenikirimu


Rasuli ukamtuma Ili aje nifundisha
Kila jambo lilo jema Yote kanifahamisha
Akafanya kila hima Risala kukamilisha

Kwa nini nisikupende Nawe Umenikirimu


Akujuwaye yakini Hawezi kuwa mjinga
Akamfata shetani Na Wewe akakutenga
Kwani vyote ardhini Asili yake mchanga

Kwa nini nisikupende Nawe Umenikirimu


Umetuletea maji Twanywa tukiona raha
Hujayafanya ujaji Machungu yenye karaha
Ya Rabi ewe Mpaji Tuzidishie furaha

Kwa nini nisikupende Nawe Umenikirimu


Na mbingu ukaziumba Kwa nyota ukazipamba
Na kisha ukaziremba Zikapangika sambamba
Kama zimefungwa kamba Hapana kinachoyumba

Nisikupende kwa nini Nawe Umenikirimu


Wallahi tukiperemba Kutizama utukufu
Tunaelewa ya kwamba Ni kazi yako Latifu
Ni kazi yako Muumba Ilo timu kamilifu

Nisikupende kwa nini Nawe Umenikirimu


Neema zako ni nyingi Ya Rabbi L arbabu
Umetupa mambo mengi Hayana hata hesabu
Ewe Mpaji kwa wingi Ewe wangu Mahabubu

Kwa nini nisikupende Nawe Umenikirimu


Hewa hii tuvutayo Moja ya Zako neema
Neema ambayo kwayo Kukupenda ni lazima
Lau kama hatunayo Uhai ungeyoyoma

Kwa nini nisikupende Nawe Umenikirimu


Vyote ulitayarisha Hata bado kutuumba
Mahitaji ya maisha Bila hata kukuomba
Ukarimu usokwisha Kutoka kwako Muumba

Kwa nini nisikupende Nawe Umenikirimu


Ninakupenda Wallahi Na Wewe Ndiye Shahidi
Pendo kwako likisihi Ndipo nitapofaidi
Ninakupenda Ilahi Na Mtume Muhamadi

Kwa nini nisikupende Nawe Umenikirimu



M. F. S. Al Saaiy
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom