Nini kinasababisha mitafaruku ndani ya muungano?

satellite

JF-Expert Member
Nov 18, 2010
616
164
Nini kinachosababisha mitafaruku ndani ya Muungano mara kwa mara? Kama Wazanzibari hawapendelei mfumo wa serikali moja kama njia ya kumaliza mitafaruku kwa hofu ya kumezwa, nini kifanyike kuridhisha pande zote ili Muungano uendelee kwa amani na utulivu?

Majibu ya maswali haya yatapatikana kwa kuangalia tu historia ya Muungano wenyewe, kuona kilichotarajiwa, udhaifu na mapungufu yanayorekebishika.

Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar uliofikiwa April 26, 1964, ulitokana na sababu kubwa mbili: Sababu ya kwanza ni hofu ya Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, kupokonywa madaraka na wanamapinduzi wenzake Visiwani, hasa wale wa kikundi cha siasa za mrengo wa kushoto wakiongozwa na hayati Abdulrahman Babu [Umma Party] na Abdallah Kassim Hanga [ASP].

Nyerere aliwahi kukiri kwamba, Karume alipendekeza wazo la Muungano kwake kwa mara ya kwanza walipokutana Dar es Salaam [Januari 15, 1964] kuzungumzia suala la “Field Marshal” John Okello, mmoja wa walioshiriki katika mapinduzi ya Januari 12, 1964, ambaye pia ndiye aliyetangaza mapinduzi hayo kupitia Redio ya Taifa, Zanzibar. Lakini dhana hii haina nguvu baada ya ushahidi mwingi kuonyesha kwamba Karume alishinikizwa.

Sababu ya pili ni shinikizo la nchi za Magharibi kutaka Zanzibar iungane [na kumezwa] na Tanganyika ili kuviokoa Visiwa hivyo kuangukia upande wa kambi ya Kikomunisti ya Warusi na Wachina kufuatia mapinduzi Visiwani enzi hizo za vita baridi, kati ya nchi za kibepari za Magharibi na za kisoshalisti za Mashariki.
Ndiyo maana siku ya Muungano, Marekani, Uingereza na Tanganyika, ziliandaa majeshi kuivamia Zanzibar kama wananchi wangeasi au kuupinga Muungano uliopangwa. Kwa hiyo, kwa Marekani na Uingereza ilikuwa moja tu kati ya mambo mawili: ama Muungano au nguvu za kijeshi zitumike kuharibu mapinduzi ya Zanzibar. Huu ndio ukweli juu ya chimbuko la Muungano; sababu zingine zinazotolewa ni za kudandia tu.
Kuungana kwa nchi hizi mbili kulifanyika haraka haraka kiasi kwamba hapakuwa na muda wa kuandaa Katiba madhubuti ya Muungano. Kilichofanyika ni kwa viongozi wa nchi hizi mbili, Rais Nyerere na Karume kufikia makubaliano ya dharura na mambo mengine muhimu kuachwa kwa matarajio ya kuwekwa sawa baadaye hali itakapokuwa shwari. Hata hivyo hali hiyo haijatokea na inazidi kuchafuka kwa jina la kero za Muungano.
Mazungumzo juu ya Muungano yalifanyika kwa siri ya hali ya juu sana. Kumbukumbu zilizopo na maelezo ya waliokuwa madarakani enzi hizo yanaonyesha kuwa, si watu wengi katika Serikali ya Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Zanzibar waliojua kilichokuwa kikitokea. Mbali na Nyerere na Karume, wengine waliojua kilichokuwa kikifanyika walikuwa mabwana Rashid Kawawa, Oscar Kambona, Abdallah Kassim Hanga na Salim Rashid.
Mazungumzo yalipokamilika, Nyerere alimwita Mwanasheria wake Mkuu wa Serikali, Roland Brown na kumwagiza aandae haraka sana Hati ya Makubaliano ya Muungano bila mtu mwingine kujua. Hati hiyo [Articles of Union] iliandaliwa kwa muda mfupi mno siku hiyo [21/4/1964] na kutiwa sahihi April 22, 1964, kisha kupelekwa Bungeni haraka haraka kuridhiwa kuwa Sheria [Acts of Union] Aprili 25, 1964; na Aprili 26, Muungano ukatangazwa.
Kwa upande wa Zanzibar, Karume kabla ya kutia sahihi Mkataba huo, alimpa Mwanasheria wake Mkuu, Walfango Dourado, likizo ya lazima ya dharura ya siku saba; badala yake akamwita Mwanasheria kutoka Uganda, Dan Wadada Nabudere, kuja kumshauri juu ya Hati hiyo ya Muungano iliyowasilishwa na Tanganyika. Wote, Brown na Nabudere walihudhuria majadiliano kati ya Nyerere na Karume. Bado ni fumbo kubwa kwa nini Dourado hakushirikishwa; lakini inaaminika ni kwa sababu ya msimamo wake mkali wa kikomunisti kwamba asingeridhia Mkataba huo.
Hati za Muungano [Articles of Union] zilizotiwa sahihi na marais hao zilitoa picha na dira tu ya Muungano na mambo mengine yaliachwa kushughulikiwa na Tume ya Katiba iliyokuwa iteuliwe kupendekeza Katiba kabla ya kuitishwa Bunge la kupitisha Katiba ndani ya muda wa miezi 12 tangu Muungano.

Kwa mfano, tunapomfanya Rais wa Zanzibar kuwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano maana yake nini? Kwamba naye anawajibika kwa Rais na kwa Bunge la Muungano kama walivyo mawaziri wote? Maamuzi ya Baraza la Mawaziri yanamhusuje kama Rais wa Zanzibar? Anayatekelezaje Zanzibar? Kama nani?
Rais wa Zanzibar anapotembelea Bara na kutenda shughuli za kiserikali, anafanya hivyo kama nani? Kama Rais wa Zanzibar au mgeni ziarani nchini “Tanzania” au kama Waziri?
Haya ni maswali magumu yanayotaka kupitiwa upya na ili kuelewa aina gani ya Muungano unaotakiwa. Na maadam Zanzibar haiko radhi kupoteza hadhi yake ndani ya Muungano [ingawaje Tanganyika imekubali kupoteza hadhi na jina lake], hatuwezi kukwepa kufikiria juu ya Muundo wa Shirikisho kama tunataka Muungano huu udumu.

Source: Raia Mwema
 
Je tunahitaji kuwa na serikali 3 ili kuokoa jahazi?
 
Back
Top Bottom