Ningekuwa Mulongo ningeomba radhi

Ningekuwa Mulongo ningeomba radhi

Dingswayo

JF-Expert Member
Joined
May 26, 2009
Posts
4,019
Reaction score
2,932
Edson Kamukara

NAJUA ni jambo gumu sana hasa kwa mtu mzima na tena kiongozi kukubali kujishusha kuomba radhi pale anapogundua kuwa amekosea na kuwakwaza wananchi kwa matendo yake.

Kwa waliosoma vizuri ahadi 10 za TANU, watakuwa wanakumbuka ahadi hii ya ‘cheo ni dhamana, sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu'.

Aprili 24 mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo aliliagiza Jeshi la Polisi kumkamata Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) kwa madai kuwa alichochea vurugu katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
Lema alifika chuoni hapo kuzungumza na wanafunzi waliokuwa wakitaka kuandamana kwenda kwa mkuu wa mkoa kushinikiza wapewe ulinzi baada ya mwenzao kuuawa kwa kuchomwa kisu na mtu asiyejulikana jirani na chuo jana yake.
Mbunge huyo alijitahidi kwa kila mbinu kuwashawishi wanafunzi hao wasiandamane, huku akifanya juhudi za kumpigia simu mkuu wa mkoa afike kuwasikiliza.

Mulongo baadaye alifika chuoni hapo, lakini akataka apewe kipaza sauti na kutoa angalizo kuwa hawezi kuzungumza na watu wasio na nidhamu.

Kauli hiyo iliwaudhi wanafunzi ambao kimsingi walikuwa na majonzi ya kumpoteza mwenzao, hivyo walianza kumzomea Mulongo na kisha kurusha mawe na kusababisha mkutano uvunjike.

Wakati wote Lema alipowahutubia wanafunzi, askari walikuwep eneo hilo wala hawakumkamata kwa kuwa hawakuona kosa lolote alilofanya. Lakini muda mfupi baada ya hapo, Mulongo aliagiza mbunge huyo akamatwe akidai ndiye aliyechochea vurugu hizo.
Siku moja baada ya Mulongo kutangaza Lema akamatwe, mbunge huyo alifanya mkutano na waandishi wa habari katika moja ya hoteli jijini Arusha, akawaonesha ujumbe wa vitisho aliotumiwa na kiongozi huyo.

"Umeruka kihunzi cha kwanza, nitakuonyesha kuwa mimi ni serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi ninayotaka mimi,'' ulisomeka ujumbe huo uliotumwa kupitia simu namba 0752 960276 ambayo Lema alidai ni ya Mulungo.
Siku hiyo usiku wa manane, Lema alizingirwa nyumbani kwake na askari polisi pamoja na maofisa Usalama wa Taifa akatishwa kisha baadaye akajisalimisha na kupelekwa kituoni alikowekwa rumande kwa siku tatu hadi juzi alipofikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa uchochezi.

Mtiririko wote huu ni matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji mkubwa wa ahadi ile ya TANU niliyoinukuu hapo awali.
Inachekesha na kushangaza kuona Lema ambaye ni kiongozi wa kuchaguliwa na watu, anayetambulika makazi yake, ofisi yake eti askari wanaacha kupumzika usiku wanakesha kuzingira nyumba yake kumkamata.
Askari hawa walitumia mafuta yaliyonunuliwa na fedha ya walipakodi, wakafanya kazi muda wa ziada kumsaka na kumdhalilisha kiongozi aliyechaguliwa na watu kwa amri ya mkuu wa mkoa.

Laiti Mulongo angekuwa kiongozi makini alipaswa kushirikiana na Lema, wanafunzi na uongozi wa chuo kuvitumia vyombo vya ulinzi kumsaka mtuhumiwa wa mauaji ya mwanafunzi wa IAA.

Ningekuwa Mulongo ningewaomba radhi wakazi wa Arusha kwa kumdhalilisha mbunge wao. Pili kutumia rasilimali fedha za walipa kodi kushughulikia jambo jepesi na kuacha kiini cha tatizo.

Alichokifanya Mulongo ni taswira ya viongozi wa kuteuliwa, wasiowajibika moja kwa moja kwa wananchi bali kwa yule aliyewateua, ndiyo maana hata wanapoharibu wanaweza kuondolewa na kupelekwa kwingine bila kuhojiwa.
Siamini kiongozi kama mkuu wa mkoa, anakosa hekima katika kutenda majukumu yake. Maana inashangaza kidogo kuona mbunge anapangiwa kazi za kufanya na maeneo ya kwenda na mkuu wa mkoa.

Hivi Mulongo kweli hajui kama Lema amechaguliwa na wananchi wa Arusha. Mbunge anaweza kujificha miaka yote kama wahalifu wengine wakati akijua wapiga kura wake lazima wambane kutimiza ahadi zake?

Kama ndivyo, kulikuwa na haja gani ya kupoteza muda wa wanafunzi kufunga chuo, kuwachosha askari kumsaka mtu ambaye wangeweza kumpigia simu akaripoti mwenyewe, kodi za wananchi kwa ajili ya magari badala ya kuimarisha ulinzi chuoni na kumkamata muuaji? Tafakari!
 
Kule katika kabila letu, ni udhaifu kwa mwanaume kuomba samahani. Inaaminika kuwa mwanaume hakosei bali anapitiwa tu kidogo na akipitiwa basi wengine walioona inabidi wamezee!! Inafika mahali ambapo mwanaume inambidi kumeza kiburi mambo yanapomzidia na kusimama mbele za watu kusema," Ndugu zangu, kama utelezi ni mkubwa kiasi cha kumfanya kuku ateleze, je binadam inakuaje mahali kama hapa? Nisameheni! Anasamehewa na wanaanza kunywa pombe pamoja!
 
Back
Top Bottom