...ninachokumbuka ni ,,,,,,,,,,,,,, | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

...ninachokumbuka ni ,,,,,,,,,,,,,,

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, Mar 25, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Mar 25, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Wanamuziki wa kundi la Five Star Modern Taarab walionusurika kwenye ajali wameeleza kuwa vishawishi na masikhara kwa dereva ndivyo vyanzo vikuu vya ajali ile mbaya iliyowaua wenzao 13.

  Wakizungumza na wanahabari kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, wasanii hao walisema kuwa dereva huyo alikuwa kwenye mwendo wa kasi na alikuwa akipewa sifa na baadhi ya wasanii waliokuwa kwenye msafara huo uliokuwa umegubikwa na utani miongoni mwao.

  Baadhi ya walionukuliwa:

  Kiongozi wa Five Star, Ally Jay alisema:
  "Baadhi yetu tulikuwa tumekunywa lakini sio kuwa tulilewa kushindwa kujitambua, mfano mimi nilikunywa bia mbili tu, dereva naye ni binadamu alikuwa kwenye mwendo mkali sana, naweza kusema vishawishi ndio vilivyoleta maafa yote ingawa pia kila jambo linapangwa na Mungu."

  "Siku zote huyu dereva anaitwa Chala Boy mimi huwa sipendi uendeshaji wake anaendesha spidi (mwendo mkali) sana tulikuwa na madereva wawili tulipokuwa tunatoka Kyela (Mbeya) nilitaka dereva msaidizi ndiye atuendeshe, lakini kama unavyojua wenzangu walinipinga kwa madai kuwa atawalaza njiani, ndio huyu dereva mkuu akaendesha toka kule Kyela alikuwa kwenye spidi sana hata tulipomwambia punguza mwendo yeye ndio kwanza alifanya masihara."

  "Unajua watu wazima wanapokutana hususani wasanii wanakuwa na mambo ya kitoto hata hao watoto wenyewe wana afadhali, zile hadithi, masihara ndivyo vilivyompa kichwa dereva akawa spidi zaidi, na kwa vile ndio tulimzoea na siku zote ndo tunasafiri naye wengine walifurahia uendeshaji wake..."

  "Dereva yupo hai, simu yake ninayo mimi kwani baada ya ajali mimi niliweza kuokota simu nne za wenzangu na moja ilikuwa ya kwake kwani muda mfupi nikiwa nasaidia kutoa maiti alinipigia na kujitambulisha ni yeye akadai anaenda hospitali ya Morogoro, lakini mpaka hivi ninapozungumza nawe wewe hatujamuona wala hatujui yupo wapi, ila tunajua yupo hai."
  Msanii Shaban Azizi 'Mfupa' alisema:
  "Dereva tulimwambia usiendeshe kasi akawa hasikii tulikuwa tukielekea Songea tukitokea Kyela, nusura tule mzinga (tuanguke) pale kwani kuna kona moja mbaya aliiingia vibaya na kusababisha gari letu kuyumba, Kitonga yote ile Ruaha alikuwa spidi, na baadhi yetu walikuwa wakimpa kichwa achape ilale tuwahi kufika kwa vile tulikuwa tumemzoea tuliona ni kawaida, tulipofika Mikumi tulikutana na tembo, lakini bahati nzuri aliwahi kufunga breki."

  "Muda ule Issa Kijoti (marehemu) alikuwa amekaa mbele akarudi nyuma na kumpisha mbele Rajabu Kondo na yeye akakaa nyuma kabisa ya gari na Mwanahawa Ally. Tembo walipovuka nasi gari letu likapita, lakini dakika tano tu baada ya kuwavuka wale tembo ndio tukapata ajali na wenzetu kupoteza maisha, mpaka sasa siamini kilichotokea naona kama nipo ndotoni."

  Msanii Zena Mohamed alisema:
  "Tulitoka vizuri kwa furaha zote, shoo yetu ilifanikiwa tulikuwa tunataniana sana , tulipofika Songea tukagundua kuwa shoo yetu ya Songea ilikuwa imeshatolewa hela na Hamer Q alikuwa amechukua Shilingi 1,000,000 na bila kutuambia, na muda huo yeye alishukia Iringa hakwenda nasi Songea na wala hakusema kama ameshachukua hela ya shoo ile na Issa Kamongo ndio tuligundua kuwa alisaini Hamer Q apokee hizo hela, sasa kwenye gari mazungumzo karibu njia yote yalikuwa ni kuhusu suala hilo."

  "Tulitaniana kwa kweli, watu wawili tu kwenye lile gari, yaani Mwanahawa Ally na Rajabu Kondo ndio waliokuwa wanamsihi dereva asiendeshe kwa kasi, lakini wengine walifurahia na waliendelea na simulizi zao tena kama Haji Mzaniwa alikuwa akipiga kelele kabisa akimwambia dereva chapa ilale, hatujaona ongeza na dereva naye akazidi spidi, sijui kilichotokea ninachokumbuka ni sauti ya ya Issa Kamongo alipiga kelele kwa nguvu akisema, Chala 'unatuuaa' nilijikuta chini sijui chochote kilichoendelea baada ya hapo, mpaka sasa sijawa sawa."

  Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamikia juzi maeneo ya Mikumi, Morogoro na wasanii 13 walipoteza maisha huku watano wakiwa majeruhi.Kufuatia ajali hiyo, wasanii mbalimbali wa bendi za muziki wa dansi na taarabu wamepanga kufanya tamasha maalum Mei Mosi la kuwaenzi wasanii wenzao waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo ambayo haijawahi kutokea nchini.
   
 2. Lyimo

  Lyimo JF-Expert Member

  #2
  Mar 25, 2011
  Joined: Mar 7, 2006
  Messages: 3,828
  Likes Received: 33
  Trophy Points: 145
  Inasikitisha sana.
  Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awalaze pema peponi marehemu wote wa ajali hii, na awajalie neema na uponaji wa haraka wale wote walionusurika, pia awajaze imani na nguvu ya kulikabili tukio hili wale wote walioguswa na msiba huu. Amina
   
 3. Saint Ivuga

  Saint Ivuga JF-Expert Member

  #3
  Mar 25, 2011
  Joined: Aug 21, 2008
  Messages: 39,516
  Likes Received: 19,940
  Trophy Points: 280
  Inasikitisha sana.
  soo sad
   
Loading...